Asasi za kiraia (NGOs) zinazojihusisha na masuala ya wafugaji katika Wilaya ya Ngorongoro, hasa Loliondo, zinajua kwamba uhuni na ghiliba zake sasa zinaelekea ukingoni.
 Kwa miaka mingi zimetumia umaskini wa ndugu zetu Wamaasai kama kitegauchumi kikuu cha kuomba na kupokea fedha kutoka kwa wafadhili wa ndani na nje ya nchi.
 Hivi karibuni kumekuwapo mkakati maalum unaofanywa na wenye NGOs kadhaa kutaka kuuaminisha umma kuwa Loliondo kuna uonevu unaofanywa na Serikali dhidi ya raia wake.
 Wenye mashirika haya wanajua bila kusambaza uongo huo, na bila kuifanya Loliondo isitawalike, hawawezi kupokea fedha za misaada kutoka kwa wafadhili wao.
  Nimekuwa mmoja wa waandishi tunaolifuatilia suala la Loliondo kwa jicho la karibu mno. Tumeibua uhuni mwingi unaofanywa na NGOs hizo kwa ghiliba za kujipatia fedha kutoka kwa wafadhili. Zipo NGOs zilizodiriki kuweka uongo kwenye ripoti zake kwa kutumia miradi inayotekelezwa na Serikali na kuuaminisha ulimwengu kwamba ni miradi inayotekelezwa na fedha za wafadhili kupitia asasi hizo. Mara zote tumeuanika uongo wa NGOs hizo kwa kutumia ripoti zake hizo hizo.
 Zilipoona zimeumbuliwa kwa uongo wao, zimejitokeza, kwa vielelezo dhaifu na kwa wingi wa hisia, kudai kwamba kuna kundi la wanahabari wanaolipwa kwa kazi hiyo. Huu ni utetezi dhaifu.
Tumeandika na kutangaza bila woga kuwa NGOs hizi ni wakala wa wafanyabiashara na wafugaji kutoka Kenya ambao maisha yao yote kwa kiwango cha juu kabisa yanawezeshwa na mgogoro wa Loliondo.
 Hatukuona soni kuwataja baadhi ya Wakenya wanaochochea vurugu katika Loliondo, akiwamo Mkenya, Mama Tina Timan ambaye ameweza kuwa Diwani wa Viti Maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ilhali akiwa si raia wa Tanzania! Kwa maneno rahisi, Tina amepata uraia akiwa tayari ni diwani. Haya yanatokea Tanzania pekee. Tunapoyasema haya, tunayasema kwa sababu nchi hii ni mali ya Watanzania. Kila Mtanzania, kwa nafasi yake anapaswa kuwa sehemu ya kuilinda Tanzania.
 Tumeandika na kutangaza bila woga kuwa karibu asilimia 70 ya binadamu wanaoishi Loliondo si raia wa Tanzania. Kuna Wakenya wengi waliojipenyeza na kudai kwamba ni Watanzania. Hawa ndiyo walioko kwenye NGOs wanazoziongoza kifamilia na kiukoo. Hawa ndiyo wanaoifanya Loliondo isitulie na kwa sababu hiyo, isitawalike. Wamehakikisha wanatumia kivuli cha utetezi wa wafugaji ili kuibua vurugu kila mara.
  Wanafanya hivyo wakiwa na mipango mahsusi. Mosi, kuingiza mifugo kutoka Kenya ili ivuruge na hatimaye imalize Pori Tengefu la Loliondo. Hilo wamelifanikisha. Wanaona wasifuge tu, bali waanzishe kilimo. Matreka kutoka Kenya yanakwatua maelfu ya ekari za ardhi ya Tanzania. Loliondo si ya uhifadhi sasa, isipokuwa kilimo. Wameona hiyo haitoshi. Baada ya kuiua Liliondo, wameshaingia kilometa 10 ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA).
  Pili, Wakenya hawa wamejiingiza kwenye siasa za Tanzania. Wamediriki kugombea uongozi wa vitongoji na hata udiwani. Wapo waliokwama kwa sababu JAMHURI ilitekeleza wajibu wake halali wa kuilinda nchi yetu. Wanawania uongozi kupitia kwa watakaochaguliwa, waweze kuwaruhusu wenzao kutoka Kenya kuingiza mifugo bila kizuizi.
 Hivi karibuni tuliandika juu ya uzushi uliopangwa na NGOs hizo kwa kushirikiana na vyombo vya habari mamluki vya ndani na nje ya nchi (waandishi kutoka Kenya), kuuhadaa ulimwengu kwamba Serikali ya Tanzania imechoma maboma ya wafugaji wa Kimaasai katika eneo la Liliondo. Tupo tuliosema wazi kwamba ingawa tunatambua hatuna Waziri wa Maliasili na Utalii mwenye weledi, katika hili walau tunamtetea hata kama tunajua hana la maana alilofanya katika kuilinda Loliondo na Serengeti.
