Katika makala zilizopita nimeshauri Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuanzisha Kitengo cha Kuanzisha na Kukuza Biashara. Ni wiki ya tano sasa nikiwa naandika makala hii kuunga mkono uamuzi wa Rais John Magufuli na Waziri wa Fedha, Dk. Philip Mpango, kupiga marufuku TRA kufunga biashara ya mtu yeyote hapa nchini, isipokuwa kwa wakwepa kodi sugu, ila hiyo nayo ni lazima iwe kwa kibali cha Kamishna Mkuu wa TRA.
Katika makala ya wiki iliyopita, nilieleza umuhimu wa wananchi kupimiwa ardhi wakawa na hati miliki watakazozitumia kukopesheka benki na kulala maskini wakaamka matajiri. Nimeeleza mfumo wa kibaguzi katika masuala ya fedha unaowanyima fursa Watanzania wazawa dhidi ya wageni.

Sitanii, wageni wamewekewa Kituo cha Uwekezaji (TIC) ambacho kinawasaidia kukimbiza makaratasi yao ya usajili, kuwapa ushauri wa kikodi, kuwatafutia maeneo ya kuwekeza kama ni ardhi kupitia Kamati ya Taifa ya Ardhi na kuwashauri juu ya aina ya kodi zinazolipwa. Mimi nafahamu hapa kwetu hatuna kitengo cha kiserikali kinachosaidia Watanzania kupata taarifa hizi muhimu. Kama kuna mtu anasema ninachosema si cha kweli, ajifanye anajikuna!
Baada ya makala ya wiki iliyopita, nimepata mrejesho mkubwa hadi nikaogopa. Sikufahamu kuwa Watanzania wengi wanafanya biashara kwa kutegemea matangazo yanayopeperushwa na magari yenye maofisa wa TRA.
“Niliposikia TRA wanasema Desemba 31, ni siku ya mwisho ya kulipa kodi, nikaenda kuuliza ninalipa kiasi gani na ninalipaje? Ofisa wa TRA aliniambia kama sijakadiriwa mapato, hadi siku hiyo sipaswi kulipa kodi,” huyu ni mfanyabiashara mmoja.
“Mimi mpaka juzi nilikuwa sifahamu kuwa kumbe kodi inalipwa kutokana na faida unayopata. Nilifikiri wanakata mtaji wako unalipa kodi hadi msingi unakwisha. Baada ya kusoma makala yako nilikwenda TRA, nikaambiwa nikitengeneza hesabu za biashara yangu kama sikupata faida sitalipa kodi. Nilishangaa sana,” amesema mfanyabiashara mwingine aliyeko Dar es Salaam.

Sitanii, mwingine kutoka Shinyanga, ambaye nimeamua kumfikishia ujumbe huo Mkurugenzi wa Elimu kwa Walipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo, na ninamshukuru ameufanyia kazi, mtu huyo anasema vitambulisho vya ujasiriamali wanaviogopo kwani hadi kupatiwa wanapewa Namba ya Mlipa Kodi (TIN), hivyo kwao hii wanaiona ni hatari kubwa watadaiwa ‘Kodi ya Kichwa.’
Kimsingi, nimebaini kuwa eneo la biashara kuna upungufu mkubwa wa uelewa. Ni kwa msingi huo, nimeamua kuanzia wiki ijayo nitaandika makala inayoonyesha taratibu za kisheria na mazingira tunayoishi Tanzania juu ya jinsi ya kuanzisha biashara, aina ya biashara, kampuni au mtu binafsi, aina ya kodi zinazolipwa, aina na idadi ya leseni unazopaswa kuwa nazo, jinsi na umuhimu wa kutunza hesabu, andiko la mradi, bajeti ya biashara yako, masoko, umiliki wa mali-ardhi kisheria kama msingi wa utajiri na mada nyingine nyingi zinazohusiana na biashara.

Sitanii, kwa mrejesho nilioupata na kwa kutumia elimu yangu ya Shahada ya Uzamili (MSc) katika Uongozi wa Biashara, naamini nitachangia kuinua au kuboresha mazingira ya Watanzania kufanya biashara, kukopesheka benki na mwisho wa siku kuwa washiriki katika uchumi wa viwanda na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Katika kufanya hivyo, na kwa kufahamu kuwa wafanyabiashara wengi muda wao umebana na hawataki kusoma maandiko marefu, kwanza nitachapisha makala katika Gazeti hili la JAMHURI na pili, mbele ya safari vitabu kutokana na maandiko haya, vitakavyokuwa na kurasa kati ya 80 na 100 nikiamini kuwa vitaongeza uelewa wa wananchi kufanya biashara, kulipa kodi na kuwa matajiri.
Mwisho, ingawa sikutaka kuandika siasa, ila kwa kuwa nimeulizwa na wengi niseme kidogo juu ya Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa kuwa umeleta mapinduzi makubwa Tanzania.
Marekebisho ya Kifungu cha 11B na 11C sasa yanaruhusu vyama vya siasa kuungana au kuunda umoja kisheria badala ya kuwa na ushirikiano wa kienyeji kama wapinzani walivyounda UKAWA mwaka 2015. Jambo hili halijapata kuwapo tangu nchi hii imezaliwa, ni hatua kuelekea mgombea binafsi.

Sitanii, fursa hii ikitumiwa vema, inaweza kukuza upinzani wenye malengo ya kujenga taifa imara, na si wa kufuja ruzuku. Hili serikali imefanya jambo jema. Nasisitiza, hiyo nimechepuka kidogo tu, kwani nimeamua kuandika biashara, siasa naziweka kando. Tukutane wiki ijayo kupitia safu hii ya SITANII katika makala mpya ya ‘Jinsi ya Kuanzisha Biashara Tanzania.’ Mungu ibariki Tanzania.

657 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!