Palipo na upendo kuna maisha. Somo la kwanza katika maisha ni upendo. Somo la kwanza la kiroho ni upendo. Somo la kwanza la familia ni upendo. Somo la kwanza la uongozi ni upendo. Somo la kwanza la mafanikio ni upendo. Somo la kwanza la ujirani mwema ni upendo. Somo la kwanza la upendo ni upendo. Somo la kwanza la msamaha ni upendo. Somo la kwanza la furaha ni upendo. Somo la kwanza la shukrani ni upendo. Palipo na upendo kuna maisha. Tupendane.

Katika jamii yetu tunayoishi tumeshuhudia au tumekutana na tunaendelea kukutana na watu ambao hawana furaha katika maisha yao. Tunakutana na watu wanaojilaumu na kuwalaumu wengine. Tunakutana na watu wanaotamani kujiua. Tunakutana na watu ambao wanahisi jamii imewatenga. Tatizo ni nini? Tuwasaidie kwa namna gani watu hawa? Tunao wajibu mkubwa wa kuwasaidia watu hawa. Tusiwatenge. Tuwaonjeshe joto letu la upendo. Tuwaonyeshe uso uliojaa tabasamu na matumaini. Kwa sababu watu hawa ni ndugu zetu, ni majirani zetu, ni watoto wetu.

Jibu la upendo ni upendo. Dunia inahitaji sana upendo ili mambo mengine mazuri yawezekane. Yesu Kristo aliwahimiza wanafunzi wake wapendane. Aliwaambia hivi: “Amri yangu ndiyo hii: Mpendane kama nilivyowapenda ninyi. Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.” (Yoh. 15:12-13).  Mwandishi Friedrich Rucket anafundisha hivi: “Upendo ni kitu kikubwa sana ambacho Mungu anaweza kutupa, na kitu kikubwa ambacho tunaweza kumpa Mungu.” Upendo ni sauti ambayo kiziwi anaweza kuisikia na mwanga ambao kipofu anaweza kuuona. Tupendane.

Kwa nini tunahitajika kuishi maisha yanayoongozwa na upendo? Kwanza ni kuishi vizuri. Tukipendana tutaishi vizuri. Tutaelewana. Tutaonyana kwa upendo. Tutasameheana. Tutashauriana vizuri. Tutasaidiana. Dunia ina njaa ya upendo. Familia nyingi zina njaa ya upendo. Palipo na vita ya kidini kuna njaa ya upendo. Palipo na vita ya kikabila kuna njaa ya upendo. Palipo na vita ya kisiasa kuna njaa ya upendo. Mwalimu Julius Nyerere alijua kwamba ili Taifa la Tanzania liwe na umoja lazima mbegu ya upendo ipandwe. Nyerere alipanda mbegu ya upendo Tanzania kwa kivuli cha ujamaa. Leo hii Taifa la Tanzania watu wake wanaelewana kwa kuzungumza lugha moja (Kiswahili). Ni kwa msingi huo, Mkurya anamuoa Mchaga na wanaishi maisha ya upendo, Msukuma anaolewa na Mnyiramba na wanaishi vizuri. Hizi ni juhudi za Mwalimu Nyerere. Aliwaunganisha Watanzania wakawa kitu kimoja. Kwa tafsiri fupi ni kwamba Mwalimu Nyerere alifukuza njaa ya upendo Tanzania kwa kuwaunganisha Watanzania kuwa kitu kimoja.

Tufukuze njaa ya upendo kwenye familia zetu kwa kupendana. Tufukuze njaa ya upendo kwenye nyumba zetu za kitawa kwa kupendana. Tufukuze njaa ya upendo kwenye nyumba zetu za ibada kwa kupendana. Tufukuze njaa ya upendo kwenye jamii yetu kwa kupendana.

Tufukuze njaa ya upendo kwenye kazi zetu kwa kupendana. Kuna watu wanahisi kwamba wanaishi hapa duniani kimakosa kwa sababu tu wana njaa ya upendo. Kuna baadhi ya wanandoa wanahisi ndoa ni msalaba wa zege kwa sababu tu ndani ya ndoa zao hakuna harufu ya upendo.

Mwanaharakati Martin Luther King Jr anasema: “Nimeamua kujishughulisha na upendo. Chuki ni mzingo mzito sana ambao haubebeki.” Upendo ni mzigo mwepesi ambao unabebeka. Chuki ni mzigo mzito ambao haubebeki. Nani anafahamu mzigo wa chuki? Pengine unaweza ukawa haufahamu mzigo wa chuki. Niulize nikwambie. Chuki ni sumu isiyo na tiba ya kisayansi wala tiba ya kiasili. Tiba ya chuki ni upendo. Njia rahisi ya kuepuka chuki ni kuishi maisha ya upendo.

Maisha ni upendo. Maisha yanazungumza katika upendo. Ukitaka kuuona upendo, ishi upendo. Uruhusu upendo uyatawale maisha yako. Usiruhusu hata siku moja ipite pasipo kupanda mbegu ya upendo wa kweli, upendo usio wa kinafiki, upendo utokao moyoni na upendo ushindao majaribu. Yesu Kristo aliwahimiza wanafunzi wake kwa nasaha hii. “Pendaneni kama nilivyowapenda ninyi.’’ (Yn 13:34). Ni lazima tujitahidi kuyajenga maisha yetu katika msingi wa upendo. Furaha kamili ipo katika kuishi maisha ya upendo.

By Jamhuri