0l7c0711Nilimsikiliza Rais John Pombe Magufuli aliposema na Askari Magereza pale Ukonga, pia nilikuwako gerezani Ukonga wakati Rais Jakaya Mrisho Kikwete alipotembelea gerezani na kutoa kauli tete “pasua raha ndani ya taabu.”

Kikwete hakuwakusudia wafungwa mabaya isipokuwa aliukumbuka usemi walioutumia wapiganaji wa majeshi ya Tanzania mwaka 1978 walipokuwa mstuni kwenye vita ya kuyaondoa majeshi ya uvamizi ya Idd Amin Dada. Kikwete alikaribishwa na wafungwa kwa shangwe akaimbiwa wimbo uliomthibitishia jinsi wafungwa walivyofurahi, akijua wafungwa walivyo taabuni ndipo akakumbuka kauli ya wapiganaji hapo walipofungua chupa ya bia na kusema “pasua raha ndani ya taabu” lakini baadaye akatafsiriwa vibaya.

Wafungwa walifurahia ziara ya Kikwete magerezani kwasababu ilifufua matumaini yaliyopotea walijua baada ya Rais kujionea hali halisi atafanya mabadiliko yatakayowapunguzia mateso.

Magereza ni mfumo mgeni usio na asili ya kiafrika, tulianzishiwa na wakoloni lakini wao waliotuanzishia jela, wakaturithisha tuendelee nazo, huko kwao jela zao haziko kama zetu. Inabidi tuyabadilishe magereza yetu ili yatunze ubinaadamu yasigeuke taasisi zinazosimika ‘ushetani.’

Nilipomsikiliza Rais Magufuli nilitambua haielewi jela, hamwelewi mfungwa wala hajui kinachoendelea ndani ya ngome. Namshauri awasiliane na msaidizi wake Bw Msigwa ampatie kitabu changu kiitwacho “Maisha yangu gerezani- simulizi la siku 1888 za mateso.” Nilimpelekea Msigwa Ofsini kwake nikiamini angempatia Rais akisome ili akiupata uhalisia wa jela ulivyo ajue mabadiliko anayotakiwa kuyafanya.

Lakini nilipomsikiliza Rais Magufuli nikatambua aidha kijana wetu Msigwa hakumpatia kitabu kile ama kama alimpatia basi Rais hajapata wasaa wa kukisoma, namsihi mheshimiwa JPM atafute japo muda mfupi akipitie kitamsaidia katika dhamira yake ya kuibadilisha Tanzania.

Magereza ina majipu mengi yanayoumiza wafungwa pia yanayoumiza Askari wa kada ya chini, rais anatakiwa ayaelewe na kuyashughulikia ili kuwaletea wahanga ukombozi na pia kuinufaisha Tanzania kama taifa.

Matatizo ya Magereza yanagawika kwenye mafungu matatu, kwanza ni matatizo ya kisera ambayo ufumbuzi wake unaangukia moja kwa moja kwenye serikali kuu na unamtegemea Rais kama mtawala na kama mwanasiasa.

Pili yapo matatizo ya kimfumo ambayo ufumbuzi wake unaangukia kwenye utaalamu inatakiwa sheria na kanuni zisizofaa walizotuachia wakoloni zirekebishwe zisiendelee kutuathiri baada ya uhuru. Tatu ni matatizo yanayotokana na utawala au menejimenti ya magereza yenyewe, wahusika ni wakuu wa magereza na RPO wao. Uendeshaji wa gereza unatofautiana toka gereza moja hadi jingine, uendeshaji wa gereza la Ukonga hautafanana na gereza la Keko ama gereza la Segerea ingawaje magereza yote yako Dar es Salaam na yako chini ya bosi mmoja (RPO). “Ujelajela” unalazimisha kila gereza liendeshwe kivyake usiniulize ujelajela ni kitu gani itahitaji kurasa nyingi kuufafanua.

Kilichonihuzunisha kwenye kauli ya rais aliposema wafungwa wahenyeshwe tena wahenyeshwe kweli kweli, ni kujua kwamba hilo lazima litatafsiriwa vibaya na madhara yake na ‘impact’ yake haitabiriki.

Kutokana na mfumo wa Jela ulivyo kila mmoja ataitafsiri kivyake, tafsiri ya Kamishina mkuu haitafanana na tafsiri ya Mkuu wa gereza, wala tafsiri ya “Bwanajela” haitafanana na tafsiri ya Askari anayesimamia genge wanayemwita “meja.”

Tafsiri ya “meja wa genge” haifanani na tafsiri ya nyapara wala

‘Kiherehere’ hao kwenye jela za kilimo wana madaraka makubwa ambayo Magufuli hayaelewi, ndio wafalme wa jela.

