RATIBA YA SERIKALI KUHAMIA DODOMA

Mheshimiwa Spika, ili kufanikisha azma ya Serikali kuhamia Dodoma, tayari imeandaliwa ratiba itakayowezesha Serikali kuhamia Dodoma kwa awamu, kuanzia mwezi Septemba, 2016 hadi mwaka 2020, bila ya kuathiri bajeti yetu ya mwaka 2016/2017 kama ifuatavyo:

Kwanza: Awamu ya Kwanza itakuwa kati ya mwezi Septemba, 2016 na Februari, 2017. Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mawaziri wote, Makatibu Wakuu wote, Manaibu Makatibu Wakuu wote watahamia Dodoma katika Awamu ya Kwanza. Aidha, kila Wizara itatakiwa kuhamisha Watumishi wa Idara moja au mbili, na wakati huo huo kuendelea kuweka utaratibu wa kupeleka Watumishi wa Idara nyingine kuhamia Dodoma;

Pili: Awamu ya Pili itakuwa kati ya mwezi Machi 2017 na Agosti 2017. Kipindi hiki kitawapa fursa watendaji wa wizara mbalimbali kuweka katika Bajeti zao za mwaka 2017/2018 gharama za kuendelea kuhamisha watumishi wake kuja Dodoma;

Tatu: Awamu ya Tatu itakuwa kati ya mwezi Septemba 2017 na Februari 2018; ambapo Wizara zitaendelea na uhamishaji wa Watumishi wa Idara zilizo ndani ya Wizara.

Nne: Awamu ya Nne itakuwa kati ya mwezi Machi 2018 na Agosti, 2018; na Awamu ya Tano itakuwa kati ya Mwezi Septemba 2018 hadi Februari, 2020. Katika kipindi hiki cha Awamu ya Tatu na Nne; Wizara zinatakiwa kuendelea kuhamisha watumishi wake.

Tano: Awamu ya Sita, itakuwa kati ya mwezi Machi, 2020 na Juni, 2020ambapo Ofisi ya Rais ikiongozwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, watakuwa wanahamia Dodoma.

Nazishauri Wizara zote kuanzisha mifumo ya utunzaji kumbukumbu wa kielektroniki badala ya kuhama na mafaili kutoka Dar es Salaam kuja Dodoma, tunataka Dodoma iwe ya kielektroniki.

Mheshimiwa Spika, naomba kutumia fursa hii kuwakaribisha wawekezaji mbalimbali wa sekta binafsi na wadau wa maendeleo wa ndani na nje kuwekeza Dodoma ili kuboresha zaidi miundombinu iliyopo na kuongeza majengo ya Ofisi na makazi ya Watumishi kuwekeza katika huduma za afya na elimu, huduma za kibiashara kama mabenki, maduka makubwa (Shopping Malls) na masoko, mahoteli na maghala. 

Aidha, napenda kurejea maelekezo niliyoyatoa kwa Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu Dodoma (CDA) na Mkoa wa Dodoma na Manispaa kuhakikisha kwamba Mji Mkuu wa Dodoma unaendelezwa kwa kasi ili kupokea watumishi wengi na familia zao pamoja na sekta binafsi watakaohamia Dodoma.

Mheshimiwa Spika, napenda kusisitiza kuwa Mkoa wa Dodoma na CDA wahakikishe kuwa pamoja na kuandaa maeneo ya makazi na Ofisi, pia watengemaeneo maalumu ya huduma muhimu kama vile maeneo kwa ajili ya kituo kikuu cha biashara, bustani, bandari kavu na kuendelea kuongeza eneo la viwanda na huduma mbalimbali za kibiashara. 

Aidha, naagiza Mamlaka za Mipango Miji Mkoani Dodoma na hasa CDA wahakikishe wanaweka mfumo wa kielektroniki wa upatikanaji wa viwanja ambao utatambua mahitaji kwa utaratibu wa wazi, na bila urasimu usio wa lazima. 

