Fanya kazi kwa bidii

 

Nyuma ya ndoto nyingi zilizofanikiwa kuna kufanya kazi kwa bidii. Kama haupo tayari kufanya kazi kwa juhudi sahau kabisa ndoto zako kutimia.

Ukimuuliza kila mtu aliyefanya makubwa katika dunia hii, sentesi “fanya kazi kwa bidii” huwa haikosi kinywani mwake. Uvivu siku zote huchochea umaskini. Mvivu hapendwi.

Jambo jema na la kufurahisha kuhusu bidii ni kwamba haijawahi kumwangusha mtu yeyote.

Kadri unavyoweka juhudi kubwa ndivyo unavyopata matokeo makubwa. Mbuzi hula kwa kadri ya urefu wa kamba yake, hivyo hivyo mtu hufanikiwa kwa kadri ya juhudi anayoiweka.

Jeshi la Maji la Marekani lina msemo wa, “Hakuna aliyewahi kuzama kwenye jasho.” Hapo walitaka kutuonesha kwamba tusiwe waoga na tuendelee kufanya kazi kwa bidii. Nao watu wa Scotland wanasema, “Kazi inayofanywa kwa bidii, haijawahi kumuua mtu.”

Ukifanya kazi kwa bidii utafanikiwa bila kujali umetoka wapi, ulizaliwa na nani, una rangi gani. Naunga mkono maneno ya Baraka Obama aliyewahi kuwa Rais wa Marekani aliyesema, “Kama ukifanya kazi kwa bidii na kutimiza majukumu yako, unaweza kuwa mbele, bila kujali unatoka wapi, unafananaje au unampenda nani.”

Unapofanya kazi kwa bidii, watu siku zote watajitahidi kukurudisha nyuma. Hakuna anayependa ufanikiwe zaidi yake, kama wapo ni wachache, hivyo utasikia maneno mengi ya kukurudisha nyuma. Endelea kuchapa kazi.

Fanya kazi zako bila kusikiliza wengine wanataka nini. Dunia ya leo ina kelele nyingi, huwezi kumfurahisha kila mtu.

Usifanye kazi kama mashindano. Shindana na wewe kwanza. Mtu pekee unayepaswa kushindananaye kila siku ni yule unayemwona pale unapotazama kwenye kioo.

Siku zote tanguliza upendo kwenye kazi unayoifanya. Unapopenda unachokifanya si rahisi kukichoka na kukikatia tamaa. “Kazi bila upendo ni utumwa,” alisema Mama Teresa wa Calcutta.

Unapofanya kazi kwa bidii usilazimishe kila mtu ajue kile unachokifanya. Jijifunze kufanya mambo yako kimya kimya, itakusaidia na utaepusha vikwazo vingi. “Fanya kazi kwa bidii kwa ukimya, yaache mafanikio yapige kelele,” anasisitiza Frank Ocean.

Weka mipango yako sawa. Hatupangi kushindwa tunashindwa kupanga. Katika mipango yako, kufanya kazi kwa bidii uwe mpango mmojawapo. “Mipango huwa ni kitu pekee cha msingi endapo kitawekwa haraka katika kufanya kazi kwa bidii,” anasema Peter Drucker, mwandishi wavitabu na mbobezi katika masuala ya manejimenti.

Usilalamike kwa kufanya kazi kwa bidii na huoni matokeo. Juhudi unazoweka kila uchao kuna siku utakuja kushukuru wakati huu ambako ulikuwa unaona kama kazi bure ilikuwa ikifanyika.

Sarah Prince anasema, “Alama ya mtu anayefanya kazi kwa bidii ni yule anayefanya kazi bila kulalamika.”

Bwana Chris Myler alikuwa fundi seremala mzee. Alihitaji kustaafu kazi hiyo. Aliajiriwa katika kampuni ya ujenzi. Angekosa mshahara kila wiki, lakini alitaka kustaafu.

Alitaka kuacha kazi ili apate muda wa kupumzika na kuwa karibu na familia yake kwa muda mrefu.

Alimwambia bosi wake alihitaji kustaafu kazi. Bosi yake kusikia hivyo alihuzunika sana kuona fundi bora wa kampuni yake akiondoka kazini. Bosi huyo akalipokea ombi hilo kwa mikono miwili, lakini hakuishia hapo, bali alimuomba

Chris amjengee nyumba moja ya mwisho. Fundi akakubali ombi la bosi. Kazi ya ujenzi ikaanza. Kwa sababu ilikuwa kazi yake ya mwisho alifanya kazi kwa nusu moyo. Hakuweka juhudi zozote. Muda wote alikuwa akisema, “Kwaheri.”

Wakati wa ujenzi hakujali mchanganyiko mzuri wa saruji na mchanga. Hakujali rangi aliyopaka kutani, milango ilitengenezwa kwa mbao mbovu, bati akaweka za bei ya chini. Hakutaka kuwekabwawa la kuogelea kama alivyozoea kujenga nyumba nyingine. Samani alizoweka ndani zilikuwa za hadhi ya chini, zikitengenezwa kwa mbao mbovu pia.

Baada ya ujenzi kukamilika, mwajiri alimuita fundi seremala ofisini kwake na kumkabidhi funguo za nyumba mpya iliyojengwa akisema, “Hii ni zawadi yangu kwako kwa kazi nzuri uliyoifanyia kampuni yangu kwa kipindi cha miaka zaidi ya 15.”

Seremala alibaki akiwa amepigwa butwaa. Haya ndiyo maisha yetu ya kila siku. Tunajenga nyumba ambazo baadaye tutakuja kuishi. Nyundo na misumari umevishika wewe, hakikisha siku zijazo unaishi katika nyumba uliyojenga kwa ubora. Fanya kazi kwa bidii. Kuwa na ndoto kubwa.

609 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!