Desemba 22 mwaka jana, Rais Jakaya Kikwete alihitimisha mjadala wa sakata la Escrow pale alipozungumza na wazee wa Dar es Salaam.

Pamoja na kuongelea mambo mengine, Rais Kikwete alifafanua mambo makuu matatu ambayo, kimsingi, ndiyo yaliyokuwa msingi wa maazimio manane yaliyopitishwa na Bunge, Novemba, mwaka jana.

Mambo hayo ni usahihi wa kiasi cha fedha kilichokuwa kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow hadi Bunge linapitisha maazimio yake; hadhi ya fedha hizo na uhalali wa mauzo ya hisa ya asilimia 30 kutoka VIP kwenda PAP.

Kuhusu usahihi wa kiasi cha fedha kilichokuwa kwenye Akaunti ya Escrow, Rais Kikwete alifafanua kiasi sahihi kilikuwa Sh bilioni 202 tu, na wala si Sh  bilioni 306 au Sh bilioni 321 kama ambavyo umma umekuwa ukiaminishwa.

Kuhusu hadhi ya fedha, Rais Kikwete alisema hazikuwa za umma, bali zilikuwa za kampuni binafsi ya IPTL. Aidha, Rais Kikwete aliagiza mapunjo au kodi stahiki ilipwe kwa mujibu wa sheria za nchi.

Kuhusu uhalali wa mauzo ya hisa za VIP asilimia 30 kwenda kwa PAP, Rais Kikwete alifafanua kwamba mauziano hayo kwa thamani ya dola milioni 75 za Marekani (sawa na Sh bilioni 120) yalikuwa halali, na kwamba kodi stahiki ya Serikali (Sh bilioni 38) ilikuwa imelipwa kutokana na mauzo hayo.

Katika mazingira ya kawaida, na hasa ambako mfumo wa misingi ya utawala bora inaheshimika, ilitarajiwa kwamba mjadala kuhusu sakata la Escrow ungefikia tamati baada ya ufafanuzi huo wa Rais Kikwete.

Lakini cha kushangaza ni kwamba hata baada ya hotuba hiyo ya Rais Kikwete, bado kuna baadhi ya watu wanaendeleza mjadala huo, tena kwa namna ya upotoshaji mkubwa, ambao kama Watanzania hatutakuwa makini, Taifa litaingia majaribuni.

Kuna sababu zaidi ya 20 zinazothibitisha kwamba maazimio manane ya Bunge yalikuwa matokeo ya mchezo mchafu wa kisiasa, unaoratibiwa na baadhi ya watu kwa maslahi yao binafsi ya kisiasa na kibiashara. Wana sababu zao ikiwamo ya kulazimisha Bunge kupotosha umma kuwa fedha zilizokuwamo kwenye akaunti ni Sh bilioni 202 tofauti na Sh bilioni 306 au Sh bilioni 321.

Kuna hili la mmiliki wa fedha, Rais anasema ni za Kampuni ya IPTL, lakini jambo la kushangaza kwamba Kamati ya PAC ya Zitto Kabwe na hata Bunge zima limekuwa linapotosha umma kwamba fedha zilizokuwa kwenye Akaunti ya Escrow zilikuwa za umma.

Kinachosikitisha ni kwamba pamoja na kamati ya PAC kujidai kwa mbwembwe kwamba ilifanya kazi kiuchunguzi, lakini bado ilificha ukweli kwamba hata CAG aliishawahi kuwashauri Tanesco waondoe kwenye hesabu zao fedha zilizokuwa kwenye akaunti ya escrow.

Hakuna ubishi kwamba hekima na busara ya Rais Kikwete kuagiza kwamba taarifa za CAG na PAC zote zichapishwe kwenye magazeti na mitandao ili wananchi wapate fursa ya kuzichambua, imesaidia kuubaini ukweli wa mambo.

Ni dhahiri kuwa baadhi ya maazimio yaliyopitishwa na Bunge hayatokani na hadidu za rejea wala taarifa ya CAG, bali yalichakachuliwa tu na kamati ya PAC na Bunge. Kwa sababu hiyo maazimio ya namna hiyo yanakosa uhalali wa kutumika kama vigezo vya kuwawajibisha watuhumiwa.

