Muda pekee wa kutazama nyuma ni kutazama ni hatua kiasi gani umepiga.

Ingawa Waswahili waliwahi kusema: “Yaliyopita si ndwele, tugange yajayo.” Si kila muda ni wa kusahau yaliyopita.

Nyakati zilizopita zina mafunzo tunayoweza kukutana nayo kwenye wakati ujao.

Kosa si kosa kama halijarudiwa. Ukirudia kosa maana yake haukujifunza muda ule ulipoanguka.

Yakobo baba yake Yusufu alisahau alipotoka. Siku moja kaka yake Esau ambaye alikuwa mwindaji akiwa ametoka kuwinda bila kuambulia kitu alirejea nyumbani akiwa amechoka sana. Akakuta Yakobo ametengeneza chakula safi. Akamwomba mdogo wakechakula. Mdogo wake akamwambia: “Kwanza niuzie leo haki ya mzaliwa wa kwanza.”

Esau akajibu: “Tazama, mimi ni karibu kufa, itanifaa nini haki hii ya uzazi?” Yakobo akampa Esau chakula. Kilichofuata ni historia. Yakobo aliweza kuiona kesho, lakini Esau hakuona kesho, hivyo akaona haki ya uzao wa kwanza si kitu. Kilichofuata ni historia.

Wakati Yusufu anamwambia baba yake ndoto yake ya pili, baba yake akamkemea na Kusema: “Ni ndoto gani hii unayoiota? Je, utakuwa kiongozi wetu?” Hayo yalikuwa maneno ya kukatisha tamaa. Yakobo aliweza kuiona kesho yake, lakini hakuweza kuona kesho ya mwanae.

Kilichotokea kwa Yusufu ndicho kinachowatokea watoto katika familia nyingi. Wazazi wengi wamekuwa chanzo cha kuua ndoto za watoto wao.

Kuna watu wengi walikuwa madaktari bingwa, lakini leo ni wanasheria. Kuna watu walikuwa walimu, lakini leo ni wahandisi. Kuna watu walikuwa wakulima bora, lakini leo ni walimu.

Wazazi  wamewafanya watu wengi kufanya kazi zisizo za ndoto zao. Kwa sababu baba ni daktari anamlazimisha mwanae asomee udaktari. Au kwa kuwa kwenye hiyo familia hakuna mhandisi, mtoto analazimishwa kusomea uhandisi eti asafishe nyota ya ukoo.

Kuna watu wengi wapo mahali pasipo pao.

“Mtu ambaye hayupo mahali pake ni kama mfupa ambao umeteguka – anaumia na kuwafanya wengine waumie,” anasema Padri Faustin Kamugisha.

Kuna watu walio na machozi kutokana na kazi wanazofanya. Kadiri ya takwimu za mwaka 1987, Wamarekani asilimia 24.3 hawana furaha kwa sababu walichagua kazi ambazo hazikupaswa kuwa zao. Idadi hiyo imepanda hadi asilimia 85 mwaka 2017.

Tunalalamika kila siku kuongezeka kwa ukosefu wa ajira, lakini chanzo kikubwa ni watu kusomea mambo wasiyoyapenda. Unaweza kumwambia mtu ajiajiri, lakini hakuna mtu aliyejiajiri na anafanya kitu asichokipenda.

Aliko Dangote ni mfanyabiashara maarufu, lakini alipenda biashara akiwa bado mdogo.

Phil Knight alipenda viatu vya kufanyia mazoezi ya kukimbia, hiyo ikampa msukumo wa kuanzisha Kampuni ya viatu vya Nike. Mark Zuckerberg alipenda mambo ya mitandao, ikamsababishia kutengeneza mtandao wa facebook.

Bill Gates na rafiki yake, Paul Allen, walipenda sana kompyuta tangu wakiwa wadogo, ikawafanya waanzishe Kampuni ya Microsoft. Mbwana Samatta alipenda mpira wa miguu. Usain Bolt alipenda riadha.

Kuna haja kubwa kwa wazazi kuzipa vipaumbele ndoto za watoto wao kuliko kuwalazimisha kufanya mambo wasiyoyapenda. Tukiweza kuwapa motisha watoto wenye ndoto kubwa kuanzia nyumbani ni faraja kubwa kwa mtoto. Wajerumani wanasema: “Upendo huanzia nyumbani.”

Kukosa furaha maishani ni msalaba usiobebeka. Tusiwatwishe watoto wetu misalaba wasiyoweza kuibeba kwa kuwachagulia kazi wasizozipenda. “Hakuna kinachotokea mpaka tukiote kwanza,” anasema Carl Sandburg. Mwanao kama ana ndoto fulani ni ishara kuwa itakuwa ya kweli.

Naunga mkono hoja ya Walter Disney aliyewahi kusema: “Kama unaweza kukiota, unaweza kukifanya.”

Baada ya Mama Teresa kufanikiwa na kuwa maarufu kwa sababu aliwahudumia wagonjwa na watu waliokuwa wakifa katika mitaa ya Calcutta, India; watu ambao aliwahamasisha walimtafuta. Muda mrefu walisema: “Ooh Mama Teresa! Nataka kufanya unachokifanya! Nataka kuacha kila kitu ninachomiliki na kujiunga na kazi yako!”

Muda wote alikuwa akiwajibu maneno haya matatu: “Tafuta Calcutta yako.” Kwa lugha rahisi tunaweza kusema: “Fuata ndoto yako.”

Tunahitaji wazazi wenye moyo na ujasiri kama wa Mama Teresa wa Calcutta ambao watakuwa na uwezo wa kuwaambia watoto wao: “Fuata ndoto yako mwanangu.”

Watu waliofuata ndoto zao ndio walioibadili dunia. Je, unataka kuibadili dunia pia? Jibu ni moja, fuata ndoto yako.

By Jamhuri