Siasa ni itikadi inayofuatwa na kundi au jamii fulani ambayo ni msingi wa kuendesha uchumi, utamaduni na mwenendo mzima wa maisha ya jamii hiyo. 

Demokrasia ni mfumo wa kuendesha Serikali iliyochaguliwa na watu kwa manufaa ya watu. Sheria ni kanuni zinazotungwa na bunge la nchi fulani ili kusimamia taratibu za nchi hiyo na ambazo ni lazima zifuatwe na watu waliomo humo, na anayekwenda kinyume nazo hupewa adhabu na Mahakama.

Nimeweka maana ya siasa, demokraia na sheria kwa muhtasari kama yalivyoainishwa katika Kamusi ya Kiswahili Sanifu, toleo la 3, mwaka 2013, nikiwa na madhumuni ya kuangalia dhana hizo kisiasa zinavyoelimisha, zinavyohamasisha, zinavyoyumbisha na zinavyotatanisha watu wanapokuwa katika medani za siasa, katika kutafuta haki ndani ya demokrasia waliyokubaliana.

Natambua wanazuoni, wasomi na wataalamu waliochukua taaluma hizo, wana maelezo na uchambuzi wa kina juu ya siasa, demokrasia na sheria. Naweza kusema asili ya yote hayo ni falsafa. Lakini naleta mada hii mbele yako msomaji tuipe uchambuzi wa ukweli na stahili bila kwenda kombo na kumung’unya maneno. Nina maana tuache upendeleo na uzandiki katika hili.

Ukizingatia tafsiri niliyoweka mwanzoni, siasa ni mwendo mzima wa maisha kwa mtu yeyote katika utafutaji mlo wa siku, utengenezaji na uboreshaji wa hali ya kuishi kimavazi na kimakazi. Pia ni ushirikiano kati ya watu katika kudumisha mila na desturi bila bughudha ugomvi au vita.

Wewe na wenzako (jamii) mnapokubaliana kuweka mfumo wa kuendesha na kusimamia mamlaka kuanzia nyumbani, mitaani, kwenye vyama vya siasa hadi kwenye vyombo vya umma na dola, ukweli mnaweka taratibu bora na uongozi. Huo ndiyo utekelezaji wa demokrasia ya kweli iliyokubaliwa.

Mnapovunja utaratibu au mfumo mliyokubaliana kwa hiari ni dhahiri shahiri mnajenga matatizo katika kuishi na kuongoza, mithili ya mkulima anayepanda magugu katikati ya ngano shambani mwake. Wakati wa kuvuna ngano hiyo atapata tabu kwanza ya kung’oa magugu na pili, asipate mavuno bora na mengi ya ngano. Hilo ni tatizo.

Taratibu mlizokubaliana na kuziweka ziweze kutoa haki na kujenga amani na utulivu, hamna budi kuweka kanuni na sheria zitakazosimamia na zitakazolinda makubaliano. Hapa ndipo unapoona faida na maana ya demokrasia katika uendeshaji siasa na itikadi yake. Kinyume chake ni uwenda wazimu, fujo na chuki.

Jamii inayopenda na kujali utulivu na amani huzingatia sana taratibu za kuendesha siasa nchini; utekelezaji wa demokrasia yao na usimamizi wa sheria za nchi. Mathalani, nchi yetu (Tanzania) huko nyuma kuanzia mwaka 1967-1991 ilikuwa na ilipata sifa ya kuwa kisiwa cha amani. Sababu; wananchi walielewa na kuzingatia maana ya siasa na itikadi yake, demokrasia na utekelezaji wake na sheria na hukumu zake.

Imani ya kujenga siasa na uchumi wa kijamaa kwa njia ya kujitegemea, demokrasia ya kweli iliyolala katika misingi ya kijamaa ya kuthamini utu wa mtu na sheria iliyozingatia misingi ya haki ndani ya Ujamaa na Kujitegemea. Dira ya yote hayo ilikuwa Azimio la Arusha. Leo Azimio hilo halipo. Na ile dhana ya kutambua “Nia Njema” ya chama cha siasa huenda haiko!

