maguNdugu Rais, vitabu vyote vitakatifu vimeandika habari za Nabii Musa.

Mwenyezi Mungu alipomwita kwenye kichaka kilichokuwa kikiwaka moto alimwambia: “Musa, hapo ulipo ni mahali patakatifu, vua viatu vyako!”

Mafundisho ni mengi kutokana na tukio hilo, lakini hapa pia tunafundishwa kuwa kila jambo lina utaratibu na masharti yake. Ukiwa mahali patakatifu ni lazima uvue viatu. Musa alivua viatu vyake kuonesha utayari wake wa kumsikiliza Mwenyezi Mungu!

Kama Musa angekataa kuvua viatu vyake nina hakika Mwenyezi Mungu asingemkabidhi zile Amri Kumi. Angemtafuta mtu mwingine.

Ndugu Rais, yako mambo mengi katika maisha yetu yanayotutaka kuvua viatu vyetu ili kuyafanikisha. Umewataka wananchi wakuombee, sawa tumekusikia, lakini je, na wewe unawasikia watu wako wanapokuuliza kama uko tayari kuombewa? Vua viatu vyako kama Musa alivyovua viatu vyake ili amsikilize Mwenyezi Mungu na watu wako watakuombea.

Maombi yanataka utayari wa kujutia yaliyopita, kudhamiria mema kwa yajayo na kuachana na mazingira yaliyokufikisha hapo mpaka umekuwa chukizo. Wale ambao ulishirikiana nao katika uongozi mpaka mkaifikisha nchi hapa

ilipo ni viatu- wavue!

Najua una viatu vya bei mbaya, lakini viatu vyako hapa ni wale wote waliowafikisha wananchi wa nchii hii katika umasikini huu wa kustaajabisha kwa sababu tu ya unyang’au wao, kwa ukora wao, wizi na kupenda anasa! Viatu ni wale wote walioshindwa uongozi wa nchi na badala yake wakavutiwa na uroho wa kuwa na mali nyingi, nao wakaanza kuipora nchi! Wavue hao- ni viatu, nasi tutakuombea!

Wale wote ambao wamewakumbatia wanaokuhujumu wewe na serikali yako ni

viatu, wavue. Majipu yote uliyokwisha tumbua ni ufisadi uliofanywa na mafisadi. Lakini baadhi ya mawaziri wako na watendaji wengine ambao

kwao hawa si mafisadi kwa sababu tu ndio wafadhili wao wakuu, ni viatu wavue!

Walioficha sukari wanakuhujumu wewe binafsi na serikali yako ni mafisadi wanaolindwa na ufadhili wao kwa chama. Sasa wanaficha mafuta ya kupikia ili wananchi wakuchukie. Hao mawaziri na baadhi ya viongozi wanaowakingia kifua kwa sababu ya ufadhili wao ni viatu, wavue! Uliwajaza hofu kubwa pale uliposema: “Watu waliofanya madudu katika utawala uliopita au watakaofanya sasa, hawatachomoka kwa kuwa nimejipanga kuwashughulikia wote bila kujali uwezo wala vyeo vyao.

“Nawaomba watanzania mwendelee kuniombea kila siku na naamini mnafanya hivyo… Salamu zangu kwa watu waliozoea kujinufaisha na rasilimali za nchi, waambieni hapa kwangu hachomoki mtu.”

Kwa wanaokuhujumu na wanaowalinda maneno yako yalikuwa kama mwiba uchomao kote kote. Maamuma bado wanadhani wananchi wanaendelea na ujinga. Wanawaonesha watu wa Mungu waliojikalia kimya kuwa eti ndio mafisadi.

Hawa wamekufanya hata wananchi wa kule vijijini walioanza kukupenda kwa kazi njema unayofanya, sasa wakuchukie wakidhani ni wewe uliyewatuma

wakaidhulumu haki yao ya kuona wanachofanya wawakilishi wao wawapo

bungeni- ni viatu, wavue! Mtu asiyekupenda atasema hayo ni mambo ya Bunge. Omba Mungu akunyime vyote, lakini akupe akili kichwani ya kuielewa

dunia! Wapambe wengi waliishia kujuta! Mambo ya Bunge, wakati anatangaza kuzima TV bungeni alitumwa na Bunge?

