Ndugu Rais, yanayoandikwa katika ukurasa huu hayalengi kumpendeza mtu wala kumchukia mtu. Nchi yangu kwanza ndiyo dira; watu, vyama vya siasa na mengine baadaye! Hachukiwi mtu hapa kwa sababu imani ya ukurasa huu ni kwamba kila mtu ameumbwa kwa mfano wa Mungu mwenyewe!

Lengo la ukurasa huu ni moja tu! Kuililia nchi yangu, kuwalilia masikini wa nchi hii! Kukulilia na wewe baba ndugu Rais na kujililia na mimi mwenyewe!

Ndugu Rais masikini wameacha kuongea juu ya umasikini wao na sasa wanazungumza juu ya vyama vyao vya siasa. Wamesukumwa kuongea juu ya watu! Ni wakati huu kweli wa kuongea juu ya siasa za chuki? Ni wakati huu kweli wa kuhubiri siasa za kututenganisha! Nani sasa atahubiri upendo, umoja na mshikamano, urithi tulioachiwa na Baba wa Taifa hili?

Ah! Watanzania, Taifa limepungukiwa busara! Tumwombe Mungu wa Ibrahim, Mungu wa Isaka, Mungu wa Eliya atuepushe na mkosi huu! Watu wazima wanaongea juu ya wale huku wao wakijiita sisi! Fahamu zimetutoka masikini Watanzania, zimeenda kwa wanyama! Wanawema kama watoto wa mama mmoja, Tanzania, tushikamane na kumkataa yeyote anayetuhubiria habari za kututenganisha! Tuihubiri amani, umoja na mshikamano wetu!

Ndugu Rais, umasikini wa Watanzania ni kama wa kulogwa, hauwezi kuwatoka bila kuaguliwa! Swali lililokosa jibu miaka yote tangu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere atutoke ni je, huyo wakuja kutuagulia sisi ni nani? Yako mambo makubwa na ya msingi katika nchi hii ambayo hayapewi uzito wowote! Lakini kuna mambo ya hivi hivi tu ambayo yanapewa uzito mkubwa usiostahili.

Tuna baadhi ya viongozi wetu ambao wanafikiri sana mahali ambako hakumhitaji mtu kufikiri hata kidogo. Analiona jiwe na anajua kuwa hili ni jiwe, lakini unamwona mtu anafikiri kweli kweli! Unajiuliza anafikiri nini huyu? Fikiri upindukie jiwe litabaki kuwa jiwe!

Ukidhani kuwa ukifikiri sana utapata namna ya kulisaidia unajipumbaza mwenyewe kwa sababu jiwe ni jiwe tu na litabaki jiwe daima!

Ndugu Rais tuhuma kuwa baadhi ya viongozi wetu wamedanganya elimu yao na kwamba vyeti vya kielimu wanavyotumia si vyao zimeachwa zienee mpaka sasa zimeenea nchi nzima. Ni kwa bahati mbaya au ni kwa makusudi haijulikani. Tulidhani ni jambo jepesi tu kuwa mamlaka ingekwisha mtaka mtuhumiwa aoneshe vyeti vyake. Ikikuta ni uongo iwaambie wananchi kuwa ni uongo – mambo yaishe. Sasa unamkuta mtu anafikiri mahali ambako kwa kweli hapahitaji mtu kufikiri. Anafikiri mpaka hata yale mambo makubwa anayoifanyia nchi, wananchi wanashindwa kuyaona maana sasa muda wote wanaulizana kwanini hatua hazichukuliwi! Wananchi wanaacha kufikiria mambo ya msingi kwa nchi yao wanabaki wanafikiria watu! Kutazama cheti cha elimu ya mtu kama ni cha kufoji au ni halali kunahitaji kweli mtu afikiri? Cheti feki kitabaki kuwa cheti feki tu.

Anayeendelea kutumia vyeti vilivyothibitika kuwa siyo vyake anaendelea kuliibia Taifa kwa njia za hila na udanganyifu! Tunanyoshaje nchi bila kuwaadhibu wahalifu? Mwananchi gani atamheshimu mtu wa aina hiyo?

