Kwa muda sasa  yamekuwapo maelezo ya kuonesha jinsi pikipiki zilivyo janga la kitaifa. Pikipiki zimekuwa zikishutumiwa kwa kusababisha ajali, kupoteza nguvu kazi na kuongeza idadi ya walemavu au vifo kwa kasi ya ajabu hapa nchini.

Vijana waendesha pikipiki wameanzisha jeshi lisilo rasmi. Hawa wanafanya kila chembe ya kosa barabarani, lakini hatimaye wao ndiyo wanaoadhibu wanaotanda makosa. Pikipiki wanaziendesha kwa kasi ya kutisha, wanajigonga kwenye magari au kutumbukia kwenye mitaro, lakini wakitoka hapo tu wanakuwa kama kunguru.

 

Wakishasababisha ajali wanawageukia watu waliowatia hasara. Wanatumia marungu, mapanga na visu kuwachoma na kuharibu mali za watu wengine kama kuvunja vioo vya magari. Huko Geita wiki iliyopita tumeelezwa kuwa waendesha pikipiki wamemkwida mganga wa Hospitali ya Geita hadi wakamg’oa meno.

 

Sitanii, kwenye taa nyekundu Dar es Salaam waendesha pikipiki hawaziheshimu. Mbaya zaidi wanavunja sheria mbele ya askari polisi. Wanavuka taa zikiwa nyekundu, wanapakia watu bila kofia ngumu na wakati mwingine wanaendesha pikipiki kwa kasi ya kutisha.

 

Hili limenipa shaka. Nimejiuliza polisi wanashindwaje kuwadhibiti hawa waendesha pikipiki. Polisi wanashindwaje kuwakamata kila wanapothibitika kuendesha pikipiki kama vile roho zao wameziazima. Ni kwa misingi hiyo nasema hapana. Hawa watu wadhibitiwe.

 

Sitanii, wakati nikikerwa na vurugu hizi za waendesha pikipiki kuigeuza Tanzania kuwa sawa na nchi isiyo na sheria, limeibuka jingine baya. Hili si jingine, bali ni wizi wa ajabu. Mwanzoni katika Jiji la Dar es Salaam maeneo ya Sinza wenye pikipiki wanapora simu, mikoba ya fedha kwa kina mama na kompyuta.

 

Kwa sasa hali limebadilika. Pikipiki ilitumika kumuua padre kule Zanzibar, ndani ya wiki iliyopita pikipiki zimetumika kupora Sh milioni 40 Dar es Salaam, kumwagia watalii wawili tindikali Zanzibar na kumpiga risasi iliyomuua Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

 

Nchini Rwanda walipata tatizo kama hili. Ujambazi ulikua kwa kiasi kikubwa kutokana na matumizi ya pikipiki. Walichofanya, walianzisha usajili upya. Pikipiki ziliondolewa kwenye usajili wa namba za magari, zikapewa namba yake maalum.

 

Waendesha pikipiki wote wakasajiliwa. Wakapewa namba na namba hizo zimebandikwa kwenye makoti wanayovaa. Hakuna mtu anayeruhusiwa kuendesha pikipiki bila kuvaa koti hili lenye namba. Namba ni kubwa na zinazosomeka kwa mbali. Yeyote anayetumia pikipiki kufanya uhalifu anatambulika mara moja.

 

Anayekutwa anaendesha pikipiki bila namba hiyo, anakamatwa mara moja. Sisi hapa kwetu tunawaza uchaguzi wa 2015. Tunaziacha pikipiki zinasambaza machangudoa. Tunaziacha pikipiki kwa kisingizio cha kupalilia mazingira ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kubembeleza wapigakura 2015.

 

Sitanii, si lazima uwabembeleze wapigakura ili wakupende. Wengi tunamfahamu John Pombe Magufuli anavyosimamia sheria. Anasimamia sheria kwa kiwango cha kukera wanaodhurika na uamuzi wake wa kisheria, lakini bado watu wanampenda. Watu wanamuona kama mtu pekee anayeweza kutoa kauli akaisimamia. Wanampenda kwa msimamo wake.