Bunge lilitoa maagizo ya vyombo viwili kufanya uchunguzi. Lakini wakati taarifa ya CAG ikitumiwa PAC kutoa maelekezo kwa Bunge, Takukuru (chombo kingine cha uchunguzi) walikuwa wanaendelea na uchunguzi katika baadhi ya maeneo.

Swali la kujiuliza hapa, je, kwa nini PAC ilikuwa na haraka kuwasilisha taarifa ambayo vyanzo au misingi yake ilikuwa haijakamilika sawasawa? Matokeo ya udhaifu huu ni mapendekezo ya kutaka kuwaadhibu watuhumiwa bila kuwapa fursa ya kujitetea, jambo ambalo halikubaliki.

Ni jambo la kushangaza kwamba mhimili wa kutunga sheria, umepitisha maazimio yenye nguvu ya kimahakama bila kuwapa fursa ya kujitetea baadhi ya watuhumiwa! Watanzania wamewasikia viongozi wa dini wakipaza sauti zao kwamba wamesulubiwa bila kupewa fursa ya kujitetea.

Aidha, imebainika kwamba hata wanasiasa wanaotuhumiwa kama akina Profesa Anna Tibaijuka, Andrew Chenge, William Ngeleja, Victor Mwambalaswa na hata huyo James Rugemalira wa VIP, watu hawa taarifa zinasema hawakupewa fursa ya kujitetea mbele ya kamati ya PAC.

Kitendo hiki kinashtua watu wengi, ndiyo maana Waziri Mkuu mstaafu, Joseph Warioba, alihoji, “Uamuzi ule ni kama wa kimahakama, Bunge limekaa na kuamua kwamba fedha hizi na hasa alizolipa Rugemalira zilikuwa chafu na wote waliopokea fedha hizo walizipokea zikiwa chafu, hivyo na wao waadhibiwe, wana ushahidi gani? hawakuwasikiliza wale watu.

“Unasema kuna Askofu amepewa fedha unamhukumu kwani alijua ni fedha chafu? Kuna Jaji hapa alipata fedha unasema alijua ni fedha chafu; kuna waziri alichukua fedha alijua ni chafu lakini hawakuwasikiliza…”

Mzee Warioba anahitimisha kwa kusisitiza; “Nasisitiza Bunge wasije wakatumia madaraka yao tukatoka kwenye mfumo wa kuheshimu sheria tukaacha mambo yetu yaendeshwe kisiasa…”

Jaji Mkuu wa Tanzania, Othman Chande, amewahi kunukuliwa na vyombo vya habari akisisitiza umuhimu wa kupewa fursa ya kujitetea kwa watuhumiwa. Alisema, “Tunatakiwa kupewa nafasi ya kujibu, Mahakama haitakiwi kuhukumiwa kabla haijapewa nafasi ya kujitetea, ndiyo maana hata tunaposikiliza kesi lazima pande mbili zisikilizwe ndiyo hukumu itolewe, ikitokea hukumu imetolewa kwa kusikiliza upande mmoja tu inaweza kufutwa.”

Kadhalika, pamoja na kufanya uchunguzi, Kamati ya PAC haikutaja majina ya miamala iliyofanyika kupitia Benki ya Stanbic. Taarifa ya PAC imeuaminisha umma kwamba kiasi cha zaidi ya Sh bilioni 73.5 zilitolewa kwa siku moja kutoka kwenye akaunti ya PAP inayomilikiwa na Harbinder Singh Sethi na kugawanywa kwa watu mbalimbali.

Jaji Warioba alisema, “La pili ambalo linaonekana kama kuna kulindana ni kwamba waliopokea fedha kutoka kwa Rugemalira (James) wote wametajwa…lakini wanaohusika na fedha zilizotolewa Benki ya Stanbic, ambazo Kamati ya PAC imesema zilichukuliwa kwenye mifuko ya rambo, lumbesa na kwenye magunia, hawakuwataja ni nani alichukua.

