NINA NDOTO (21)

Tumia kipaji chako

 

Kipaji ni kitu chochote unachoweza kukifanya kwa urahisi bila kutumia nguvu nyingi. Kimsingi kipaji huwa hakichoshi.

Kuna watu wana vipaji vya uandishi, uongozi, kuimba, kucheza muziki, kuchora, kuigiza, kushona, kupamba, kupika, orodha ni ndefu, kwa kutaja machache.

Kwenye kipaji kama ni kufundisha hautatumia nguvu nyingi, kama ni kuandika hautatumia nguvu nyingi, hivyo hivyo kwenye kucheza mpira, kuimba na mengineyo.

Kipaji ni nuru, kipaji ni mwanga, kipaji ni taa ya maisha. Unapokuwa na kipaji na kukitumia unaweza kuwa na mafanikio makubwa. Kila mtu ana kipaji ambacho amejaliwa na Mwenyezi Mungu lakini ni watu wachache sana hutumia vipaji walivyonavyo.

Kuna aliyewahi kusema: “Kila mtu amezawadiwa lakini ni watu wachache hufungua maboksi ya zawadi zao.” Usiruhusu kuwa mmoja wa watu wasiotumia vipaji vyao.

Watu wengi wanalalamika hawana mitaji lakini kipaji ni mtaji kamili. Ukiwa na kipaji wewe ni tajiri mkubwa sana, lakini utajiri huo utaupata kama utaamua kutumia kipaji chako.

Kama watu wakijua kipaji chako, watakuwa tayari kukulipa na maisha yatakwenda vizuri. “Kipawa ni kito cha thamani machoni pake yeye aliyenacho, kila kigeukapo hufanikiwa.” (Mithali 17:8).

Unapokuwa na kipaji kila unalolifanya kwa ubora lazima lifanikiwe, kila unapokwenda lazima utambulike. Yusufu alikuwa na kipaji cha uongozi, pamoja na kufungwa gerezani, alipofika gerezani mkuu wa gereza hakutazama makosa yake, alimfanya kuwa mkuu juu ya wafungwa wengine.

Kipaji chako kinaweza kuwa ndiyo ndoto yako ambayo unatamani siku moja dunia nzima ikutambue, anza sasa kutumia kipaji hicho.

Papa Francis alishauri akisema: “Wapendwa vijana, msizike vipaji vyenu, zawadi ambazo Mungu amewapa! Msiogope kuwa na ndoto za mambo makubwa.”

Wataalamu wa mambo ya ubongo wanasema ili mtu awe mbobezi katika eneo fulani anahitaji saa zisizopungua elfu kumi. Tumia muda wako mwingi kukuza kipaji chako. “Ukitaka kupiga zumari, sharti ucheze zumari,” alisema Aristotle.

Sarah Silverman ni muigizaji, mwandishi na mchekeshaji, watu wengi ambao humfuata ili awape ushauri wakiwa wana ndoto za kuwa waandishi huwa anawapa ushauri huu: “Andika. Waandishi wanaandika. Usisubiri mtu aanze kukulipa ndipo uandike.”

Inawezekana bado hautambui kipaji chako ni kipi, usiwaze, nipo hapa kwa ajili yako rafiki.

Zifuatazo ni mbinu ambazo unaweza kuzitumia kutambua kipaji chako:

Hapa nitaomba uchukue kalamu na karatasi yako na uandike majibu ya maswali yafuatayo (asikwambie mtu maandishi yana nguvu kubwa).

Moja,  ni vitu gani unapendelea kuvifanya?

Mambo ambayo tunayafanya muda mwingi, mara nyingi huwa yamebeba vipaji vyetu. Mimi napenda sana kuandika, hivyo kuandika ni kipaji changu. Je, unapendelea kufanya mambo gani?

Waafrika wana methali isemayo: “Mahali moyo wako ulipolalia ndipo miguu huamkia.” Hazina yetu inapokuwa ndipo mioyo yetu inapokuwa.

Ukitazama mambo yanayokuzunguka yanaonyesha kila unachopendelea. “Kwa mvuvi unasikia harufu ya samaki. Kwa mwandishi pamejaa magazeti. Kwa mwalimu amezungukwa na vitabu. Daktari amezungukwa na dawa na vitabu vya magonjwa mbalimbali,” anasema Padri Faustin Kamugisha.

Pili, ni mambo gani ulipendelea kufanya ukiwa mtoto?

Mara nyingi vipaji huanza kujionyesha tangu tukiwa watoto wadogo. Waulize ndugu, marafiki na hata wazazi mambo uliyopendelea kufanya ukiwa mdogo. Au kama unayakumbuka yaandike pia.

Tatu, ni kitu gani unaweza kufanya bila kulipwa pesa?

Nne, ni kitu gani unaweza kufanya vizuri zaidi ya mtu mwingine yeyote?

Kuna mambo ambayo ukiyafanya kila mtu anakusifia au unaonekana mtu wa ajabu. Andika mambo hayo. Au ni mambo gani ambayo bila wewe kuwapo hayaendi sawa, inaweza kuwa nyumbani, shuleni na hata kazini.

Tano, ni ujuzi gani ambao unao? Inawezekana unaweza kutumia kompyuta zaidi ya watu wengine. Andika ujuzi ulionao.

Sita, kama ningejulikana kwa kitu fulani kikubwa kingekuwa kitu gani?

“Kama ni wito wako, utajitahidi watu wajue unachokipenda kwa kuwashirikisha. Utahitaji kushirikisha furaha, nia na upendo wako kwa watu wengine,” anasema Jeremy Lopez, mwandishi wa vitabu. Je, unapenda tukikutana na wewe tukutambue kwa lipi?

Usikubali kuficha kipaji chako. Kipaji chako ni mtaji. Kipaji chako ndiyo mafanikio yako. Kipaji chako ni fursa timilifu ambayo inakupasa uichangamkie haraka iwezekanavyo. Wewe mwenyewe ni fursa, ukijidharau wengine watakufanya fursa.