Wakati wa ziara yake nchini Marekani, Januari mwaka jana, Rais wa China ‘alimuondoa’ hofu bwana mkubwa wa dunia, Rais wa Marekani, Barack Obama, kwa kumwambia kuwa China haina mpango wowote wa kuutawala uchumi wa dunia.

Kauli hiyo ilikuja baada ya gazeti la Financial Times kuibuka na utafiti uliothibitisha kuwa China inaongoza kwa zaidi ya asilimia kumi; kumwaga misaada kwa nchi maskini ikilinganishwa na inayotolewa na Benki ya Dunia.


Enzi za Marekani, kufanya uamuzi wa mwisho dhidi ya masuala tete ya kidunia, sasa zinaonekana kupoteza makali na huenda zikawa ndiyo zinafikia mwisho. Hii inatokana na kuibuka kwa China ambayo uchumi wake unazidi kuimarika kwa kasi kubwa. Kukua kwa China kiuchumi kunaonesha dhahiri kuichanganya na kuichachafya Marekani vilivyo.


Tayari China imejitambua kuwa inaitisha Marekani na kwa maana hiyo inaonekana kuvuka mistari ya kimaslahi iliyochorwa na Marekani kwa miongo mingi. Pamoja na kwamba China na Marekani zina ushirikiano mkubwa kibiashara, lakini zinakoelekea kunaonekana dhahiri kuwa zitakuja kuwa hazipikiki katika chungu kimoja.


Kwa mfano, China inaelezwa katika baadhi ya nadharia kuwa ilichangia kwa makusudi kutokea kwa mdororo wa uchumi ulioikumba dunia kuanzia mwishoni mwa 2010. Inaelezwa katika nadharia hii kuwa China iliwekeza mabilioni ya dola katika masoko ya Marekani kwa makusudi na hivyo benki za Marekani kujikuta zina wingi uliopitiliza wa fedha (excess deposits).


Wingi huu wa fedha ukafanya benki hizo kujisahau na kuanza kukopesha wawekezaji wa biashara ya nyumba kwa fujo, bila kuzingatia mzunguko wa fedha na mwenendo wa kibiashara. Baadhi ya benki zilifikia hatua ya kushusha riba za mikopo hiyo ili kuwavutia wakopaji.


Ushushaji wa riba, ukopeshaji usiozingatia masharti na kuanguka kwa soko la nyumba kukasababisha benki kukosa fedha. Mdororo ukatokea kwa vile benki hazikuwa na uwezo wa kukusanya madeni na hivyo kushindwa kuwalipa wawekezaji.

 

Wakati Marekani ikiilaumu China ‘kiaina’, China nayo imekuwa ikiipiga vijembe Marekani kuhusu mdororo huo. Wanauchumi kadhaa wanaoiunga mkono China, walitoa maoni yao, na kusema kuwa mdororo wa uchumi ulioikumba dunia ni janja ya Marekani ili kuyumbisha uchumi wa China.


Wao wanasema mdororo huu wa uchumi ulipangwa makusudi na Marekani ili ipate sababu za kujipanga upya namna inavyoshughulikia sera za uchumi wa kimataifa na uchumi wake wa ndani. Ndiyo maana China mara kwa mara imekuwa ikiweka ngumu maoni ya Marekani kuitaka China ipandishe thamani ya fedha yake na kurekebisha kiwango cha bidhaa inazosafirisha nje ya nchi hasa kuelekea Ulaya.

 

Mgongano mkubwa unaojitokeza baina ya Marekani na China ni katika sera zao za kiuchumi na mambo ya nje. Wakati China ni nchi inayoendesha sera za kijamaa, imeendelea kujipatia faida kwa kuunganisha tabia fulani za kibepari katika mfumo wake wa kiuchumi.Hii imeiwezesha China kuzalisha bidhaa na huduma kwa gharama ndogo (ndani ya nchi) na wakati huo huo ikitumia fursa za ulimwengu wa kibepari kuuza bidhaa zake Ulaya, Marekani, Asia na Afrika. China inazidi kunyang’anya masoko ya bidhaa yaliyokuwa yakitawaliwa na Marekani.Maji yameifika shingoni Marekani kiasi ambacho badala ya kuamuru kiubabe inalazimika kutumia diplomasia kushauriana na China.

China haina muda na kitu kinachoitwa demokrasia na haki za binadamu. Si kwamba haiamini katika dhana hizo, ila imeamua kutowekeza muda na rasilimali nyingi katika mambo hayo kuanzia ndani hadi katika mataifa inayoshirikiana nayo. Mahali pengi duniani watu wanaamini kuwa China inakiuka haki za binadamu na haina demokrasia, lakini hili lina ukweli mweusi.

 

Vyombo vya habari na taasisi za Magharibi na Marekani vinaeneza propaganda hii kwa sababu China imekataa kuendesha demokrasia na haki za binadamu kwa viwango vya nchi za Magharibi. Upofu walio nao Marekani na nchi za Magharibi ni kudhani kuwa wanachokiamini wao ni bora kwa binadamu wote.


Kutokana na msimamo wa China kuhusu demokrasia, haki za binadamu na mwelekeo wa sera zake za nje, imejikuta ikipata marafiki wengi wa kweli na walio tayari kuitetea kufa na kupona. Kwa mfano, katika mgogoro wa Ivory Coast (unaoendelea), China ilipingana na msimamo wa Marekani na kutoa tamko la kutaka mambo ya ndani ya Ivory Coast waachiwe Waivory Coast wenyewe.