“Kwa sababu kama wanajua zilichukuliwa kwa njia hiyo, lazima watakuwa wanajua ni nani alichukua. Hivyo ni kwa nini hao waliochukua upande huu hawakutajwa? Unaanza kuwa na maswali kwamba hapa kuna dalili za kulindana na wameendelea hivyo na kutoa uamuzi… Tuambiwe waliochukua fedha Stanbic ni kina nani…vinginevyo tutakuwa tumefanya mambo kisiasa, tutakuwa tumewatoa watu kama kafara lakini tumeacha mambo mengine yanayoonesha kwamba kuna kulindana.”

Ukweli wa kilichotokea hapa ni mchezo, tena mchafu, wa kisiasa wa kutaka kuwachafua baadhi na kuwalinda baadhi.

Jambo jingine la kushangaza ni kwamba siku mbili tu baada ya Warioba kuzungumza hayo akisema “Ripoti ya Zitto dhaifu”, mjumbe wa Kamati ya PAC, David Kafulila, naye aligeuka kuwa jaji na kujidai kuwasafisha viongozi wa dini waliotajwa kwenye taarifa ya PAC, ingawa hawakutajwa kwenye taarifa ya CAG. Picha inayoonekana hapo ni kwamba Kafulila alichofanya ni unafiki.

Kwanza, mpaka siku alipojidai kuwasafisha viongozi wa dini, Kafulila hakuwa na mamlaka ya kufanya hivyo kwa sababu maazimio ni ya Bunge na wala siyo ya Kafulila binafsi. Pili, kama Kafulila aliamini kwamba viongozi wa dini hawakustahili kutuhumiwa, alipaswa kuishawishi kamati yake kuwaondoa kwenye orodha ya watuhumiwa kabla ya taarifa ya PAC kuwasilishwa bungeni na maazimio kupitishwa. Alichofanya Kafulila kilitokana na kiwewe alichopata baada ya sehemu kubwa ya jamii kutoridhishwa na maazimio ya Bunge.

Ukipata muda, ukazisoma taarifa za Kamati ya PAC na Bunge kwa ujumla, hazifafanui vya kutosha kuelezea ukweli kwamba fedha zilizokuwa kwenye Akaunti ya Escrow ilipewa kampuni ya PAP yenye akaunti yake Benki ya Stanbic. Fedha hizo hazikwenda moja kwa moja kwenye akaunti ya VIP iliyopo benki ya Mkombozi. Hata malipo waliyolipwa VIP kutokana na mauzo ya hisa zao yalifanywa na PAP kutokea Benki ya Stanbic.

Kukosekana kwa ufafanuzi wa kina kutoka bungeni kuhusu ukweli huu, kumeendelea kuwachanganya wananchi kiasi cha kuendelea kuamini kwamba VIP ya Rugemalira nao walipokea fedha za Escrow kutoka BoT, jambo ambalo si la kweli hata kidogo. Sintofahamu hii nayo imeendelea kukoleza mjadala na kufarakanisha jamii bila sababu ya msingi.

Kitu kingine ambacho kinaendelea kuichanganya jamii hadi sasa ni kuaminishwa kipotoshaji kwamba kampuni ya VIP ya Rugemalira, haikuwa na uwezo wa kufanya miamala ya kuwapa watu fedha mbalimbali kama walivyotajwa kwa jumla ya kiwango kinachofikia shilingi bilioni 3 kabla fedha za escrow hazijalipwa kwa PAP. Huu nao ni upotoshaji wa makusudi wenye lengo la kuwachanganya wananchi.

Ukweli ambao Bunge lilipaswa kuwafafanulia wananchi ili kupunguza sintofahamu katika sakata hili ni kwamba, hata kabla ya PAP kupewa fedha za Escrow Novemba 2013, kampuni ya VIP ilikuwa na uwezo wa kufanya hiyo miamala ya jumla ya Sh bilioni 3 kwa watu mbalimbali kutokana na salio lililokuwa kwenye akaunti yake iliyoko benki ya Mkombozi. Ikumbukwe kwamba VIP ililipwa na PAP fedha (USD 75 mil) za mauzo ya hisa (30%) kwa awamu mbili.

