*Aeleza anavyokunwa na kazi nzuri inayofanywa na Tanzania

*Amsifia Rais Kikwete, aunga mkono Jeshi la Tanzania Congo

*Aeleza wazazi wake walivyoishi Tanzania, JK aishukuru USA

Rais Barack Obama wa Marekani ametua nchini na kupokewa kwa kishindo na kutoboa siri ya anayojua juu ya Tanzania, huku akieleza kuguswa na mapokezi ya aina yake.

Ndege ya Rais Obama, Airforce One, ilitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, saa 8:38 mchana jana, na alilakiwa na mwenyeji wake, Rais Jakaya Kikwete.

 

Baada ya kushuka kutoka kwenye ndege akiwa na mkewe na watoto wake; Michelle na Malia na Sasha, alikwenda kwenye jukwaa na kupigiwa wimbo wa taifa kabla ya kukagua gwaride la heshima, huku mizinga 21 ikipigwa.

 

Baada ya hapo alikagua vikundi vya ngoma na kushiriki kucheza ngoma, hali iliyoulipua kwa furaha umati uliokuwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere. Kisha Rais Obama alifika Ikulu na kulakiwa na maelfu ya wananchi waliokuwa wamejipanga pande zote za lango la kuingilia Ikulu wakipunga bendera za Marekani.

 

Alipofika Ikulu, Rais Obama alifanya mazungumzo na mwenyeji wake, Rais Kikwete, kisha akafanya mkutano na waandishi wa habari. Katika mkutano na waandishi wa habari, Rais Obama alishukuru kwa mapokezi makubwa aliyopewa, na akaeleza jinsi anavyoifahamu Tanzania tangu enzi hizo.

 

Alisema yeye ana uhusiano wa moja kwa moja na Tanzania kwani wazazi wake walipata kumsimulia kuwa baba yake aliishi miaka mingi.

 

“Najisikia wa aina yake… kwani baba yangu alitumia muda mwingi kuishi na kutembelea mara kwa mara Tanzania,” alisema Obama kisha akasema kwa Kiswahili: “Habari zenu” Alitumia tena Kiswahili kuhitimisha hotuba yake kwa kusema: “Asanteni sana.”

 

Akimsifia Rais Kikwete, alisema alikuwa kiongozi wa kwanza kutoka Afrika aliyemwalika kwenye Ikulu ya Marekani kwa nia ya kujadili mikakati ya maendeleo ya muda mrefu kwa ajili ya Tanzania na Bara la Afrika. Alisema walijadiliana mambo mengi ikiwamo usalama wa chakula.

 

Alisema jana ilikuwa ni miaka 50 tangu uhusiano wa Tanzania na Marekani uanzishwe rasmi kati ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa 35 wa Marekani wa wakati huo, mwaka 1963 John F. Kennedy, wakati Mwalimu alipoalikwa kwenye Ikulu ya Marekani (White House). Kennedy alifariki miezi minne baada ya Nyerere kutoka Marekani kwa kupigwa risasi.

 

Obama aliisifia Tanzania kuwa ilikuwa nchi ya kwanza kushiriki ulinzi wa amani nje ya mipaka yake, hali inayodhihirisha kuwa Tanzania ni nchi sahihi kujenga urafiki nayo.

 

Alisema Tanzania imelea demokrasia, ina Bunge linalofanya kazi, vyama vya upinzani huru na Kikwete amewezesha kuwapo kwa uhuru wa vyombo vya habari, hali inamyofanya Kikwete awe kiongozi mwenye mchango wa pekee katika kuwezesha dunia iliyostaarabika.

 

Katiba mpya

Obama aliwapongeza Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, kwa uamuzi wao wa kukubali kuanzisha mchakato wa Katiba mpya itakayowezesha demokrasia pana na kutoa uwanda mpana wa watu kutoa mawazo yao.

 

Aliipongeza Tanzania kwa kuhitimisha vyema mradi wa kwanza wa Changamoto za Millennia na kuongeza kuwa Tanzania kutokana na kwamba imefanya vyema katika MCC1, imepata fursa ya kupewa ufadhili kwa mara ya pili chini ya MCC2. Aliwataka Watanzania kutumia nafasi za ufadhili wa kupeleka Waafrika nchini Marekani kujifunza masuala mbalimbali.