 

Nchi maskini zimeendelea kujikunyata kwa China kwa sababu imekuwa nchi pekee inayonguruma wazi wazi katika Umoja wa Mataifa na katika Baraza la Usalama ikizitetea nchi hohehahe. Ingawa China nayo huzitetea nchi hizi kwa maslahi yake binafsi, angalau inajua kula na vipofu (wenye macho?)

 

Kwa upande wake, Marekani inaamini na kutekeleza ubepari wa kibabe. Inazunguka duniani kote ikihubiri demokrasia na haki za binadamu. Hulka hii imesababisha Marekani kujikuta inaingilia mambo ya ndani ya nchi mbalimbali duniani na kuzusha ghadhabu katika nchi hizo.

 

Bila kificho wala aibu, Marekani inatangaza ulimwenguni pote ya kuwa haina rafiki wa kudumu wala adui wa kudumu ila ina maslahi ya kudumu. Kutokana na mataifa mengi kukazana na juhudi za kujikwamua kiuchumi, falsafa hii ya Marekani inaanza kuwa shubiri kwakwe.

 

Marekani inazidi kutengeneza maadui wengi kila kukicha, na inaziburuza nchi nyingine kuungana nayo kupambana na maadui iliowatengeneza kwa raha zake. Mataifa mengi sasa yapo makini sana jinsi yanavyoshirikiana na Marekani kwa sababu leo anaweza kuwa rafiki kesho akawa adui. Marekani haiaminiki!

 

Mchakamchaka umekuwa ukitokea katika nchi ama maeneo ambako Marekani na China vinataka kuvuna rasilimali. Kutokana na mnyukano huu, Bara la Afrika limebaki njia panda likiwa ‘halijisomi’ na kwa maana hiyo linacheza ngoma ya ukunguru. Bara la Afrika linapenda kuiridhisha China na wakati huo huo halipendi kuiudhi Marekani. Kinachofuatia ni Afrika kubaki kama nyasi katika mapigano ya wababe hawa.


China ambayo haikuwa imejikita Afrika kwa miaka mingi huko nyuma, sasa inataka kumiliki maslahi ya kirasilimali ya bara zima. Mbinu inayotumiwa na China ni ile ya ‘Generic Mass Penetration’ (kujiimarisha pote). China inafanya mikutano ya mara kwa mara na wakuu wa Afrika, inamwaga misaada yenye masharti nafuu na inaonesha ukarimu wa hali ya juu kwa nchi za Afrika. Jicho la China kwa Afrika linaonekana kuikera Marekani.

 

Angalia hili. Wakati wa mgogoro wa Darfur kule nchini Sudan, Marekani iliushinikiza Umoja wa Mataifa kuiwekea vikwazo Sudan lakini China ilisimama kidete na kuviwekea ngumu vikwazo hivyo. Sudan ni miongoni mwa nchi ambazo China inavuna mafuta kwa wingi sana.

 

Ubabe wa China ukasababisha hasira ya Marekani kuhamia mbinu nyingine. Kwani Marekani ilitoa shinikizo kwa Mahakama ya Uhalifu wa Kivita ya Umoja wa Mataifa (ICC), kufungua mashitaka na kutoa kibali cha kukamatwa kwa Rais wa Sudan, Omar al Bashir, ambaye haivi chungu kimoja na Marekani.


Umoja wa Afrika (AU) ulitoa msimamo wake dhaifu kulaani hatua hiyo ya ICC. Ni msimamo dhaifu kwa sababu AU haisemi kuwa Omar al Bashir asikamatwe kabisa isipokuwa inasema kumkamata kwa sasa kutavuruga mchakato wa uletaji amani huko Darfur na katika Sudan ya Kusini. Kwa picha nyingine, msimamo wa AU unasema Omar al Bashir akamatwe lakini si muda huu!


Tayari nchi kadhaa zilizo wanachama wa ICC ambazo Omar al Bashir ametembelea na hakukamatwa, zimepigwa ‘mkwara mzito’ na Marekani. Vita ya mafuta ya Sudan baina ya Marekani na China inazitaabisha na kuzitoa jasho nchi za Afrika. AU inajua kuwa Bashir hana makosa ya kufikishwa mbele ya ICC, ndiyo maana imepinga (japo kwa muda) kukamatwa kwake; lakini itafanyeje na wakubwa wamewakiana hasira?Ubabe na vikumbo vya China havipo Afrika tu bali ni duniani kote. Wakati Marekani inahangaika kuishawishi dunia kuitenga nchi ya Iran kutokana na mpango wake wa nyuklia, China inaitetea nchi hiyo kwa nguvu zote.


China inalazimika kufanya hivyo kwa sababu imesaini mkataba wa nishati unaofikia dola bilioni 70 (sawa na zaidi ya shilingi za Kitanzania trillioni 100). China inalinda maslahi yake ikitishia kupinga kwa kura ya veto hatua yoyote ya Marekani dhidi ya mataifa inayonufaika nayo.


Marekani inaonekana kutolewa jasho vilivyo na inatafuta kila mbinu kuishawishi China kukubaliana na matakwa yake. Lakini China ikikubaliana na matakwa mengi ya Marekani, ni lazima ikubali kuwa chini yake, na China inataka kuongoza uchumi wa dunia.

 

Je, China itazifuta kabisa enzi za Marekani? Tusubiri historia inayoandikwa sasa itatuambia wakati ukifika.

stepwiseexpert@gmail.com; 0719 127 901


 

 

4160 Total Views 5 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!