Kati ya watu wagumu kuwajadili hapa duniani ni Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Ni kwa sababu ya wingi na ukubwa wa mambo makubwa aliyoyashughulikia kabla ya urais wake na baada ya urais, uliodumu zaidi kidogo ya miongo miwili.


Wakati Nyerere anafariki dunia kutokana na kansa ya damu akiwa katika Hospitali ya Mtakatifu Tomaso mjini London, Oktoba 14, 1999, alikuwa amedumu katika siasa kwa takriban miaka 45. Huu ni muda mrefu na ulikuwa na mengi – iwe mafanikio au mitikisiko. Alifariki akiwa na umri wa miaka 77.


Nyerere alianza siasa Julai 7, 1954 alipolichukua jukumu la kuongoza harakati za Uhuru wa Tanganyika kupitia TANU; akawa Waziri Kiongozi Septemba 2, 1960 hadi Mei 1, 1961 alipobadilishwa kuwa Waziri Mkuu hadi Januari 22, 1962. Alikuwa Rais wa Tanganyika Desemba 9, 1962 hadi Aprili 26, 1964 alipokuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania.


Nyerere alistaafu urais wa Tanzania mwaka 1985 lakini akabaki kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) hadi mwaka 1990. Baada ya hapo aliendelea kutamba katika duru za kimataifa akiitwa huku na kule kufanya mengi makubwa kama kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Nchi za Kusini na kuwa Mpatanishi wa Mgogoro wa Burundi.


Kuna jambo moja la uhakika kuhusu urithi wa uongozi wa Nyerere. Jambo hilo ni uzalendo wa dhati ulioijengea Tanzania sifa madhubuti kama Taifa, na mapenzi yake kwa nchi na watu wake katika muda wake. Hii ndiyo sifa kuu ya kiongozi yeyote mahali popote duniani.

 

Ni kweli, wapo wafitini wanaotaka kufanya makosa yake ya kibinadamu kuwa nongwa, lakini kamwe hawataweza kuubadili ukweli kwamba Nyerere aliwatumikia Watanzania na Tanzania kwa moyo wa dhati na hata kuvuka mipaka na kuwa mtumishi wa Afrika na ubinadamu mzima.


Rais Yoweri Museveni wa Uganda, kiongozi wa nje aliyehudhuria mazishi ya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam na maziko ya Nyerere kijijini Butiama, na pia mmoja wa viongozi wengi wa Afrika waliokulia ama kupitia Tanzania, husema waziwazi bila kuuma maneno: “Nyerere alikuwa mtu mkuu zaidi kati ya watu weusi waliopata kuishi hapa duniani.”


Ili kuthibitisha kwamba Nyerere hakuwa kiongozi wa ujanja ujanja bali mtu wa kazi, ama Mfalme-Mwanafalsafa kama walivyokuwa wakisema Wayuyani wa kale, ni heri tukapitia baadhi ya sifa alizomwagiwa na walimwengu kwa sababu za kwetu tunazisikia kila uchao.

HESHIMA KABLA YA KIFO

Nchini Marekani kuna vyuo vikuu vitatu vilivyowahi kumtunukia Nyerere shahada za heshima ya udaktari wa falsafa ambavyo ni Duquesne, Howard na Lincoln. Nchini Uingereza Chuo Kikuu cha Edinburgh alichosomea kilifanya hivyo pia, na hali kadhalika Chuo Kikuu cha Toronto nchini Kanada.


Barani Asia, Nyerere alipewa heshima hiyo ya udaktari wa falsafa na Chuo Kikuu cha Ufilipino pamoja na Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru cha India. Huko Amerika ya Kati, nchini Kuba, Chuo Kikuu cha Havana hakikubaki nyuma kwenye kumtunuku Nyerere shahada hiyo ambayo msingi wake mkuu ni kuheshimika kwa utendaji, akili na uadilifu.

 

Barani Afrika ndiko alikopata shahada nyingi zaidi za heshima za udaktari wa falsafa ukianzia na Chuo Kikuu cha Cairo nchini Misri, Chuo Kikuu cha Nigeria, Chuo Kikuu cha Ibadan nchini Nigeria pia, Chuo Kikuu cha Liberia, Chuo Kikuu cha Taifa cha Lesotho, na Chuo Kikuu cha Fort Hare cha Afrika Kusini. Nchini Tanzania Nyerere amewahi kutunukiwa heshima hiyo na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na pia Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine.