 

Katika hili la pikipiki nasema polisi hebu simameni na wananchi. Waendesha pikipiki wanatumaliza. Silaha zimezagaa hovyo mitaani, na hata ugomvi wa ngumi sasa hivi unaamuliwa kwa risasi. Nchi yetu ilipofikia kwa sasa tunahitaji kukarabatiwa. Tukiruhusu hali iliyopo ikaendelea hatutafika.

 

Viongozi wa vyombo vya dola wanapaswa kubadili mwelekeo. Wakati IGP Mwema anaingia madarakani nchi ilikuwa haikaliki. Kinachoendelea sasa hivi ni hatari tupu. Tumelemea kule kule kwa watu kuogopa hata kwenda kwenye baa kunywa pombe.

 

Mauaji ni kila kona. Watu sasa hivi wanapigwa mapanga, risasi na visu kama vile nchi iko vitani na hakuna utawala wa sheria. Taarifa iliyotolewa na Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC) inaonesha kuwa hadi kufikia Juni mwaka huu watu zaidi ya 900 wameuawa katika matukio mbalimbali hapa nchini.

 

Hali hii haivumiliki, tumeifikisha nchi yetu kwenye kona ambayo hatukustahili. Tunasema Tanzania ni nchi ya amani, lakini utulivu hatuwezi kudai kuwa upo wakati kuna Watanzania zaidi ya 900 wameuawa. Na hapa nasema tatizo letu ni siasa.

 

Sitanii, nasema matukio ya kisiasa yanayoendelea ambayo Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) inawafungulia mashitaka ya ugaidi wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kisha miezi mitatu wanaondoa mashitaka hayo tunajenga usugu wa ajabu.

 

Mbinu hizi zilitumiwa na wakoloni wakati nchi nyingi za Kiafrika zikipigania uhuru. Wanasiasa wengi waliopigania uhuru walitajwa kama magaidi. Walifungwa na wengine kupotezwa. Kitendo cha DPP kufungua mashitaka ya ugaidi dhidi ya Wilfred Lwakatare na Joseph Ludovick kisha akayafuta na watuhumiwa wa kule Igunga nayo yakafutwa ni aibu.

 

Kama kuna ofisi italiingiza Taifa letu katika machafuko, basi ni Ofisi ya DPP. Ofisi hii ikikubali kutumika kisiasa, na polisi wakakubali mashinikizo ya kisiasa ya aina ya Nape Nnauye, nchi hii itafika pabaya. Vyama vya siasa lazima vifike mahala vikubali matokeo.

 

Najua CCM nao wanafahamu kuwa hawatatawala nchi hii milele. Wanapaswa kuangalia uwezekano wa kubadili au kuboresha sera ikiwa hizi zilizoko wanaona watu wamezichoka. Wanapaswa kujiuliza hayo wanayodai wananchi ni ya kweli au la.

 

Sitanii, badala ya kutumia Polisi, Mahakama na Ofisi ya DPP sawa na mkoloni alivyofanya, ni bora CCM ikachagua mkondo wa mazungumzo. Zanzibar akina Seif Shariff Hamad wameswekwa ndani mara nyingi hadi maafisa wa Magereza wakawazoea kila wakirejeshwa wanawaambia ‘karibu tena mzee’.

 

Hatimaye, CUF wameishia kuzungumza na CCM wakaunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Hapa dawa ni moja. Kama Chadema wanasema wanaweza kuuza bati Sh 5,000 au saruji mfuko Sh 5,000, ni CCM kueleza kwa nini haiwezekani au kuwapa fursa Chadema wakatawala kipindi kimoja na kama kuna ugumu, basi wananchi wataona kuwa wameshindwa kutekeleza hayo waliyoahidi na kurejesha kijiti kwa CCM.

 

Sitanii, hebu turejeshe heshima ya nchi yetu. Tudhibiti waendesha pikipiki na DPP aache kufungua kesi hewa za ugaidi. Mungu ibariki Tanzania.

1089 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!