 

Umeme kwa Afrika

Rais Barack Obama alisema moja ya mambo ya msingi yaliyomleta Tanzania, ni kutangaza mpango mkubwa wa umeme kwa Afrika. “Nitahakikisha chini ya mpango huu tunapata umeme wa uhakika na wa bei nafuu mara mbili ya kiwango cha sasa,” alisema.

 

Leo atatangaza rasmi mpango wa umeme kwa Afrika utakaogharimu Sh bilioni 7 kwa ajili ya nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Ethiopia, Ghana, Nigeria na Sudan Kusini.


Katika sekta ya afya, alisema Marekani imewezesha kudhibiti malaria, ambapo imewezesha watu milioni 1.2 wenye virusi vya Ukimwi kupata dawa za kupunguza makali (ARV), huku ikiokoa maisha ya watoto zaidi ya 500,000.

 

Ulinzi na Usalama

Katika suala la ulinzi na usalama, aliipongeza Tanzania kwa kushiriki ulinzi wa amani katika Jimbo la Darfur na kuwezesha mazungumzo yenye lengo la kumaliza mgogoro wa kisiasa nchini Zimbabwe.

 

Alisema jana amesaini Amri ya Rais wa Marekani kupambana na ujangili, na kusema kuwa Marekani itashiriki vita dhidi ya ujangili kwa nia ya kuiachia Afrika na kizazi kijacho maliasili. Alitangaza dola milioni moja kwa ajili ya kazi hii ya kupambana na ujangili.

 

Huku akitania, alisema kwa mashabiki wa mpira wa kikapu alikuwa ashauriane na Rais Kikwete juu ya mchezaji wa kikapu Mtanzania Hashim Thabeet, anayecheza ligi ya NBA ya Marekani.

 

Akimkaribisha, Rais Obama kwenye mkutano na waandishi wa habari, Rais Kikwete alisema: “Nataka nikwambie, Watanzania wanakupenda. Sijawahi kumpokea mkuu wa nchi yeyote, akapata watu wengi kiasi hiki,” alisema Kikwete.

 

Alimshukuru Rais Obama kwa kuendeleza ushirikiano kati ya Marekani na Tanzania ulioachwa na mtangulizi wake, Rais George W. Bush, katika maeneo ya afya, elimu, usalama wa chakula, ujenzi wa miundombinu, umeme na sekta ya barabara.

 

Rais Kikwete hakuficha hisia zake katika mradi wa Millennium Challenge Cooperation (MCC). “Kwa ushirikiano tulionao… hakika sisi [Tanzania na Marekani] ni marafiki wa kweli,” alisema Kikwete.

 

Kipindi cha maswali

Rais Obama aliulizwa iwapo anaridhishwa na kiwango cha misaada inachotoa Marekani na iwapo kiwango hicho kinakidhi haja, huku Rais Kikwete naye akiulizwa swali hilo hilo.

 

Akijibu swali hilo, Rais Obama alisema misaada ya Marekani imekuwa msaada wa pekee kwa nchi nyingi zenye kupokea misaada hiyo, akitolea mfano jinsi misaada ya Marekani ilivyoiwezesha Tanzania kudhibiti malaria, kupunguza vifo vya watoto, kuwaongezea tija wakulima kwa kuwawezesha kupata masoko bora. “MCC imekuwa yenye ufanisi mkubwa hapa nchini Tanzania,” alisema.

 

Alisema kutokana na mafanikio yaliyopatikana, Marekani imeamua kutoa awamu ya pili ya MCC2, mradi ambao utapeleka umeme vijijini. Pia aliongeza kuwa uhusiano wa Marekani na Afrika anaoulenga katika mfumo wa ushirika ni kufanya biashara badala ya misaada.

