Ndugu Rais, imeandikwa; wacha tukuchezee Bwana kwa matendo yako makuu.

Wacha tukutukuze Bwana kwa ukuu wako! Mbingu na nchi zinatangaza ukuu wako Bwana, milima nayo yapendeza yamtukuza Yeye. Alipo Wewe Bwana utukufu unashuka!

Canaan mji ule! Mji wa divai iliyo njema. Alitutahadharisha mapema kiongozi wetu kuwa mtakapofika Canaan mtakaribishwa kwa divai aina kwa aina, lakini msionje zote kwa maana mnaweza kusahau mlango wa kutokea.

Kama ilivyo maana ya pombe kwa Wachaga kuwa ni mbege, ndivyo ilivyo rubisi kwa Wahaya. Wengine wana chimpumu, isute, ulanzi na mnazi.

Canaan divai ni pombe na pombe yao ni divai. Hii ndiyo Canaan, mji wa harusi kumbukwa.

Tuliambiwa ni Canaan mahali ambako Bwana Yesu alifanya muujiza wake wa kwanza. Yeye na mama yake walialikwa harusini. Walipofika wakakuta divai imeisha. Mama yake Yesu aliwaambia wahudumu watii kila watakachoambiwa. Ndipo Yesu akawaambia wajaze maji makasiki na wawape watu wanywe ili waendelee na burudani. Nao walipokwisha kunywa wakakiri ubora wa divai ya Yesu wakisema, “Harusi nyingi huanza kwa divai nzuri na mwishoni hulewa divai hafifu. Lakini hii, imeanza kwa pombe nzuri na mwishoni imeletwa pombe nzuri zaidi.’’ Abarikiwe mwanamwema yule aliyeniwezesha kuufikia mji wa Canaan.

Ndugu Rais, tuongoze katika njia ielekeayo Canaan tukajazwe bashasha mioyo yetu ipate ukunjufu na uchangamfu. Canaan ukatuvushe salama katika mto Jordan! Jordan mto ule! Tulishuhudia watu wa mataifa wakitoka pembe zote za dunia wakibatizwa kwa namna alivyobatizwa Yesu Kristu. Baba tulee katika njia ifaayo nasi hatutaiacha hata tuzeeke sana sana.

Haya yote yanajiri baada ya mwanamwema kuniandikia akisema, “Mwalimu Mkuu kumbe wewe ni mwanasiasa mkubwa tena wa upinzani.’’ Ulofa hauna mwenyewe. Baba kilichomuwasha ni pale nilipoandika kuwa Watanzania wamemsikia Rais akiongea kwa makini kabisa katika kongamano la Kigoda cha Mwalimu Nyerere, lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika ukumbi wa Nkrumah.

Alisema, “Nafahamu kiu ya Watanzania ya katiba mpya…’’ Baba amesema kiu ya Watanzania. Vuvuzela huyu anadhani madai ya katiba mpya ni madai ya wapinzani. Wapinzani wanaweza kuwa na madai yao kama walivyokuwa nayo wasio wapinzani, lakini hii sisi hapa inatuhusu nini? Baba amesema anafahamu kiu ya Watanzania ya katiba mpya. Kiu ya Watanzania ndiyo kiu ya nchi yao Tanzania. Ukijaliwa kuifahamu kiu ya nchi ujue umebarikiwa. Ili ubaki mbarikiwa hakuna cha kuchagua, bali ni kuikata kiu hiyo. Wape watanzania katiba mpya ukate kiu ya nchi. Kudhani kuwa katiba mpya ni kiu ya wapinzani ni mawazo ya vuvuzela peke yao.

Baba kasema, “Nafahamu kiu ya Watanzania kuhusu katiba mpya.’’ Kuifahamu kiu ya nchi nasi tukaonesha nia ya kutotaka kuikata kiu hiyo tunajiondolea wenyewe sababu ya sisi kuendelea kuwapo hapo tulipo.

