Benki ya NMB imekwisha kutoa kiasi cha zaidi ya Sh milioni 570 hadi sasa kati ya Sh bilioni 1 ilizotenga kama uwajibikaji wake kwa jamii kwa mwaka huu wa 2019.

Kiasi hicho kimetumika zaidi kusaidia miradi mbalimbali ya kijamii kama elimu, afya na kusaidia majanga mbalimbali yanayoipata nchi, ikiwa ni utaratibu wa benki wa kila mwaka kutenga asilimia moja ya faida yake kusaidia miradi mbalimbali ya kijamii.

Utaratibu huo uliendelea tena mjini hapa juzi ambapo NMB imetoa kiasi cha madawati 607 yenye thamani ya Sh milioni 55 kwa shule tisa za msingi katika Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza na mbili Wilaya ya Nzega.

Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kukabidhi sehemu ya madawati hayo iliyofanyika katika Shule ya Msingi Budushi wilayani hapa juzi, Kaimu Meneja wa Kanda ya Ziwa wa NMB, Amos Mubusi, alisema mchango huo ni katika kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano.

“Ingawa Serikali ya Awamu ya Tano inafanya makubwa, sisi kama wadau tuna wajibu wa kuunga mkono juhudi hizi za maendeleo kwa kusaidia jamii iliyoifanya NMB kufikia hapa ilipo kama benki kubwa kuliko zote hapa nchini.

“Ni kwa kutambua juhudi hizo za serikali, NMB iliamua kuyafanyia kazi haraka maombi iliyopokea kutoka shule tisa za msingi wilayani Misungwi, hivyo kukabidhi madawati hayo,” alisema Mubusi.

Alizitaja shule zitakazonufaika na msaada huo kuwa ni Mhalo, Sangu, Mwankulwe, Luhala, Budushi, Bumyengeja, Mwabaratulu, Kabale na Shule ya Msingi Ng’wambisu zitakazopata kati ya madawati 55 na 58 kila moja.

Akizungumza kabla ya kupokea madawati hayo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kwimba, Ally Nyakia aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo, Senyi Ngaga, amesema sekta ya elimu inatakiwa kupewa kipaumbele wakati serikali ikipiga mbio kuelekea uchumi wa kati.

Amesema wadau kama NMB ni muhimu sana kuelekea azima hiyo ya Serikali ya Awamu ya Tano na kuomba wadau wengine wa maendeleo kuiga mfano wa benki hiyo katika kuunga mkono jitihada mbalimbali za maendeleo.

“Bila kupiga hatua kubwa katika sekta ya elimu hatuwezi kama taifa kufikia kikamilifu safari ya kuelekea kwenye uchumi wa kati wa viwanda na maendeleo ya sayansi na teknolojia kwa hiyo nichukue fursa hii kuishukuru NMB kwa msaada huu,” amesema Nyakia.

Amewapa changamoto watumishi mbalimbali wa serikali katika wilaya yake kuiunga mkono Benki ya NMB kwa kufungua akaunti na kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo badala ya kutumia huduma za taasisi nyingine za kifedha zinazotumia mwanya huo kuwadhalilisha watumishi hao.

Aliishauri pia NMB kufungua tawi katika mji mdogo wa Sumve ili kuwapungumzia usumbufu watumishi na wananchi kusafiri kwenda Ngudu – mwendo wa kama kilometa 40 hivi kufuata huduma mbalimbali za kibenki.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Godfrey Ngupula, alitoa shukrani kwa benki hiyo baada ya kupokea madawati 100 kwa ajili ya Shule ya Msingi Nata na ya Sekondari Undumo zilizopo wilayani Nzega, akisema msaada huo utachangia kuongeza ubora wa mazingira ya kusoma kwa wanafunzi kwenye shule hizo mbili.

Mapema, Afisa Elimu (Ufundi) wa Wilaya ya Kwimba, Vedastus Nyambalije, alisema wilaya ina jumla ya wanafunzi wapatao 118,026 katika shule za msingi zipatazo 151 za umma na walimu 1,621 na kwamba idadi hiyo ni sawa na mahitaji ya madawati 33,514.

Amesema kabla ya ufadhili wa NMB, Wilaya ya Kwimba ilikuwa na madawati 27,727, hivyo kuwa na upungufu wa madawati 6,978 na kwamba kwa msaada huo sasa upungufu umebaki madawati 5,280 tu.

Sambamba na madawati, amesema wilaya bado ina upungufu mkubwa kwenye maeneo mengine kama vile nyumba za walimu, vyumba vya madarasa, ujenzi wa matundu ya vyoo na samani nyingine.

By Jamhuri