Kwa muda sasa nchi yetu imetikiswa. Imetikiswa si na kingine, bali ishara na viashiria vya udini. Tumepata misukosuko huko Buseresere kwa Wakristo kuamua kuchinja. Tumepata misukosuko huko Zanzibar kwa Padre Evarist Mushi kupigwa risasi na Kanisa kuchomwa moto.

Nilipata kuandika na hapa narejea msimamo wangu, tena kwa uwazi kuwa sioni sababu ya kuwa na mgogoro katika hili. Sioni pia hata haja ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuunda Kamati ya Kujadili mgogoro huu. Hakuna mgogoro hapa ni upuuzi tu.

Najua na nakumbuka simu za vitisho na sms za matusi nilizotumiwa baada ya kuandika makala ya kupinga upuuzi huu wa hata Wakristo kutaka kuchinja. Wanatumia hoja dhaifu kabisa. Eti kuchinja ni ajira, na wakati mwingine wanasema anapochinja mtu inakuwa sehemu ya ibada.


Sitanii, nilisema na sasa narudia. Tuache uchokozi usio wa lazima. Mimi naitwa DEODATUS ni Mkristo. Nimeona na nimefunga ndoa ya Kikatoliki na nimebahatika kupata watoto wanne. Miaka yote zaidi ya 40 niliyoishi duniani, wamekuwa wakichinja Waislamu.


Nasema Waislamu waendelee kuchinja. Kama mtu ana hamu ya kuchinja, achinje kuku, mbuzi au ng’ombe nyumbani kwake ale yeye na jamaa zake lakini si kuiuza buchani. Serikali kuendekeza mambo ya kipuuzi kama haya inapalilia migogoro. Ebu kamata wahalifu wanaodai nao wanataka kuchinja na kuwasweka ndani.


Sitanii, nilichosema nakirudia kuwa katika hili tuvumiliane. Waislamu tunafahamu kuwa wao hawali visivyochinjwa kwa imani yao, ila nao wanafahamu kuwa tunakula nguruwe. Tabia ya baadhi ya Waislamu kututukana eti hatuna imani kwa kula nguruwe nayo ikome. Mzee Ali Hassan Mwinyi alishatoa ruksa.


La pili katika mada ya leo, ni hizi taarifa nilizopata kutoka Zanzibar. Nimeelezwa na watu kadhaa kuwa mgogoro unaoendelea huko wala si udini, ni chokochoko za kuvunja Muungano. Kwanza niseme katika hili kuwa inasikitisha. Leo ningetamani Afrika yote iungane na kuwa moja. Kila mtu kipande chake haitusaidii.


Sitanii, nimedokezwa na wadau kuwa baadhi ya Wazanzibari sasa wana mashaka na ushiriki wa Rais mstaafu wa Zanzibar, Abeid Amani Karume iwapo yeye si sehemu ya chokochoko hizi. Karume anatajwa sasa kuwa kauli zake zinaashiria naye ni sehemu ya kundi la Uamsho.


Tena baadhi ya watu wanakwenda mbali zaidi, wanasema hata Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad naye ni mfuasi wa Uamsho kama Karume. Kauli ya Karume mjini Dodoma hivi karibuni kuwa polisi wanawaonea watu Zanzibar kwa kuwakamata imeacha maswali mengi.


Kauli nyingine iliyotia shaka wananchi na wachambuzi wa mambo ni maelezo ya Karume kuwa anataka kuuona Mkataba wa Muungano. Karume hapa ndipo nami amenitia shaka. Amenifanya nikumbuke alivyoingia madarakani kwa mtutu mwaka 2000.


Wala hii sio siri. Karume alibebwa mara zote mbili dhidi ya Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein. Amekingiwa kifua na wakati mwingine watu wanasema kura hazikutosha. Cha ajabu baada ya kuupata Urais wa Zanzibar akawasahau waliomkingia kifua.


Sitanii, Karume akaanza kujiona ni kidume. Akamuinga Komandoo Dk. Salmin Amour. Naye akagoma kuingia kwenye vikao vya Baraza la Mawaziri wa Muungano. Sikumuona Karume akiapishwa kuingia kwenye vikao hivi. Dk. Mohamed Shein aliyempokea, mwaka uliopita tumeona anaapa kuingia kwenye vikao hivi.


Nakumbuka wakati Karume anafanyiwa kampeni mwaka 2000, wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF) walikuwa wakiimba: “Baba kaleta pombe, baba kaleta pombe. We usiseme pombe, sema maji ya usiku. Mwenye nyumba hii, ni mnywaji. Akikusikia, atakufukuza.”