Mbali ya shahada hizi, itakumbukwa pia Januari 26, 1996 Nyerere alikuwa mtu wa kwanza kupewa Tuzo ya Kimataifa ya Amani ya Mahatma Gandhi ya mwaka 1995 iliyotolewa na Serikali ya India. Nyerere aliwashangaza viongozi wa India siku hiyo aliposema kwamba hakustahili kupewa Tuzo ya Gandhi kwa sababu yeye alishiriki kwenye mapambano ya bunduki ya kuwang’oa wakoloni barani Afrika.


Ilibidi watu kama Nelson Mandela kusubiri hadi mwaka 2000 kuipata tuzo hii, na baadaye Askofu Desmond Tutu wa Afrika mwaka 2005. Huko huko nchini India Nyerere pia aliwahi kutunukiwa Tuzo ya Nehru ya Ufahamu wa Masuala ya Kimataifa mwaka 1976.


Tuzo nyingine ni pamoja na Tuzo ya Dunia ya Tatu mwaka 1982, Medali ya Nansen ya Huduma za Wakimbizi mwaka 1983, na hata baada ya kuacha urais wa Tanzania aliendelea kuheshimiwa wakati mwaka 1987 alitunukiwa Tuzo ya Amani ya Lenin, na Tuzo ya Kimataifa ya Simon Bolivar mwaka 1992.


Hizi ni baadhi tu ya tuzo zinazothibitisha hoja kwamba kiongozi wetu aliheshimika duniani na hivyo Tanzania na Watanzania tuliheshimika kwa Utanzania wetu.

HESHIMA BAADA YA KIFO

Siku dunia ilipotangaziwa kifo chake, Oktoba 14, 1999, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilisimama kwa dakika moja kuomboleza kifo chake, heshima ya nadra kwa viongozi wastaafu. Rais wa Baraza wa wakati huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia, Theo-Ben Gurirab, alitoa hotuba akimwita Nyerere kiongozi aliyeheshimika, mashuhuri, makini na aliyependwa barani Afrika.


Mzee Nelson Madiba Mandela akiwa kwake Afrika Kusini alisema: “Uhuru wa nchi yake (Tanzania), ukombozi wa watu waliokuwa wakionewa, umoja na mapambano dhidi ya ukoloni barani Afrika vilikuwa ndivyo vitu vikuu kwake.” Kwa sababu za kiafya Mandela alishindwa kuja kumzika Nyerere ingawa baadaye alikwenda Butiama kuhani msiba.


Rais wa Marekani aliyekuwa madarakani wakati huo, Bill Clinton, alisema: “Kifo cha Nyerere ni pengo kubwa kwa Tanzania, Afrika na jumuiya ya kimataifa kwa ujumla,” huku Waziri wa Mambo ya Nje wa Clinton, Mama Madeleine Albright, ambaye alihudhuria mazishi, alidokeza: “Mwalimu alikuwa mtu mkubwa kwenye jukwaa la dunia na mzungumzaji mkuu wa nchi zinazoendelea.”


Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair, alimsifia Nyerere kwa kufanikiwa kuzima ukabila nchini Tanzania na kujenga utaifa na kuongeza kwamba: “Kwa sababu ya Mwalimu leo hii Tanzania ni nchi yenye amani ndani yake na nje ya mipaka yake.”


Rais wa Zambia, Frederick Chiluba, alisema: “Waafrika tumeporwa kiongozi wetu mkubwa” wakati Rais Museveni alisema: “Kwa kumuondoa Idi Amin Mwalimu alitupa Waganda fursa mpya ya kuanza upya kulijenga taifa letu.”


Rais wa Benki ya Dunia, James Wolfensohn aliyefahamiana vema na Nyerere, alisema: “Kwa watu waliowahi kuyatumikia maendeleo ya dunia hii, taa moja ya maisha yetu imezimika leo,” na kisha akaongeza: “Nyerere alikuwa mmoja wa mababa wa Afrika ya leo.”


Ni aibu kwamba leo hii, baadhi ya Watanzania wakiwamo viongozi wanakwepa kumwita Nyerere kwa hadhi yake ya heshima – Baba wa Taifa – kwa sababu za kiwendawazimu wakati watu wa mbali wanamwona kama ‘Baba wa Afrika,’ zaidi hata ya Tanzania yetu. Ni ulofa tu wa mawazo!


Profesa maarufu wa siasa nchini Kenya, Anyang’ Nyong’o, naye alisema: “Nyerere aliwapita mbali mno viongozi wenzake wa Afrika katika uadilifu, utendaji, na heshima,” huku msomi mwingine wa Kenya anayeishi Marekani, Profesa Ali Mazrui akisema kwamba Nyerere alikuwa kiongozi pekee wa Afrika aliyebahatika kuwa na vitu vyote viwili muhimu – uadilifu na akili.


