JESHI la Polisi limeingia matatani kwa kumtangaza ‘mbaya wao’ aliyeibua kile alichodai kwamba ni mtandao wa uhalifu na mauaji ndani ya Jeshi hilo mkoani Mwanza, kwamba ni kichaa.

Kijana Mohamed Melele, aliyetoboa siri za kuuawa kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow, ameingizwa kwa nguvu kwenye wodi ya vichaa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) akipewa dawa kali zinazotumiwa na watu wenye matatizo ya afya ya akili.

 

Si Muhimbili anakotibiwa, wala Mahakama ambayo imeshatoa taarifa rasmi za kumtambulisha Malele kama kichaa. Kazi hiyo imefanywa na Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, SSP Advera Senso, Mei 28, mwaka huu.


Jeshi la Polisi limekuwa na desturi kwa siku za karibuni kuwatangaza baadhi ya watu na watumishi wake kuwa ni vichaa. Miezi kadhaa iliyopita, polisi mmoja mkoani Morogoro aliwatuhumu wakuu wa Jeshi hilo mkoani humo, akisema wanashiriki uhalifu. Majibu ya Polisi yakawa kwamba polisi huyo alikuwa na matatizo ya afya ya akili.

Wiki kadhaa baadaye, polisi mwingine mkoani Arusha alitoa tuhuma nzito za upendeleo kwenye upandishaji vyeo. Polisi walimtia msukosuko wakisema alikuwa amerukwa akili. Wachunguzi wa mambo hawakuona ajabu kwa Jeshi la Polisi nchini kuibuka na kusema Malele aliyeutaja mtandao na matukio ya ujambazi, kwamba ni kichaa na sasa amewekwa Muhimbili.

Jambo linalotia shaka ni kuona kuwa Malele alitiwa mbaroni bungeni wakati akitaka kuonana na wabunge ili awape habari nzima za mtandao huo, lakini badala ya kupelekwa Milembe ambako ndiko kwenye wataalamu wanaosifika wa afya ya akili, alisafirishwa hadi Dar es Salaam na baadaye kupelekwa Muhimbili.

Wakati Malele akiendelea kulishwa dawa, ilhali yeye akiapa kwamba si kichaa, wanasheria kadhaa wamezungumza na JAMHURI na kusema Polisi wamefanya kosa la kisheria kumtangaza Malele kuwa ni kichaa, wakitambua kwamba hawana mamlaka hiyo.

Kwa upande wake, Wakili Mayomba Duncan wa FK Law Chambers ya jijini Dar es Salaam, amesema mwenye mamlaka ya kuthibitisha na kumtangaza mtu kama ni kichaa, ni daktari pekee.

“Kichaa hatangazwi na polisi wala mtu mwingine, hata Makahama ili itoe uamuzi kama mtu ni kichaa au laa, ni lazima izingatie ripoti ya daktari,” amesema.

Mmoja wa wanasheria hao, amesema Malele akitolewa Muhimbili, ana haki ya kuwafungulia Polisi kesi kwa kumkashifu, au hata kuutangaza ugonjwa wake bila ridhaa yake.

Kwa tukio hili la ‘kichaa’ cha Malele, mwanasheria huyo amesema, “Kisheria ni kosa la jinai kwa mtu asiye na taaluma ya utabibu kumtangaza mwingine kuwa ni mgonjwa wa akili bila kuwa na uthibitisho au kielelezo kutoka kwa daktari.


“Kila mtu ana haki ya kulindiwa heshima yake. Huwezi kumtangaza mtu kuwa ni kichaa, au mgonjwa wa ukimwi bila kuegemea kwenye ‘quotation’ ya daktari. Kufanya hivyo ni kukiuka law of tort (sheria ya kosa la daawa/madhara).”


Mwanasheria mwingine aliyeomba jina lake lihifadhiwe, amesema, “Kama mtu (asiye daktari) hana uthibitisho wa daktari, hana nguvu ya kisheria kukwepa shtaka la kumdhalilisha mtu kwa kumtangaza katika jamii kuwa ana ugonjwa fulani.


“Ninasema hivi kwa sababu hata madaktari wenyewe huwa makini sana katika kutangaza ugonjwa wa mtu. Vinginevyo unaweza kujikuta unapandishwa kizimbani kujibu ama shtaka la kukashifu, au kudhalilisha utu wa mtu.”


Juhudi za kumpata dakatari anayemhudumia Malele, hazikuzaa matunda baada ya daktari huyo kukwepa kuzungumza na JAMHURI, huku Ofisa Uhusiano wa MNH, Aminieli Alingaisha, akiwa likizo.


Malele anatajwa kuwa na siri nzito zinazohusu mtandao wa uhalifu unaowahusisha Polisi, wafanyabiashara, wanasiasa na watumishi kadhaa wa vyombo vingine vya ulinzi.

 

Mtandao huo unatajwa na Malele kwamba ndiyo uliohusika kumuua Kamanda Barlow usiku wa kuamkia Oktoba 13, mwaka jana, katika eneo la Kitangiri jijini Mwanza wakati akimrejesha nyumbani Mwalimu Doroth Moses, aliyekuwa naye katika kikao cha harusi.

 

 

 

 

 

 

 

By Jamhuri