Maneno haya yalikuwa yakimlenga Karume. Sasa mimi sina uhakika kama Karume ni mlevi kweli au la, lakini kauli aliyoitoa hivi karibuni wakati wa kutoa maoni ya Katiba Mpya kuwa eti anataka kuona Hati za Muungano, inamshawishi kila awaye kumweka katika kundi hilo.


Karume amekuwa Rais miaka 10, achilia mbali kubebwa kisiasa, bado anaweza kudai kuwa katika hiyo miaka 10 hakupata fursa ya kuziomba na kuziona hizo hati? Kama aliziomba akakataliwa si aseme nani alimkatalia? Nasema hapa, utetezi wake dhidi ya Uamsho na kauli anazotoa sasa, zinaashiria kuwa Karume ni mshirika wa wanaotaka kuvunja Muungano.


Akiwa Waziri wa Uchukuzi, alikuwa na msaidizi wake ambaye baadaye alipelekwa mamlaka ya Mapato Tanzania, ana sura ya kishombe hivi. Baadhi ya Wazanzibari wanasema tena kwa sauti ya masikitiko kuwa Msaidizi huyu wa Karume ana viashiria vya Uamsho.


Kama hiyo haitoshi, Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla wanakumbuka jinsi Karume na Maalim Seif walivyojifungia Ikulu na kufanya uamuzi ulioiwezesha Zanzibar kujiondoa katika Muungano kisheria kupitia mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 2010.


Baada ya mabadiliko haya Zanzibar sasa inatambuliwa kuwa nchi katika Muungano wa nchi mbili zinazounda Muungano. Uamsho wanachodai ndo hicho hicho. Wanataka Zanzibar ijiondoe katika Muungano na Karume amewasadia kulifikia hilo kisheria.


Lililonitisha zaidi ni hizi taarifa kwamba Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa anawabagua Wapemba ndani ya Jeshi hilo. Zipo nyingine nisizoweza kuzithibitisha kuwa Kamishna Mussa anamuona hata Rais Shein kama Mpemba kwanza kabla ya kumuona kuwa ni Rais wa Zanzibar.

Sasa hili nimelisikia kuwa anawasiliana kwa karibu na Rais Karume, lakini siwezi kulithibitisha. Ikiwa Karume ana mwelekeo wa kuiondoa Zanzibar kwenye Muungano, mawasiliano yoyote ya karibu kati ya Kamanda Mussa na Karume yanapaswa kuchunguzwa.


Sitanii, wakubwa hawa wanayo fursa ya kujitokeza hadharani wakaunga mkono taarifa hizi au wakafafanua ukweli walionao moyoni. Haiwezekani nchi yetu ikafikishwa katika vurugu za aina hii zenye kuondoa uhai wa binadamu wenzetu kwa kisingizio cha dini kumbe watu wanataka kuvunja Muungano.


Nimezungumza na Kamishna Mussa kuhusiana na tuhuma hizi, akasema si kweli na hayo ni maneno ya watu tu. Nikamwambia wanalalamika kuwa watuhumiwa wa mauaji ya Padre Mushi anawaachia, yeye akasema anawahoji na kuwaachia wasio na ushahidi wa moja kwa moja, lakini pia katika kukamata washukiwa anatanguliza haki za binadamu. Sawa bwana.


Narudia, polisi wanapaswa kufanya uchunguzi wa kina kupata kiini cha mgogoro wa Zanzibar. Wachunguze watu wanapata wapi nguvu ya kuchoma Kanisa baada ya kumuuliza Mchungaji nani kampa kibali cha kujenga Kanisa.


Napenda kuhitimisha makala haya kama nilivyoanza. Suala la uchinjaji lisiundiwe Kamati. Waislamu ndio waendelee kuchinja, maana siungi mkono ibada za kafara ikiwa Wakristo wanadai haki ya kuchinja kutoa sadaka ya kuteketeza.


Sitanii, sikubaliani na mtu au kikundi chochote chenye lengo la kuvunja Muungano. Polisi wawachunguze kwa kina hawa niliowataja, akiwamo Karume, Maalim Seif, Kamishna Mussa na viongozi wa Uamusho kujiridhisha juu ya chimbuko la machafuko ya Zanzibar. Tubaki taifa moja, bila kubaguana. Mungu ibariki Tanzania.

By Jamhuri