*Manowari, ndege vita kufunika anga la Tanzania

*Mashushushu zaidi ya 60 kumlinda akiwa D’Salaam

*Vioo maalumu visivyopenya risasi vyaletwa toka USA

Rais Obama anayetarajiwa kuwasili hapa nchini wiki ijayo, ziara yake itakuwa na mambo mengi ya kusisimua na kuonesha ukwasi wa Taifa hilo lenye nguvu za kijeshi na kiuchumi kuliko taifa lolote katika sayari hii ya dunia.

Limekuwa ni jambo la kawaida kwa marais wa Marekani kuwa na mbwembwe nyingi za kiulinzi, lakini ikakadiriwa kwamba hii ya Rais Obama katika Tanzania na kwenye mataifa mengine mawili ya Afrika – Senegal na Afrika Kusini – itavunja rekodi za gharama.

 

Mwishoni mwa wiki, dege kubwa la Jeshi la Anga la Marekani lilitua kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere, na kushusha magari na vifaa mbalimbali kwa ajili ya ulinzi wa Rais Obama.

 

Marais wawili wa Marekani wameshazuru Tanzania. Marais hao ni Bill Clinton na baadaye alikuja Rais George W. Bush. Hata hivyo, ziara hii ya Obama inatarajiwa kuvunja rekodi kwa mapokezi na mbwembwe nyingine za kiulinzi ambazo kwa kawaida hufanywa na Wamarekani.

 

Kiasi cha dola milioni 80 hadi milioni 100 za Marekani kinatarajiwa kutumia. Kiasi hicho ni sawa na Sh bilioni 131.2 hadi Sh bilioni 164. Hadi wiki jana, kiwango cha kubadilisha fedha dola moja ya Marekani kilikuwa sawa na wastani wa Sh 1,640.

 

Mamia ya mashushushu wa Kikosi cha Ulinzi wa Rais wa Marekani (US Secret Service) tayari wameshasambazwa katika maeneo ya usalama nchini Tanzania, Senegal na Afrika Kusini. Marekani inatambuliwa kwa kuwa na nguvu kubwa za majeshi yote – nchi kavu, angani na majini. Kwa sababu hiyo, manowari za Jeshi la Vita la Marekani zinazotumika kubeba ndege vita, zitakuwa karibu na maeneo yote atakayozuru Rais Obama ambaye baba yake ni Mkenya. Kwa Tanzania, manowari itatia nanga pwani kwa ajili ya dharura, ikiwa na timu ya matabibu.

 

Ndege za kijeshi za kubeba mizigo zitasafirisha magari 56, zikiwamo Limousines 14 na magari ya mizigo matatu yote yakiwa na vioo visivyopenya risasi. Hotelini atakamofikia kiongozi huyo na familia yake, vioo visivyopenya risasi vitawekwa katika madirisha ili kuzuia hatari zozote.

 

Kati ya magari hayo, kutakuwapo pia gari maalum kwa ajili ya mawasiliano ya simu na video, gari la kuzuia mawasiliano ya redio kuzunguka gari la Rais Obama, na gari la wagonjwa linalojitosheleza kwa kila kitu. Gari hilo lina uwezo wa kudhibiti maambukizi ya kibaiolojia na kikemikali.

 

Mashushushu wa Secret Service husafirisha magari kama hayo, pamoja na vioo vya kuzuia risasi, katika ziara nyingi, ikiwa ni pamoja na zile za ndani ya Marekani. Lakini kwa vile kuna nchi tatu zinazohusika katika ziara hiyo, kunahitajika seti tatu za maandalizi hayo kwa vile hakuna muda wa kutosha wa kuhamisha vifaa.

 

Mashushushu 100 wanahitajika kama ‘waangalizi’ – kumudu maeneo ya kumzunguka Rais – katika kila mji atakaozuru. Mashushushu 66 wanahitajika kumpokea Rais Obama jijini Dar es Salaam. Kabla kufutwa kwa ziara ya mbugani, ziada ya mashushushu 35 ilijumuishwa kwenye maandalizi hayo ili kumlinda Rais, mkewe na mabinti zao.