Profesa Mazrui alisema kwamba Leopold Sedar Senghor wa Senegal alijaaliwa akili nyingi pengine kuliko viongozi wote wa Afrika, wakati Mandela alijaaliwa uadilifu mkubwa pengine pia kuliko viongozi wote wa Afrika, lakini Nyerere yeye alijaaliwa vyote.

 

Vyombo vya habari vya Uingereza, nchi ambayo aliidhalilisha wakati alipovunja nayo uhusiano wa kibalozi kwa ajili ya uhuru na haki za Wazimbabwe, vilimsifu. Gazeti la The Independent lilisema: “Mwalimu alikuwa kiongozi wa kitaifa mwenye kanuni zake, akili, umaarufu wa kupendwa na watu wake, mwanafalsafa wa siasa, mpiganaji, mtu mwenye fikra, na mwanademokrasia aliyekuwa mmoja wa viongozi wachache wa Afrika waliopata madaraka kupitia sanduku la kura na kisha kuyaachia kwa hiari.”


Nalo Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) lilimmwagia sifa likisema: “Dk. Nyerere alisimama kama kiongozi wa Afrika aliyekataa mitego ya madaraka.”

 

Mwaka 2007, Rais Museveni alimtunukia Nyerere tuzo iitwayo Nishani ya Kijeshi ya Katonga ambayo ndiyo ya juu zaidi nchini humo na ilipokewa na familia yake. Hii ilitokana na heshima ya kumpiga na kumng’oa Nduli Amin. Mwaka 2009, yaani miaka kumi baada ya kifo chake, Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Miguel d’Escoto Brockmann, alimtangaza Nyerere kuwa mshindi wa tuzo iitwayo Shujaa wa Dunia wa Haki za Jamii. Hali kadhalika, familia yake iliipokea tuzo hiyo mjini New York.


Hizi sifa haziji hivi hivi tu kwa kuzungukazunguka na kupiga picha kwani wameshakufa viongozi wengi wa Afrika, kuanzia na akina Kwame Nkrumah, Gamal Abdel Nasser, Seretse Khama, Augustino Neto, Jomo Kenyatta, Samora Machel, Kamuzu Banda, Milton Obote, na wengine wengi lakini hakuna aliyekaribia sifa alizopewa Nyerere. Vijana wa leo wana mengi ya kujifunza kutoka kwa Mtanzania huyu aliyekufa aliyetamba kwa aana yake duniani.

URITHI WAKE

Je, ni nini hasa alichotuachia Watanzania? Katika uongozi wake mrefu Nyerere alilazimika kufanya mengi na kwa mujibu wa katiba ya wakati ule, na uduni wa maendeleo yetu, na kwa kuzingatia kuwa alikuwa na elimu kubwa na uwezo mkubwa kichwani, angeweza kufanya madudu ya ajabu kwa makusudi, lakini hakufanya hivyo.


Mwalimu angeweza kujilimbikizia mali, ama kujaza nduguze madarakani, au kupendelea kwa misingi ya ubaguzi wa rangi, dini au kabila lakini hakufanya hivyo katu. Ndiyo ukweli huu. Wapo wachache wenye njaa za kifikra wanaopiga kelele za njaa njaa lakini wawaulize Wakenya walivyofanywa na Jomo Kenyatta, au Waganda walivyokorogwa na Amin na Obote.


Siku moja mwaka 2006 nikiwa darasani kwenye Chuo Kikuu cha Johns Hopkins nilikumbana na mtu mmoja kutoka Afrika Magharibi. Baada ya darasa tukaambatana naye njiani tukipiga soga na akaniuliza: “Wewe watoka wapi?” Nikasema kwa kujidai:

 

“Tanzania.” Akasimama na akanyoosha mkono kunipongeza na nikabaki nimeduwaa. Akasema: “Ninyi Watanzania mna bahati sana, Mungu aliwapenda kwa kuwapa Nyerere. Kama si Nyerere, mimi binafsi ningekufa; kwetu ni Biafra, Nigeria.” Nikamsalimia upya na kumpa pole kwa sababu ninakijua kilichowapata.


Nyerere alisimama kidete kuwatetea watu wa Biafra wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Nigeria baada ya kujitangaza kuwa taifa mwaka 1967 ili kujikwamua na uonevu wa dhahiri. Kiongozi wa watu wa Biafra, Chukwuemeka Ojukwu, alihudhuria mazishi ya Nyerere Dar es Salaam. Nyerere alijali utu na alisisitiza: Binadamu wote ni sawa na Afrika ni moja.