Nafahamu katiba mpya haiwezi kuwa mwarobaini wa matatizo yetu yote, lakini kwanini hatutaki kujifunza kwa ndugu zetu wa Kenya? Watu waliuana kwa maelfu na kwa maelfu mengine Wakenya wengi walipoteza makazi yao. Kwanini sisi tungoje mpaka tufike huko? Leo Wakenya kwa katiba yao mpya wamekuwa kama tulivyokuwa sisi zamani, wanaitana ndugu! Akitokea kiongozi yeyote anayeweka shingo ngumu katika hili hatufai.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Warioba Butiku ameungana na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba, kuzungumzia suala la katiba mpya akisema mjadala wa kuipata haujafa kwa sababu wenye katiba ambao ni wananchi bado wanaishi na kusisitiza kwamba katiba bora ndiyo inabeba misingi ya uendeshaji wa nchi na wananchi wa Tanzania wanahitaji misingi hiyo iwekwe kwenye katiba yao.

Wakati akiurejesha mfumo wa vyama vingi vya siasa, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alisema, “Iwe isiwe vyama vingi vitakuja kwa sababu wanaotaka vyama vingi wapo. Ni busara kuvikubali sasa ili CCM ndiyo iongoze mabadiliko hayo.’’

Na kwa maneno hayo ya Mwalimu Nyerere, ije mvua, lije jua katiba mpya itapatikana kwa sababu wananchi wanaoitaka wapo. Ni busara kwa wenye mamlaka sasa kuikubali katiba mpya sasa ili wao ndiyo wawe wasimamizi wa upatikanaji wake.

Kwa kuwa tumekiri hadharani kuwa katiba mpya ni hitaji la wananchi na nchi yao, ni lazima tuhakikishe kuwa inapatikana. Katiba mpya ingesaidia kuwaelimisha wasioelewa kuwa mahitaji ya nchi na wananchi wake ndiyo kipaumbele cha kwanza katika nchi yoyote inayojiendesha kidemokrasia na wala si kwa matarajio ya kikundi cha watu au mtu fulani. Nchi ni ya wananchi wakiwamo viongozi wao, lakini kamwe nchi si mali ya viongozi.

Ije katiba mpya itakayosaidia kuwaelimisha baadhi ya viongozi wetu kuwa wao ni watumishi tu wa wananchi na kamwe si watawala wetu. Iwape ufahamu wa kutambua kuwa timamu wote wanamchagua mtu awe kiongozi wao ili awaongoze ingawa wapuuzi wachache wanaweza wakamchagua mtu ili awatawale.

Ndugu Rais, tuongoze kwenda Canaan tutoke huku kulikojaa hofu, ubabe, unafiki na uvuvuzela. Maendeleo ni mchakato, huwezi kuyaona katika muda mfupi huu. Kamusi kuu ya Kiswahili inatafsiri pongezi kuwa ni zawadi au maneno yanayojenga hamasa ambayo huambiwa mtu kama ishara ya kutambua na kufurahia mafanikio aliyoyapata. Profesa Rwekaza Mukandala aliwaambia Watanzania kuwa baba hawezi kusema amefanikiwa kwa kuwa analeta chakula nyumbani wakati mama na watoto hawana furaha. Kupongeza kwa sasa ni kwa unafiki tu.

Ninapomalizia mjadala wa katiba napokea ujumbe ambao nami nauweka kama ulivyokuja, “Naitwa Kijazi wa Majohe. Mzee Mayega wewe ndiyo msemaji wetu sisi wanyonge tusiosikika. Kwa kuwa Rais wetu mara kwa mara tumemsikia akisema ni Rais wa wanyonge, tunakuomba umjulishe na muombe atuondolee gharama za matibabu kwa marehemu wapendwa wetu. Baadhi ya familia zimelazimika kuzitelekeza maiti zao kwa kushindwa kulipia gharama za matibabu waliyopata marehemu wao.’’ Anasema marehemu alitibiwa kwa siku nne akafariki, lakini wakalazimika kulipa shilingi laki sita kuuchukua mwili. Najua baba ni msikivu atatupeleka Canaan kwenye matumaini!

By Jamhuri