Tanzania ni nchi inayoheshimika sana kimataifa. Inaheshimika kwa kuwa moja ya nchi chache duniani zilizokubali kuendesha mambo yake kwa uwazi. Imetia saini mkataba wa Open Government Initiative (Serikali ya Uwazi) uliohasisiwa na Rais Barack Obama wa Marekani. Si hilo tu, Rais Jakaya Kikwete amekuwa kiogozi wa kwanza kusikia kilio cha Watanzania juu ya Katiba mpya.

Uamuzi wa kuandika Katiba mpya si uamuzi wa mchezo. Ulihitaji mtu kujitoa. Rasimu ya Katiba mpya inaweza nuru mpya, inaweka mwelekeo mpya inaweka msingi imara katika utekelezaji wa haki za binadamu. Ndiyo rasimu inaweza ikawa na upungufu, lakini kwa mara ya kwanza ndani ya rasimu hii Uhuru wa vyombo vya habari unatambulika.

 

Nasema ni bahati mbaya tu, kuwa nchi hii inayo Sheria Na 3 ya Magazeti ya mwaka 1976 pamoja na kanuni zake za mwaka 1977. Sheria hii ikiunganishwa na sheria nyinginezo zilizopo kama ile ya Nyaraka za Siri ya Mwaka 1963, Usalama wa Taifa ya mwaka 1970, Magereza ya Mwaka 1967 na nyingine, kwa pamoja zinafifisha au kuua kabisa uhuru wa vyombo vya habari nchini.

 

Septemba 27, waziri mwenye dhamana na masuala ya habari kupitia kwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, Asah Mwambene, ameyafungia magazeti mawili. Gazeti la kwanza amelifungia Mwananchi kwa siku 14 na gazeti la pili amelifungia gazeti la Mtanzania kwa siku 90. Uamuzi huu ni halali kwa mujibu wa sheria iliyopo isipokuwa unaharamishwa na mikataba ya kimataifa tuliyoingia kama nilioutaja hapo juu.

 

Sitanii, ukiacha kuharamishwa na mikataba ya kimataifa, unaharamishwa pia nia ovu ya mtu aliyeyafungia magazeti haya, kama nitakavyoeleza hapa chini. Si hilo tu, unaharamishwa pia na utaratibu unaotumika kuufikia uamuzi husika. Nimesema Waziri mwenye dhamana, Dk. Fenella Mukangara kwa muda mrefu amekuwa na nia ovu dhidi ya vyombo vya habari.

 

Julai, mwaka jana tukiwa katika Hoteli ya Dodoma mjini Dodoma, wakati tunafanya mazungumzo rasmi na Waziri Mukangara, walikiwapo Theophil Makunga, Pilly Mutambalike, Neville Meena na marehemu Alfred Mbogola na wengine, Dk. Mukangara alitoa kauli iliyotushitua wengi na sasa ndipo tunaona inatekelezeka kwa vitendo.

“Nikipata fursa Mwananchi nitalifuta, mimi linanikera sana. Tena na Nipashe nao naona wanakuja, ikibidi nitawafungia tu, mimi siogopi kitu,” Waziri Mukangara alitwambia. Baada ya kauli hii tuliendelea na mazungumzo mengine, lakini Meena akatwambia kuwa Dk. Mukangala aliwahi kutoa kauli kama hii ofisini kwake walipokwenda akina Jesse Kwayu, Makunga, Meena na Absalom Kibanda kuomba gazeti la Mwanahalisi lifunguliwe. Mwanahalisi alilifungia kwa muda usiojulikana na sasa imepita miezi 15 likiwa kifungoni.

 

Kwa mawazo yangu nilidhani Dk. Mukangara ni mlezi wa vyombo vya habari. Hakuteuliwa kuwa waziri wa kupambana na vyombo vya habari, bali kuviongoza. Kwa nia yake ovu ya kujiandaa kisaikolojia kuvifuta vyombo vya habari, ni wazi kuwa uamuzi huu unamfurahisha katika nafsi yake na ndio maana anaufanya bila hofu kama alivyopata kusema kwa kinywa chake.