Awamu ya kwanza ya malipo ilihusu asilimia 10 ya bei ya mauziano (USD 7.5 mil) ambayo ilikuwa sawa na zaidi ya Sh bilioni 10. PAP ilimlipa VIP kiasi hiki Agosti 2013, miezi mitatu kabla fedha PAP hajakabidhiwa fedha za Escrow. Malipo haya tu ambayo hayatokani na fedha za Escrow yaliiwezesha kampuni ya VIP kufanya hiyo miamala ya shilingi zinazofikia bilioni 3.

Hoja ya msingi hapa ni kwa nini PAC au Bunge hawakuzingatia ukweli huu kabla ya kupitisha maazimio ambayo sasa yanatatiza umma? Ukimya wa Bunge katika suala hili umesababisha watu waendelee kujadili kadhia hii kwa mwelekeo kwamba VIP ya Rugemalira haikuwa na uwezo wa kufanya miamala ya Sh bilioni 3 hadi ilipolipwa na PAP, baada ya PAP kupokea fedha za Escrow. Tafsiri hii siyo sahihi, na kama Bunge lingefafanua vizuri jambo hili, ingepunguza mhemuko wa jamii.

Na kwa kadri maazimio yalivyosimama na kauli ambazo zimeendelea kutolewa na baadhi ya viongozi wa Bunge, inaonesha kwamba Bunge sasa limeamua kuhodhi mamlaka na madaraka yote ya mchakato wa kutoa haki, jambo ambalo ni kinyume kabisa na misingi ya utawala bora.

Alichofanya Kafulila na Zitto wakati wakiongea na vyombo vya habari kujaribu kuwasafisha viongozi wa dini ni ushahidi wa mwelekeo wa Bunge letu. Ningeungana na Ikulu hivi karibuni kwamba “Waheshimiwa hao hawawezi wao kuwa wapigaji mbinja (whistle blowers), wakawa wachunguzi, wakawa na mamlaka ya kukamata watu, wakawa na madaraka ya kushitaki, wakawa na madaraka ya kuhukumu na wakawa na madaraka ya kuwafikisha watu jela na kuendelea kuwalinda huko.”

Niamini tu kwa kusema kwamba wabunge wanajua kwamba angalizo hili la Ikulu ndiyo msingi bora wa uendeshaji wa nchi. Kufanya vinginevyo, ni kubaka misingi ya utawala bora wa nchi hata kama si Tanzania.

Hakika Kamati ya PAC imejichanganya. Kwanza wameeleza kwamba wao hawana tatizo na mauzo ya hisa za VIP kwa PAP, na tena hawana sababu ya kumchagulia marafiki James Rugemalira, lakini wakati huo huo wamependekeza baadhi ya watu (wenyeviti wa kamati) wavuliwe nyadhifa zao kwa sababu ya kupokea mgawo kutoka kwa mtu ambaye PAC wenyewe wanasema hawana mamlaka ya kumchagulia marafiki. Pendekezo hili ambalo ndiyo lililozaa azimio la Bunge lina walakini unaotokana na kujichanganya kwa maelezo ya PAC.

Maelezo ya PAC na namna azimio lilivyowekwa ni mwendelezo wa mkakati ule ule wa kuwalinda baadhi na kuwamaliza wengine kisiasa. Msimamo wa PAC na Bunge ungeeleweka vizuri kama taarifa ya CAG na PAC zingeonesha dhahiri maelezo ya hao wanaotuhumiwa ikiwa ni pamoja na Rugemalira, kwa kadri walivyohojiana nao.

Bahati mbaya au nzuri taarifa hizi hazina ushahidi wa maelezo ya watuhumiwa hawa. Ilikuwa muhimu sana kumhoji Rugemalira ili kujiridhisha sababu zilizomfanya awagawie fedha watuhumiwa hawa. Kilicho wazi katika mazingira haya ni kwamba Bunge limewatuhumu na kuwahukumu watu hawa bila hata ya kuwapa fursa ya kujitetea, kinyume kabisa na misingi ya utawala bora.

Kutokana na kupishana kwa maudhui ya taarifa ya CAG na PAC katika baadhi ya maeneo, tunapata mashaka makubwa kuhusu uhalali wa kutekeleza maazimio ya kuwawajibisha watumishi wa umma waliotuhumiwa na kutajwa katika taarifa ya PAC ingawa hawakutajwa katika taarifa ya CAG.