Wenye maadili wanasema wangekuwa wao wangeiomba milima iwafunike kuliko kuendelea kutembea utupu mbele ya jamii!

Baba hakuna timamu anayeweza kusema vita dhidi ya dawa za kulevya ni upuuzi. Wanauliza ni kwanini kamanda alipowataja wengine alimficha mwandani wake, mpaka shemeji-mtu aliyekuwa kolokoloni alipopiga kelele kuwa mwandani wa kamanda ni ‘patina’ wake katika biashara hiyo ya dawa za kulevya ndipo akakamatwa tena na wengine? Anayetuambia kuwa tunapigana vita hiyo kilevi tusimpuuze, bali tumuulize ana maana gani!

Ndugu Rais, zamani tulipokuwa tunaongozwa na viongozi ndugu, chini ya Rais Ndugu Julius Kambarage Nyerere kiongozi yeyote aliyefikwa na tuhuma chafu kama hizi, alijiweka pembeni kwa kujiuzulu mara moja. Hii ilitokana na heshima kubwa waliokuwa wanapata viongozi wetu kutoka kwa wananchi. Hawa wa sasa kujiuzulu ni vigumu kwa sababu wao ni watawala tena waheshimiwa. Nafasi walizonazo wengine wamezipata kama hivi, kwa hila. Wamezigeuza kuwa ni vijiwe vyao!

Ndugu Rais, wako na baadhi ya viongozi wetu ambao hawafikiri pale wanapohitajika kufikiri. Ndiyo maana si ajabu kumsikia mtu mzima akisema serikali inatoa elimu ya bure. Bure maana yake nini? Serikali kukusanya fedha kutoka kwa wazazi na kuwasomeshea watoto wao unaita

bure? Kama ni bure, basi ni bure kutoka kwa wazazi wao! Serikali ina nini cha kutoa bure kwa wananchi?

Yawapasa viongozi wetu watambue kuwa wale wa kuwaamini bila kufikiri kwa sasa wamekwisha, na hawapo tena. Vivyo hivyo unaposema Tanzania ya viwanda ili kulinda heshima yako hakikisha vinavyokuwapo ni viwanda.

Ni Mtanzania gani asiyependa Tanzania ya viwanda? Lakini Tanzania ya viwanda ni Mtanzania gani timamu ambaye haelewi kuwa Tanzania ya viwanda haiwezekani kuwapo leo au kesho au hata mwaka 2020? Itapita miaka mingi mbele! Mtu mzima atakayekwambia Tanzania ya viwanda inawezekana wakati wa uhai wake huyo usimhesabu kati ya watu timamu!

Ndugu Rais, ulipokuja ulikuja kifua mbele ukawaambia Watanzania kuwa nchi hii ni tajiri sana. Ulisema ukweli na kwa sababu hiyo wewe ni mpenzi wa Mungu! Wananchi walikuona kama Masiya! Wakatarajia kuwa maisha yao angalau kwa kiasi fulani yangeboreka. Lakini ni ukweli kwamba Watanzania sasa wana maisha magumu zaidi kuliko ulivyowakuta.

Je, huko siyo kulogwa? Kama huku ni kulogwa wa kutuagulia atakuwa nani kama siyo wewe, baba? Ni wakati sasa viongozi wetu wakae wafikiri jibu la kuwapatia Watanzania iweje maisha yao yazidi kuwa magumu pamoja na utajiri wote huu? Ni lini au ni katika uongozi upi Watanzania watakuja kuufaidi utajiri huu mkubwa wa nchi yao?

Ndugu Rais, ni nini kimekutokea hadi sasa huwaombi tena watu wako wakuombee kama ulivyokuwa ukiomba mwanzo? Baraka za Mungu huwa hazijai tuseme zimejaa au kutosha tuseme sasa zimekutosha! Ukimya na utulivu ni ishara ya mtu mwenye busara kama ukali na kufokafoka tu kulivyo ishara ya mtu aliyepotoka!  Baba rudia kwenye maombi kwa kuwa unazihitaji baraka za Muumba wetu!

1647 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!