 

Sitanii, hapa ndipo tunaona tofauti. Si kwamba Mukangara alipopewa nafasi hii ndipo sheria imebadilishwa na kuwa kali zaidi, la hasha. Sheria hii imekuwapo hata wakati wa mawaziri watangulizi wake kama Dk. Emmanuel Nchimbi. Dk. Nchimbi kwa muda wote aliokuwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, hakupata kufungia gazeti hata moja.

 

Ni katika hatua hii nakumbuka mfano wa Mfalme Suleimani katika Biblia takatifu. Mbele yake alipewa fursa ya kupata kila kitu, isipokuwa kwa mshangoa wa wengi, yeye aliomba Mungu amjalie BUSARA. Busara iliujaza moyo wake hekima, busara ilimfanya atende kwa haki katika kila atendalo, busara ilimfanya aheshimike kwa kufikia uamuzi unaokubalika kwa kila awaye.

 

Binafsi naona tatizo la uwapo wa sheria hii mbaya ambayo tumekuwa tukipambana muda wote irekebishwe na kuepusha kutumiwa vibaya na watu wasiojaliwa sawa na Mfalme Suleimani. Nilipata kulisema hili mbele ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda, lakini hadi leo sijaona mabadiliko.

 

Matarajio yangu halali, ni kwamba Waziri wa Kilimo kwa kila hali atakutana na wakulima mara kwa mara. Waziri wa Nishati, mara kwa mara atakutuana na wafanyabiashara ya mafuta, Waziri wa Maji mara kwa mara atakutana na wauza maji, lakini pia Waziri wa biashara nilitaraji naye atakutana na wafanyabiashara na wenye viwanda.

Kwa bahati mbaya, Waziri wetu wa Habari pamoja na kuelekezwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuwa akutane na vyombo vya habari hajawahi kufanya hivyo. Najua inawezekana kwa mimi kuyaandika haya, anaweza kuagiza hata gazeti hili lifungiwe. Uwezo huo anao, lakini nasema akipenda afanye, ila saa ya ukombozi ikifika siku tukifika mbele ya haki, maisha yetu yatakuwa tofauti.

 

Sitanii, kwa imani takatifu niliyonayo, ikitokea akatufungia kwa sisi kutetea haki, huko mbinguni nitaishi kama Lazaro naye huenda akaishi kama Tajiri aliyefurahia maisha yake akiwa hapa duniani. Waziri mwenye dhamana na habari asiyekutana na wanahabari anaongoza wizara ipi? Kwa kweli, Mhe Dk. Mukangara anapaswa kubadilika kwa kila hali. Avipende vyombo vya habari ndiyo kazi yake ya msingi kuvilea si kuvivizia kuvifungia.

 

La pili, ni hii dhana ya utawala bora. Kwamba miaka ya 1800 Mfaransa aitwaye Montesquieu, alibuni dhana ya utawala bora kwa njia ya mgawanyo wa madaraka (separation of powers). Kwamba Serikali ikagawanywa katika mihimili mitatu; Bunge, Mahakama na Utawala. Mihimili hii inakuwa imekamilisha kitu kinachoitwa Serikali.

Kwamba Bunge – kazi yake ni kutunga sheria, Mahakama ni kutafsiri sheria na Utawala ni kusimamia utekelezaji wa sheria. Dhana hiyo imetokana na ukweli kwamba enzi za ufalme ilikuwa Mfalme ndiye aliyekuwa anatunga sheria kwa njia ya kauli, anatoa hukumu na kuzisimamia. Hofu ilikuwa ni kwamba kama umemuudhi mfalme, ukipelekwa kwake na wasaidizi wake ndiye awe hakimu wa kesi hiyo hiyo ambayo yeye ni mlalamikaji, basi kuna hatari kubwa ya kutomtendea haki mshitakiwa.

