Privatus Karugendo, katika makala yake iliyochapishwa chini ya kichwa cha maneno, “Papa Benedict wa XVI Mfungwa wa imani anayetaka kuwa huru”, iliyoandikwa Februari 17, 2013, kurasa 11, 12 na 13, angeweka wazi kwamba Papa Benedict huyo aliwahi, kabla ya Aprili 5, 2009, kumvua madaraka ya shughuli za upadri, pengine nisingekuwa na hamu ya kuandika makala haya.

Karugendo anapaswa kuzingatia kwamba, ingawa ibara ya 18 (a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kama ilivyorekebishwa (Katiba ya Muungano), inatoa haki kwa kila mtu kuwa na maoni na kueleza fikra zake.

 

Haki hiyo haimaanishi kwamba maoni au fikra hizo lazima zikubaliwe, itategemea mtiririko wa maoni hayo au fikra hizo ulivyopangwa. Maadili ya jamii ya Tanzania yanataka mtu atangaze maslahi yake kuhusu maoni yake anayoyatoa au fikra zake anazozitoa.

 

Mfano mzuri wa mgongano wa maslahi utaukuta katika Kanuni 3 ya Kanuni za Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka ya Miji) Kanuni za Maadili Mema ya Madiwani) chini ya sura ya 288 ya Sheria za Tanzania 2002. Mgongano wa maslahi umefafanuliwa katika Kiingereza ambacho nitakitafsiri katika Kiswahili kwamba una maana na ni pamoja na pale ambapo diwani ambaye ana jukumu katika kutoa uamuzi ambao hauna upendeleo au ni adilifu, yeye mwenyewe ana ushabiki nao, au ana maslahi nao moja kwa moja au kwa namna isiyo dhahiri ya kupata faida au kutarajia kupata faida kutokana na uamuzi huo.

 

Badala ya “diwani” weka “mtu”; badala ya “jukumu” weka “hamu’; badala ya “kutoa uamuzi ambao hauna”, weka “kutoa maoni au fikra ambayo/ambazo hazina”; endelea kubadilisha kulingana na maoni au fikra. Nadhani sasa umepata maana ya ufafanuzi kulingana na makala haya.


Katika makala yake, Karugendo anatamka, miongoni mwa mingine: “… ni aibu Papa kujiuzulu. Ili uwe Papa ni lazima uwe mfungwa wa imani. (Uk 11); … Askofu na Makardinali. Hawa wote ni wafungwa wa imani (Uk 11); … imani inaambatana na kufikiri.  Kuamini bila kufikiri ni matusi  kwa Mwenyezi Mungu aliyetuumba na akili na  utashi. (Uk. 11); mfungwa wa imani hawezi kuwa huru (Uk 11); analindwa na kuongozwa na chombo cha uongozi wa Kanisa.

 

Huko nyuma, mapapa walikuwa ni wafungwa ndani ya Vatican; hivyo walijua yale tu ambayo chombo cha uongozi wa Kanisa kilitaka wayajue… Ratzinger (yaani Papa Benedict XVI) alianza kurudi nyuma kidogo. (Uk 11)… Hivyo inawezekana kabisa Papa Benedict XVI ameshinikizwa kuachia ngazi baada ya kugundua kwamba hawawezi kumzima na nafasi yake ni kubwa kwa kuweza kufanya chochote na akasikilizwa. (Kurasa 12 na 13) … Anataka kuwa huru.

 

(Kurasa 12 na 13) Ukikutana naye kwa faragha unaweza kujadiliana naye juu ya uzazi wa mpango, kutoa mimba… lakini akisimama kama ‘mfungwa wa imani’.  (Uk 12)… kama mtakumbuka kitabu chake cha mwisho ni ‘Yesu wa Nazareti’…. Ukisoma kitabu hicho …. (Uk 12).

 

Katika kujadili makala ya Karugendo, nitaongozwa na uamuzi wa Jaji Mkuu mstaafu, Barnabas Samatta, katika kesi ya Kabulofwa Mwakalile na wengine 11 dhidi ya Jamhuri 1980 TLR 144, alioutoa Oktoba 27, 1981, akiwa Dodoma.

 

Kuhusu kuhoji. Mheshimiwa Jaji alisema, katika Kiingereza ambacho nakitafsiri katika Kiswahili, kwamba ni mtambo wa moto wa kisheria katika kufichua ukweli kuhusu mtu na maslahi yake. Tabia, jinsi alivyopata kujua bila kosa na bila shaka mambo ambayo yametendeka, ambayo atayatolea ushahidi, kama jinsi hizo alizitumiaje, uwezo wake wa utambuzi, kukumbuka na kutoa maelezo, na wakati huo akichunguzwa na kubainika na kutizamwa mwenendo wake ili ushahidi wake upimwe kama ni mnyofu.

 

Sasa kuhusu kauli ya Karugendo kwamba kuamini bila kufikiri ni matusi kwa Mwenyezi Mungu aliyetuumba na akili na utashi, Karungendo hakumbuki kwamba amefungwa na imani bila kufikiri anaposema kwamba ana baba na mama wazazi? Je, alikuwapo wakati mimba yake inatungwa na hadi anazaliwa baada ya miezi tisa hivi?


