MAELEZO YA MHIFADHI MKUU NCAA,  DK. FREDY MANONGI

Ngorongoro ya miaka mitatu

Ukiangalia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na eneo lenyewe kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita, mabadiliko yaliyoonekana ni makubwa kuliko kipindi chote eneo hili lilipoanzishwa mwaka 1959. Mabadiliko yametokea makubwa sana.

Nianze upande wa mapato: Mapato kabla ya mwaka 2015 yalikuwa yamekwama kwenye takriban Sh bilioni 60 kwa mwaka, lakini kwa kipindi cha miaka hii mitatu mapato yamepanda mara mbili – kwa hesabu za mwaka ulioishia Juni 30, 2018 tulipata takriban Sh bilioni 127.

Na haya yote ni kutokana na juhudi na nia ya Rais John Magufuli ya kutaka kuona mashirika ya umma yanaongeza kipato, kwa hiyo imefanyika mikakati hasa kubadilisha mfumo wa maduhuli ambao umeweza kuipatia Mamlaka fedha nyingi kiasi hicho. Na hii imekwenda sambamba na ongezeko la gawio la Mamlaka kwenye Serikali [Hazina] ambayo ni asilimia 15 ambayo imepanda kutoka chini ya Sh bilioni 1 mwaka 2015 mpaka Sh bilioni 22 mwaka 2018.

Hizi zote ni tone at the top – ikibadilika watu wanafanya kazi, wanabadilika. Kwa hiyo kwa misingi hiyo watu wengi wamebadilika. Dhana ya mapato imekuwa kubwa na takwimu zimejionyesha wazi kwamba kwa kweli mabadiliko ya miaka mitatu yameweza kutuletea impact kubwa sana ya mapato. Hilo ni la msingi sana ambalo ni vizuri tuliseme na lina uhusiano wa moja kwa moja na mabadiliko ya uongozi wa juu [serikalini]. Suala la mapato siwezi kuli-underestimate, ni muhimu sana.

Suala jingine muhimu ni la mabadiliko ya kisera – tumeanza na karibu tukamilishe – ndani ya kipindi hiki cha miaka mitatu. Tumekamilisha Strategic Corporate Plan. Ilikuwa inasuasua huko nyuma, lakini tumekamilisha ambayo ndiyo sasa inatupa dira ya miaka mitano kuanzia mwaka 2017 hadi 2022. Kwa hiyo ni mafanikio makubwa kuweza kutengeneza hiyo dira.

Inatupa mwongozo wa wapi tunataka kwenda na twende kwa namna gani. Ni mafanikio makubwa sana kwa sababu ndiyo yanatupa mwongozo. Lakini nje ya hiyo Corporate Strategic Plan tumeweza kuanza kutengeneza mpango mkakati unaoainisha maeneo ya matumizi na aina ya matumizi ndani ya hifadhi. Inaweka viwango kwa maana ya nini kifanyike ndani ya hifadhi, kwa maana ya matumizi, kifanyike wapi, kifanyike kwa namna gani na kifanyike kwa kiwango kipi. Tumeanza kuitekeleza ndani ya miaka hii mitatu na itakamilika mwaka huu [2018]. Tofauti na Corporate Strategic Plan, GNP inaongelea sana matumizi ya ardhi. Kuna mgongano mkubwa sana kati ya uhifadhi, utalii na matumizi ya ardhi kwa ajili ya jamii. GNP kwa sababu inaainisha nini kifanyike wapi, kwa kiasi gani na kwa kiwango gani, basi inapunguza migogoro ya ardhi ndani ya hifadhi. Ilikuwa imesuasua kuanza, lakini imetengenezwa na sasa karibu ikamilike iweze kupitishwa. Kuainisha maeneo ya matumizi ya ardhi ni kitu muhimu sana ili kupunguza migogoro ya matumizi ya ardhi. Hilo ni suala muhimu.

Kwa maana ya uhusiano kati ya jamii na uhifadhi kuna maeneo mengine ambayo yamekuwa yakichanganya uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii, lakini kipindi hiki kwa kushirikiana na serikali – kulikuwa na mwingiliano holela kati ya uhifadhi na shughuli za jamii na utalii, na hii ilikuwa inaathiri utalii; lakini Serikali ya Awamu ya Tano ilipiga marufuku uingizwaji wa mifugo ndani ya kreta. Na hii kwa kiasi kikubwa imeongeza quality ya utalii ndani ya kreta. Naamini hizi ni juhudi kubwa sana za serikali kuweza kuhakikisha kwamba utalii unakuwa endelevu. Lakini hawakuzuia tu mifugo kuingia ndani ya kreta, bali serikali ilitoa concession kwa wananchi, kwa maana ya kujenga chanzo cha maji cha Ndepesi ambacho ndicho kikubwa ili kuweza kupunguza athari ya kuzuia uingizaji mifugo ndani ya kreta. Vilevile yamejengwa mabwawa mengine mbali kidogo na kreta ambayo yanasaidia mifugo katika kuhakikisha wenyeji wanapata maji kwa ajili ya mifugo. Kuna chanzo kingine cha maji – bwawa limejengwa kubwa sehemu ya Enduleni ambavyo ni miradi mikubwa kwa jamii na inapunguza maumivu makali ya maisha ya binadamu.

