‘Tumezaliwa kwa ajili ya wengine’

 

Hapo zamani za kale kulikuwa na mkulima aliyenunua vibuyu viwili vya kutekea maji. Baadaye alikuja kugundua kwamba kibuyu kimoja kilikuwa kimetoboka sehemu ya chini.

Mkulima huyo alizoea kutekea vibuyu hivyo maji kutoka mtoni na kuyapeleka mjini kwake. Kibuyu kilichokuwa kimetoboka kilimwaga maji njia nzima, hivyo kilijiona hakifai.

Kibuyu kingine kilijigamba na kujisifu huku kikikitania kile kibuyu kingine muda ule kilipokuwa kikimwaga maji njiani.

Siku moja kibuyu kile kilichotoboka kilishindwa kuyatunza yale machungu moyoni na kumuomba mkulima akitupilie mbali. Mkulima baada ya kuyasikia mawazo ya kibuyu kile alitabasamu huku akisema: “Umeona barabara ya mji wetu siku za hivi karibuni?”

Walikwenda tena kwenye ile barabara ambayo wanapita karibu kila siku na kuona maua mazuri. “Unaona? Maji ambayo umekuwa ukimwaga hadi sasa hivi yamekuza mimea hiyo.”

Kuna muda tunaona tumebeba mabaya mengi na kubaki katika hali za masikitiko, hatupaswi kuwa katika hali hiyo kwani tunaweza kutoa msaada kwa watu wengine kwa kutumia maji tunayomwaga njiani. Furahi. Maisha ni mazuri.

Mshumaa haupotezi chochote unapowasha mishumaa mingine, bali unasaidia kuongeza mwanga katika chumba ulimowashiwa. Kutoa ni moyo, usambe ni utajiri. Kutoa ni moyo, vidole huachia. Ili ndoto zako zitimie, unahitaji kuwa msaada kwa watu wengine.

Wasaidie wengine kutimiza ndoto zao nawe ndoto zako zitakuwa za kweli.

Yusufu akiwa gerezani, alifungwa na wafungwa wawili, mmoja alikuwa mnyweshaji wa mfalme wa Misri na mwokaji wake. Wakiwa gerezani waliota kila mtu ndoto yake katika usiku mmoja. Ilipofika asubuhi wote waliamka wakiwa wamefadhaika.

Yusufu akawauliza wale wafungwa, kwanini wamefadhaika vile. Wakamwambia wameota ndoto na hawajui maana zake. Yusufu akawatafsiria ndoto zao kila mmoja na ndoto yake. Ilipofika siku ya kuzaliwa kwake Farao, akamwachia mkuu wa wanyweshaji na kumuua yule mkuu wa waokaji, kama Yusufu alivyowatafsiria. Mkuu wa wanyweshaji akamsahau Yusufu.

Ikapita miaka miwili Farao akaota ndoto mbili, na hakuna aliyeweza kuzitafsiri ndoto zile katika nchi yote ya Misri, kuanzia kwa waganga hadi kwa watu wote wenye hekima waliokuwapo wakati ule. Muda huu mkuu wa wanyweshaji akamkumbuka

Yusufu, akamwambia Farao habari za Yusufu.

Basi, Farao akawatuma watu wakamfuate kule gerezani alikokuwa, akanyoa, akabadili nguo zake na kuingia kwa Farao. Farao akamhadithia Yusufu zile ndoto zake, Yusufu akazitafsiri vema kabisa. Farao akatokea kumpenda na kusema: “Tupate wapi mtu kama huyu mwenye roho ya Mungu ndani yake?” Siku hiyo muujiza ukatokea, Yusufu akafanywa kuwa waziri mkuu wa nchi ya Misri.

Inawezekana fursa ya ndoto yako ikafunguka pale unapowasaidia watu wanaokuzunguka.

Yusufu alikuwa tayari kuwasaidia wenzake ndipo ndoto zake zilipokuwa kweli. “Hakuna zoezi zuri sana kwa moyo kama kufika chini na kuwainua wengine juu,” ni maneno ya John Holmes.

“Haujaishi leo kama haujafanya kitu kwa mtu ambaye hawezi kukulipa,” alisema John Buyan, naye Marcus Tullius Cicero alisema maneno ya Kilatini, “Non nobis solum nati sumus,” akimaanisha: “Hatukuzaliwa kwa ajili yetu.” Tumezaliwa kwa ajili ya wengine.

Maisha yenye furaha ni maisha ya kujitoa kwa ajili ya watu wengine. Saidia watu wengine na usitake wakulipe, tenda wema nenda zako. “Na mtu atakayekulazimisha

mwendo wa maili moja, nenda naye mbili.” (Mathayo 5:41).

Zig Ziglar anasema: “Utapata chochote unachokitaka kwa kuwasaidia wengine kupata wanachohitaji.”

“Ingekuwaje kama kila mtu angejitoa na kuwa mzuri kila siku? Fikiria ofisini, shuleni na nyumbani,” anaongezea Joel Osteen, mchungaji na mwandishi. Ni

kweli dunia ingekuwa mahali pa furaha kama kila mtu angejitoa kwa ajili ya watu wengine. Kila siku hakikisha kuna kitu umefanya kuwasaidia watu wengine.

Ukitaka furaha ya saa moja, lala. Ukitaka furaha ya siku moja, nenda kavue samaki, ukitaka furaha ya mwezi mmoja, oa au olewa. Ukitaka furaha ya mwaka mmoja, shinda bahati nasibu. Ukitaka furaha ya maisha yako yote, jitoe kwa ajili ya wengine, uwe mwema na mzuri kwa watu wengine. Wasaidie na ishi na watu vizuri hata kama hawana kitu, maana siku moja watakuwa na kitu.

987 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!