*Wananchi, Serikali wahadharishwa

*Machafuko ya kiuchumi yatatokea

*Yasema ikiamuriwa ina fedha za kulipa

Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) halijachoka kuwaasa Watanzania na Serikali juu ya athari za kutekelezwa kisheria kwa fao la kujitoa.

Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk. Ramadhan Dau, amesema kuna athari kubwa za kiuchumi na kijamii kwa uamuzi huo ambao sasa unashabikiwa na Watanzania wengi.

 

“Tunasisitiza watu wasijitoe, kama Serikali ikiamua, wakipitisha sheria, tutatekeleza. Wakilazimisha kujitoa, sisi tutakuwa hatuna lawama. Tutakuwa tumetekeleza wajibu wetu wa kuonya na kushauri, mbele ya safari tutasema, tulisema,” anasema Dk. Dau alipozungumza na wahariri wa vyombo vya habari mjini Zanzibar, mwishoni mwa wiki.


Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NSSF, Cricentus Magori, amesema kuwa Shirika hilo limeshindwa kesi mahakamani na wafanyakazi wa Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (TAZARA) kutokana kuwalipa fao la kujitoa ambalo halipo kisheria.


“Wale wafanyakazi waliamua walipwe fao la kujitoa, wakapokea fedha zao, wakazitumia na kuzimaliza. Wenzao waliokataa kuchukua hilo fao wao wameendelea kuneemeka, kuona hivyo wale waliochukua fao la kujitoa wakatushitaki kwamba hatukuwashauri vizuri ndiyo maana walichukua fedha na maisha kuwawia magumu. Wameshinda kesi kwa sababu hatuna sheria ya kulipa fao la kujitoa,” amesema.


Magori alitumia muda mrefu kueleza faida za kuacha kuchukua fao la kujitoa, akisema kama fedha za mwanachama hazitamnufaisha mwanachama, basi zitawasaidia warithi wake.

“Lakini hapa ikumbukwe kuwa kuna mambo matatu muhimu-uzee, ulemavu na kifo. Kwa mfanyakazi na binadamu hivyo vitu vipo. Havikwepeki, unaweza kukwepa ulemavu lakini si uzee au kifo.


“Leo unachangia, kwa mfano Sh 20,000 kwa mwezi, lakini unapostaafu unalipwa Sh 80,000 kwa mwezi. Hii ni faida kubwa,” amesema.

 

Tofauti na uvumi kwamba Mifuko ya Jamii, ikiwamo NSSF inakabiliwa na hali mbaya kifedha, Magori amesema hali ya Shirika ni nzuri, na kwamba kwa uamuzi wa kulipa fao la kujitoa, kama itaamuriwa na wanachama, Serikali na Bunge, hilo itakuwa nafuu kwao kwani hawatakuwa na mzigo wa kuwalipa watu wengi pensheni.


“Tunabeba mzigo mkubwa kulipa pensheni ya uzeeni kuliko kulipa fao la kujitoa. Tunacholilia hapa ni kupewa mzigo mkubwa wa kulipa pensheni, tofauti na watu wanavyodhani kuwa tunataka unafuu,” amesisitiza.


Kwa upande wake, Dk. Dau amesema, “Sasa tuchukue tu scenario ya kwanza Serikali iseme aah si mlikuwa mnafanya kazi na mkaamua kuchukua mafao yenu, sisi tumekuwekeeni utaratibu wa kukusaidieni kustaafu, ulichukua hela zako, shauri yako. Hiyo ‘scenario’ kwamba Serikali haiwajibiki, hii ni matatizo yako mwenyewe.


“Scenario ya pili, Serikali iseme hapana, hawa watu ni Watanzania, idadi yao inaongezeka, ilianza laki tano, milioni, milioni mbili, lazima Serikali iingilie kwa kufanya moja kati ya mawili, ama Serikali iawaache kwa sababu walishachukua hela zao, au Serikali ichukue jukumu la kuwahudumia. Uamuzi wote huo una madhara. Serikali ikiamua kuchukua hatua itabidi itafute utaratibu wa kuwaunga mkono hawa.


“Lakini Serikali kama Serikali, haina pesa. Chanzo cha mapato ya Serikali ni mimi na wewe (wananchi), kitakachotokea ni kwamba Serikali itasaidia wale watu kwa sababu haitakuwa tayari kuwaacha, lakini kimsingi atakayekuwa anawasaidia wale watu ni mimi na wewe. Tutapaswa kuwalipa ili kuwahudumia watu ambao walitumia fedha zao. Hiyo ndiyo maana yake.

“Serikali iliamua kuchukua hatua za kuwajibika lazima walipa kodi waongeze uwezo wa kuwahudumia wale Watanzania ambao wako nje ya pensheni.


“Uamuzi wa pili, Serikali iseme potelea mbali. Walichukua fedha zao, sasa shauri yao. Watakuwa laki moja, idadi itaongezeka, laki tatu, milioni, milioni mbili, hatimaye itafikia mahala utakuta sisi ambao ni wananchi tunaowajibika, tutashindwa kufurahia maisha mazuri. Hapa kutakuwa na tatizo kubwa. Watu wataingia kwenye machafuko ya kijamii. Watasema hawa washenzi mafisadi wanaendesha magari makubwa makubwa. Matokeo yake unakuwa na matatizo katika nchi.


“Ama tutapata matatizo kwa kulipa kodi zaidi, au tutapata matatizo kwa kuingia kwenye machafuko ya kijamii kati ya walio nacho na wasio nacho. Inawezekana ikawa miaka 10, miaka 20 au miaka 30 ijayo lakini kwa vyovyote vile tutaingia kwenye matatizo.


“Sasa ni kuamua, ama tuwaruhusu watu wachukue fedha zao kwa kudhani hili si tatizo letu…. ama Serikali iwatelekeze, baadaye waingie mitaani kwa kupambana na wanaowaita mafisadi kumbe tatizo ni wao wenyewe hawakupanga maisha yao vizuri.


“Kwa hiyo mjadala ulipoibuka (wa fao la kujitoa) watu waliuchukulia juu juu tu. Lazima tuuangalie kwa uangalifu zaidi. Februari (2013) tutakuwa na mkutano wetu wa wanachama Arusha. Tumeandaa hili suala kama mada, na tutalifafanua kwa takwimu… tutaeleza namna gani na kwa mwaka gani Serikali itapaswa kuingilia, na hiyo itagharimu kiasi gani kwenye bajeti, na hiyo itakuwa na maana gani kwa maana ya kodi.


“Tutatahadharisha kuwa tukiacha hivi hivi, mwisho wa siku ni mimi na wewe tutakaolipa. Tutawaita watu wanaounga mkono kuwapo fao la kujitoea, na wale wanaopinga kuwapo kwa fao hilo. Wanachama watakuwapo, watatoa uamuzi. Kama wanachama wakiamua kuwa ni jambo zuri kwa fao la kujitoa, tutalipa, lakini tuna wajibu wa kuwaeleza watunga sera hatari iliyopo mbele yetu.”


Wabunge wengi, ama kwa kujua, au kutojua, wameshabikia utaratibu wa kuwapo sheria ya kuruhusu fao la kujitoa.

By Jamhuri