Dodoma. Benki ya NMB jana ilikabidhi gawio la Shilingi Bilioni 10.17 kwa
serikali kutokana na faida iliyopatikana mwaka 2017.
Pesa hizo ni sehemu ya jumla ya Shilingi Bilioni 32 ambazo ziliidhinishwa
na mkutano mkuu wa mwaka wa wanahisa wa Benki ya NMB uliofanyika
hivi karibuni Jijini Dar es Salaam.
Katika mkutano huo, wanahisa waliidhinisha kutolewa kwa gawio la jumla
ya Shilingi Bilioni 32 baada ya NMB kupata faida ya baada ya kodi ya
Shilingi Bilioni 93.3 kwa mwaka 2017.
Akizungumza muda mfupi kabla ya kukabidhi mfano wa hundi ya Shilingi
Bilioni 10.17 kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango,
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB, Bi. Ineke Bussemaker alisema
benki yake imejikita katika kuhakikisha kuwa Watanzania wengi zaidi –
hususani wakulima – wanapata huduma zakibenki popote pale walipo.
Alisema mbali na gawio la Shilingi Bilioni 10.17, NMB pia ni miongoni mwa
walipa kodi wakubwa nchini, ikiwa imelipa jumla ya Shilingi Bilioni 127
kama kodi mbali mbali za serikali kwa mwaka 2017 pekee.
“Pamoja na hayo, tunatenga asimilia moja ya faida yetu na kuipeleka katika
kuboresha huduma zakijamii ambapo mwaka jana pekee tulinunua na
kusambaza jumla ya madawati 6,000,” alisema Bi. Bussemaker.
Takwimu zinaonyesha kuwa ni asilimia 17 tu ya Watanzania watu wazima
ambao humiliki akaunti katika benki za biashara.
Kutokana na hali hiyo, NMB imeongeza juhudi za kuhamasisha wakulima
wafungue akaunti ambapo kwa mwaka jana pekee, jumla ya akaunti
300,000 zilifunguliwa na kuiwezesha benki kuongeza idadi ya wateja
kufikia jumla ya milioni 2.7.
Akizungumza kabla ya kukabidhiwa mfano wa hundi yenye thamani ya
Shilingi Bilioni 10.17, Dk Mpango aliishukuru NMB kwa kuendelea kupata
faida licha ya kukiri kuwa mwaka jana (2017) ulikuwa na changamoto
nyingi kwa sekta ya fedha.

“Mwaka 2017 haukuwa mzuri kwa sekta ya fedha ila ninayo furaha kujua
kwamba NMB iliweza kupata faida na leo wanatoa gawio kwa Watanzania
maskini…Hii inadhihilisha ukweli kwamba NMB inao uongozi na usimamizi
madhubuti katika utoaji wa huduma zake,” alisema Dk Mpango.
Aliuhakikishia uongozi wa NMB kuwa gawio hilo litatumika kwa malengo
yaliyokusudiwa huku akitoa rai kwa kampuni nyingine zote ambazo kuna
hisa za serikali kuiga mfano wa NMB na kuanza kutoa gawio.
Benki ya NMB ina jumla ya matawi 220 nchini. Kupitia NMB Wakala,
huduma zake pia hupatikana katika vituo 6,000 nchini kote huku ikiwa na
lengo la kufikisha idadi ya mawakala 10,000 ifikapo mwisho wa mwaka
huu.

1480 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!