Ndugu zangu, nchi inateketezwa

Wapendwa, nimeshindwa kujua simanzi hii iliyonipata niielekeze kwa nani. Kilio hiki nakileta kwenu ili kwa pamoja tuweze kupata jibu la hiki kinachojaribu kukieleza hapa.Wiki iliyopita nilisafiri kutoka Dar es Salaam hadi Kyela mkoani Mbeya kwa kutumia gari. Nilirejea Dar es Salaam kwa usafiri huo huo. Njiani nilishuhudia mambo kadhaa ambayo naomba sana ndugu zangu tushirikiane kuyajadili.

Nawashirikisha hili suala kwa sababu nilichokiona, athari zake si kwa wakazi wa Morogoro, Iringa, Njombe au Mbeya pekee. Athari zile ni zinaligusa Taifa zima. Ndugu zangu, uharibifu wa mazingira, ukataji miti na uchomaji mkaa niliouona, umenifanya nikose amani. Hii si Tanzania tuliyoijua -Tanzania ya watu waungwana, Tanzania ya watunza mazingira, Tanzania iliyosifika ulimwenguni kote kwa uhifadhi.

 

Ndugu zangu, ukataji miti sasa nchini ni janga kama lilivyo janga la ukimwi. Miti imekumbwa na mauaji ya kimbari! Matatizo haya ya ukataji miti na uchomaji mkaa hayapo huko nilipopasema. Ukisafiri katika mikoa ya Singida, Shinyanga, Mwanza, Dodoma, Mara, Tabora, Lindi na mingine, utakutana na haya haya.


Miti inakatwa mno kuanzia Mkoa wa Pwani. Sasa hata miembe inakatwa! Miaka si mingi hatutakuwa na maembe. Ujangili tuliozoea kuuona ni ujangili wa wanyamapori. Ujangili sasa umepanuka zaidi – umeingia hadi kwenye miti na hifadhi zetu!


Kuanzia Kibaha mkoani Pwani, Morogoro yote hadi Iringa, biashara nyepesi inayofanywa na kila mtu sasa ni ya ukataji miti kwa ajili ya kuni na mkaa. Biashara hii inafanywa na kila anayeona kuwa hana namna nyingine ya kuukabili umasikini, isipokuwa kwa kukata miti.

 

Ndugu zangu, uvuvi haramu unaweza kuwa na athari kiafya – kwa kutukosesha kitoweo – lakini ukataji miti unaweza kuwa na madhara makubwa zaidi. Tukikosa samaki tunaweza kula mboga za majani au nyama. Lakini kwa kukosa hifadhi za miti, hatuwezi kubaki salama. Miti ni maji, miti ni hifadhi, miti ni uhai.


Biashara ya mkaa imeachwa iwe huria kana kwamba katika nchi hii hakuna Serikali za Mitaa wala Serikali Kuu. Mkaa unachomwa kana kwamba Tanzania sasa haina mwenyewe. Hakuna mwenye uchungu.


Viongozi wetu wanasafiri kila siku kwa kutumia magari. Wanatoka Dar es Salaam hadi Dodoma. Njiani wanashuhudia maelfu kwa maelfu ya magunia ya mkaa. Hakuna anayehangaika kuhoji wapi yalipo hayo mashamba ya miti inayochomwa mkaa.

 

Sina hakika kama kuna siku waziri mwenye dhamana ya mazingira, ameweza kusimama njiani na kuwahoji hao wachuuzi wapi wanakotoa miti wanayochoma mkaa. Nchi yetu ni kama haina waziri, haina mabwana miti, haina wana mazingira, haina yeyote awaye anayeweza kuhoji mauaji haya ya kimbari yaliyoelekezwa kwenye mapori na hifadhi zetu.

 

Tunaweza kusingizia kwamba biashara ya mkaa inashamiri kwa sababu vijana hawana ajira. Tunaweza kwenda mbali zaidi hata tukasema kuwa mkaa na kuni vinatumika kwa wingi kwa sababu bei ya nishati – umeme, mafuta na gesi – ni kubwa. Wananchi wa kawaida hawaimudu. Sawa, nakubaliana kabisa na hoja hizo.

 

Lakini ni busara kweli kukubaliana na hoja hizi dhaifu? Watu wazima wanaotambua faida za misitu, na hasara za kutokuwa na misitu, tunaweza kweli kuacha hali hii ya ukataji miti iendelee? Hapana.