Yawezekana Rais Magufuli alikwenda na kauli mbiu ya ‘hapa kazi tu’ akidhamiria wafungwa wasikae bure bali wafanye kazi, lakini nadharia za uraiani wakipelekewa wafungwa zitageuka janga kwasababu gerezani hakuna kazi ila kuna adhabu.

Kinachotakiwa kupelekwa gerezani ni sera na mipango iliyohakikiwa kwaajili ya kutekelezwa tu wasipewe mwanya wa kutafsiri chochote kama waonavyo.

 ‘Wajelajela’ wana usemi wa ‘adhabu kuambatana’ unaomaanisha Hakimu anapomhukumu mfungwa kwamba atakwenda jela kutumikia miaka 30, hasemi mfungwa atatumika kwa shughuli zipi wala mambo yatakayojitokeza wakati wa kuifanya shughuli hiyo. Yakitokea mabaya na yenye kuumiza maana yake mabaya hayo yameambatanishwa kwenye adhabu.

Msomaji piga picha ya watu wanaofungiwa saa tisa mchana ili waamke saa tisa usiku (usiulize nini kinasababisha walale mapema na kuamka mapema maelezo yake yatahitaji kurasa nyingi).

Wakifunguliwa baada ya kuhesabiwa ili kuhakiki kuwa wametimia, huenda kufoleni kunywa uji kikombe kimoja lakini usio na sukari, (usiulize sukari inayonunuliwa na serikali hupelekwa wapi kulijibu swali hilo itahitaji kurasa nyingine zaidi).

Baada ya kunywa uji wanachuchumaa kwenye foleni ya kutoka nje ya ngome kwenda ‘kuhenyeshwa’ nyapara anabeba mzigo wa majembe na ‘kiherehere’ anabeba mzigo unaofanana na kuni (huo ni mzigo wa fimbo). Nyuma na pembeni ‘mameja’ wa genge walionuna wamebeba bunduki zenye risasi za moto tayari kulikabili tukio lolote litakalojitokeza.

Msafara ukifika shambani wafungwa wanapangwa ama wanatandazwa kwenye ‘ngwe’ zao, wao wajelajela huwaita ‘watandan’gwe.’ Upana wa ‘ngwe’ huwa mita mbili au tatu lakini urefu ni mpaka unapoishia upeo wa macho. Wafungwa wakikabidhiwa majembe wanatakiwa  kuinama hawaruhusiwi kusimama wala kugeuza macho kushoto ama kulia, ‘mtandangwe’ anayepepesa macho kushoto na kulia maana yake anatafuta nafasi ya kutoroka, kazi ya kiherehere ni kumdhibiti kwa fimbo, hizo fimbo za kiherehere hazina idadi ‘mtandangwe’ anachapwa kama farasi anavyochapwa ili kumwongezea kasi.

Shughuli ya kulima ikianza ndipo zinapoanza kusikika sauti za fimbo wafungwa wakicharazwa migongoni, mtu halii isipokuwa kuugua kimya ndani kwa ndani, hata akilia ni kazi bure kilio hakibadilishi lolote. Kiherehere atachapa kama atakavyo, Jua likiwaka ndoo ya maji huwekwa mwishoni mwa ‘n’gwe’ mfungwa anapomaliza ndipo hujipoza akinywa maji, asiyemaliza ngwe yake kiu itamtesa ndipo hutokea wengine kuzimia. ‘Wajelajela’ huita ‘kufloti’ mfungwa akifloti nyapara atakwenda kugusa mboni ya jicho akiona mtu hastuki ndipo atamwambia meja huyu kweli amefloti. Naye meja ataingiza mtutu au mdomo wa bunduki yake kwenye haja kubwa ya aliyezimia kujihakikishia mwenyewe akiridhika kuwa mtandangwe amefloti, atawaamuru manyapara wamweke kivulini.

Hayo siyo ndiyo ya mwisho kwa mfungwa kwani asipomaliza ngwe yake akirudi jela kama ni siku ya ugali atakutana na ‘kipaso’ kama ni siku ya wali atakutana na ‘kibangala.’

Kipaso ni kiasi kidogo cha ugali anaopewa mfungwa mara nyingi huwa kwenye bakuli lililopondeka kiasi cha kuwa nusu ‘fulu’ badala ya fulu kamili, ugali uliojaa kwenye bakuli jela huitwa fulu.

Mfungwa anayeambulia ‘kipaso’ ama ‘kibangala’ anaweza kukutana na balaa jingine kwamba ametoka gengeni wakifika gerezani hasa wale wanaochelewa kurudi na kukuta wenzao wamekwishafungiwa ndani ya selo, hukutana na kazi za dharula zinazoibuka papo kwa papo.

Hapo hatakumbukwa kwamba asubuhi amepata kikombe kimoja tu cha uji, wakikutana na kazi ya kuteremsha magunia ama matofali na nyinginezo watatakiwa kuanza upya na wanaweza kuendelea na kazi hiyo ya dharula hadi iishe hata kama ni saa mbili usiku.

