magufuli1Salaamu kwako Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Magufuli.

Baada ya salamu, mimi ni mzima na ninaendelea kutega masikio na macho yangu kuhusu kasi uliyoingia nayo madarakani.

Rais Magufuli, nakuandikia barua hii kukupongeza, lakini pia kukueleza kwamba pamoja na kuanza utendaji wako kwa kasi nzuri usije ukayumbishwa na mtu yeyote.

Itakumbukwa kwamba mara baada ya kuanza kazi ulifanya ziara za ghafla Hazina na Muhimbili tena kwa miguu na kujionea namna Watumishi wa Serikali wanavyofanya kazi kwa mazoea.

Lililonifurahisha kuliko yote ni lile la hivi majuzi wakati ukihutubia Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Dodoma ulipotoa makucha yako na kuamua kutangaza vita na mafisadi, wafanyakazi wazembe, watu wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya hasa mapapa na wengine.

Pia namna ulivyoamua kufyeka pesa za sherehe ya wabunge zilizokuwa na lengo la kupongezana ambazo zilifikia Sh milioni 250 ambazo zilikusudiwa kutumiwa na Ofisi ya Bunge kwa ajili ya kupongezana baada ya kumaliza mkutano wa kwanza.

Katika hilo nakupongeza kwa kuamua kuzifyeka fedha hizo na kuamua zitumike sh milioni 15 pekee kwa ajili ya shughuli hiyo huku ukielekeza fedha zinazosalia zikasaidie kununulia vitanda katika hospitali ya Muhimbili. 

Binafsi umenikosha kwa kasi uliyoanza nayo ya kuamua kutumia nafasi uliyonayo kutuhakikishia Watanzania namna ambavyo utaiongoza nchi hii kwa namna ya pekee.

Dk. Magufuli binafsi sina shaka wala ubishi na nafasi uliyoishika kwani matunda ya utukufu wako kikazi nilianza kuyaona tangu ulipokuwa Waziri tangu serikali ya awamu ya tatu iliyokuwa ikiongozwa na Rais Mstaafu Benjamin Mkapa pamoja na ile ya  awamu ya nne iliyoongozwa na Rais Mstaafu Dk. Jakaya Kikwete.

Pamoja na kuahidi kufanya kazi kikamilifu katika serikali yako ya awamu ya tano hasa kwa kushughulikia masuala yasiyokuwa na tija kama vile kutoruhusu safari za nje, matumizi mabaya ya fedha yasiyo na mpango na mengine nakushauri pia uhakikishe baraza lako utakaloliunda linakuwa na mawaziri wanaojali watendaji wao kikamilifu.

Dk. Magufuli, zipo wizara ambazo ni nyeti zinazohitaji kuwa  na mawaziri wenye kusimamia vyema shughuli zao kama ulivyo wewe na ambao watahakikisha tizara na taasisi watakazoziongoza zinatenda haki kwa watendaji wake kwa kuhakikisha wanapata maslai  mazuri.

Baadhi ya wizara ambazo unastahili kuwaweka mawaziri wa uhakika ni wizara ya fedha, wizara ya mambo ya ndani, wizara ya nishati na madini, wizara ya ulinzi na jeshi la kujenga taifa, wizara ya elimu na wizara ya afya. 

Ndugu rais, wizara ya fedha ndio muhimili mkuu wa nchi hii hivyo una wajibu wa kumteua waziri ambaye atahakikisha anaisimamia ipasavyo wizara hiyo vinginevyo ukimweka mtu atakayeshindwa kufuata nyayo zako utasababisha nchi ikose mapato yake ipasavyo.

Dk. Magufuli, wizara ya mambo ya ndani vivyo hivyo ni wizara muhimu katika nchi hii hivyo unapaswa kumweka mtu atakayeisimamia vyema hasa ambaye ataweza kuhakikisha maofisa wa jeshi la polisi, la magereza,uhamiaji,  na wengine maslai yao yanasimamiwa na hata kuongezwa kwani wao ndio nguzo kuu ya nchi.

Ndugu Rais, ni ukweli ulio wazi kwamba bila askari polisi usalama wa nchi hii utakuwa shakani hivyo tafadhali kupitia barua yangu hii naomba utafakari kwa kina niliyokuandikia.

Vivyo hivyo wizara ya elimu inatakiwa kuwa na waziri mwenye ari ambaye ataiongoza kikamilifu hasa utekelezaji wa maagizo yako uliyoyatoa ya kuhakikisha elimu kuanzia darasa la kwanza hadi kitano cha nne inatolewa bure, pia kusitisha michango yote ambayo imekuwa ikitozwa katika miaka mingi sasa.

Ndugu Rais, tumeshuhudia huko nyuma watangulizi wako wakiweka sera ya elimu bure kwenye shule za msingi pamoja na kuweka ada kiasi kwa shule za sekondari za serikali lakini kilio kikubwa kimekuwa kikiwakumba wazazi kutokana na kudaiwa michango mingi isiyo na tija ambayo ukiijumlisha inaweza kufikia ada ya shule za sekondari binafsi ambazo ni za kawaida,

Ndugu Rais, jingine muhimu la kuliangalia kupitia waziri wako wa elimu utakayemteua ni jinsi ada za shule za msingi binafsi na sekondari zinavyowachoma wazazi.

Kama ambavyo tamko kutoka wizara ya elimu lilivyotoka hivi karibuni la kuweka ada elekezi  kwa shule za msingi binafsi na za sekondari namshauri waziri wa elimu utakayemteua ayasimamie hayo kwa ukamilifu bila kumwogopa mtu yeyote!.

Kwa wizara ya ulinzi na jeshi la kujenga taifa nakushauri umteue pia waziri bora ambaye atahakikisha mipaka ya nchi yetu inakuwa salama pia atakayesimamia vilivyo wizara hiyo.

Na kwa upande wa wizara ya afya waziri utakayemteua una haja ya kumtafakari kwa macho mawili ili aweze kuyafatilia kwa kina masuala ya afya hasa kwa kuzimulika taasisi atakazozisimamia ili kuzifanya afya za Watanzania ziwe mahali pazuri na salama.

Dk. Magufuli, katika kutekeleza majukumu yako yote nakushauri usiyumbishwe na mtu wa aina yeyote bali simamia dhamira yako kwa haki na usawa. 

Ndugu Rais, kwa leo sina mengi zaidi ya hayo. Nakutakia utendaji kazi uliotukuka utakaosimamiwa na mikono mitukufu ya Mwenyezi Mungu kwa maombi ya Watanzania.

Wako mtiifu katika kulijenga taifa.

1566 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!