 Vilevile, nashauri Wakazi wa Mkoa wa Dodoma na Sekta binafsi kutumia fursa hii kujenga nyumba za kuishi za kutosha, nyumba za kulala wageni na mahoteli ili watumishi na wageni wanapokuja Dodoma wasipate taabu kutafuta mahali pazuri pa kuishi.

 

HOTUBA YA WAZIRI MKUU BUNGENI LEO

UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika, awali ya yote, naomba kutumia fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutulinda na kutupa afya njema hadi kutufikisha siku ya leo tunapohitimisha Mkutano wa Nne wa Bunge lako Tukufu tuliouanza tarehe 6 Septemba, 2016.

Nitumie fursa hii pia kukupa pole, Mheshimiwa Spika, kwa maradhi yaliyokusibu lakini kikubwa nielezee furaha yangu kwa uponyaji ambao Mwenyezi Mungu amekujaalia na hivi sasa tuko pamoja humu ndani. Tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu uendelee kupata nguvu na afya njema.

Mheshimiwa Spika, tangu tulipokutana mara ya mwisho, kumekuwepo majanga na matukio mbalimbali ya maradhi, ajali, ujambazi na matukio mengine ambayo yamesababisha vifo na majeruhi kwa Watanzania wenzetu, wakiwemo Waheshimiwa Wabunge. Hivyo, ninatoa pole kwa wafiwa wote na wale wote waliopatwa na majanga kutokana na matukio hayo. Tunawaombea afya njema wale waliopata majeraha na waliopo hospitali.

Mheshimiwa Spika, leo tunahitimisha mkutano huu tukiwa tumekamilisha shughuli zote zilizopangwa kwenye Mkutano huu. Naomba nitumie fursa hii ya awali kabisa kukupongeza sana Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wenyeviti na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kukamilisha kazi zote kwa ufanisi mkubwa. Kazi hizo zilijumuisha kujadili na hatimaye kupitisha Miswada mbalimbali ya Serikali. Napenda kukiri kwamba mijadala ya mkutano huu ilikuwa ya uwazi na hoja zilizotolewa zililenga kuiletea maendeleo nchi yetu. Kutokana na michango mizuri ya Waheshimiwa Wabunge na yenye tija, ilibidi mara kadhaa vikao vyetu kuendelea hadi usiku nje ya muda wa kikanuni.Nawapongeza sana!

 

TUKIO LA JANGA LA TETEMEKO LA ARDHI LILILOTOKEA MIKOA YA KANDA YA ZIWA

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge mtakumbuka kuwa tarehe 13 Septemba, 2016 Serikali iliwasilisha hapa Bungeni taarifa ya masikitiko kuhusu maafa makubwa yaliyoikumba Nchi yetu tarehe 10 Septemba, 2016 kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa ya Kagera, Geita, Mwanza na Mara. Tukio hilo ambalo liliathiri zaidi Mkoa wa Kagera lilitokea siku ya Jumamosi majira ya saa 9.27 alasiri, ambapo Mji wa Bukoba ulikumbwa na tetemeko la ardhi, lenye nguvu ya mtetemo wa kipimo cha 5.7, kwa kutumia skeli ya “Ritcher”. Tetemeko hilo limesababisha vifo vya watu 17 na majeruhi253. Napenda nitumie nafasi hii kwa mara nyingine kuwapa pole wafiwa wote na wale waliopata majeraha mbalimbali. Tunaomba Mungu aziweke roho za Marehemu mahali pema peponi. Amina. Kwa wale waliopata majeraha, tunamuomba Mungu awaponye haraka.

Mheshimiwa Spika, tukio hilo limesababisha uharibifu mkubwa sana wa nyumba, vituo vya afya, shule pamoja na miundombinu ya barabara. Aidha, shule nne za Nyakato, Ihungo, Kashenge na Buhembe, zimeharibika ikiwemo vyoo, nyumba za walimu, kumbi za shule na mabweni. Nyumba 840 zimeteketea kabisa, na nyingine 1,264 kupata nyufa. Kwa sasa uongozi wa Mkoa wa Kagera pamoja na Kamati ya Maafa ya Mkoa na Wataalamu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, wataalamu wa masuala ya matetemeko, na wadau wengine wanaendelea kufanya tathmini ya kina ya kiasi cha hasara iliyopatikana.