Mwalimu alitufundisha kuwaheshimu watu wote bila kuwabagua kwa namna yoyote ile na hata Serikali ya Tanganyika na baadaye Tanzania zilikuwa na watu wote, Wazungu, Waarabu, Wahindi na Waafrika. Huu ndiyo Utanzania alioujenga Nyerere na ndiyo msingi wa Tanzania kuwatetea watu kama Wapalestina ambao leo hawana kiongozi hata mmoja wa Afrika anayewatetea. Ndiyo msingi wa kuyapigania mataifa mengine ya Afrika ili yapate uhuru wakati nchi nyingine kama Malawi na Kenya zilikuwa zikidharau.


Nyerere alitufundisha kutenganisha dini na siasa na akasema wazi kwamba Tanzania haina dini isipokuwa watu wake ndiyo walio na dini; na kweli wakati wa Mwalimu tabia za viongozi wa siasa kujikomba kwa viongozi wa dini na kujibanzabanza kwenye majumba ya ibada haikuwapo. Leo hii ni aibu!


Nyerere aliwaachia viongozi wa dini wafanye kazi za dini zao tu, wasitukane dini nyingine kamwe, na watoe huduma za jamii, lakini si kuikaribia siasa. Nyerere alijua kuwa viongozi wa dini wanaweza kuwa hatari kwa taifa lolote lile pasipo kutarajia. Leo eti wamekuwa vinara kwenye kila jambo hadi sensa; hivi itakuwaje wakiwarubuni Watanzania na kisha kusema wametumwa na Mwenyezi Mungu?


Nyerere alikataa katakata kuruhusu makabila kuiburuza nchi yetu na akaanza na kuwafutilia mbali machifu. Waingereza walipenda kuendekeza makabila na ndiyo maana wenzetu kama Uganda na Kenya walipotelea humo humo; si kwa sababu walikuwa wakabila tangu zamani, la hasha, bali kwa sababu walianza na viongozi ambao hekima kwao ilikuwa bidhaa adimu.

Leo hii Tanzania tunaona balaa la ajabu kwa viongozi wetu kuvutia ukabila, ukanda na umikoa; dalili kubwa ya kufilisika kisiasa, kiitikadi na kiakili. Hii si dalili njema na mifano ipo mingi Afrika, sijui kwanini hawaioni?


Nimalizie na vitu vinne: Muungano, ulinzi wa maliasili, lugha ya Kiswahili, na ujenzi wa jeshi letu imara. Sitagusia uchumi na elimu kwa leo zaidi ya kudokeza tu kwamba ndiye kiongozi pekee wa Afrika aliyemudu kujenga viwanda 400 nchini na pia ndiye kiongozi pekee wa Afrika aliyefuta ujinga hadi kufikia asilimia 92 kwa mujibu wa UNESCO katika miaka 25 ya kwanza ya Afrika baada ya uhuru. Leo tuko chali kwenye yote haya mawili.


Sasa, ingawa leo hii Watanzania wachache wanazungumzia kuuvunja Muungano wa Tanzania, lakini kwa hakika huo si uamuzi mzuri kama alivyosema Balozi wa Ujerumani wiki hii jijini Dar es Salaam, kwamba Watanzania watakuja kujuta wakiuvunja Muungano huu. Ni kweli na mataifa ya nje na watu wake watatucheka. Kuvunja taifa haijawahi kuwa utatuzi wa tatizo.


Nyerere na mwenzake, Rais wa Zanzibar, Abeid Amani Karume, ama kwa hakika wanastahili pongezi kubwa. Iwapo tunaota kuwa Shirikisho la Afrika Mashariki na baadaye Muungano wa Mataifa ya Afrika, tunauvunja huu wa sasa ili iweje? Si kwamba ni tamaa na uhuni tu wa viongozi wachache?


Katika ulinzi wa maliasili, Nyerere aliamua jambo moja kubwa, kwamba kama hatuwezi kuzifukua kutoka huko ardhini, basi ni heri zikae humo humo hadi watakapopatikana Watanzania wajuzi ili wazitoe humo kwani madini hayaozi. Bahati mbaya leo hii tumeingiwa na mdudu kichwani na kuamua kuwaleta wageni kuja kuchukua kila kitu chetu kwa kisingizo cha uwekezaji. Nchi inaliwa kushoto na kulia na tunabaki kutoa machozi. Huu ni ulofa wa kufikiri kwa kudhani kuwa mwekezaji wa nje hawezi kutuibia.