Pamoja na kuzuia mifugo kuingia ndani ya kreta, mafanikio mengine ni kuzuia mifugo kuingia eneo la msitu wa Nyanda za Juu Kaskazini, ambako kuna mazalia ya faru na kuna vyanzo vya maji kwa ajili ya watu wa nje ya maeneo ya hifadhi na ndani ya kreta. Nayo imesaidia kuboresha msitu huo. Hizi ni juhudi kubwa sana za serikali.

Serikali vilevile imeendelea kuhudumia wananchi kwa maana ya kuwapa chakula. Tuna mkataba na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ili kusambaza takriban tani 300,600 kwa ajili ya wananchi waishio ndani ya hifadhi. Bajeti ya chakula cha wenyeji ni takriban Sh bilioni 2 kila mwaka. Fedha hizo ni za kununua mahindi na kuyasafirisha mpaka ndani ya hifadhi. Tuliingia mkataba ndani ya kipindi hiki cha uongozi wa Awamu ya Tano na NFRA ili kuhakikisha chakula kinapatikana kwa wakati na kwa bei nzuri.

Matumizi mseto ya Hifadhi

Kumekuwa na malalamiko ya mfumo kutoka kwa wanasiasa na watu mbalimbali kwamba huu mfumo wa eneo mseto una changamoto nyingi. Je, tunazikabili namna gani? Serikali ya Awamu ya Tano imeunda timu ya wataalamu wanane kutoka sekta mbalimbali nchini kufanya tathmini ya changamoto zilizopo kwa huu mfumo wa maeneo ya matumizi mseto na watatoa mapendekezo yao serikalini. Hayo mapendekezo yatasaidia kubadilisha Sheria ya Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro.

Kwa hiyo hiki ni kitu ambacho hakijafanyika kwa miaka 59 iliyopita, lakini sasa hivi kimeweza kufanyika. Serikali ya Awamu ya Tano ndiyo imeanzisha hiyo juhudi ili kuweza kutatua changamoto za matumizi mseto ya eneo hili. Hili ni suala muhimu kwa sababu tumekuwa tukilalamika tu watu wanaishi vipi na wanyamapori, na athari za wanyamapori kwa binadamu na kinyume chake. Kuna athari yake. Hakuna kitu cha msingi kilichokwisha kufanyika, kwa hiyo kwa mara ya kwanza Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Waziri [wa Maliasili na Utalii] imeunda timu imo kazini na itaishauri serikali nini cha kufanya. Hayo ni mafanikio makubwa sana kiuongozi kwa eneo hili.

Kuna tatizo la njaa ndani ya hifadhi. Wananchi wanapata sana shida. Hawaruhusiwi kulima ndani ya hifadhi. Katika kipindi hiki cha miaka mitatu Mamlaka kwa kushirikiana na serikali imetengeneza mpango mkakati wa usalama wa chakula ili kuhakikisha wananchi hawapati njaa tena. Mpango mkakati umetengenezwa na sasa utaanza kutekelezwa katika kipindi hiki.

Unaangalia zaidi uwezekano wa kutafuta mashamba nje ya hifadhi na wananchi kwa kutumia vyama vyao vya ushirika ili waweze kulima na kupata chakula nje ya hifadhi.

Hatima ya matumizi ya ardhi

Timu iliyoundwa na waziri imo kazini. Itakuja na majibu. Lakini kwa kipindi hiki cha miaka mitatu serikali kwa kutumia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) wameweza kufanya sensa ya watu na makazi ili kujua kuna watu kiasi gani, ujenzi uko wa namna gani ndani ya hifadhi, na watu wanafanya shughuli gani. Haya ni mafanikio makubwa sana kwa sababu itatusaidia kuja na mipango ambayo ni endelevu. Hilo ni fanikio kubwa sana kwa kweli, na mipango yote hii niliyoitaja inajaribu kujibu hizo changamoto za ongezeko la watu. Kuna watu 93,000 ndani ya eneo la hifadhi kwa Tarafa ya Ngorongoro pekee.