 

Kadhalika, kati ya mashushushu 80 hadi 100 watasafiri na kufanya kazi kwa shifti kwa saa 24, kwa ajili ya ulinzi wa Rais Obama na familia yake, vikosi vya kupambana na mashambulizi (counterassault teams) na waandaaji wa lojistiki.

 

Maafisa walisema Secret Service haitaki ziara ya Rais pasipo kituo cha hali ya juu cha jirani cha kukabili maradhi. Kitengo cha utabibu cha Ikulu hufanya uamuzi kuhusu hospitali gani Rais awapo ziarani nje ya nchi kinakidhi viwango.

 

Wakati wote huo, anga ya Tanzania itakuwa ikitawaliwa na ndege vita kwa lengo la kuimarisha ulinzi kwa saa 24. Wakati huo wote Jeshi la Marekani kwa kushirikiana na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ndiyo watakaokuwa vinara wa ulinzi wa anga. Hata hivyo, bado ukweli unabaki pale pale kwamba ni Wamarekani watakaoshika kila idara inayohusu ulinzi na usalama kwa wakati wote ambao Rais Obama atakuwa hapa nchini.

 

Familia ya Obama – mkewe Michelle na watoto wao wawili, Natasha (Shasha) na Malia – inatarajiwa kuwapo kwenye ziara hiyo ya kihistoria hapa nchini.

 

Famili hiyo ilipanga kuzuru Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, lakini safari hiyo imefutwa. Awali ilitarajiwa kwamba ziara hiyo ya Mikumi ingehusisha kikosi maalum cha kupambana na mashambulizi kutoka kwa magaidi au kwa wanyama wakali. Walipangwa kuwapo wadunguaji mahiri wenye uwezo wa shabaha wa hali ya juu ambao wanaweza kuwaua wanyama wakali kama simba, duma na wengine bila shaka yoyote.

 

Ziara hiyo imefutwa kutokana na kile kilichoelezwa kwamba ni kupunguza gharama za kusafirisha walenga shabaha hao na vifaa vyao, jambo ambalo lingepandisha juu mno gharama nzima za ziara ya kiongozi huyo. Kufutwa kwa utalii mbugani ndiko kulikoibua mjadala kwenye mitandao na vyombo vya habari kwamba Rais Obama ameahirisha ziara yake nchini Tanzania. Neno safari wao walidhani ni safari ya kutembelea Tanzania, lakini kwa kimombo neno hilo lina maana ya utalii mbugani.

 

Kutokana na kufutwa kwa ziara ya hifadhini, sasa familia hiyo, pamoja na Rais Obama watatembelea Kisiwa cha Robben kilichopo Cape Town, Afrika Kusini, mahali ambako Mzee Nelson Mandela alifungwa muda mrefu wa kuwapo kwake kizuizini kwa miaka 27.

 

Taarifa nyingi kuhusu ziara za Rais nje ya nchi hufanywa siri kwa sababu za kiusalama wa taifa, na kuna ufahamu kidogo tu kwa umma kuhusu gharama za jumla. Ripoti kutoka Ofisi ya Uwajibikaji wa Serikali ilionesha kuwa ziara ya Rais Clinton barani Afrika mwaka 1998 alipozuru nchi sita, iliigharimu Serikali ya Marekani dola milioni 42.7. Kiwango hicho kilitumiwa zaidi na jeshi ambalo lilifanya safari 98 kusafirisha watendaji, magari na kuandaa maeneo ya dharura za kimatibabu katika nchi tano.

 

Kiwango hicho hakikujumuisha gharama za Secret Service ambazo zinachukuliwa kuwa ni siri.

 

Rais Obama atafanya mikutano na kila kiongozi wa nchi atakayotembelea kwa minajili ya kujenga ushirikiano bora wa kiuchumi katika wakati huu ambao China inawekeza vya kutosha barani Afrika. Afya ni upande mwingine utakaotiliwa mkazo kwenye ziara hiyo.

1314 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!