 

“Hatutaki kuwanunulia dawa, bali kujenga mifumo ya afya. Hatutaki kuwanunulia chakula, bali kuboresha kilimo,” alisema Rais Obama. Kwenye suala la umeme, amesema mbali na mpango wa dola bilioni 7, tayari kuna karibu dola bilioni 9 nyingine zinazoelekezwa katika sekta ya umeme zilizotolewa na sekta binafsi, ila akaonya: “Ni jukumu la Waafrika kuijenga Afrika kwa ajili ya Waafrika.”

 

Kwa upande wake, Rais Kikwete alisema swali la MCC halikupaswa kuulizwa kwa Rais Obama, bali yeye ndiye anayejua jinsi MCC ilivyoisaidia Tanzania. Alisema chini ya MCC, Tanzania ndiyo yenye kueleza inataka Marekani isaidie wapi na ndiyo maana kuna miradi ya barabara zimejengwa Namtumbo, Tanga na Mbeya chini ya MCC.

 

Alisema swali la MCC jinsi ilivyosaidia liko wazi, kwani imeongeza upatikanaji wa umeme kwa Watanzania kutoka asilimia 10 hadi 21, vifo vinavyotokana na malaria, vimepungua kwa zaidi ya asilimia 40, watoto wanaozaliwa na kina mama wenye virusi vya Ukimwi wanazaliwa bila Ukimwi na Marekani chini ya MCC iko mbioni kuwezesha kila mtoto kupata kitabu chake, hali aliyosema ni lazima kila awaye awashukuru Wamarekani kwa mafanikio hayo.

 

Vurugu zinazoendelea nchini Misri

Rais Obama akijibu swali kuwa haoni kama Rais wa Misri, Mohamed Morsi, nchi imemshinda kutokana na vurugu zinazoendelea nchini humo, alisema anaguswa na anafuatilia kwa karibu kila kinachoendelea nchini Misri. Hata hivyo, alisema Marekani bado inamuunga mkono Rais Morsi kutokana na ukweli kwamba alichaguliwa katika uchaguzi ulio huru na wa haki, ingawa alisema nchi hiyo inapaswa kuhakikisha kila sauti ya mwananchi inasikilizwa.

 

Alisema Marekani inahakikisha kipaumbele namba moja ni ubalozi wao uko salama pale Cairo, na amezisikia taarifa za wanawake kudhuriwa, jambo lisilokubalika. Hata hivyo, alisema demokrasia bado ni changa nchini Misri, hivyo bado wanahitaji muda wa kujijenga.


Alisema wameshikilia baadhi ya misaada iliyokuwa iende Misri kwa nia ya kufuatilia hali inavyoendelea, lakini akaonya kuwa vigezo vya Marekani kuendelea kushirikiana na taifa lolote ni kuangalia iwapo inafanya uchaguzi huru na wa haki, inawasikiliza wananchi, haitumii vyombo vya dola kukandamiza wananchi na kwamba idadi ya maandamano si kigezo cha Marekani kuichukulia nchi kuwa haina utawala bora.

 

Mgogoro wa DRC

Rais Obama aliisifia Tanzania kwa kushiriki kikamilifu kurejesha amani nchini DRC, akisema kuwa Marekani itasaidia panapowezekana, lakini haitaki kuielekeza Afrika nini cha kufanya katika jambo lolote.

 

Alisema Congo ina madini mengi, lakini kutokana na vurugu watu wake hawajapata fursa ya kufurahia matunda ya madini hayo. “Wakongo wanaostahili kupewa nafasi,” alisema.

Alisema ameshauriana na Rais Kikwete, na wakati akimpongeza kwa Tanzania kupeleka majeshi nchini Congo akasema Tanzania inapaswa kuongeza juhudi za kurejesha amani nchini humo.

 

Rais Obama alizitaka nchi zinazoizunguka Congo kuacha kuvipa fedha vikundi vya waasi na badala yake zihakikishe amani inatamalaki na kufanya biashara badala ya kupalilia vita.

 

Mawaziri walioruhusiwa kukutana na Rais Obama Ikulu jana ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.


Wengine ni Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi, na Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima. Kwa Zanzibar alikuwapo Waziri wa Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika, Haroun Ali Suleiman.

 

By Jamhuri