Itumie intaneti isikutumie

 

Kama kuna watu waliishi kuanzia miaka ya 1990 na kurudi nyuma ukiwarudisha leo duniani wataona maajabu mengi. Dunia imebadilika sana, imekuwa kama kijiji. Leo hii unaweza kuwasiliana na mtu aliyeko nje ya nchi kana kwamba ni jirani yako nyumba ya pili.

Leo hii jambo lolote likitokea duniani ndani ya muda mfupi utakuwa umepata taarifa.

Ama kweli karne ya 21 inayo mengi yanayofurahisha.

Pamoja na kwamba mengi yanayofurahisha yapo, kuna vitu vingi ambavyo tunaweza kuvitumia kwa matumizi yaliyo bora na vikabadilisha maisha yetu, lakini bado hatujaamua kufanya hivyo.

Kitu kimojawapo kinachoweza kubadili maisha yetu ni intaneti. Siku hizi  wengi unaokutana naoni watumiaji wa simu janja (smart phone) au anatumia simu yenye uwezo wa kuingia mtandaoni.

Jambo la ajabu ambalo wengi wetu  linatutesa ni kwamba bado hatujafahamu umuhimu wa intaneti. Wengi hufikiri kwamba intaneti ni sehemu ya kuweka vyakula vizuri wanavyokula, au nguo nzuri walizovaa au sehemu ya kutazama burudani, au sehemu ya kuonyesha maeneo mazuri waliyotembelea.

Badala ya kutumia intaneti sasa inatutumia. Muda mrefu ambao watu wengi wanautumia kwenye intaneti ni muda unaopotea bure. Hakuna  lolote wanalofaidi na kama lipo, basi halina tija.

Hivi umewahi kujiuliza kila unaponunua vocha na kuweka kwenye simu yako na kisha kununua kifurushi, vocha hiyo huwa inakusaidia au unazisaidia kampuni za simu kukuza kipato chao? Hili ni swali muhimu ambalo kila mmoja inabidi ajiulize.

Tambua kuwa unapoweka vocha, unapoingia kwenye mtandao fulani kuna watu wanafaidika, kuna watu wanatajirika. Amka sasa acha kufaidisha watu wengine ilhali wewe hufaidiki.

“Bado tupo katika mwanzo wa matumizi ya intaneti, tuitumie vizuri,” anashauri Jimmy Wales mwanzilishi wa Wikipedia na Wikitribune.

Kimsingi, intaneti ni sehemu ambayo unaweza kujifunza mambo mengi. Kuna watuwanajifunza mtandaoni na wanapata shahada. Intaneti inaweza kukufanya utimize ndoto zako mapema.

Intaneti inaweza kukupatia marafiki, siyo marafiki tu, bali marafiki faida. Intaneti inaweza kukupatia wateja wengi ambao hata bila duka unaweza kuuza bidhaa au huduma.

Makampuni makubwa kama Spotify, Uber, Taxify, Lyft, Alibaba na mengineyo yamekua na kutengeneza kipato kikubwa kupitia intaneti.

Ni wakati sasa wa sisi kubadilika na kuanza kuitumia intaneti kwa manufaa yetu.

Kwanza kabisa kama unafanya kitu fulani hakikisha watu wanakufahamu kwenye mitandao unayotumia. Kwa mfano,  wengi ambao wananifuatilia kwenye mitandao wanajua mimi ni mwandishi.

Haina maana una kipaji Fulani, lakini kwenye mitandao yako umejaza picha za vyakula au picha za maeneo mazuri unayotembelea. Unatumia nguvu kutangaza biashara za watu na unasahau kutangaza biashara au kazi zako.

Tumia intaneti kujifunza kwa watu wanaofanya kitu kama unachofanya, wafuatilie, wasome hasa, jiunganishe nao.

Kama unajua kitu fulani tumia fursa hiyo kukifundisha na kuwapa wengine elimu mtandaoni. Bilionea Strive Masiyiwa ni mfano wa kuigwa. Huyu anatumia ukurasa wake wa facebook kuwafundisha wajasiriamali namna wanavyoweza kukuza biashara, namna ya kupata mitaji na kadhalika.

Unapoanza kuonyesha kitu unachokifanya mara nyingi unaweza usieleweke, lakini baada ya siku kadhaa watu wataanza kukuelewa. Mara nyingi hii huchukua kipindi kisichozidi miezi sita mfululizo.

Watu wengi wanatumia muda wao mtandaoni, kuna haja ya kuwafuata huko. Wataalamu wa mambo ya biashara wanasema, “Biashara inafuata watu wanapokwenda.” Watu wengi wapo kwenye mitandao, kuna haja ya kuwafuata huko.

Unapoweka picha kwenye mitandao, nyingi ziwe zinazohusu kazi zako. Huwezijua ni watu wangapi watakusema  kwa wengine. Ukificha kitu unachokifanya tambua hakuna atakayejisumbua kutaka kukujua.

Mwanamuziki Justin Bieber (1994) alikuwa akiimba nyimbo za watu na kisha kurekodiwa na mama yake, video hizo viliwekwa Youtube. Scooter Braun, meneja anayehusika na vipaji aliona video zake.

Scooter alifuatilia shule ya Justin na kisha akapata mawasiliano ya mama yake.

Akampeleka Atlanta. Katika muda huo Justin akaonwa na msanii Usher Raymond katika mashindano ya muziki. Akapewa mkataba na kampuni ya RBMG Records. Kilichobaki ni historia.

Intaneti inaweza kuwa sehemu nzuri ya kutimiza ndoto zako, endapo utaitumia vizuri. Itumie intaneti, isikutumie.

By Jamhuri