Mashaka yanajengeka kwenye ukweli kwamba msingi wa taarifa ya PAC ni taarifa za CAG na Takukuru. Swali la kujiuliza hapa ni kuhusu watu ambao hawakutajwa kwenye taarifa ya CAG, lakini PAC imewatuhumu, je, watatendewa haki kweli kama maazimio yatatekelezwa kama yalivyo bila uchunguzi wa kina?

Miongoni mwa watuhumiwa katika eneo hili ni wanasiasa hasa wabunge waliopata mgawo kutoka kwa VIP ya Rugemalira. Azimio la kuwawajibisha wanasiasa waliopokea msaada kutoka VIP limejengwa kwenye tuhuma za kukiuka sheria ya maadili.

Naam, inafahamika si kosa kwa mbunge kupokea msaada kutoka kwa wahisani mbalimbali. Wahisani kama Mzee Sabodo, Mohammed Enterprises, Said Salim Bakhressa, Yussuf Manji, Subhash Patel, Abraham Mengi na kampuni zake za IPP, mifuko ya jamii, benki mbalimbali, na kadhalika wamekuwa mstari wa mbele kutoa misaada kwa wabunge ili kusaidia kutatua kero majimboni mwao. Jambo hili siyo jipya na wala halishangazi.

Bunge lina uzoefu kuhusu uhalali wa misaada inayotolewa kwa wabunge. Kwa mfano, mwaka jana wakati wa mjadala kuhusu Bajeti ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Bunge lilipata mtihani wa kutafakari endapo msaada anaopata mbunge kutoka kwa wahisani mbalimbali kupitia kampuni yake au yeye mwenyewe binafsi ni ukiukaji wa maadili ya viongozi wa umma.

Hoja ya tuhuma za kukiuka maadili ilitolewa bungeni na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ikimtuhumu Zitto Kabwe kwamba kwa kipindi kati ya Desemba 2012 na Machi, 2013 kwamba kupitia kampuni yake ya Leka Dutigite alikuwa amepokea msaada wa takribani Sh 119 milioni kutoka taasisi za umma (TANAPA na NSSF), kinyume cha miiko ya maadili ya viongozi wa umma. Hata hivyo, Bunge lilipuuzia tuhuma hizo na Zitto hakuchukuliwa hatua yoyote.

Mfano huu unasaidia kujua msimamo wa Bunge kuhusu masuala ya misaada inayotolewa na wahisani kwa wabunge. Hivyo, hata katika kadhia hii ya Escrow hatutarajii kwamba Bunge litabadili msimamo na kuwaadhibu wale waliopata msaada kutoka kampuni binafsi ya VIP ya Rugemalira.

Baada ya ufafanuzi wa kina wa Rais Kikwete kuhusu yale mambo makuu matatu kama yalivyotajwa kwenye utangulizi wa makala hii, wanaoendekeza mjadala huu kiupotoshaji sasa wanajiegemeza kwenye hoja ya ukiukaji wa maadili kwa baadhi ya watuhumiwa.

Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995 haimzuii mtumishi wa umma kupokea msaada. Sheria hii inamtaka kila mtumishi wa umma ajaze fomu ya Tamko la Viongozi wa Umma kuhusu Rasilimali na Madeni yake kila ifikapo Desemba 31 ya kila mwaka na kuiwasilisha kwa Kamishna wa Maadili.

Kwa kadri mjadala unavyoendelea mitaani, kuna mwelekeo wa kutaka kuwahukumu watu (mob justice) wanaotuhumiwa kwamba kila aliyepata mgawo kutoka VIP basi amekiuka maadili ya viongozi. Hii ni kinyume cha sheria. Sharti hili la Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma inawalinda na kuwakinga vizuri watu wanaotuhumiwa kukiuka maadili eti kwa kigezo kwamba hawakutangaza mgawo wao kwenye fomu za maadili.

Taarifa ya PAC inaonesha kwamba miamala ya mgawo kwa watu mbalimbali iliyofanywa na kampuni ya VIP kupitia Benki ya Mkombozi ilifanyika Februari 2014. Ukweli huu unadhoofisha hoja ya tuhuma za Bunge kwamba waliopata mgawo hawakuonesha migawo hiyo kwenye fomu za maadili.

