Tarehe 9 Desemba mpiga solo mahiri Tanzania kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Nguza Viking, kwa lakabu ya muziki, Big Sound alitoka Gereza la Ukonga, Dar es Salaam ambako alikuwa akitumikia kifungo cha maisha. Aliachiwa baada ya kunufaika na msamaha wa Rais John Magufuli alioutoa kwa baadhi ya wafungwa wapatao elfu nane katika hotuba aliyoitoa mjini Dodoma kusherekea siku ya Uhuru wa Tanganyika tarehe 9 Desemba 1961. Alitoa msamaha huo kwa mujibu wa ibara 45 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kama ilivyorekebishwa mwaka 2005.

Nguza Viking na mwanaye Johnson Nguza Viking, kwa lakabu, Pappy Kocha, pamoja na watoto wake wengine wawili – Nguza Mbangu na Francis Nguza – walifungwa kifungo cha maisha na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam mwaka 2003 baada ya kupatikana na hatia ya makosa ya kubaka na kulawiti vigori wa shule moja ya msingi Sinza, Dar es Salaam.

Hukumu na kifungo hicho vilizua taharuki na fazaa kubwa mno kwa wadau wa muziki wa dansi Tanzania na hata nje ya mipaka ya nchi hii. Na hata kwa watu wa kawaida tu!

Tanzania imepata kuwa na wacharazaji gitaa la solo mahiri wengi wazalendo kama vile Rashid Hanzuruni, Abel Balthazar, Joseph Mulenga (King Spoiler), Mbaraka Mwinshehe, Joachim Ufuta, Shem Karenga, Wema Abdallah, Wilson Peter, Hamza Kalala, Yohana (Wanted), Duncan Njilima, Kassim Rashid (Kizunga) na wengine wengi tu. Aidha, imekuwa na wapiga gitaa la kati rythm matata sana kama vile Kassim (Marythm), Harrison Siwale (Satchmoo), Abdallah Gama (String Master) na kadhalika. Pia imekuwa na wapiga solo mahiri wengi kutoka nje, hususan Congo kama vile Ilunga Lubaba, Freddy Ndala Kasheba (Supreme au Maestro), Nguza Viking mwenyewe, Dikula Kahamba (Vumbi) bila kumsahau mpiga rythm matata Mulenga Kalonji. Lakini ni Nguza Viking na mwenzake Freddy Ndala Kasheba ndiyo walijitokeza zaidi kwa umahiri wa kucharaza gitaa la solo. Na umahiri wao ulikuzwa zaidi na ushindani wa bendi zao Macquis Du Zaire ambako Nguza alikuwa anapiga na Ndala Kasheba wa Safari Sound. Ilikuwa ni mfano wa  ushindani uliokuwepo zamani Congo kati ya Dr. Nicolas Kassanda wa African Jazz na baadye African Fiesta, kwa upande mmoja, na Franco wa TP OK Jazz, miaka ya sitini hadi themanini.

Kwangu binafsi kilele cha Nguza cha ucharazaji gitaa la solo kwa ustadi mkubwa ni pale aliposhirikiana na mpinzani wake kimuziki, Ndala Kasheba,  katika mwimbo “Kwa Heri Mama Maria Nyerere.” Mwimbo huo ulitungwa kumuaga aliyekuwa mke wa hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere wakati alipong’atuka urais wa Tanzania mwaka 1985.

Wakati Nguza Viking akiwa gerezani wadau wa muziki wa dansi walipata pigo jingine kubwa kwa kifo cha Ndala Kasheba. Ikumbukwe sio hivyo tu, takriban wapiga solo wote maarufu niliowataja hapo awali walikuwa karibuni wote wamefariki. Kwa kifupi wadau wa dansi walighumiwa. Pengine aliyeghumiwa zaidi ni mwimbaji mkongwe na stadi kabisa Kikumbi Mpango (King Kiki)! Maana huyu, kwa nyakati tofauti, alipiga muziki na Nguza na Kasheba katika bendi ya Fauvette, Maquis Du Zaire na baadaye Zaita Muzika kisha Wazee Sugu. Nakumbuka onyesho lao la mwisho pamoja kabla ya Nguza kufungwa pale Bwalo la Polisi, Osyterbay! Ilikuwa habari kubwa, yataka wasaa kusimulia. Muulize sahibu yangu Mabere Nyaucho Marando ambaye tulisakata naye dansi kisawasawa katika mkesha huo! Kwa kifupi Nguza alilikung’uta gitaa la solo kwa ustadi mkubwa mno.

