Matukio makubwa matano yaliyoathiri Haki za Binadamu mwaka 2017

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimetoa ripoti ya hali ya Haki za Binadamu kwa mwka 2017 na kuipa jina la Watu Wasiojulikana ambapo imechambua kwa undani masuala mbalimbali yaliyoathiri na pia yale yaliyoimarisha haki za binadamu nchini katika kipindi hicho.

Kituo hichi kimeeleza kuwa, matukio ya kutekwa na kuteswa nkwa raia na watu wasiojulikana, uvamizi wa ofisi za IMMA na Clouds Media Group, kukataza mikutano ya kisiasa nje ya majimbo, miili ya watu kukutwa ndani ya viroba na kushambuliwa/kuuawa kwa watu mbalilimbali ni matukio makubwa yaliyochangia kuathiri haki za binadamu mwaka 2017.

Akiwasilisha ripoti ya haki za binadamu Tanzania (2017), Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dkt Hellen Kijo Bisimba amesema, ukiukwaji wa haki za binadamu kwa mwaka 2017 uliongezeka zaidi ukilinganisha na mwaka 2016 ambapo hatua muhimu zisipochukuliwa inaweza kuvuruga amani na demokrasia iliyojengwa kwa muda mrefu na waasisi wa taifa.

“Haki za kiraia na kisiasa zilivunjwa zaidi, hasa haki ya kuishi, haki dhidi ya ukatili, haki ya kuwa huru na usalama wa mtu, uhuru wa kujieleza, uhuru wa kukusanyika na uhuru wa kujumuika. Kuminywa kwa haki hizi pia kuliathiri haki ya kushiriki katika utawala/serikali hususan haki ndogo ya kushiriki katika muasuala ya siasa,” alisema Dkt. Hellen

Ripoti hiyo ikielezea matukio hayo, imebainisha kuwa, Mwanamuziki la Roma Mkatoliki na mwenzake waliripotiwakutekwa na kuteswa na ‘watu wasiojulikana, watu wasiojulikana kuvamia ofisi za IMMMA na mkutano wa Chama cha Wananchi (CUF) na kuvamiwa kwa Clouds Media Group na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Matukio mengine ni, kukataza mikutano ya kisiasa nje ya majimbo, Mnadhimu Mkuu wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, alishambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na ‘watu wasiojulikana’ nje ya makazi yake Dodoma. Kushambulizi na mauaji ya kutisha ya askari polisi, raia na viongozi katika eneo la Kibiti na maeneo mengine ya Mkoa wa Pwani.

Tukio jingine ni kutoweka katika mazingira ya kutatanisha kwa mwanahabari kutoka kampuni ya Mwananchi Novemba 2017 Azory Gwanda, ambaye alidaiwa kuchukuliwa na ‘watu wasiojulikana’ nje ya nyumba yake katika Mkoa wa Pwani.

Ripoti hiyo imebainisha kuwa haki iliyovunjwa zaidi ni haki ya kuishi kutokana na kuendelea kwa mauaji ya kujichukulia sheria mkononi, mauaji yanayofanywa na vyombo vya dola na mauaji yatokanayo na imani za kishirikina.

“Mpaka kufikia Disemba 2017, idadi ya vifo vilivyotokana na na wananchi kujichukulia sheria mkononi ilifikia 917 ambavyo ni vifo 5 zaidi ya vile vilivyoripotiwa mwaka 2016. Mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa kwa matukio ya kujichukulia sheria mkononi, ukifuatiwa na Mbeya, Mara, Geita, Tanga na Kigoma.” Imeeleza ripoti hiyo.

Dkt. Hellen alisema kuwa, hatua za makusudi zinahitajika kutetea na kulinda raia na mali zao ili amani izidi kushamiri kwenye jamii ya watanzania.

By Jamhuri