 

Mipango ya muda mfupi

Baada ya sensa tulifanya vitu viwili; cha kwanza tuliiwekea mifugo yote alama. Sasa hivi tunajua tuna mifugo kiasi gani, na yote ina alama. Hili limesaidia kuanza kuzuia mifugo inayoingia ndani ya hifadhi kiholela. Hilo ni la msingi sana.

Pili, tumeanza kuandikisha watu ili kuwapatia kitambulisho cha taifa na kazi hii imekamilika muda mrefu uliopita. Kila raia atakuwa na kitambulisho cha taifa. Itasaidia sana kuzuia watu wengine kuingia kiholela ndani ya hifadhi, na hili limefanyika mwaka jana ndani ya kipindi cha miaka mitatu ya Mheshimiwa Rais Magufuli.

Jingine la msingi ambalo ni vizuri niliseme, kwa mara ya kwanza yalikuja maelekezo ya waziri mkuu, na napenda niipongeze sana Serikali ya Awamu ya Tano – kuhakikisha eneo lote limewekewa mipaka ya kudumu (vigingi). Kazi hii imekamilika. Tumeweka vigingi kwa eneo zima la Hifadhi ya Ngorongoro. Haya ni mafanikio makubwa sana. Hiki kitu kilikuwa hakijafanyika tangu eneo hili lianzishwe. Kipindi hiki cha miaka mitatu ya uongozi wa Mheshimiwa Rais John Magufuli, tumefanikiwa. Tumeweka vigingi katika kila eneo la mpaka wetu. Hii inazuia waingiaji holela, vilevile inazuia migogoro kati ya wananchi na hifadhi, kwa sababu sasa mipaka inajulikana.

Kupanda kwa mapato

Wageni wamekuwa wakija takriban 600,000 kwa mwaka kwa kipindi hiki cha miaka mitatu. Hawajaongezeka sana. Kilichoongeza mapato cha msingi ni kuja na mfumo mpya wa malipo ambao uko robust, ambao kwa kweli ni vigumu kuweza kuiba. Ni mfumo mzuri. Kwanza, mteja analipa haraka na kwa urahisi benki. Anachagua huduma anayoitaka na kuilipia benki. Ni mfumo ambao kwa kiasi kikubwa sana ni salama na unadhibiti mapato.

Tulipandisha bei kidogo mwaka mmoja uliopita, nalo hilo limeongeza kidogo. Mianya karibu yote ya rushwa iliondolewa. Hivi vyote vimechangia kuongeza mapato.

 

Ongezeko la tozo

Sisi hapa Ngorongoro hatujaona athari yoyote ya ongezeko la bei [tozo] ya huduma. Tuliongeza dola 10 kwenye entry fee kutoka dola 50 kwenda dola 60 [za Marekani]. Tuliongeza crater fee kutoka dola 200 hadi dola 250. Kwa hiyo ongezeko halikuwa kubwa.

Suala la low season [msimu wa watalii wachache] na high season [kipindi cha watalii wengi] na mimi nimeliona hasa mwaka huu wa 2018. Low season kimsingi ilikuwa iwepo Aprili katikati na Mei, lakini mwaka huu ilikuwepo japo si kubwa sana. Mwaka huu ilikuwa ianze Oktoba na Novemba, lakini ukiongea na waongoza utalii wanasema wana miadi ya kutosha. Kwa kweli low season imeanza kupotea. Kupotea kwa ujumla wake inaashiria kuwa Tanzania inaanza kujulikana kuwa ni destination muhimu sana kwa watalii na hata vitu vilivyokuwa vinasababisha seasonality vinaanza kuondoka kwa sababu vingi ni vya nje, si vya ndani. Kwa hiyo inaelekea Tanzania inakuwa destination muhimu sana, na sasa wageni wanaweza wakaja wakati wowote. Hakuna woga wa kuja kipindi chochote.

Hii seasonality haikuwa inaletwa sana na sababu za ndani ya nchi. Kwa hiyo hizo sababu zinaweza kuwa zimebadilika na kuwaruhusu watu kuja kwa mwaka mzima.

 

Faida za ujio wa watu maarufu

Wingi wa watalii inawezekana vilevile hii imechangiwa na ujio wa wageni maarufu kwa sababu kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka mitatu hii kumekuwa na wageni wengi sana mashuhuri wamekuja. Wengi wanakuja kimya kimya, ni wengi. Baadaye wana – ‘twit’ kwa wenzao na wao wanapata habari wanakuja. Kwa hiyo kuna uwezekano, kwa kweli kuna uhusiano kati ya uongozi imara wa Awamu ya Tano na viongozi maarufu kuja Tanzania. Viongozi maarufu wakija wanakuwa na influence ya viongozi na wageni wengine kutaka kuja kutembelea hizi destination.

