Ndoto inahitaji uthubutu

“Ili uwe mtu ambaye hujawahi kuwa lazima ufanye mambo ambayo hujawahi kuyafanya,” anasema mhamasishaji Les Brown. Kufanya mambo ambayo hujawahi kufanya ni kuthubutu.

Kamusi ya Kiswahi Sanifu (TUKI) imetafsiri neno “thubutu” kwamba ni kuwa na ujasiri wa kufanya jambo.

Maisha yanahitaji watu jasiri, ndoto hutimizwa na watu wanaothubutu.

Kulikuwa na mbegu mbili zilizokuwa zimekaribiana ardhini. Siku moja mbegu ya kwanza iliiambia mbegu nyingine kuwa inataka kuotesha mizizi chini kabisa katika umbali mrefu ifikie hata miamba migumu iliyoko ardhini.

Haikuishia hapo tu, ikasema inataka kuchipuka iote matawi na iufurahie mwanga wa jua. Siku zikapita, kile mbegu ya kwanza ilichokitaka kikatokea.

Ile mbegu ya pili ikasema, “Nikiotesha mizizi yangu umbali mrefu wadudu na nyoka wataitafuna mizizi yangu.” Ikasema, “Tena siwezi kuchipuka, itakuaje nikichipuka mtoto akaja na kuninyofoa ardhini maisha yangu yakaishia hapo?” Mbegu hiyo ikaamua isifanye chochote, ibaki hivyo hivyo ardhini.

Siku moja kuku akiwa anachakura katika maeneo, ile mbegu ya pili ilipopandwa akaiona, akaila; ukawa mwisho wake.

Maisha ya mtu mwenye ndoto hayatakiwi kufanana na maisha ya mbegu ya pili. Mbegu ya pili inakosa ujasiri wa kusema ‘ninaweza’ na kutanguliza ‘haiwezekani’. Mbegu ya pili haipo tayari kufanya lolote.

Huwezi kufika unakokwenda kama hutokubali kutoka ulipo -kama hutakubali kupiga hatua ya ziada.

Ukikwepa kutafuta yale unayoyataka yale usiyoyataka yatakuja kwa spidi kwenye maisha yako. Amua leo kutafuta yale unayoyataka, fanana na mbegu ya kwanza.

Kanuni ya asili ya uvutano inasema kwamba, “Chochote akili inachokiwazia inaweza kukileta katika uhalisia.” Jenga tabia ya kuweka kichwani mwako mambo unayoyataka kwenye akili yako na anza kuthubutu kuyafanyia kazi.

Anashinda yule anayethubutu, bila uthubutu mambo mengi yasingewezekana. Watu wengi unaowaona wametimiza ndoto kubwa katika dunia hii ni kwamba kuna mahali walifika wakaweka ujasiri mbele na kutupilia nyuma uoga wao.

Rose Mhando aliwahi kuimba akisema, “Uoga wako ndio umasikini wako.” Watu wengi wameshindwa kufikia mafanikio wanayotaka kwa sababu ya kuuishi uoga wao. Kuthubutu ni bora kuliko kuwa mwoga.

Hakuna aliyepata zawadi maishani kwa kuuishi uoga wake, lakini kuna mamia na maelfu ya watu waliopata zawadi kwa kuwa na roho ya uthubutu na kufanya mambo makubwa.

Kabla mwaka huu haujaisha tafuta jambo moja au mawili ambayo kila ukijaribu kuyafanya unaingiwa hofu- anza kuyafanya sasa. Kuna muujiza mkubwa umejificha ndani ya kile unachoogopa kukifanya.

Mara nyingi nimegundua mambo mengi niliyokuwa naogopa kuyafanya yalikuwa yamebeba vitu vikubwa ndani yangu. Kuna wakati nilifika nikasema liwalo na liwe, nitafanya, baadaye nilijishukuru mwenyewe kwa kuwa jasiri na kusonga mbele.

Nakubaliana na Sarah Parish aliyesema, “Kuishi na woga hutufanya tuache kuthubutu, na kama huwezi kwenda kwenye tawi, hutawahi kupata tunda bora.” Naye Esme Bianco anasema, “Huwezi kufika popote maishani kama huthubutu.”

Karibu kila kitu kwenye maisha yetu kinahitaji uthubutu. Ukitaka kufanya biashara lazima uthubutu ndiyo maana Adena Friedman alisema, “Huwezi kufanikiwa kwenye biashara kama huthubutu. Ni rahisi hivyo.”

Siyo tu kwenye biashara, hata kama una kipaji lazima uonyeshe uthubutu. Bila kuthubutu kipaji chako kitakufa, bila kuthubutu kipaji chako hakiwezi kukufikisha kwenye mafanikio unayotaka. Mwanamuziki Drake anasema, “Nahisi kwamba unapojali kuhusu muziki kuthubutu ni kitu unachotakiwa kukifanya ili mambo yaendelee kusonga mbele.”

Kuna watu waliamini kuwa hakuna binadamu anayeweza kukimbia maili 26.22 (Kilomita 42) chini ya saa mbili. Oktoba 12, 2019 huko Vienna, Eliud Kipchoge (34), raia wa Kenya aliithibitishia dunia kuwa anaweza kufanya jambo hilo. Alikimbia umbali huo akitumia saa 1:59:40.

Eliud Kipchoge anatufundisha kwamba ukithubutu unaweza. Kipchoge awe motisha kwetu kwamba tunaweza kuzifikia ndoto zetu kama tutakubali kuthubutu.

“Tunaacha alama kwa kuthubutu,” ni maneno ya Shenae Grimes. Usikubali kuondoka duniani bila

kuacha kitu ambacho dunia itabaki ikishangilia miaka nenda rudi kwamba kililetwa na mchango wako.

Hatukuja duniani kuzurura. Tulikuja kuacha alama. Kila siku kuthubutu kwako kuwe kama kupiga mswaki, huhitaji mtu wa kukukumbusha. Wanafanikiwa wale wanaothubutu, si wale wanaoishi katika maneno yao ya faraja.

By Jamhuri