Mwenyekiti wa Friends of Simba, Mkoa wa Tabora, Sadiki Kalimauganga, amesema kuwa kufanya vibaya kwa Wekundu wa Msimbazi Simba Sports Club ya Dar es Salaam, katika Ligi Kuu ya Vodacom iliyomalizika hivi karibuni, kunatokana na uongozi mbovu wa Ismael Aden Rage.

Akizungumza na JAMHURI Dar es Salaam hivi karibuni, Kalimauganga amesema Rage ni kiongozi mbinafsi anayeendekeza makundi katika timu hiyo, hali ambayo imefanya kutokuwapo kwa umoja ndani ya klabu hiyo.

 

“Niilishasema mwanzo na ninarudia tena kuwa uongozi wa Rage haukubaliki…nasema hivyo si kwa nia mbaya, namheshimu sana kaka yangu Rage, lakini uongozi ndani Simba umemshinda.

 

“Hataki mshikamano ndani ya Simba, anaongoza kwa kufuata makundi na si katiba ya Simba, timu imeharibika hakuna umoja wala maelewano.

 

“Kutetereka kwa Simba katika msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom ni kwa sababu Mwenyekiti Rage kaipata Simba na si Simba imepata mwenyekiti, Rage yuko pale kwa maslahi yake  binafsi.

 

“Nina shaka na huyo  Rage kama kweli ana mapenzi na Simba, inawezekana kuwa ni mamluki kwani hawezi kuwa na vyeo vitano nje ya Simba na huku anataka kuongoza Simba, ni lazima kuna majukumu mengine anayaacha kama ilivyo kwa Simba. Tunaomba ajiuzulu atuachie timu yetu,” amesema Kalimauganga.

 

Amesema kuwa kulifuta Tawi la Mpira Pesa ni sawa na kuichimbia Simba kaburi, kwani tawi hilo limekuwa likitoa mchango mkubwa kwa timu hiyo na kufanikisha kutwaa ubingwa wa mwaka jana.

 

Amesema kikatiba Tawi la Mpira Pesa lilikuwa na haki ya kuitisha mkutano, kwa kuwa katiba ya Simba inaruhusu wanachama 500 kuitisha mkutano na wao walijiandikisha na kufikia 800.

 

Amesema kuwa katika mkutano ulioitishwa kumn’goa Rage, wanachama 800 wa Mpira Pesa walijiandikisha lakini kutokana na ubabe wa Rage akawaita kuwa ni ‘Simba Toilet’.

 

Kalimauganga amesema ilikuwa jambo la ajabu kwa Rage kuwafukuza wachezaji wazuri katika ya ligi, kwa madai ya kuwa ni watovu wa nidhamu.

 

Kitendo cha Rage kumruhusu kocha wa timu hiyo, Patrick Liewig, kuwasimamisha Haruna Moshi ‘Boban’, Amir Maftah, Mwinyi Kazimoto, Abdallah Juma, Komanbil Keita na Felix Sunzu kwa madai ya utovu wa nidhamu, kilikuwa cha kuiua Simba katika mashindano hayo.

 

Amesema kama timu hiyo inataka kufanya vizuri msimu ujao, inatakiwa kumng’oa Rage katika uongozi kwa kuwa ameshindwa kuulinda ubingwa na kuufanya uchukuliwe na wapinzani wao Yanga.

 

Amesema baada ya kumfukuza Rage, Simba inatakiwa kurudisha upendo na Kundi la Friend of Simba ili kufanya vizuri katika mechi zijazo.

 

“Rage hawezi kuniambia kitu kuhusu Simba hii ambayo imenisababishia nifukuze wake zangu wawili ili niitumikie, sisi ndiyo tunaoijua Simba kuliko yeye…atuachie Simba yetu  aingie kwenye siasa, mpira siyo siasa bali ni dakika 90 tu,” amesema Kalimauganga.

 

Hata hivyo JAMHURI ilipomtafuta Rage ili kuzungumzia tuhuma hizo simu yake ya mkononi hakupatikana.

 

Simba ilimaliza mechi hiyo ikiwa imeshika nafasi ya tatu huku nafasi ya pili ikishikwa na Azama FC.

 

Watani wao wa jadi Dar es Salaam Young Africans (Yanga), wenye makao yao mitaa ya Jangwani na Twiga jijini, ndiyo waliochukua ubingwa kwa mara ya 24, huku wakiwa bado na mechi mbili mkononi.

 

Wekundu hao wa Msimbazi kushindwa kutamba katika ligi hiyo, kunatajwa kusababishwa na migogoro ndani ya klabu hiyo.

 

By Jamhuri