Kampuni ya Mafuta ya Puma iko mbioni  kuihama  Bandari ya Dar es Salaam na kupitishia bidhaa zake katika Bandari ya Beira nchini Msumbiji.

Hatua hiyo ya Puma itazihusisha bidhaa za mafuta na vilainishi vinavyosafirishwa kwa ajili ya matumizi ya nchi za jirani.

Mtoa habari kutoka ndani ya kampuni hiyo aliieleza JAMHURI kwamba sababu ya kufanya hivyo ni kutokana na mfumo usioridhisha uliopo katika Bandari ya Dar es Salaam katika ulipaji gharama za kuhifadhi mizigo na kodi.

Amesema kampuni hiyo imefikia uamuzi huo baada ya kubaini kwamba katika Bandari ya Beira kuna unafuu wa kodi na siku za kuhifadhi mizigo katika bandari hiyo ni miezi sita wakati katika Bandari ya Dar es Salaam ni siku 30.

“Kampuni ya Puma inatoa huduma zake katika nchi 40 na tuko katika mabara matano, tuna mizigo mingi ambayo huingia nchini inakaa bandarini kwa muda mrefu.

“Ukihifadhi mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam wanatoa siku 30 wakati Bandari ya Beira wanatoa hadi miezi sita ya kuhifadhi mizigo na baada ya hapo wanaanza kukuchaji gharama za kuhifadhi na kulipa kodi, hali hii ni tofauti kabisa na Bandari ya Dar ikifika siku 30 tu TRA wamefika na kukutaka ulipe kodi na ukishindwa wanakufilisi,” amesema.

Amesema kampuni hiyo huagiza mafuta mengi na kuyahifadhi katika matenki makubwa katika Bandari ya Dar es Salaam, kwa nia ya kuyapeleka kidogo kidogo katika nchi za Namibia, Botswana, Zambia na Malawi, lakini hulazimika kuanza kuyalipia kodi na gharama za bandari baada ya siku 30 kwisha.

Amesema sababu ya pili ni mpango wa sasa wa Serikali kuwa na nia ya kuanza kutoza kodi katika mizigo ya nje kabla ya kufika katika nchi husika, jambo ambalo litaipa mzigo mkubwa kampuni hiyo.

Mtoa habari huyo ameendelea kusema kwamba uongozi wa Bandari ya Dar es Salaam umejisahau, haufanyi kazi kwa wakati.

Amesema si kampuni hiyo tu ambayo itahamisha mizigo yake katika bandari hiyo bali hata wafanyabiashara kutoka nchi za Malawi, DRC, Zambia na Zimbabwe.

Amesema kwa kufanya hivyo kampuni hiyo itafanya kazi kwa uhuru na kwa faida zaidi.

Amesema Tanzania ilikuwa ni tegemeo kwa kupitisha mizigo katika nchi za Zimbabwe, Zambia, Malawi, DRC, Burundi, Uganda na Rwanda, lakini  sasa uongozi umejisahau nchi hizo hazipitishi tena.

Amesema kwamba kujisahau huko kumesababisha kuzaliwa kwa bandari nyingi kama Beira ya Msumbiji,  Mombasa nchini Kenya, Durban, Cape Town za Afrika Kusini na Walvis Bay ya Namibia.

Hata hivyo, JAMHURI ilipofika Makao Makuu wa Puma yaliyopo Mtaa wa Bandari Kurasini jijini Dar es Salaam ili kupata ukweli wa jambo hilo, haikufanikiwa kupata majibu.

JAMHURI baada ya kufika katika ofisi hizo na kujitambulisha alijitokeza binti aliyejitambulisha kwa jina la Doris, lakini baadaye ilikuja kubainika kuwa jina lake halisi ni Faidha, aliiambia JAMHURI kuwa anayetakiwa kuzungumzia jambo ni Meneja wa Kitengo cha Operesheni.

Faidha aliitaka JAMHURI kupiga simu namba 022 2167300 hata hivyo, baada ya kupiga simu hiyo mtu aliyepokea hakuwa tayari kutoa ushirikiano.

Gazeti hili bado linaendelea kuwatafuta viongozi wa Kampuni ya Puma kupata ufafanuzi zaidi. JAMHURI ilifika katika ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ajili ya kupata ufafanuzi, lakini haikufanikiwa kumpata msemaji wa Mamlaka hiyo kwa madai ya kuwa alikuwa katika semina.

 

Historia ya Puma

 

Puma ni kampuni tanzu ya kampuni za Bidhaa ya Kimataifa ya Trafigura Beheer BV. Inajihusisha na kusambaza, kuhifadhi, kusafisha, uuzaji wa aina  mbalimbali ya bidhaa za petroli katika nchi 40 katika mabara matano.

Kampuni hiyo ilianzishwa Amerika ya Kati mwaka 1997 ikiwa inahifadhi na kusambaza mafuta na sasa ina mtandao, katika mabara  ya Amerika ya Kusini, Afrika, Baltics, Mashariki ya Kati, Asia, na Australia.

Kampuni ya Puma ilinunuliwa na Trafigura mwaka 2000.

Mwaka 2010 kampuni ilitangaza kuinunua BP na kupatikana  kampuni tano za rejareja kutoka BP Afrika.

Tangu wakati huo ilipewa zaidi mali, mafuta, masoko katika Amerika ya Kati, Caribbean, Asia ya Kusini, na Australia.

Puma inamiliki vituo vya kutoa huduma zaidi ya 1,500 vikiwa na ujazo wa mita milioni 3.8 (mapipa milioni 24) ya vifaa vya kuhifadhia mafuta.

Kampuni hiyo ambayo  imeajiri wafanyakazi 6,000 Makao Makuu yake nchini Singapore na pia ina viwanda katika mji ya Geneva, Johannesburg, San Juan na Tallinn na Kuingia Afrika.

Kampuni hiyo iliingia katika soko la Afrika mwaka 2002 na kufanya biashara zake katika nchi za Magharibi, Kati na nchi za kusini mwa Afrika.

Puma ilianzia nchini Congo-Brazzaville na kujipanua katika nchi ya Ghana baadaye Msumbiji, Nigeria, Ivory Coast, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Angola.

Septemba 2011 Puma ilikamilisha mpango wake wa kuinunua Kampuni ya Mafuta ya BP Afrika katika nchi za Namibia ambapo iliinunua kwa asilimia 100, Botswana (100%), Zambia (75%), Malawi (50%) na Tanzania (50%) kwa thamani ya dola 296,000,000 za Marekani.

Pia mwaka 2010 Kampuni ya Puma iliingia ubia na kampuni ya Castrol kwa lengo la kusambaza vilainishi katika masoko mapya kusini mwa Afrika, kama vile Angola na DRC.

Mwaka huo huo, Puma walipewa leseni ya kuagiza gesi ya kupikia mita za ujazo 180,000 katika nchi za Benin na Senegal.

1450 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!