Hivyo, wametuhumiwa na kuhukumiwa kinyume na sheria kwa sababu sheria inaagiza tarehe ya mwisho kujaza fomu za maadili kwa kila mwaka ni Desemba 31. Maana yake ni kwamba kama migawo hiyo ilistahili kuoneshwa kwenye fomu za maadili basi ni fomu zilizojazwa Desemba 31, 2014. Kama hivi ndivyo inavyopaswa kuwa, kwa nini Bunge liliamua kuwatuhumu na kuwahukumu watuhumiwa kinyume cha sheria? Bunge lilikosea, ni muhimu likakiri makosa yake, vinginevyo tutaendelea kuamini kwamba huo ni mwendelezo wa mchezo mchafu kisiasa.

Bunge lijihadhari na lijiepushe na mwelekeo huo kwa sababu inawezekana kila mtuhumiwa amepata mgawo kwa sababu tofauti. Tumeona baadhi ya watuhumiwa ni wabunge, kwa hiyo huwezi kujua kama alipewa kama msaada kusaidia utatuzi wa kero jimboni kwake au la.

Wengine ni wanasheria, hivyo inawezekana walichopata ni malipo halali kwa kazi waliyomfanyia aliyewalipa na kadhalika. Katika mazingira hayo si haki kuwaadhibu watuhumiwa kwa adhabu ya aina moja kabla ya uchunguzi wa kina ikiwa ni pamoja na kuwahoji watuhumiwa. Ukweli ni kwamba Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma inatamka bayana kwamba kosa la ukiukwaji wa maadili ni sawa na kosa la jinai.

Kwa sababu Bunge ndiyo chombo cha kutunga sheria, tunaamini wakati wa utekelezaji wa maazimio yake litazingatia msingi mkuu unaohusu vigezo vinavyotumika kumtia mtuhumiwa hatiani kwa kosa la jinai.

Ni sharti la sheria zote duniani kwamba mtuhumiwa wa kosa la jinai anaweza tu kutiwa hatiani endapo ushahidi wa kosa lake umethibitika bila kuwa na chembe yoyote ya mashaka juu ya ukweli wa ushahidi huo. Uchunguzi unaonesha kwamba umebaini kwamba kwa mazingira ya sakata la Escrow haitakuwa rahisi kwa Bunge kupata ushahidi usiokuwa na chembechembe ya mashaka utakaohalalisha kisheria kuwatia hatiani watuhumiwa.

Nimejiridhisha na msimamo wetu kwa sababu tayari Rais ameishafafanua kwamba fedha zile hazikuwa za umma. Ukweli huu tu unazaa maswali mengi sana kuhusu uhalali wa tuhuma kwa watuhumiwa.

Kauli na matamko mbalimbali yanayoendelea kutolewa tangu Bunge lilipopitisha maazimio kuhusu sakata la escrow na baada ya hotuba ya Rais Kikwete aliyoitoa Desemba 2014 zinahitaji tafakuri ya kina kutoka kwa kila mzalendo wa nchi yetu, hususan, viongozi wenye dhamana kwa mihimili ya nchi.

Maangalizo ya baadhi ya viongozi wa dini na wanasiasa kama John Shibuda yenye viashiria vya hofu ya kubaguliwa, kudharauliwa na kunyanyaswa kisiasa na kiuchumi kwa baadhi ya Watanzania wanaoishi au kutoka katika kanda fulani ya nchi yetu, ni mambo mazito yasiyostahili kupuuzwa, na yanayohitaji kuzingatiwa ili kulinda amani na mshikamano wa Taifa letu.

Muhtasari wa ufafanuzi wa Rais Kikwete kuhusu sakata la Escrow ni kwamba Bunge liliupotosha umma kuhusu ukweli wa kadhia ya akaunti hiyo. Hivyo, Bunge lisipuuze kilio cha sauti za watu wanaolishauri lijitafakari upya badala ya kulazimisha kibabe utekelezaji wa maazimio ambayo yanaweza kuvuruga amani na mshikamano wa Taifa letu.