 

Mababu zetu walilinda miti kwa kauli na kwa vitisho. Kuna misitu tuliaminishwa kuwa kukata mti humo ndani ni kujitafutia laana. Kuna misitu tuliaminishwa kuwa wanaishi miungu! Kweli haikuguswa. Ipo salama hadi leo. Mfano mzuri ni msitu wa Muhunda, Butiama.


Litakuwa jambo la ajabu kwa Serikali kupiga marufuku matumizi ya kuni na mkaa. Suala hapa tunalopaswa kulitazama na kulipatia ufumbuzi haraka ni namna ya kuwa na uwiano mzuri wa ukataji kuni na uchomaji mkaa, pamoja na upandaji miti. Tunapaswa kuwa na kasi ya upandaji miti, ama inayolingana, au inayozidi kasi ya ukataji miti.

 

Kasi kama hiyo tumeiona kwenye mahitaji ya mbao zinazotumika katika ujenzi wa nyumba. Hatujawa na upungufu wa mbao nchini, kwa sababu tuna mashamba makubwa ambayo ukataji wake unawiana na kasi ya upandaji.


Hali si hivyo kwenye kuni na mkaa. Kwenye kuni na mkaa hatuna mashamba maalumu kama ilivyo kwenye mbao za ujenzi. Kwa bahati mbaya, ukataji kuni na mkaa tumeuelekeza kwenye miti ya asili ambayo ukuaji wake si wa kasi kama ilivyo kwa miti ya kisasa. Hii ni hatari kubwa. Tumeshuhudia miti adimu na yenye thamani kubwa kama mipingo ikikatwa na kuchomwa mkaa.


Maeneo ya Tanzania yaliyokuwa na misitu ya kuvutia kama kule Handeni, Muheza, Korogwe; yote sasa imekwisha! Mkaa unachomwa na kupelekwa kuuzwa nchi jirani. Miti inakatwa kwa sababu haina mwenyewe!

 

Zamani hizo biashara ya mkaa iliruhusiwa kufanywa na watu wenye vibali maalumu. Leo kila anayejisikia kupata fedha, nguvu na akili zake anazielekeza kwenye misitu. Mazao ya misitu hayakuruhusiwa kusafirishwa kwa kutumia magari yaliyofunikwa. Leo hii lori lolote linaruhusiwa kusafirisha mkaa hata kama ni la kubeba mafuta. Hii ni nchi gani ambayo haina utaratibu wala sheria inayoheshimiwa?

 

Ndugu zangu, nayasema haya kwa uchungu kwa sababu nchi yetu sasa inakabiliwa na hatari kubwa mno ya kuwa jangwa. Hatari hii inaongezeka kwa kasi kutokana na ujio wa pikipiki. Vijana wengi wanatumia pikipiki kuingia maporini kukata miti na kuchoma mkaa.

 

Anayetaka kuyaona haya azuru maeneo kama Malela Mlandizi mkoani Morogoro. Hali ni mbaya mno. Tena kibaya zaidi, ukataji miti na uchomaji mkaa vimeruhusiwa hadi kwenye vijiji vilivyo kando ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi. Miti inakatwa ndani ya hifadhi. Mkaa unachomwa ndani ya hifadhi!


Ndugu zangu, ukataji miti athari zake si za kuhangaika kuzibaini. Kwa sasa tunashuhudia ongezeko la joto, ukosefu wa mvua, unyeshaji mvua usio wa kawaida, marufuriko, vimbunga na kadhalika. Mahitaji ya maji yanaongezeka, lakini vyanzo vya maji vinakauka kila siku. Uvamizi wa misitu kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji umeshamiri. Je, tukubali kuendelea na hali hii? Hapana.


Ushauri wangu. Kama nilivyosema hapo awali, suala hili la ukataji miti na uchomaji mkaa ni mtambuka. Linahitaji ushirikiano wa pamoja wa wadau wote kulikabili.


Serikali za Mitaa na Serikali Kuu pekee hawawezi kulikabili tatizo hili. Hii ni vita ya kila Mtanzania mzalendo mpenda nchi. Majemedari wa kwanza wa kusimamia vita hii ni viongozi na wananchi katika vijiji.


Zianzishwe tuzo kwa vijijini, wananchi na viongozi wanaosimamia utunzaji misitu katika maeneo yao na katika Taifa kwa jumla. Vita hii ni ya dharura. Tunapaswa kuipigana sasa. Nchi inakwisha ndugu zangu.

Tuamke.