Kumfanya rais awe chukizo kwa watu wake ndio usaliti mkubwa kabisa anaoweza kufanyiwa rais wa nchi! Anatenganishwa na wananchi ili kumpunguza kasi ya kupendwa!

Ndugu Rais, wazazi tumepewa wajibu wa kuwalea vijana wetu katika njia ifaayo ambayo nao hawataiacha hata watakapokuwa wazee. Maandiko

yanasema Mwenyezi Mungu alimpatia Nabii Musa Amri Kumi. Kati ya hizo Amri Kumi za Mungu, moja inasema waheshimu baba yako na mama yako ili uishi miaka mingi na upate heri hapa duniani. Kijana aliyempiga baba yake au

mzee anayeheshimika na jamii na hata kuaminiwa na Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, hadharani huku nchi nzima ikishuhudia, ni mwana

mlaanifu! Huyu amevunja amri ya Mungu mwenyewe aliyompa Nabii Musa!

Kumfanya kuwa kiongozi ni kukaribisha mikosi katika nchi. Kiongozi kama huyu hawezi kuheshimika popote bila msaada wa polisi. Nchi hii haina uhaba wa viongozi makini na wenye historia iliyotukuka! Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kabla Mwenyezi Mungu

hajamchukua katika makazi yake ya milele alituachia wosia akisema:

“Ikulu ni mahali patakatifu!” Kama hivyo ndivyo ilivyo, ndugu Rais vua hivi viatu vyako!

Watanzania wanaitaka nchi yao mpya siyo hii iliyovurugwa! Nchi ya Watanzania wenye fikra sahihi. Wanaoelewa kuwa nchi ni moja na ni yao

wote katika umoja na usawa wao. Wenye uelewa kuwa vyote vilivyowekwa katika nchi hii na Mwenyezi Mungu, iwe juu ya ardhi au chini ya ardhi na majini, viliwekwa kwa ajili yao wote.

Nchi ya viongozi watumishi watakaowatumikia wananchi na siyo nchi ya  viongozi waheshimiwa waporaji wakuu wa mali za nchi. Wako viongozi wasioamini katika dini yoyote. Hiyo ni haki yao na ni lazima watambuliwe na waheshimiwe. Nao lazima watambue kuwa hali ya kutokuwa na imani katika dini yoyote siyo ya kujivunia na kujisifu mbele za wenye kuamini, kwa sababu wale waliotuletea hizo dini ndio waliotuaminisha kuwa asiyekuwa na dini ni mshenzi. Dini zetu na vyama vya siasa viliikuta nchi navyo vitapita, lakini nchi itabaki!

Watanzania wapya wataimba kwa pamoja uzalendo kwa nchi yao kutoka katika vifua vyao na siyo kutoka katika midomo ya walaghai! Nao wote kwa pamoja watakiri na kusema, ‘Nchi yangu kwanza’.

Ndugu Rais, Mwalimu mwema aliwauliza wanafunzi wake akisema: “Nimtume

nani?” Mwanafunzi wake mnyenyekevu na mtiifu kwake akamjibu: “Nitume mimi Bwana!”  Ndugu Rais, yule mwanafunzi kuomba atumwe yeye alikuwa hatafuti kazi ya mshahara! Alikuwa anatafuta kusikilizwa na mwalimu wake! Alizongwa katika kifua chake na mateso ya watu wa nchi yake!

Alikuwa anaomba naye abarikiwe kwa kushirikishwa katika kuwakomboa watu wa Mungu kutoka katika machungu yao waliyosababishiwa na manyang’au! Viongozi waliotawaliwa na uroho wa mali na anasa

wakamwacha Mungu! Ndugu Rais, nitume mimi Ee, Bwana!

1124 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!