Profesa Muhongo ni uteuzi makini

muhongoBaraza la Mawaziri la Rais John Pombe Magufuli limetoa kile ambacho walio wengi walikuwa wanakitarajia kufuatia mambo mengi aliyoanza nayo, ambayo walikuwa hawakuyazoea.

Rais Magufuli alianza kwa kumteua waziri mkuu ambaye kusema ukweli hakuna aliyekuwa akimuwazia. Ilikuwapo idadi kubwa ya watu waliokuwa wakisemwa kwamba mmoja wao angeweza kuipata nafasi hiyo, lakini JPM akawaonesha waliofikiria hivyo kimazoea  kwamba yeye ni sampuli nyingine, mtu asiyetabirika kimazoea,  kwa kumwibua Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa.

Na kwa kitu ambacho hakuna aliyekitarajia, Majaliwa kaanza kazi kwa kasi ileile ya JPM huku akiwashangaza walio wengi waliodhani kwamba asingeweza kuimudu nafasi hiyo. Huo ndiyo uzuri wa kuachana na mazoea.

Katika Baraza la Mawaziri nako ilikuwa hivyo hivyo, wananchi walio wengi walipanga baraza lao la mawaziri wakisema fulani na fulani ni lazima wawemo kwenye Baraza jipya la Mawaziri, huku wengine wakiwa wanatilia maanani kwamba kwa vile fulani na fulani waliwahi kufanya namna hii na namna ile, hawawezi kuwamo kwenye baraza la JPM. Hilo ni tatizo linalotokana na usemi wa kwamba mazoea yana tabu. 

Lakini kwa vile Rais hapaswi kufanya kazi kwa kufuata minong’ono ya watu, Magufuli akaja kudhihirisha tena kwamba yeye ni mtu asiyetabirika kimazoea. Akateua Baraza jipya la Mawaziri kwa kufuata utendaji kazi wa kila mmoja aliyemteua. Aliangalia zaidi tija ya aliyemteua bila kuangalia sura yake wala umaarufu wake. Alichokizingatia yeye ni kile kinachotokana na usemi wake ambao umetokea kuwa maarufu wa ‘hapa kazi tu’.

Kwa leo ninayetaka kumtazama ni Profesa Sospeter Muhongo, Waziri wa Nishati na Madini. Wengi wanakumbuka kwamba waziri huyo aliondolewa kwenye kazi yake, uhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na kufanywa mbunge kabla ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo ya uwaziri wa Nishati na Madini na Rais mstaafu, Jakaya Mrisho Kikwete.

Sidhani kama Kikwete alifanya hivyo kwa kutoa zawadi kwa mhadhiri huyo, la hasha, jukumu alilomkabidhi haliwezi kuwa zawadi, ule ni mzigo mkubwa ambao JK alitaka Muhongo amsaidie kuubeba kwa kutumia ustadi wake wa muda mrefu.

Bahati mbaya ni kwamba Muhongo alikuta uchafu mkubwa ndani ya wizara hiyo, ambapo uchafu huo ulipowekwa wazi ilibidi naye umrukie na kumchafua na hakuwa na namna nyingine isipokuwa kukaa kando na kujisafisha na uchafu huo kwanza. Sababu, iwe umependa au hukupenda ukichafuka umechafuka, huwezi kusema huogi kwa vile umechafuka kwa bahati mbaya tu.

Kwa hiyo, suala la kwamba Profesa Muhongo asingeweza kuteuliwa tena kwenye Baraza la Mawaziri ulikuwa ni upotofu wa kutoyachambua mambo kiuhalisia. Ukweli ni kwamba sakata lililomfanya Muhongo akalazimika kuachia ngazi ndani ya Serikali ya Awamu ya Nne lilianza tangu wakati wa Serikali ya Awamu ya Pili. 