Mfungwa hathubutu kutamka kwamba nimechoka, kwani kutamka hivyo kunahesabiwa sawa na kumtukana meja, ataambulia kipigo na kazi ataifanya ‘kiserikali.’

Jela ‘kiserikali’ ina maana tofauti na inavyojulikana uraiani, nyapara akitumwa kumchukua mtu ama kumleta ‘kiserikali’ maana yake ni kumleta kinguvu bila chembe ya ubinaadamu, mfungwa atafika akiwa hoi kwa vipigo kutoka kwa manyapara na kuburuzwa kama gogo.

Vivyo hivyo akiagizwa asimamiwe ‘kiserikali’ maana yake afanyishwe kazi kinguvu na ubinaadamu uwekwe kando kinachotakiwa kazi iishe.

Hao ndio ambao Rais Magufuli anataka ‘wahenyeshwe’ sijui wahenyeshwe vipi zaidi ya wanavyohenya siku zote? Rais akitaka kuupata uhalisia afanye ziara ya ghafla kwenye gereza lolote la kilimo, akifika amwambie bwana jela ampeleke akalione genge shamba, kisha atembee tu kwa miguu toka mwanzo wa ngwe hadi mwisho. Kwakuwa yeye ni mwalimu wa mahesabu anaweza kukisia uzito kwa binaadamu aliyetumia nguvu kupalilia tangu mwanzo hadi mwisho kwa masaa nane au tisa.

Najua Maaskari hawatakubali rais aone wafungwa wanavyolimishwa lakini walau Rais Dk. Magufuli ayaone mashamba wanayolima baadhi ya Watanzania wanaosulubiwa kwenye nchi inayodhaniwa iko huru.

Rais Magufuli atembelee mashamba ya mpunga ya magereza ya mkoa wa Morogoro na Pwani awaone wafungwa walivyoathirika ngozi kutokana na kuzama kwenye madimbwi wakati waking’olea mpunga, wanaonekana kama watu waliougua ugonjwa wa ndui, atembelee shamba la Bi Monica (siyo shamba la mtu bali ndilo jina lake) shamba linaloongoza kwa ‘upupu.’

Mtu angetarajia kwamba jeshi la Magereza linalotumia nguvu kazi ya wafungwa (kikatili hivyo) katika uzalishaji, lingejitegemea likajilisha na isingekuwako haja ya serikali kutoa zabuni kwa wafanyabiashara kupeleka gerezani vyakula kama maharage, unga wa mahindi, mchele, mikate, dagaa, nyama na maziwa.

Kwasababu jeshi lenyewe lina uwezo wa kuzalisha, mahindi, maharage, mchele, ngano, linaweza pia kuendesha shughuli za uvuvi, hata ufugaji samaki, ng’ombe wa maziwa na nyama. Lakini mambo hayako hivyo kwasababu tenda ni dili na wafungwa hutumikishwa tu hawafanyi kazi za serikali kulinufaisha Taifa.

Inabidi Rais Magufuli auelewe uhalisia wa magereza yetu, ili aanzishe mchakato wa kuligeuza jeshi hili likamilishe ndoto yake ya kuiona Tanzania yenye viwanda. Jeshi la Magereza likiendeshwa kisayansi linaweza kujitegemea, linao uwezo wa kuzalisha mahindi, maharage, ngano mchele na miwa, lakini kilimo chake lazima kibadilike wafungwa wasilimishwe kwa mikono. Jeshi liwe mfano wa mapinduzi ya kilimo kinachotumia utaalamu na zana za kisasa, kila kinachozalishwa kiratibiwe ili kinufaishe taifa badala ya kuishia kunufaisha watu binafsi.

Jeshi linaweza kuwa na viwanda likazalisha sukari, nguo hasa khaki, linaweza kuwa na kiwanda cha kubangua korosho, kiwanda cha kuzalisha viatu endapo litatengewa fedha ikanunuliwa mitambo kama ilivyotengwa fedha za kanunulia ndege alipoamua kuifufua ATCL.

Rais afufue kiwanda cha gereza la Ukaranga (Moshi) zamani lilitengeneza viatu vilivyotumika JKT, Polisi na JWTZ, afufue kiwanda cha gereza la Ukonga zamani lilishona sare zote za Polisi, JWTZ na Magereza, Gereza la Ukonga (kiwanda) wanaweza kutengeneza samani badala ya serikali kuagiza samani kutoka nje iwape zabuni hiyo. Ila haya ninayopendekeza yatawezekana ndani ya mfumo mpya sio ule aliotuachia mkoloni, huo mfumo mpya utawezesha serikali kuu kunufaika, gereza la mahali pamoja litanufaika, askari anayewasimamia wafungwa atanufaika na pia wafungwa wanaoshirikishwa kwenye uzalishaji watanufaika.

By Jamhuri