Ulimwengu wa leo unahitaji kuhubiriwa namna mpya ya kuishi maisha ya upendo. Ni hatari watu wa ulimwengu kuishi bila upendo. Bila kuishi maisha ya upendo, dunia yetu itageuka kuwa jehanamu. Mungu hutabasamu pale anapoona mwanadamu anaishi maisha ya upendo. Nafsi yako haiwezi kuwa na amani kama haipendi wala kupendwa. Njia bora ya kuishi ni kuishi maisha ya upendo. Namna bora ya kupendwa ni kupenda. Jaribu kumtumikia Mungu kwa kuishi maisha yanayotawaliwa na upendo, sambamba na hilo sambaza mbegu ya upendo kwenye jamii ya walimwengu.

Kila binadamu aliumbwa na Mungu, lakini si kila mmoja ni mtoto wa Mungu. Njia pekee ya kuhesabika kuwa mtoto wa Mungu ni kuishi maisha yanayotawaliwa na upendo. Jina jingine la Mungu ni upendo. Inafahamika kwamba, upendo ni jina la Mungu. Na majivuno ni jina la shetani. Huwezi ukaishi maisha yanayotawaliwa na upendo ukaitwa mtoto wa shetani, utaitwa mtoto wa Mungu. Hali kadhalika huwezi ukaishi maisha yanayotawaliwa na majivuno ukaitwa mtoto wa Mungu, utaitwa mtoto wa shetani. Maandiko matakatifu yatujuza: “Mungu ni upendo, naye akaaye katika pendo hukaa ndani ya Mungu.” ( 1 Yohana 4:16).

Tunatakiwa kujenga na kukuza tabia ya kupendana katika maisha yetu. Baraka ya watu wema katika jamii, familia, taifa ni upendo. Upendo ndiyo zawadi aliyonayo kila mtu na ambayo anaweza kuitoa na kuipokea bila masharti. Jamii bora haijengwi kwa matofali wala fedha, jamii bora inajengwa kwa upendo. Familia bora inajengwa kwa upendo. Bahati nzuri ni kwamba kila siku kuna sauti inatuambia, pendaneni. Sauti hiyo ni hii: “Nawapeni amri mpya…. pendaneni kama nilivyowapenda.”’ [Yn 13:34].

Jibu la upendo ni upendo. Hakuna tabia yoyote inayoweza kuyageuza maisha yako yavutie kama ua la jasmine zaidi ya tabia ya upendo. Ukipenda, utapendwa. Usipopenda huwezi ukapendwa. Penda, upendwe. Wapo watu wanaishi na majirani zao kama paka na panya. Hawaelewani. Hawasalimiani. Hawataki hata kuonana uso kwa uso. Wanapishana njia. Mwandishi George MacDonald anashauri hivi: “Upendo kwa jirani yako ndio mlango pekee wa kutoka kwenye gereza la ubinafsi.” Ndugu msomaji, unapata faida gani unaposhindwa kusalimiana na jirani yako?

Upendo ni marashi. Wapulizie wenzako marashi ya upendo. Njia ya kuwa na furaha ni kuwafanya wengine wawe na furaha. Mtawa wa Kanisa Katoliki, Mother Teresia wa Kalkuta anafundisha hivi: “Sambaza upendo kila mahali unapokwenda. Mtu yeyote asije kwako bila kutoka akiwa na upendo na furaha.” Matumizi mazuri ya maisha ni upendo.

Maisha bila upendo hayana thamani. Wakati mzuri wa kupenda ni sasa. Kwa nini sasa ndiyo muda muafaka wa kupenda? Kwa sababu hujui utakuwa na muda wa kuishi mpaka lini. Mazingira hubadilika. Watu hufa. Watoto hukua. Huna dhamana ya kesho. Kama unataka kuonyesha upendo ni bora uonyeshe kuanzia sasa. Mwanafalsafa wa Dernmark Soren Kierkegaard anasema: “Mara unapozaliwa katika ulimwengu huu tayari u mzee wa kutosha kuweza kufa.” Tusikubali kufa tukiwa bado tunadaiwa deni la upendo. Unapotamani kuishi, tamani kuishi maisha yanayotawaliwa na upendo. Maisha yako yawe na chapa ya upendo.

Upendo ni kutoa na kupokea. Ilikuwa ni saa nne kamili za asubuhi Desemba 23, 1923, mwanadada Sophie Hone alipouawa. Sophie Hone aliuawa kwa kutetea haki za watoto katika mji wa Dunmore. Katika kitabu chake cha kumbukumbu, Sophie Hone alikuwa ameandika maneno haya: “Kusudi la maisha yangu ni kupenda.” Chukua muda kutafakari kusudi la maisha yako. Wamebarikiwa wenye maisha ya kupenda na kupendwa. Matumizi bora ya maisha ni kupenda.

Tumeumbwa kupenda na kupendwa. Hatuwezi kuishi bila kupenda na hatuwezi kuishi bila kupendwa. Septemba 8, 1890, Mt. Theresia wa Mtoto Yesu alifunga nadhiri zake za kwanza za utawa katika Shirika la Karmel. Mtawa Theresia baada ya kufunga nadhiri alisali sala hii: “Ee Yesu mimi siombi kitu kingine, ila tu Upendo.” Mt. Theresia anajulikana kwa jina jingine kama: “Ua la upendo.” Moyo wenye upendo ni moyo uliojaa fadhila za utakatifu.

Upendo ni uwepo wa Mungu katika maisha ya mwanadamu. Padri Karol wa Foucauld, Februari 27, 1903 alimwandikia barua Mgr. Guerin. Sehemu ya barua yake ilisomeka hivi: “Naililia injili ya upendo.”  Upendo ni injili. Padri Karol wa Foucauld anasema: “Msingi wa ndani wa mioyo yetu, unaamuru kila mtu ampende jirani yake. Kwa maneno mengine mpende kila binadamu kama unavyojipenda wewe mwenyewe.”

388 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!