Habari kubwa katika toleo la leo inahusu mtandao wa mauaji ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza Liberatus Barlow. Ndani ya habari hiyo, gazeti hili la JAMHURI linamtaja mtuhumiwa Mohamed Edward Malele, Mkazi wa Kijiji cha Igoma, Wilaya ya Kwimba, mkoani Mwanza anayekisiwa kuwa na umri wa kati ya miaka 30 hadi 40 kuwa anashikiliwa na dola.

Malele anasema ameshiriki matukio mengi ya ujambazi katika Kanda ya Ziwa. Ametaja majina mazito na ya kutisha ya watu aliokuwa akishirikiana nao kufanya ujambazi.

 

Miongoni mwa majina aliyoyataja ni pamoja na  maofisa wa Polisi, Usalama wa Taifa, wafanyabiashara na wanasiasa ambao anasema wamegombea vyeo vya kisiasa kwa nia ya kuficha madhambi yao katika mikoa ya Mwanza na Geita.

 

Kamanda Barlow aliuawa usiku wa kuamkia Oktoba 13, mwaka jana katika eneo la Kitangiri jijini Mwanza alipokuwa akimrejesha nyumbani Mwalimu anayetajwa kwa jina la Doroth Moses, ambaye alikuwa naye katika kikao cha harusi.

 

Kijana huyo kwa sasa anashikiliwa na vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa maelekezo kutoka ngazi za juu za uongozi wa Taifa. Malele ambaye hajui kusoma wala kuandika, alikamatwa Ijumaa ya Mei 10, mwaka huu katika lango la Bunge mjini Dodoma.

 

Anasema yeye ndiye alitumwa kumuua Barlow akagoma. Maelezo yake yanatishia kuwa hata Barlow uchunguzi wa kina ukifanyika juu ya mali alizonazo, aina ya watu aliokuwa anashirikiana nao inawezekana akawa mmoja wa watuhumiwa wa matendo ambayo ni kinyume cha sheria.

 

Anasema watu waliomuua Barlow ni kwa sababu alikuwa amewanyima mgao katika ‘kazi’ waliyokuwa wamefanya, na hivyo akawambia wasubiri ipatikane ‘kazi’ nyingine kubwa angewapatia wanachodaiana. Habari hizi sisi zimetusikitisha. Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi amekiri kuzifahamu.

 

Tunatumaini uchunguzi wa kina utafanywa kwa watumishi wa umma waliotajwa na kijana huyu, kisha fagio la chuma lifanye kazi yake. Itakuwa ni hatari kubwa kama watu tuliowaamini na kuwakabidhi jukumu la kulinda usalama ndio wamegeuka wanyang’anyaji. Hii inaweza kufifisha usalama wa nchi yetu.

 

Tunasema tuhuma hizi ni nzito, zichunguzwe na taarifa yake kutolewa kwa uwazi na kwa haraka. Hii itakuwa fursa kwa chombo muhimu kama Polisi kujisafisha na kuondoa virusi ikiwa vimejipenyeza katika utumishi huu muhimu wenye kupaswa kutawaliwa na uaminifu na uadilifu mkubwa. Mungu ibariki Tanzania.

1056 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!