  Mamluki wetu wa vyombo vya habari hawakutaka kusema ukweli kwamba maboma yaliyochomwa yalikuwa ndani ya SENAPA kwa kilometa 10 na zaidi. Sisi tulikuwa wa kwanza kuandika habari hizo na bila shaka yoyoye vyombo vya dola vikaingia kazini na kuubaini ukweli huo.
  Ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Daudi Ntibenda, imesaidia kuanika ukweli wa mambo. Operesheni hii nyepesi iliyofanywa ndani ya siku chache imeibua mambo mengi na makubwa. Imeibua mambo ya hatari kwa nchi yetu kiusalama na kiuchumi.
Wakenya kadhaa wamebainika kuwa na maelfu kwa maelfu ya ng’ombe na mifungo mingine ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
 Naziomba NGOs hizi zijitokeze kuyakanusha haya. Nawataja Wakenya. Amebainika Konio Oleletoluo, huyu anatoka Ngosesya Olmesutie, Kenya. Baada ya kuondolewa SENAPA, sasa amejishikiza Nyore Kusini – Arash. Sangei Kipuker anatoka Enairebuk Olmesutie, Kenya. Hivi sasa amesogezwa hadi Nyore Kusini – Arash. Ole Kondo Kipuker anatokea Enairebuk Olmesutie, Kenya. Kwa sasa yupo Nyore Kusini– Arash. Yupo mwigine anaitwa Kipamet. Huyu ni Mkenya anayetoka Narida Ngorkiding'a Olmesutie, na sasa yupo Nyore Kusini– Arash.
  Mfugaji Simiren Munka aliyehifadhiwa Ilmolelian, Arash ni Mkenya anayetoka Endasikira Loita; kuna Ole Mburkoi Parmayo huko Nyore Kusini – Arash, anatoka eneo la Engoyangalani Olmesutie, Kenya.
 Melubo Moti ambaye ana mifugo yake Kijiji cha Ilmolelian, Arash anatoka Enairebuk Olmesutie; Noorkitoip Moti kwa sasa yupo Nyore Kusini – Arash, na nyumbani kwao ni Enairebuk Olmesutie nchini Kenya.
 Wengine ni Ole Poyo aliyepelekwa Nyore Kusini – Arash, na nyumbani kwako ni Naibala Endasikira; Parani Ole Kikonyi  yupo Ilmolelian – Arash, anatoka Irkerin Loita; Ole Murkuk  yupo Nyore Kaskazini – Losoito; huyu kwao ni Ngipangasi Olmesutie, Kenya.
 Pia wamo Ole Puya katika Kijiji cha Ilmolelian – Arash, na nyumbani kwao ni Endasikira Loita; Ole Kipurda (Oldarpoi – Losoito) anatoka Iltumaro-Olmesutie, Kenya; Murera Ole Keko ameondolewa ndani ya SENAPA Oldarpoi-Losoito. Huyu anatoka Esendu- Irkerin, Kenya. Kadhalika, kuna Olonuku aliyefurushwa hadi katika eneo la Oldarpoi – Losoito, na imebainika kuwa nyumbani kwake ni Ngipangasi Olmesutie nchini Kenya.
  Wenye NGOs zinazotetea uhalifu huu wanatambua kuwa tunapokuwa tukishughulikia masuala mazito ya kulilinda Taifa letu, huwa hatuzomoki. Tunafanya kazi kwa weledi mkubwa na kwa kuzingatia maslahi mapana ya Taifa letu kwa faida ya sasa kwa kwa vizazi vijavyo. Tunafanya hivyo tukiamini kuwa kila Mtanzania mzalendo, bila kujali ukubwa au udogo wake, umaarufu au kutojulikana kwake, ana fursa kubwa ya kusaidia kulinda rasilimali za Taifa letu. Huu ni wajibu wa kikatiba.
  Uchunguzi tuliofanya unaonesha kuwa idadi ya Wakenya wenye maelfu ya mifugo ndani ya Loliondo na Serengeti ni kubwa zaidi ya hii niliyoitaja hapo juu. Kuna Wakenya wengi kutoka eneo la Olderekeresi, Wilaya Narok nchini Kenya walioingia Tanzania na kujifanya ni Watanzania.
  Wengi wanaishi katika vitongoji vilivyopo Kata ya Ololosokwan.
Wamo kina Ole Ringa anayeishi Engong Nairowa (Maji Moto). Wengine na vitongoji wanakoishi vikiwa kwenye mabano ni Ole Kapiro (Osero Sopia), Ole Terta (Endengeteng), Ole Loinyo (Endengeteng), Ole Kitapa (Endengeteng), Ole Ketuta (Osero Sopia), Ole Nyengo (Osero Sopia), Ole Kelong (Osero Sopia), na Oletemutu  ambaye pia anaishi Osero Sopia.