Siku moja niliongea na King Kiki pale Mtaa wa Samora, Dar es Salaam akanieleza jitihada zake za kumpata mpiga solo kutoka Congo kuziba pengo la Kasheba na Nguza. Lakini ziligonga mwamba.

Tukiachia mbali bashrafu hiyo ya wasifu wa Nguza na wanawe watatu ambako wawili waliachiwa baadaye na Mahakama ya Rufaa, kesi yao ilizua mjadala mkubwa mno nchini hadi hivi leo. Kweli Nguza na wanawe walifanya ngono ya pamoja dhidi ya wanafunzi wale? Kwa kifupi basi kesi hii iliibua hisia kali mno Tanzania kwa vile ilitokea baada ya kupitishwa Sheria ya Makosa ya Kujamiiana mwaka 1998 iliyodhamiria kudhibiti makosa ya aina hiyo kama vile kubaka, kulawiti na kadhalika. Aidha, ilihusu vigori kati ya miaka sita hadi nane. Katika mazingira kama hayo dhahiri wengi waliwachukia washitakiwa bila kujali kama kweli kulikuwa na ushahidi komesha dhidi yao. Walisahau kabisa kuwa mshitakiwa, kwa mujibu wa sheria, hawajibiki kuthibitisha kuwa hakutenda kosa. Anachotakiwa ni kuonyesha shaka ya maana tu kuwa inawezekana hakufanya kosa analokabiliwa nalo. Na shaka hii ndiyo imetamalaki tangu Nguza atiwe mbaroni, kushtakiwa hatimaye kufungwa hadi alipopata msamaha wa Rais tarehe 9 Desemba 2017. Dhahiri basi hata msamaha wenyewe utaendelea kuzua mjadala mkali kwa miaka mingi ijayo. Tayari mbunge mashuhuri amelaani msamaha huo.

Masuala ya ngono za pamoja kama yanavyojulikana huko Ulaya ‘orgy’ ni nadra mno kutokea Afrika. Ni vigumu sana kufikiria baba wa Kiafrika anaweza kufanya unyama huo tena kwa kushirikiana na wanawe. Allwahu ya Alaam! Yaani, Mungu ajua zaidi.

Hivyo mengi yakasemwa kuwa kuna nguvu iliyotaka kuwatokomeza Nguza na familia yake kupitia Mahakama. Marekani wanapenda kutumia neno la kimombo “frame up”. Kwa Kiswahili cha sasa ni kubambikiziwa. Yumkini katika fikra kama hizo Mgombea wa Urais wa Chadema  katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Edward Lowassa, aliahidi kumsamehe Nguza na wanawe kama angeshinda urais. Hatujui Rais Magufuli naye alikuwa na hisia zipi kuhusu kadhia hii!

Kwa kawaida hapa nchini misamaha huwa haitolewi kwa wafungwa wanahusika na makosa ya ngono kama yale ambayo Nguza na wanaye walihusika nayo. Hivyo wengi watajiuliza kulikoni basi Nguza na wanawe wapewe msamaha? Suala kubwa katika kesi ya  Nguza Viking (Babu Seya) ni je, mfumo wa Mahakama  nchini uko makini? Maana kuna watu wengi mno bado wanaamini Nguza alionewa kama nilivyosema hapo juu! Kama nilivyotogoa hapo awali kuwa kwanza tarehe 16 Octoba 2003 Nguza alishtakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, ambako akapatikana na hatia. Pale Kisutu alitetewa na Wakili mzoefu Hubert Nyange. Baadaye tarehe 27 Januari 2005 hukumu na adhabu yake vilithibitishwa na Mahakama Kuu ambako alikata rufaa. Na tarehe 11 Februari 2010 Mahakama ya Rufaa nayo ilithibitisha hukumu na adhabu ya Nguza na Papii Kocha na kuwaachia watoto wake wawili Nguza Mbangu na Francis Nguza.