Mipango ya kujitangaza

Kama taasisi nyingine, mipango ya kujitangaza sasa inategemea sana mitandao ya kijamii, kwa hiyo tunatumia sana mitandao kwa sababu inafika kila mahali. Vilevile tuliweza kuboresha tovuti yetu kwa kiasi kikubwa sana katika miaka mitatu iliyopita na inatusaidia mno kupata wageni. Tumewekeza huko kwenye tovuti na kwenye mitandao ya kijamii kuweza kupata wageni kutoka nje. Kwenye tovuti yetu lugha zaidi ni Kiingereza na Kifaransa, lakini kuna machapisho mengine tunatoa kwa Kichina na Kijerumani. Mpango mkakati wetu mwingine ulikuwa ni kuhakikisha eneo linapata sifa za kimataifa.

Mpango mkakati mwingine ilikuwa ni kupata uteuzi mwingine wa kimataifa. Ngorongoro mwaka huu wa 2018 ilipata hadhi ya Global Geoparks [utalii wa miamba. Kuna Geoparks 140 katika mataifa 38 pekee duniani]. Tunaonekana kwenye shughuli zao mbalimbali na hiyo inatupa fursa ya kujitangaza. Kwa hiyo Global Geopark nayo imetupa chapuo na visibility kubwa.

Matumizi ya tovuti yamepunguza gharama za kusafiri nje. Ni kweli na ndiyo maana sikuiongelea hiyo ya kwenda kwenye maonyesho. Hatuendi sana. Tumewekeza zaidi kwenye mitandao ya kijamii na tovuti. Bajeti ya kwenda nje imepungua kwa kiasi kikubwa sana lakini visibility imeongezeka.

Wakati wa high season magari yanayoingia kreta hufika wastani wa magari 700 kwa siku. Wakati wa low season yanaweza kuwa 150 hadi 250 au 300. Mwaka huu yamekuwa mengi zaidi.

Nafasi ya Tanzania kwenye utalii

Tanzania si wanyonge tena kwenye utalii. Ndiyo maana wenzetu [nchi jirani] wameanza kukopi bidhaa zetu na kuzitangaza kwamba ziko kwao…Mlima Kilimanjaro, Olduvai na kadhalika. Kwa kweli wamekuwa wakitumia hayo maneno ili kupata fursa ya wageni kuja kutembelea maeneo yao. Maeneo yetu tumeyaboresha sana. Mwaka jana Makamu wa Rais [Mama Samia Suluhu Hassan] alizindua makumbusho ya kisasa kabisa duniani ya chimbuko la binadamu. Hayo ni mafanikio makubwa katika Awamu ya Tano na yametupa faida kubwa mno kama destination ya historia ya binadamu. Idadi ya watalii imeongezeka kidogo pale Olduvai, lakini kitu cha muhimu kilichoongezeka zaidi ni mapato. Yameongezeka kutoka takriban Sh milioni 700 kwa mwaka na katika kipindi cha miaka mitatu yamefikia Sh bilioni 2 kwa mwaka. Haya ni mafanikio makubwa sana.

Hatima ya uwepo wa Ngorongoro

Hatima ya Ngorongoro tuna changamoto ambayo inabidi tuitatue, na nadhani Serikali ya Awamu ya Tano itatusaidia kutatua kitendawili hiki. Kama nilivyosema, baada ya kufanya sensa tumeona idadi ya watu inaongezeka sana, na inaongezeka sana na eneo la hifadhi limebaki pale pale [kwa ukubwa] takriban kilometa za mraba 8,300. Hili ni tishio kama idadi ya watu inaongezeka lakini eneo liko pale pale – ni tishio kwa sababu mwingiliano kati ya maisha ya binadamu na wanyamapori utakuwa very complicated. Kwa hiyo hilo ndilo tishio.

Kama hatutaweza kupunguza kwa namna yoyote ile idadi ya watu ndani ya hifadhi hili eneo litafika wakati ambao litakuwa halina ustahimilivu. Halitakuwa endelevu. Hiyo ni changamoto kubwa sana. Inabidi tuone namna ya kuhakikisha eneo hili ni endelevu – maisha ya watu yanakuwa bora, lakini bado uhifadhi unaboreka zaidi kwa njia mbalimbali.