Je, abiria ndani ya ndege akitokea Dar es Salaam kwenda London, akitumia saa nane hadi atue, abiria huyo hafungwi na imani bila kufikiri kwamba rubani wa ndege atamfikisha salama? Karugendo anaposema kwamba ili uwe Papa, ni lazima uwe mfungwa wa imani, anakumbuka kwamba Papa Benedict XVI ni Papa wa 269 wa Kanisa Katoliki?   Je, Karugendo alikutana na kuzungumza kwa faragha na kumchunguza kila Papa wa hao  268 waliotangulia ili kujua kama ni wafungwa wa imani au la, na ni mara ngapi? Je, Papa Benedict XVI alimualika Karugendo akutane naye kwa faragha, na kwa muda gani?

 

Na kuhusu kitabu chake Papa Benedict cha mwisho kwa nini anasema, “kama mtakumbuka”, kwani ana hakika tulikwishakiona? Na yeye alikisoma lini, mara ngapi alikimaliza na wanaotaka kukiona watakipata wapi na kwa bei gani? Kimeandikwa kwa lugha gani? Karugendo alikielewa vilivyo, na tutajuaje?


Na Karugendo anaposema kwamba kujiuzulu kwa Papa ni aibu na kwamba Papa analindwa na kuongozwa na chombo cha uongozi wa Kanisa, je,  Karugendo anakumbuka vema maneno ya Kanuni 749 ibara 1; 332 ibara 2; 189 ibara 3, na 333 ibara 3?

 

Hizo Kanuni zimetafsiriwa katika Kiingreza na nitazitafsiri katika Kiswahili kama ifuatavyo: “749 ibara 1- Kwa madaraka ya cheo chake, Papa wa Roma mwenye  uwezo wa juu kabisa, hana uwezo wa kukosea katika uongozi wake wakati ambapo kama Mchungaji Mkuu na Mfundishaji wa waumini wote wa Kristo, akiwa na wajibu wa kuimarisha ndugu zake wote katika imani, anatangaza, kwa msimamo,  fundisho la kushikilia kuhusu imani au maadili mema na mabaya. 332 ibara 2 – Ikitokea kwamba Papa wa Roma anajizulu, uhalali wake unataka kwamba kujiuzulu huko kumefanyika kwa halali na kutangazwa wazi vilivyo lakini si lazima kukubaliwe na yeyote.

 

189 ibara 3 – kujiuzulu ambako kunahitaji kukubaliwa hakuna nguvu hadi kukubaliwe ndani ya miezi mitatu. Kule ambako hakuhitaji kukubaliwa kuna nguvu ya kisheria, ambapo mtu anayejiuzulu anakutangaza wazi kwa mujibu wa sheria. 333 ibara 3 – hakuna rufani au kimbilio kuhusu uamuzi au amri kamili ya Papa wa Roma.


Karugendo akumbushwe pia kwamba Oktoba 26, 2009 Papa Benedict wa XVI, kwa hiari yake, kwa uwezo wake wa juu kabisa ulio na masharti na mipaka ya Mungu, kwa barua yake ya kitume kwa watu wote, alifanya mabadiliko kuhusu Kanuni 1008, 1009, 1086, 1117 na 1124.


Sasa Karugendo anapochokonoa kujiuzulu kwa Papa anataka kueleza kwamba si halali, anataka akutane na Papa kwa faragha kuhusu kujiuzulu au kwamba tusome kitabu cha Papa huyo cha mwisho, na hatimaye tukate rufani dhidi ya kujiuzulu huko au tutafute kimbilio jingine? Mbona hajazungumzia kwamba mwili wa binadamu huchoka kadiri ya umri. Umri wa Papa Benedict ni 85.

 

Au Karugendo aliwahi kuwa na umri huo na akakuta hachoki? Azingatie kwamba Kanuni 354 inaweka miaka 75 kwa kardinali kujiuzulu. Na mbona Karugendo hajazungumzia utukufu, ujasiri na unyenyekevu wa Papa Benedict XIV katika kujiuzulu cheo cha Papa wa Roma, mwenye uwezo wa juu kabisa bila vurugu, mabomu ya machozi na bunduki za polisi, na silaha za kivita za wanajeshi, akilinganisha na kung’ang’ania madaraka kwa viongozi hasa wa Kiafrika – eti wamechaguliwa na Mungu!


Labda Karugendo asome Kanuni ya 751, ili achague moja miongoni mwa matatu:- ukanaji (apostasy) kwa maana ya kukataa imani yote ya Kikristo; kukana au kushuku kikaidi (heresy) ukweli mmojawapo katika imani ya Kimungu ya Kikatoliki; na kujitenga (schism) na kuwa chini ya Papa wa Roma au na ushirikiano na waumini wake wa Kanisa.

 

Kanuni hizo nilizozitaja hapo juu, zinapatikana miongoni mwa Kanuni 1752 katika kitabu chenye kichwa cha maneno, “The Code of Canon Law New Revised English Translation.” Kitabu hicho kimeruhusiwa kusomwa na Wakatoliki wote kwa kuandikwa “Imprimatur” kwenye ukurasa wa nne mwanzoni bila namba.


Kinauzwa Dar es Salaam kwa Sh 13,600 katika duka la Paulines Books and Media Center, mkabala wa Kanisa la St. Joseph’s, Kivukoni Front. Hizo Kanuni 1752 ni zaidi ya mara 11 ya ibara za Katiba ya Muungano, ambayo ina ibara 152.

Kila la kheri, Privatus Karugendo.

Novatus Rweyemamu

Wakili Mwandamizi

Mobile: 0784 312 623

1711 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!