Sasa wenye umakini wa kutosha wanapaswa waone ni jinsi gani kashfa iliyoanza tangu wakati wote huo, inavyoweza kumhusisha mtu aliyekuja baada ya awamu mbili kupita. Ni kwamba alichokifanya Rais Kikwete wakati alipomteua Muhongo kuwa waziri, zilikuwa ni jitihada zake za kutaka kuisafisha wizara hiyo kwa kuutumia uelewa na maarifa vilivyokuwa kichwani mwa msomi huyo.

Kama tunavyoona, Profesa Muhongo hakuwa mwanasiasa, yeye alikuwa mwanazuoni, mwalimu, ambaye kazi yake kuu ilikuwa ni kuzidisha maarifa kwa kuyatoa kwa wengine walio na jukumu la baadaye la kuitumikia nchi yetu.

Kwa hiyo, Rais Kikwete alichokiona ni kwamba badala ya kumtegemea Muhongo awafundishe wengine ambao ingewachukua muda mrefu kuuingiza uelewa wao kwenye utumishi wa nchi, akaamua kumteua Muhongo ili auingize weledi wake moja kwa moja kwenye utumishi wa umma. 

Hiyo ilikuwa ni njia mojawapo kubwa ya kujinufaisha na usomi wa wananchi wetu. Yaani badala ya kuwafundisha wengine namna ya kupata utaalamu wa jambo fulani na baadaye waje kulishughulikia jambo hilo kwa njia ya kujaribu kwa vile ndiyo kwanza wanaanza kuonesha utaalamu wao baada ya kujifunza, mwalimu ndiye anayeambiwa akaoneshe utaalamu wake kwa kufanya kazi husika badala kuifanya kinadharia.

Kwa hiyo, tunaweza kuona namna profesa huyo alivyoweza kuimudu kazi hiyo aliyokabidhiwa na Kikwete kwa muda mfupi aliokaa wizarani hapo kabla ya kashfa iliyoanzia nyuma yake kumlipukia na yeye kulazimika kuachia ngazi.

Ni katika kipindi hicho ambapo umeme umeenea kwa kiasi kikubwa kwenye maeneo ambayo hayakutarajiwa kama yangeweza kupata umeme hasa yale ya vijijini, ni kwamba aliweza kutekeleza yale aliyokuwa akiyafundisha shuleni, chuoni, na hivyo kuifanya nchi inufaike na ujuzi wa wasomi wake kuliko kuacha ujuzi huo uishie madarasani tu bila uhakika wa kwamba waliokuwa wakifundishwa wangeweza kuyatekeleza waliyofundishwa kwa kiwango kile kile walichofundishwa.

Hivyo, kama Magufuli angemuacha Muhongo eti kwa vile alihusishwa kwenye kashfa ya Escrow, ambayo kiuhakika yeye hakutajwa kama mhusika wa kweli isipokuwa kimazingira, lingekuwa ni jambo la kuutelekeza ujuzi bila sababu za msingi. Na kufanya hivyo si kumkomoa mtu, Muhongo, kama baadhi ya watu walivyokuwa wakifikiria, bali kulikomoa Taifa kwa ujumla.

Na kama Rais angeamua kufanya hivyo si ajabu angekuwa anajikomoa yeye mwenyewe kwa vile linalotakiwa, kama alivyoahidi kwenye kampeni zake, ni kuwatumikia wananchi kwa kiwango kilicho bora ambacho kitawafanya wananchi kuukubali na kuukumbuka uongozi wake wa awamu ya tano. Na hawezi kulitimiza hilo kwa kuwaacha nje watu wa aina ya Profesa Sospeter Muhongo.

Jambo ambalo ningependa kusisitiza ni la kwamba wasomi waliobobea kama alivyo Muhongo ni watu muhimu sana katika maendeleo ya nchi. Kwa hiyo, wanapopewa nafasi ya kuonesha weledi wao ni jambo la kupongezwa na kuwatia moyo wanaowapatia nafasi hizo, kama tunavyofanya sasa kwa Magufuli,  hapo hapahitajiki masuala ya kiitikadi. 

Hivyo tumuache Muhongo achape kazi kwa manufaa ya nchi kwa ujumla. Heko Magufuli, heko Muhongo. Hapa kazi tu.