Na Thobias Mwanakatwe
 
JINA la William Mganga Ngeleja lilianza kufahamika zaidi ndani na nje ya nchi mara tu baada ya kugombea ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka 2005 katika Jimbo la Sengerema, mkoani Geita na kuwashinda wagombea wenzake saba katika mchakato wa kura za maoni.
Ngeleja ambaye hadi sasa bado ni mbunge wa jimbo hilo ikiwa ni kipindi chake cha tatu sasa, jina lake limekuwa likitajwa na Watanzania wengi hasa kutokana na tukio unaloweza kusema ni la kihistoria alipoamua kurejesha Sh. milioni 40.4  alizopewa na Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited, James Rwegamalira.
Kumekuwa na maswali mengi yasiyokuwa na majibu kutoka kwa wananchi juu ya uamuzi huo aliochukua na Ngeleja huku wengine wakidai amefanya hivyo pengine kukwepa vyombo vya dola visimchukulie hatua hasa kutokana na fedha hizo kuzipokea wakati wa kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow ikiwa imepamba moto, huku historia ikionyesha alikuwa Waziri mwenye dhamana ya Nishati na Madini. Hii ndiyo wizara mama ya Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO), ambalo ndilo lilipokwa fedha za Escrow. Watu wanajiuliza, je, Ngeleja alipewa “asante” kwa kuwasaidia kwa njia fulani Rugemalira na wenzake kufanikisha mchongo wa Escrow?
Ili kufahamu kwa undani sakata hilo, JAMHURI limefanya mahojiano maalum na Ngeleja na kumuuliza maswali kadhaa ambayo yamekuwa yakiulizwa na wananchi tangu alipoamua kurejesha mamilioni ya fedha kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Ngeleja anaanza kwa kukiri kupokea kiasi cha Sh.40.4 kutoka kwa Rwegamalira fedha ambazo  ni sehemu ya Sh. bilioni 306 zilizochotwa kwenye akauti ya Tegeta Escrow  iliyofunguliwa kwa pamoja kati ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kampuni ya kufua umeme ya IPTL wakati wakisubiri mzozo wa kimkataba baina yao uliokuwa mahakamani umalizike.
 
Fedha hizo ziligawiwa kwa wanasiasa akiwamo Ngeleja ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, majaji, wabunge na viongozi wa dini ambapo wakati akizirejesha alisema ameamua kuzirudisha baada ya Rugemalira kuhusishwa na kashfa ya akaunti  hiyo ya Escrow.
 
“Nilipokea msaada huo kama wapokeavyo wabunge wengine, ilikuwa ni msaada ambao nilipewa kwa ajili ya jimbo langu bila kujua kwamba Rugemalira baadaye angekuja kuhusishwa na kashfa ya fedha, za akaunti ya Escrow.
 
“Wakati nazipokea sikujua kama baadaye fedha hizo zitakuja zihusishwe na kashfa  na hata serikali ilikuwa haijamchukulia hatua Rwegamalira kutoka mwaka 2012 hadi Juni 2017 alipokamatwa mfanyabiashara huyo ikiwa ni miaka mitano.
 
“Mtu kusema kwanini nimechelewa kuzirejesha haina mashiko kwani na ndiyo maana hata serikali ilikuwa imekwisha pokea kodi kutoka kwenye fedha za Rwegamalira,” amesema.
 
Ngeleja anasema kupokea na kurejesha fedha za Rugemalira, hakujaathiri taswira yake kisiasa ndani nan je ya Jimbo la Sengerema. Anasema tangu mwanzo hali ya kisiasa katika Jimbo la Sengerema haijawahi kuathiriwa na sakata la kashfa ya Escrow kwa sababu hahusiki na kashfa hiyo na ndiyo maana uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka 2015 alishinda kwa kishindo na kuwashinda wapinzani wake kwa zaidi ya kura 20,000.
 
“Tangu nirejeshe fedha hizo nimekuwa nikipigiwa simu zaidi ya 100 na ujumbe mfupi wa maneno (sms) ndani na nje ya nchi wakinipongeza kwa uamuzi wa kijasiri na kizalendo niliouchukua,” anasema.
 
Wakati wa mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM wagombea wenzake walianza kutumia sakata la Escrow kama njia ya kutaka kumshughulikia kisiasa, lakini anasema bado aliwashinda.
 
“Pamoja na kwamba asingependa kuzungumzia ujinai au madai ya suala hili kwa vile yako mahakamani, lakini kwa vyovyote vile serikali ina mkono mrefu na haiwezi kushindwa kubaini ukweli kwenye jambo lolote inalolifanyia kazi.
 
“Kama nilivyosema kwenye taarifa yangu nilipokea fedha hizo kama msaada kwa nia njema toka kwa Rwegamalira kama wapokeavyo misaada wabunge wengine ili kuwasaidia kwenye majimbo yao na hasa kwenye shughuli ambazo hazitengewi fedha na bajeti ya serikali kama vile ujenzi wa misikiti na makanisa,” amesema.
 
Ngeleja, ambaye Januari 2007 aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini na 2008 akawa waziri kamili wa wizara hiyo baada ya Baraza la Mawaziri kuvunjwa kufuatia aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kujiuzulu nafasi hiyo, anasema asihukumiwe kwa kupokea na kurejesha fedha za Escrow kwani nchi hii ameifanyia mambo makubwa.
 