Nani alisema kwamba ni lazima sisi Tanzania tuihudumie dunia kwa madini yetu na kwa kupata hasara kubwa hivi? Tunajua mengi Watanzania katika sekta hii na jinsi tunavyoumia, hivyo niishie hapa ila tu tukumbuke kuwa, ni ujuha mkubwa kuachia mali iondoke namna hii. Nyerere asingekubali.


Kwa kuona mbali na kutambua umuhimu wa kujitambulisha kama watu huru wenye akili zao, utamaduni wao na haiba yao, Nyerere alikishika Kiswahili mapema na kukipa hadhi kubwa ya kuwa lugha rasmi na lugha ya Taifa. Leo hii Watanzania tunatamba na Kiswahili duniani, lakini kwa uzembe wetu, majirani zetu wameanza kutufunika na kwa uzembe zaidi, tunaanza kukipoteza.


Tutakuja kujuta huko mbele tutakapogundua kwamba wenzetu wanakikimbilia Kiswahili wakati sisi tunakikimbia. Nyerere aliona mbali mno kwenye hili na ndiyo maana leo hii majirani zetu wanahaha kujijenga kwenye lugha hii.

 

Uganda waliamua mwaka 2004 kiwe lugha ya Taifa, Kenya mwaka juzi wamekipa hadhi ya kuwa lugha rasmi baada ya kuwa lugha ya Taifa hapo awali. Rwanda sasa wamekichukua kama moja ya lugha zao, lakini sisi tunahangaika na Kiingereza kibovu na Kiswahili kichovu. Tunapaswa kuzimudu lugha zote mbili kwa ufasaha wa juu.


Kwenye ulinzi wa nchi yetu Nyerere atakumbukwa kama kiongozi aliyejenga jeshi la Afrika, si Tanzania pekee. Jeshi letu lilianza kwa kuwa mwalimu mkuu wa wapiganaji wa nchi za kusini mwa Afrika mara baada ya Uhuru. Baadaye kero ya mpaka wa Ziwa Nyasa kidogo imponze Rais Banda kwenye miaka ya 1960 mwishoni, hata hivyo alitulia na Nyerere akavuta subira.


Miaka ya 1970 Tanzania iliendelea na juhudi za kuzipigania nchi za Msumbiji, Angola, Namibia, Afrika Kusini na Zimbabwe ili zipate uhuru na majeshi yetu yalipigana pia, hasa Msumbiji ambako kwenye miaka ya 1980 mwanzoni ilibidi majeshi yetu yarudi tena kupambana na magaidi wa RENAMO. Mwaka 1975 Angola na Msumbiji zilipata uhuru, Zimbabwe ikapata mwaka 1980 na miaka ya 1990 Namibia na Afrika Kusini zikajikomboa, sifa kubwa zikienda kwa majeshi yetu.

 

Mataifa mawili madogo ya Bahari ya Hindi, Komoro mwaka 1975 na Ushelisheli mwaka 1977, yalihitaji msaada wa majeshi yetu pale marais wake walipopinduliwa na majeshi ya kukodiwa na waasi wa ndani. Mwaka 1980 Rais Kenneth Kaunda wa Zambia alikumbwa na machafuko nchini mwake na akaomba msaada wa Tanzania. Nchi za Zaire ya zamani, Burundi na Rwanda, nazo kwa nyakati fulani ziliwahi kuonjwa na wapiganaji wetu, yote ikiwa katika kutetea haki za waliokuwa wakionewa.


Funga kazi ya yote ni Vita ya Kagera iliyomng’oa Nduli Idi Amin Dada baada ya uvamizi wake wa Oktoba 31, 1978. Majeshi yetu yalipigana kishupavu chini ya Amiri Jeshi Mkuu Nyerere na Aprili 11, 1979 yakaipindua rasmi serikali ya Amin. Kufikia Julai taifa zima la Uganda lilikuwa chini ya Tanzania. Yalikuwa mafanikio makubwa ya kivita ambayo hakuna taifa lolote la Afrika lililowahi kuyapata hadi leo.


Huyo alikuwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Ni vigumu kumaliza yote, na inaweza hata kuwa vigumu kukubaliana, lakini ukweli haufichiki kwamba alitupa heshima ya kipekee duniani na ndiyo huwa tunaponea hadi leo. Tunapaswa kuilinda kwa nguvu na akili zetu zote.


Kwa hakika, Nyerere aliubeba Utanzania moyoni mwake; aliijenga Tanzania na aliwapenda Watanzania. Mungu ibariki Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


2144 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!