Katika maisha yangu ya uwakili nilipata mshawasha kutaka kuongeza nguvu ya kumtetea Nguza katika ngazi zote hizo, sio tu kama mshabiki wa mwanamuziki huyo, lakini nilikuwa na shaka kama kweli alitenda makosa ya ngono. Ni kama hisia niliyoipata pale nilipotaka kumtetea mwimbaji aliyeshiriki Bongo Star Search kwa mara ya kwanza kabisa, Mariam Mashauri ambaye alidaiwa eti alikuwa si raia wa Tanzania, bali Congo! Tatizo wakili hawezi kujipeleka kumtetea mshitakiwa mpaka aombwe kufanya hivyo.

Katika tasnifu yangu ya Shahada ya Uzamivu, Chuo Kikuu cha Sussex, Uingereza mwaka 1995 niliyoita Human Rights in the Criminal Process, yaani Haki za Binadamu katika Mchakato wa Jinai niligundua kuwa takriban nusu ya wakata rufaa katika kesi za jinai huhinda. Hii ina maana kuwa karibuni nusu ya wanaopatwa na hatia na kuadhibiwa huwa wamepewa adhabu hizo kwa makosa ya mahakimu au majaji waliosikiliza na kuamua kesi zao. Ndiyo maana ni vizuri kutoa fursa nyingi za kukata  rufaa ili makosa ya kiushahidi na kisheria yapembuliwe vyema zaidi katika ngazi hizo tofauti za Mahakama. Katika hili Waingereza wanayo mifumo bora zaidi kwa kuwa na ngazi nyingi za mahakama za kukata rufaa.

Kwa bahati mbaya kabisa Tanzania ni miongoni mwa nchi chache Afrika ambazo hazina Mahakama ya Juu. Maana yake aliyeshitakiwa mbele ya Mahakama Kuu kwa makosa ya mauaji ya kukusudia au uhaini ambayo adhabu yake ni kifo ana ngazi moja tu ya kukata rufaa kwenda Mahakama ya Rufaa ya Tanzania. Lakini yule aliyeshitakiwa Mahakama ya Mwanzo kwa wizi wa mbuzi ana ngazi tatu zaidi za kutafuta haki. Fikiria aliyehukumiwa kunyongwa au kifungo cha maisha anakosa haki kiasi gani!

Tatizo hili haliko kwenye kesi za jinau tu. Chukua mfano wa kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na Mchungaji Christopher Mtikila dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kudai haki ya mgombea binafsi katika uchaguzi nchini Tanzania. Hukumu iliyotolewa na jopo la majaji saba wa Mahakama ya Rufaa kupinga haki hiyo ya wazi ilipondwa na wanasheria, wanademokrasia na wananchi wengi tu. Mashuhuri miongoni mwao ni Jaji Mkuu Mstaafu Barnabas Samatta ambaye aliandika makala nzuri mno kukosoa hukumu ile. Hivyo laiti kungekuwa na Mahakama ya Juu hukumu ya Nguza  pengine ingewezwa kutenguliwa. Kwa bahati nzuri kabisa Tume ya Katiba ya Jaji Warioba ilipendekeza kuwapo Mahakama ya Juu kama vile ilivyopendekeza kuwepo Tume Huru ya Uchaguzi. Sasa kwa vile Serikali ya sasa ya CCM haitaki Katiba mpya wala kusikia kuwepo kwa Tume Huru ya Uchaguzi, basi japo ikubali kufanya marekebisho ya Katiba kuruhusu Mahakama ya Juu ya Tanzania. Naamini kuna akina Babu Seya wengi ambao wangeachiwa na Mahakama hiyo bila ya kusubiria ‘kiki’ ya Rais.

5623 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!