Amesema alipokabidhiwa Wizara ya Nishati na Madini, TANESCO ilikuwa katika hali mbaya kwasababu hakukuwa na uwekezaji wa aina yeyote kwenye shirika hilo tangu mwaka 1997 hadi 2005 kipindi ambacho TANESCO ilikuwa imewekwa kwenye orodha ya mashirika yaliyokusudiwa kubinafsishwa na Tume ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC ).
 
“Hakukuwa na uwekezaji wowote kwenye miundombinu ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji na matokeo yake kukawa na matukio ya mgawo wa mara kwa mara wa umeme kila maji yalipopungua kwenye mabwawa ya kuzalisha umeme,” anasema Ngeleja.
 
Kutokana na changamoto hiyo, alilazimika kubuni miradi ya kuzalisha umeme kutoka vyanzo mbalimbali kama vile gesi, maji, makaa ya mawe na nishati jadilifu ndipo mradi wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara-Dar es Salaam ulipobuniwa mwaka 2009.
 
Miradi mingine iliyobuniwa ni Kinyerezi One na Kinyerezi Two, ambapo ilinunuliwa mitambo mipya ya kuzalisha umeme inayotumia gesi, Somanga Funga.
 
“Mwezi Novemba 2011 tulifanikiwa kudhibiti mgawo wa umeme uliokuwa unaitesa nchi yetu. Hii ilitokana na hatua za muda mfupi, wa kati na mrefu tulizochukua wakati huo katika kuendeleza sekta ndogo ya umeme nchini. Kwa hiyo wakati najiuzulu uwaziri Mei, 2012, hapakuwa na mgawo wa umeme nchini.
 
Mwezi Januari 2012, tulianzisha utaratibu wa kuagiza mafuta kwa pamoja (Fuel Bulk Procurement) chini ya usimamizi wa EWURA.
 
“Utaratibu huu ulisaidia kuziba mianya ya baadhi ya wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu, uliirahisishia TRA ukusanyaji kodi, na ulisaidia sana kudhibiti uchakachuaji wa mafuta, na pia ulisaidia kupunguza msongamano wa meli bandarini.
 
“Tuliimarisha sana utafutaji wa gesi asili na mafuta kwa kushirikisha kampuni za ndani na nje ya nchi. Tulianzisha mpango wa kupunguza bei/gharama za kuwaunganishia umeme wananchi kupitia REA, matokeo yake leo gharama zimeshuka hadi Sh. 27,000/- tu vijijini.
 
“Tulipitia upya mkataba kati ya Tanesco na Songas, matokeo yake Tanesco ikaanza kupata unafuu wa USD milioni 1.0 kwa mwezi. Nampongeza sana Mhe Rais JPM kwa uongozi wake imara na kwa jinsi anavyopigania maendeleo ya nchi yetu. Naungana na Watanzania wenzangu kumwombea kwa Mungu,” amesema Ngeleja.
 
Amesema katika kipindi chake cha ubunge ametekeleza miradi mbalimbali aliyoahidi na kutoa mfano wa mradi mkubwa wa maji uliozinduliwa na Rais John Magufuli Julai 4, 2017 utakaowanufaisha wananchi zaidi ya 138,000  ambao unagharimu zaidi ya Sh. bilioni 22 hadi kukamilika kwake.
Ujenzi wa barabara ya Kamanga-Sengerema yenye urefu wa kilometa 35, na Sengerema –Nyehungwe km 68 ambazo maandalizi ya kuzijenga kwa lami yameanza, nayo anaitaja kama mafanikio makubwa yaliyo na mkono wake.
 
Baada ya maelezo hayo, JAMHURI lilitaka kufahamu kwa kina suala la fedha za Escrow, Ngeleja analipa uzito upi?
Alipoulizwa iwapo atawashauri watu wengine waliochukua fedha za Rugemalira nao wazirejeshe kama alivyofanya yeye, akasema: “Mimi siyo msemaji wa kila aliyepewa fedha na Rugemalira. Kila mtu aliyepokea toka kwa Rugemalira ni kwa sababu tofautitofauti. Inawezekana labda aliowapa baadhi waliishamfanyia kazi, labda wengine amewakopesha… tupo aliotupa kama msaada tu.
“Kwa hiyo siwezi kuwambia ama wazirejeshe au wafanye nini, wao wenyewe watajua.”
 
Kuhusu iwapo yuko tayari kushtakiwa iwapo dola itabaini anahusika kijinai kwa kupokea fedha za Escrow kwa maana kwamba huenda aliwezesha upatikanaji wa fedha hizo kwa Rugemalira na wenzake, amesema: “Suala hilo siwezi kuliongelea kwani ni suala la ujinai au madai kwa vile liko mahakamani.”
Alipoulizwa kwa nini amezirejesha TRA na si kwa Rugemalira, akasema: “TRA ilikuwa sehemu sahihi ya kupeleka fedha hizo na nashangaa kwa nini watu wanasema TRA wamekataa, wakati hakuna taarifa yoyote iliyotolewa na TRA kwamba wamezikataa.”
 
Ngeleja pamoja na kusema baadhi ya maswali asingependa kuyajibu kuepusha kuingilia ushahidi wa kesi inayoendelea mahakamani, amesema yeye ataendelea kulitumikia taifa kwa moyo mkunjufu na hatakatishwa tamaa na watu wachache wanaotaka kutumia suala la Escrow kubeza kazi zake.
978 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!