 

Hili ndilo lalamiko langu juu ya sheria hii ya magazeti iliyotumika kufungia magazeti ya Mtanzania na Mwananchi. Kwamba katika hili, Serikali ndiye mlalamikaji, lakini pia Serikali ndiye anasikiliza kesi hata kama amewasikiliza wahusika au la, na kisha ndiye anatoa hukumu. Hapa hakuwezi kuwapo utawala bora. Haki haiwezi kutendeka.

Kilipaswa kuwapo chombo huru, ambacho kitasimamia masuala yote ya habari kitaaluma na chombo hiki kikitoa uamuzi uwe haufungamani na upande wowote. Leo Waziri Mukangara anajigamba kuwa akipata fursa analifungia gazeti, kisha fursa hiyo inajitokeza mbele yake, ni wazi anamalizia hasira zake. Ilibidi kama gazeti limemuudhi, basi alipeleke mahakamani au kwenye chombo husika kisha uamuzi huru utolewe ndipo hatua husika zichukuliwe.

 

Nchi hii inao uzoefu wa Serikali kwenda mahakamani kuzuia baadhi ya taasisi zisitende kinyume na matakwa yake. Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kilipotaka kuitisha mgomo, Serikali ilikwenda mahakamani ikapata hati ya zuio. Chama cha Madaktari Tanzania kilipoitisha mgomo, Serikali ilikwenda mahakamani, tena usiku kuomba zuio.

Hapa shaka yangu ni moja. Inawezekana Serikali inawaheshimu sana walimu na madaktari, lakini kwayo waandishi wa habari ni vinyangarika visivyostahili haki za binadamu. Waandishi si lolote si chochote na hawana mchango wowote kwa taifa hili ndio maana hawastahili heshima yoyote kutoka serikalini. Tena nimesikia wanatunga sheria ambayo ni kali zaidi. Wanataka mwandishi atakayeandika wanachokiita uchochezi, basi afungwe jela miaka 5 na faini ya Sh milioni 5.

 

Nasema kama tumefikia huko, Rais Jakaya Kikwete waangalie sana wasaidizi wako. Wanaandaa mazingira ya kuchafua jina lako. Umejitahidi kwa kiwango kikubwa kujenga Serikali ya Uwazi na muda wote umekuwa mvumilivu, lakini sasa Waziri Mukangara anamomonyoa heshima yako kidogo kidogo. Leo angalia kuwa uamuzi huu alioufanya wa kufungia magazeti mawili dunia nzima ilivyoilaani Serikali yako.

 

Sitanii, inawezekana leo ukaona au waziri wako akasema maandishi yanayochapishwa ni kelele za mlango. Rwanda ilikuwa inaheshimika mno kimataifa. Vyombo vya habari vilianza kuhoji usafi wa Serikali ya Rais Paul Kagame, yeye akawa anavipuuza na kutunga sheria kali zaidi. Leo, tumeshuhudia Marekani ikiiwekea vikwazo Rwanda. Hata sisi kwa ubabe huu unaoendelea kupitia wasaidizi wako, unaweza kukuta tunafikia waliko Rwanda kwa sasa.

 

Naomba kuhitimisha kwa kusema mambo mawili ya msingi, na moja la nyongeza. La kwanza, Dk. Mukangara aache kuchukia vyombo vya habari. Pili, Sheria ikibadilishwa iwepo Bodi maalum au chombo kama ilivyo Mamlaka ya Mawasiliano kitakachosimamia tasnia ya magazeti badala ya utaratibu wa sasa. La mwisho dogo, nasema hata sisi waandishi wa magazeti inatupasa kuwa makini.

 

Umakini ninaousemea ni wa kujiepusha kwa hali yoyote ya kuandika habari zenye mwelekeo wa kuligawa taifa katika vipande. Nchi yetu ni hii tuliyomo. Ikiingia vitani na amani ikapotea hata hayo magazeti hatutapata pa kuyauzia. Hakuna mwananchi atakayepata muda wa kununua gazeti na kulisoma wakati risasi na mabomu vinalipuliwa na kuua watu wetu. Liwe jukumu la msingi kwa kila mwanahabari kuilinda amani ya taifa hili.

1177 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!