  NGOs zinayajua haya yote lakini zinazimwa na ukweli kwamba vurugu za kutungwa za Loliondo ni biashara zao. Zinawapa kula na kuishi kwao. Wanajua kutulia kwa Loliondo ni maumivu makubwa kwao kiuchumi. Hawa ni wale ambao mara zote wametaka kuwaona Wamaasai wenzao, ndani ya karne hii ya 21 wanaendelea kutumika kama kivutio cha utalii. Wanataka kuwaona wakiendelea kuwa chanzo chao cha mapato kwa kupigwa picha au kwa kuwatumia masikini hao kuomba fedha ambazo mwishowe huishia kwenye matumbo yao na familia zao.
  Wanadanganya kwa kutumia maandiko kukusanya mabilioni ya shilingi kutoka kwa wafadhili kwa kigezo cha kuwakomboa wenzao kimaisha na kielimu, lakini mwisho wa siku hakuna la maana wanalowafanyia ndugu zao hao. Wanapiga vita kampuni kama OBC ambayo wanaona inawasaidia moja kwa moja wananchi kwa kuwajengea miradi mingi ya huduma za kijamii.
Hawa wapo radhi kutumia fedha kutoa taarifa za uongo kwenye vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi alimradi tu kuendelea kuwahadaa walimwengu kwamba Loliondo kuna uonevu unaofanywa na Serikali.
  Serengeti ndiko mahali pekee hapa duniani ambako wanyama wamebaki katika uhalisia wake. Taifa letu linaingiza fedha za kigeni kutokana na Serengeti. Wakenya wamevuruga hifadhi zao zote kutokana na wingi wa wageni na ongezeko la shughuli za kibinadamu.
  Ardhi ya Tanzania ni ardhi ya umma. Kenya kila mmoja ana   kipande chake. Wanajua Tanzania ndiko mahali pekee ambako mtu anaweza kuja kwa ghiliba na kujitwalia uraia kihuni na baadaye kujiingiza kwenye siasa na NGOs kwa lengo la kuwakaribisha wafugaji kutoka Kenya. Wameshaivuruga Loliondo. Wanakaribia kuiteketeza. Sasa wameamua kuingia ndani ya Serengeti. Kuwaondoa iwe nongwa? Haiwezekani.
 Ngorongoro sasa ina mkuu mpya wa wilaya. Aliyekuwapo alikuwa sehemu ya matatizo. Hakuwa na msaada wa maana katika kuhakikisha Ngorongoro na Loliondo vinabaki kuwa mali ya Watanzania kwa maslahi ya Watanzania. Huyu mpya ajue anakabiliwa na wajibu halali wa kulinda maslahi ya Tanzania. Akienda mrama hatutanyamaza.
  Wakenya ni ndugu zetu. Wanapokuwa na shida ni wajibu wetu kuwasaidia. Muhimu wanachopaswa kukizingatia ni kufuata taratibu, kanuni na sheria za nchi yetu.
  Mwisho, ni vema mamlaka zinazohusika zikatoa majibu kutokana na hiki kinachoendelea ndani ya Loliondo na SENAPA kwa jumla.
Katika hali ya kawaida SENAPA ina walinzi na vitendea kazi. Haiwezekani wafugaji, tena wageni, wakaingia ndani ya Hifadhi kwa kilometa 10 na kuishi humo kwa miaka bila wenye dhamana na Hifadhi hiyo kulijua hilo.
  Haiwezekani Wakenya wakaanzisha kijiji ndani ya ardhi ya Tanzania bila askari wa doria wa SENAPA na vyombo vya ulinzi na usalama vya Tanzania kuwa na taarifa. Hapa kuna mawili. Mosi, inawezekana walijua uvamizi wa Wakenya hawa lakini wakanyamazishwa kwa fedha.
  Pili, inawezekana hawakulijua hili kutokana na weledi mdogo wa kitaaluma. Lolote kati ya haya mawili linatosha kuwaondoa na kuwapeleka Watanzania wazalendo kujaza nafasi zao. Haiwezekani Tanzania ikawa nchi ya watu wa kulalamika tu. Haiwezekani kazi kwa watu walioajiriwa kuifanya ikawa haifanywi, badala yake likaonekana kuwa ni jukumu la waandishi wa habari.
 Uvamizi wa Wakenya ndani ya Hifadhi zetu bila shaka yoyote ni moja ya sababu za kuongezeka kwa ujangili. Kuna mashirika mengi yanayodai kujihusisha na uhifadhi kama vile AWF, FZS na WWF. Je, uhalali wa mashirika haya kuendelea kuwapo huko unatoka wapi? Je, kwanini tusiamini kuwa uwepo wao unatokana na kiu na tamaa yao ya kukusanya mabilioni kwa mgongo wa uhifadhi ilhali wakiwa hawana lolote la maana wanalofanya?
  Mwisho kabisa, tunasubiri matamko ya uongo kutoka kwenye NGOs kuhusu uvamizi huu wa Wakenya ndani ya Loliondo na SENAPA. Matamko yao ndiyo yatakayosaidia kuwatambua kama kweli hawa ni Watanzania halisi au ni mamluki walioamua kuitumia Loliondo kama kitegauchumi chao kikuu.

2053 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!