Ni dhahiri kwamba maazimio yaliyopitishwa na Bunge Novemba 2014 kuhusu sakata la Escrow yalitokana na uamuzi uliofanywa kisiasa, tena siasa chafu. Maazimio hayo hayakutokana na uamuzi wa mfumo wa kisheria kama inavyopaswa iwe, ni uamuzi batili, usiostahili kutekelezwa kama ulivyo.

Ni mjadala uliokosa haki na fursa sawa kwa wote kwa kuegemea siasa chafu za itikadi za vyama vya kisiasa, dhamira ya kutaka kukomoana miongoni mwa wana CCM, na kulinda maslahi ya makundi ya kisiasa na kibiashara. Katika mkanganyiko huo ndiyo maana tuliona hata hoja za baadhi ya wabunge ambazo katika hali ya kawaida Bunge lingezizingatia, zilitupwa kapuni.

Mfano, hoja iliyoibuliwa na Livingstone Lusinde ikimtuhumu Zitto kupokea mgawo wa Sh milioni 20 kutoka kwa Sethi wa PAP haikuzingatiwa, pamoja na Lusinde kuwasilisha vielelezo vya tuhuma mezani kwa Spika. Kinyume na matarajio ya wengi pamoja na ushahidi alioutoa Lusinde, Zitto alipata mtetezi hapo hapo kwenye mjadala. Mtetezi huyo alikuwa waziri mwandamizi aliyeko madarakani sasa na ambaye alibwagwa na Rais Kikwete mwaka 2005.

Waziri huyu alisimama kwa ujasiri akamtetea Zitto kwamba asijibu hoja ya Lusinde eti kwa kigezo kwamba tuhuma zake zilihusu kiasi kidogo cha rushwa. Maneno hayo yalitamkwa na mtu anayetarajia kugombea urais tena mwaka huu.

Pamoja na kwamba ilipofika wakati wa kuhitimisha hoja Zitto aliomba apelekwe kwenye Kamati ya Maadili ya Bunge ili achunguzwe kuhusu tuhuma alizotuhumiwa na Lusinde, bado Bunge halikuona umuhimu wa kumchukulia hatua mtuhumiwa.

Assumpter Mshama naye alimtuhumu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, kupokea mgawo mzito kutoka kwa Sethi wa PAP, lakini hoja yake wala haikupewa uzito. Hata tuhuma za Habib Mnyaa kwa Spika Anne Makinda naye alikuwa amekula rushwa kutoka kwa Sethi wa PAP hazikufua dafu, zilitupiliwa mbali.

Yote hii inathibitisha dhana inayosemwa na watu wengi mtaani kwamba kadhia ya Escrow imetumika kuwatoa kafara watu fulani na kuwalinda wengine kwa maslahi ya kisiasa na biashara. Fitina na vituko hivi havihalalishi mwenendo mbaya wa uamuzi wa Bunge kwa ustawi wa Taifa letu.

Sasa, wakati vikao vya kamati za Bunge vinaendelea, Bunge litoe tamko rasmi kuwaomba radhi Watanzania kwa upotoshaji lililoufanya kupitia maazimio yake manane Novemba 2014, sambamba na kuahidi kutofanya kisiasa siku zijazo na litazingatia uamuzi wa mfumo wa kisheria.

Bunge letu halina sifa wala vigezo vya kujifananisha na kutumia falsafa ya mke wa mfalme aliyewajibishwa kwa kuhisiwa tu kufanya kosa bila ushahidi wowote. Baadhi ya wanasiasa wa Bunge wameejaa fitina, uzushi, uongo, visasi na upotoshaji ili kuwahukumu wengine.

Ikitokea wanataka kuwawajibisha watuhumiwa kwa kutumia falsafa ya mke wa mfalme, hakika hakuna atakayebaki salama. Hakuna ubishi kwamba wabunge walituhumiana wakati wa mjadala, kuanzia Spika Makinda ni mtuhumiwa, Zitto na Mbowe. Kuna wabunge wote kwamba wanatumiwa vibaya wanaoshiriki kwenye vita ya rushwa. Sasa katika mazingira hayo nani atabaki salama hapo mjengoni?

By Jamhuri