Tulikuwa na itikadi ya chama na itikadi ya nchi. Ujamaa ni Imani. Leo tuna vyama vingi vya siasa kila kimoja kina itikadi yake, kina taratibu zake za kutaka kuongoza nchi na kuendesha uchumi wa nchi na kina mfumo wake wa utekelezaji demokrasia. Kila chama kinajitahidi kuvuta na kupata wanachama wengi, lakini hakitoi mafunzo ya itikadi ya chama kwa wanachama na viongozi wake ili wasipate shida katika utekelezaji wa demokrasia.

Kwa mfano, itikadi ya Chadema ni ‘mlengo wa kati’ kukuza na kuimarisha uchumi wa nchi, katika soko huria na kutumia rasilimali ya nchi na kuwapa wazawa fursa ya kumiliki na uendeshaji uchumi na kujenga maadili mema ya kizalendo kwa wananchi wote.

CUF katika itikadi yake au falsafa yake mpya itakayojulikana ‘Uliberali’ inayozingatia haki sawa kwa wote na neema kwa wote, ikijikita katika kutumia utajiri wa rasilimali ya nchi na kuweka uchumi mikononi mwa wananchi wenyewe.

CCM, itikadi yake ‘Ujamaa na Kujitegemea’ ndiyo njia pekee ya kujenga jamii ya watu walio sawa na huru. Kusimamia haki na maendeleo ya wakulima, wafanyakazi na wananchi. Uchumi wa taifa unamilikiwa na dola, utajiri wa nchi unatumika kwa maendeleo ya wananchi na hakuna dhuluma ya aina yo yote kwa wananchi.

Hizo ni baadhi ya itikadi za vyama vya siasa nchini. Utaona itikadi hizo zinatofautiana. Tunakosa itikadi ya nchi. Hapo migongano ya utekelezaji wa demokrasia unapochomoza na kuleta ‘rabsha’ kwa wananchi. Hapa pana siri kubwa katika nia njema ya chama!

Demokrasia ya kweli inasimama wapi, kwenye Uliberali, Mlengo wa Kati, Ujamaa ni Imani au kwenye itikadi za vyama vingine nchini? Vyuo vya kujenga itikadi hizo viko wapi hapa nchini? Nani mwenye jukumu la kuandaa wanachama na viongozi bora kusimamia itikadi za chama? Je, ni kweli vyuo vya viongozi wetu wa siasa ni barabarani, kwenye mitandao au wakati wa chaguzi kuu za kitaifa?

Mara kadhaa tumeshuhudia, kuona au kusikia baadhi ya wanachama na viongozi wakitoa lugha zenye matusi na shari dhidi ya wanachama na viongozi wa chama kingine. Ukiangalia kwa makini utaona liko kosa la kutotambua au kutafsiri kinyume cha dhana ya ‘Nia njema’ ya chama fulani katika kuboresha hali ya uchumi wa nchi.

Laiti nia njema ya kila chama cha siasa ingefahamika wazi, pasingekuwako na migongano ya utekelezaji wa demokrasia, ambayo inatanguliwa na itikadi na inalindwa na sheria. Kosa tunaloliona ni utekelezaji wa sheria juu ya demokrasia badala ya itikadi ya chama inaposhindwa kuelekeza njia ya kupita demokrasia.

Maswali ni mengi na majibu ni machache yanayopatikana. Je, ‘Nia Njema’ ya kila chama cha siasa inafahamika wazi kwa wananchi hata demokrasia ya kweli inayodaiwa kuminywa isiminywe? Nadhani shida kubwa si mbinyo wa demokrasia bali ni ufahamu wa ‘Nia Njema’ ya chama kwa chama kingine na wananchi. Dadavua.

1060 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!