Wanasiasa na wasio wanasiasa walishuhudia kuona na kusikia hekaheka zilizofanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kuandaa, kuendesha na kusimamia Mkutano Mkuu Maalum wa kumchagua Mwenyekiti wa Chama hicho, wiki iliyopita mjini Dodoma.

Katika utamaduni waliojiwekea wanaCCM, walimchagua kada mwenzao, Rais John Pombe Magufuli kuwa Mwenyekiti wa CCM taifa kuchukua nafasi iliyoachwa kwa hiyari na aliyekuwa Mwenyekiti na Rais wa Serikali ya Awamu na Nne, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete.

Binafsi naungana na wana-CCM na wananchi nchini waliompongeza Rais Magufuli kuwa Mwenyekiti wa CCM. Nina imani na matarajio makubwa kuona Mwenyekiti huyo anaongoza Chama na Serikali kwa upendo na uadilifu.

Mkutano Mkuu Maalum umetoka na mitazamo mikuu miwili. Mtazamo wa kusifu na kupongeza; na mtazamo wa kubeza na kulaumu. Daima katika mfumo wa demokrasia ya vyama vingi, haijapata kutokea na wala haitatokea watu wote katika jamii wakubali uamuzi wa chama na hasa chama kinachotawala nchini.

Nimesikia upande wa pili (upinzani) wakibeza na kulaumu kuwa CCM hawakuwa na jipya. Na kauli za viongozi hapo mkutanoni zilitawala hofu, wanamwogopa aliyekuwa mgombea urais mwaka jana kupitia UKAWA (2015, Edward Lowasa).

Hapa napata shida kuelewa. Inakuwaje wapinzani waseme CCM ina mwogopa Edward Lowasa? Kwa lipi ? Wapinzani hao wanasema CCM na Serikali yake ni wababe. Sifa ya mbabe ni ujeuri, ujasiri na hata ukatili. Hutumia mabavu katika matendo bila ya kujali anayemtendea ni dhaifu au imara.

Hivi kumzungumza mtu au kiongozi mwenendo wake mzuri au mbaya ni kumwogopa ? Kumcheka au kumdhikaki mtu kutokana na vituko vyake ni kumwogopa? Kumsuta mtu kutokana na tabia yake ya ugombanishi ni kumwogopa? Kumlaani au kumkemea mtu kwa maovu yake ni kumwogopa?

Tangu jana hadi leo dunia bado inawazungumza viongozi mbalimbali wafu na hai kwa mazuri au mabaya waliyotenda mathalani, Berito Mussolini, Pandit Jawaharlal Nehru, George W. Bush, Saddam Hussein, Francois Hollande, Tom Blair, Julius Nyerere, Mao Tse Tung, Ibrahimu Lipumba, Wilbroard Slaa na wengine wengi wanaogopwa?

Mbona James Mbatia na UKAWA yake wana wazungumzia John Momose Cheyo,  Augustine Lyatonga Mrema, Fred Mpendazoe, kuhudhuria mkutano mkuu wa CCM, je, wanawaogopa? CHADEMA huko nyuma walimzungumza sana Edward Lowassa kwa maelezo ni fisadi nambari wani  nchini. Je, CHADEMA walikuwa wakimwogopa Lowasa? Nisaidieni.

Nimesikia upande wa kwanza (CCM na wananchi ) wakisifu na kupongeza taratibu za mabadiliko ya kumpata Mwenyekiti wa Taifa- CCM, Rais Magufuli bila kificho wala mizengwe. Duniani kote chama cha siasa makini ni lazima kifanye mabadiliko kuweka taratibu bora za kuongoza chama.

Chama cha siasa cho chote kisichofanya maboresho au mabadiliko na kuweka taratibu za kuendesha chama, ukweli huwa si  chama cha siasa. Bali huwa ni chama cha harakati na taratibu zake huwa za matukio na uhamasishaji vituko. Sampuli ya aina ya vyama hivyo vipo hapa nchini.

Chama cha siasa hufanya vikao yake vya kupata wanachama, kuweka viongozi madarakani kwa njia ya kidemokrasia ya chama hicho.  Chama hujitambua na viongozi wake huwa wanyenyekevu kushika madaraka. Wanachama huwa na mshikamano katika kulinda na kuendesha chama.

Hapa nchini  kuna baadhi ya vyama havichagui viongozi katika ngazi mbalimbali kama vile Mwenyekiti wa Chama kitaifa au Katibu Mkuu wa chama kidemokrasia, ingawaje chama kina katiba na kanuni.

Ni busara na vyema viongozi mchague la kusema na lenye ukweli ili mnao waongoza wawapime kutokana na hekima zenu. Mshindane kwa hoja na vigezo vya tija wala si mbwembwe na sifa za kujinadi. Mipasho ni mtindo wa taarabu si wa siasa.

By Jamhuri