Tumeanza kuangalia upya huu muundo wa matumizi ya mseto. Tumeanza kutengeneza mpango. Juhudi nyingi zinafanywa. Mojawapo ya juhudi hizo ni kufanya tathmini ya hili eneo la matumizi mseto ili kutengeneza mpango ambao utaondoa migogoro iliyoko kati ya maisha ya binadamu na uhifadhi.

Vilevile kuna miradi mingine tunataka kuanzisha – ya shule nje ya hifadhi…shule za msingi na sekondari ambazo ni za bweni ili wanafunzi wawe kule kwa lengo la kwanza la kupunguza watu; na wapate elimu ambayo ni bora zaidi itakayowawezesha kuishi maeneo mengi zaidi kama Watanzania wengine, na si tu ndani ya hifadhi.

Ujenzi wa makumbusho

Tumeanza kuongea na Serikali ya China kuhusu kuendelea kutangaza mpango wa utalii wa miamba [Geotourism], kwa hiyo wanatupa msaada. Bado mazungumzo yanaendelea ya kupata dola milioni 15 za Marekani. Tayari wameanza kuleta wataalamu wao kuangalia maeneo ambayo watatusaidia kuyaendeleza.

Pale nje ya lango kuu [la kuingia Hifadhi ya Ngorongoro] tunataka kujenga makumbusho ya kimataifa ya utalii wa miamba ili isaidie kuendelea kulifanya hili liweze kujulikana na tupate wageni wengi zaidi kutoka China.

Kilio cha wananchi, NGOs

Ni changamoto kubwa kwa kweli. Zimejitokeza NGOs nyingi sana ambazo zinaona wenyeji wananyanyaswa, wananyimwa haki zao, wanazuiwa shughuli mbalimbali pamoja na kilimo ndani ya hifadhi.

Haya maisha ya kuishi ndani ya hifadhi yana changamoto na uamuzi wa kuishi ndani ya hifadhi unafanywa na mtu mwenyewe kwa kujua limitations [mipaka] zilizoko, kwa sababu kwa kweli hifadhi huwezi ukaruhusu kila kitu kifanyike mahali popote. Hifadhi ina taratibu zake na hii ni changamoto kwa wenyeji vilevile. Pamoja na hayo, ndiyo maana hifadhi imeamua kusaidia shughuli mbalimbali ili kupunguza ukali wa taratibu za hifadhi ambazo zinajionyesha sasa hivi. Kwa mfano, serikali inatoa huduma mbalimbali za afya, elimu, matibabu na chanjo za mifugo ili kupunguza ukali wa taratibu ngumu za kuishi ndani ya hifadhi.

Ni kweli zimejitokeza NGOs nyingi zikijaribu kutetea wananchi; kitu ambacho si kibaya, ni kitu kizuri na ilimradi wanawaambia ukweli. Kama wanasema ukweli ni kitu kizuri. Ni vizuri tusaidiane na hizi NGOs kutengeneza hifadhi ambayo ni endelevu, kwa sababu ikifa maisha ya watu yatakuwa matatani zaidi – hasa wale wanaoishi ndani ya hifadhi. Ni vizuri tuweke uwiano kati ya maendeleo ya jamii na uhifadhi. Huo uwiano kidogo unakuwa mgumu na unalalamikiwa na watu mbalimbali, lakini sisi tunaendelea kutafuta huo uwiano.

 

Miaka miwili ijayo

Tutaendelea kuimarisha utalii ili tuweze kuendelea kupata mapato. Nia ni kuongeza mapato ya Ngorongoro mara mbili. Hilo ni la msingi kabisa.

Pili, tutakuwa tumekamilisha tathmini za ujumla za eneo hili mseto na tumepata majibu ya msingi kabisa ya future ya Ngorongoro na kukamilisha GNP ili kuondoa migogoro ambayo ipo ndani ya eneo hili.

 

Mwito kwa wananchi

Kwanza, tumpongeze Rais John Pombe Magufuli. Ameonyesha nia kubwa sana ya kutaka maeneo haya yahifadhiwe. Amekuwa akiongeza umuhimu wa maeneo haya kwenye uchumi wa nchi. Serikali imeona kwamba utalii ndiyo sasa uti wa mgongo wa maendeleo ya nchi yetu. Amekuwa akisisitiza kuhifadhiwa kwa maeneo haya kama Mwalimu Nyerere alivyokuwa anasisitiza. Tumuunge mkono kwa nia yake ya kuboresha uhifadhi kwa lengo la kupata mapato na kuchochea uchumi wa nchi.

Tumuunge mkono na tumuenzi Mheshimiwa Rais Magufuli kwa juhudi anazozifanya za uhifadhi na kuboresha utalii nchini.

1612 Total Views 4 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!