Kauli ya kampeni ya urais ya Rais John Magufuli ilikuwa: “Hapa ni kazi tu!”

Ni kauli nzuri kama haiishii kwenye kampeni pekee. Kwenye moja ya hotuba zake za kampeni alitamka: “Deni langu kwenu ni kufanya kazi.” Watanzania wote wanasubiri kutimizwa kwa hiyo ahadi.

Kazi ndiyo msingi wa kila kitu. Maandiko ya dini kuu zote yanasisitiza umuhimu wa kufanya kazi. Surutal Jumua, aya ya 10 inatamka: “Na itakapokwisha Sala, tawanyikeni katika ardhi mtafute fadhila za Mwenyezi Mungu, na Mkumbukeni Mwenyezi Mungu kwa wingi (ili msipate kufanya mabaya), ili mpate kufaulu.”

Kwa kifupi Uislamu unasisitiza siyo sala pekee, lakini pia kufanya kazi. Enzi hizo riziki ilipatikana kwenye ardhi, lakini leo inapatikana sehemu nyingine nyingi. Jambo la msingi ni kuwa kila mwenye uwezo wa kazi anao wajibu wa kufanya kazi.

Kwenye Biblia inatamkwa: “Kwa kweli pia, tulipokuwa pamoja nanyi, tulikuwa tukiwapa ninyi agizo hili: Ikiwa yeyote hataki kufanya kazi, basi na asile chakula” (2 Wathesolanike: 10).

Hata wasiofuata dini hizi mbili wanafuata misingi inayosisitiza umuhimu wa kufanya kazi. Kwa desturi, jamii nyingi hazikuvumilia mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi kujipangia kazi ya kula tu na kuacha kazi za uzalishaji. Ni wazee, watoto wachanga, na wasiojiweza tu ambao waliosamehewa.

Kwa hiyo labda siyo ajabu kuwa hata viongozi wetu wengi kabla na baada ya uhuru walisisitiza umuhimu mkubwa wa kazi ili kuleta maendeleo ya taifa. Kaulimbiu ya serikali ya awamu ya kwanza ilikuwa ni Uhuru na Kazi.

Lakini tukiri kuwa sasa hivi tunashuhudia rika ambayo haioni umuhimu mkubwa wa kufanya kazi ila ambayo ina haraka ya kupata mafanikio – kwa njia yoyote ile. Anayefanya kazi kwa muda mrefu akafikia kustaafu bila kuonyesha utajiri mkubwa anaitwa mjinga. Aliyekusanya mali nyingi haulizwi kazitoa wapi, bali anajenga msururu wa watu wanaompa sifa za kila aina. Na mara nyingi ni watu waliokusanya utajiri wa aina hii ndiyo ambao kila ukikaribia uchaguzi hutafutwa na wapambe kuombwa wagombee nafasi mbalimbali za uongozi.

Ndiyo maana baadhi yetu tumefuatilia kwa makini kauli ya Mheshimiwa Magufuli wakati wa kampeni ya “Hapa ni Kazi tu.” Ikibaki kuwa kauli ya kampeni tu haitusaidii kitu kama taifa kama nyenzo muhimu ya kubadilisha maisha ya kila mmoja wetu. Lakini serikali yenye watu wachapa kazi ni upande mmoja tu wa sarafu; upande wa pili ni kuwajibika kwa mtu mmoja mmoja. Nakubaliana na baadhi ya wale wanaoona kuwa wajibu wa kuleta maendeleo ni jitihada binafsi za kila mtu peke yake, na baadaye ndiyo kuiwajibisha Serikali iweke nyongeza zipi, au mazingira gani, ya kusababisha zile juhudi za kila mmoja kuwa ni maendeleo yetu mmoja mmoja na hatimaye, maendeleo ya taifa zima.

Wapo watu wengi, hasa wale wanaoishi mijini, ambao hawana kazi au uwezo wa kujiajiri, lakini kuna watu wengi wenye shughuli za kufanya, au kwa kuajiriwa au kwa kujiajiri wenyewe, ambao hawaweki jitihada, bidii, na kiwango cha kutosha cha maarifa kuhakikisha kuwa kazi zao zinaleta manufaa.

Baadhi ya wakosoaji wa Mheshimiwa Magufuli wakati wa kampeni walisema kuwa Tanzania haihitaji rais ambaye ni meneja, kwamba yeye hana uwezo wa kuwa kiongozi mkuu wa nchi. Maana yake ni kuwa meneja anafanya kazi kwa kufuata maelekezo ya wakubwa wake. Kwa lugha ya kibiashara inaweza kuwa bodi ya wakurugenzi, au mwenye kampuni. Meneja hana mipango ya muda mrefu. Haoni mbali, anaona karibu na mara nyingi mipango siyo ya kwake, ni ile iliyopangwa na bodi au anafuata maelekezo ya mmiliki au mkurugenzi mkuu.

Labda ni kweli, lakini ukweli wa hayo tunaweza kuupima baada ya miaka mitano. Lakini inafahamika pia kuwa wapo mameneja ambao walijifunza vizuri kazi yao na wakafikia hatua ya kuwa viongozi wa mfano. Mtaalamu mmoja wa meli alisema nahodha mzuri ni yule ambaye alianza kazi ya chini kabisa, kwenye mtumbwi, akijifunza mbinu nyingi na taratibu za kazi za tasnia na halafu akahamishia uzoefu wake kwenye vyombo vya maji vikubwa zaidi hadi kufikia ngazi ya juu kabisa.

Chuo cha urais hakipo, lakini uzoefu wa kazi mbalimbali serikalini na hata kwenye sekta binafsi unaweza kumpa mtu msingi wa kufanya kazi ya urais.

Lakini hata rais bora hafanyi kazi peke yake. Anahitaji watu wenye elimu ya kutosha na ambao wanakubali ajenda yake na ya chama chake juu ya maendeleo ya nchi na watu wake.

Wanapaswa kuweka jitihada kubwa kuhakikisha kuwa nguvu yote ya Serikali pamoja na sera zilizopo zinaelekezwa kutimiza ajenda hiyo. Kwa mtu yeyote ambaye amewahi kusimamia hata mtu mmoja tu kwenye kazi atafahamu kuwa msingi mkuu wa mafanikio ni kuwa na watu waadilifu wa kutekeleza malengo yaliyokusudiwa. Kabla ya hapo “hapa ni kazi tu” itaishia kuwa maneno tu mazuri yaliyosemwa kwenye kampeni za mwaka 2015.

Tunaambiwa kuwa Rais Paul Kagame wa Rwanda huwauliza wale aliyowateua kuwa mawaziri wake wamueleze watafanya kazi gani ndani ya mwaka mmoja. Baada ya mwaka huwauliza wamefanya nini kutekeleza yale waliyoahidi. Wale ambao hawajatimiza hawapewi muda wa kutoa visingizio. Wanapisha nafasi na anateua wengine kushika nafasi zilizoachwa. Watu wengine wanaita huu ni ubabe, wengine wanatumia lugha kali zaidi. Na kuna wengine wakati wa kampeni wametahadharisha kuwa Rais Magufuli naye atakuwa mbabe kwa mtindo huu.

Kama ubabe wa aina hii unazaa matokeo, na unaleta maendeleo kwa wengi ni ubabe ambao utakubalika na wengi. Tunasubiri kazi.

By Jamhuri