Mheshimiwa Spika, kama Bunge lako Tukufu lilivyojulishwa, Serikali kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali, imechukua hatua kadhaa kushughulikia athari za tetemeko hilo ikiwa ni pamoja na kufanya jitihada ya kurejesha hali ya utulivu, miundombinu iliyoharibika ili kuirejesha katika hali ya kawaida.

Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada mbalimbali zilizofanyika ikiwemo viongozi kutembelea maeneo yenye madhara, mpaka sasa Serikali imefanya mambo yafuatayo:-

(a) Kuhusu Chakula: Wananchi wenye mahitaji ya chakula wameendelea kupatiwa chakula kama vile, unga, mchele na maharage, sukari na chumvi pamoja na mafuta ya kula. Tathmini ya kubaini mahitaji halisi ya chakula inaendelea.

(b) Kuhusu Matibabu: Serikali imeimarisha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera kwa kupeleka dawa na vifaa tiba kupitia Bohari Kuu ya Dawa. Aidha, Timu ya Wataalam na Madakta 12 wamepelekwa Bukoba kutoka Hospitali ya rufaa ya Kanda ya Bugando. Napenda kuwashukuru pia wadau mbalimbali ambao wamechangia eneo hili wakiwemo Medecins Sans Frontiers, Ubalozi wa China, Jhpiego (USAID) na Chama cha Wafamasia.

(c) Makazi: Wananchi waliokosa kabisa hifadhi ya makazi wamepewa maturubai na mahema kwa ajili ya makazi ya muda. Aidha, waathirika ambao nyumba zao zimebomoka kabisa, kwa kuanzia kila mmoja ametengewa mabati 20, saruji mifuko mitano, blanketi na mikeka. Pia wapangaji waliokuwa katika nyumba hizo kila mmoja ametengewa kodi ya pango ya miezi sita ili apate mahali pa kujihifadhi.

(d) Kuhusu Shule zilizoathirika: Serikali inajenga miundombinu ya muda ya shule kama vile madarasa, mabweni na vyoo hususani katika shule za sekondari za Ihungo na Nyakato zilizofungwa kwa muda wa wiki mbili. Tathmini ya kitaalam ikikamilika, mpango wa ujenzi wa miundombinu ya kudumu itafanyika na maandalizi yanaendelea kupata rasilimali kwa ajili hiyo.

(e) Mazishi: Serikali imeshiriki katika kuwafariji wafiwa na pia kushiriki mazishi kwa kusaidia kutoa jeneza, sanda, usafiri na kutenga fedha Shilingi milioni 20 za rambirambi kwa wafiwa ambazo zitatolewa kwao muda wowote kuanzia sasa.

(f) Barabara: Tathmini ya uharibifu wa barabara imefanyika na barabara zilizoharibika zitarejeshwa katika hali ya kawaida ili wananchi waendelee kupata huduma za msingi. Vilevile, Serikali inaendelea kuchukua hatua za kuhakikisha miundombinu ya maji safi na maji taka inakarabatiwa na kuhakikisha usafi unaendelea kuwa katika viwango stahiki.

Kwa ujumla, Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa taasisi za umma ikiwemo majeshi ya ulinzi na usalama na rasilimali zake vinatumika kutoa huduma zote muhimu kwa waathirika katika kipindi hiki.

Mheshimiwa Spika, hivi sasa Serikali inaendelea kufanya tathmini ya kitaalam kupitia Wizara ya Nishati na Madini, Chuo cha Madini Dodoma na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kubaini chanzo cha tukio, kiasi cha athari zilizotokea chini ya miamba na juu ya ardhi. Tathmini hii ya kitaalamu itatupa picha na mwelekeo wa kushughulikia urejeshaji wa miundombinu iliyoharibika.

Mheshimiwa Spika, naomba nitumie nafasi hii kukushukuru sana wewe binafsi Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge kwa namna mlivyoshirikiana na Serikali katika kushughulikia janga hili la kitaifa la tetemeko la ardhi Napenda kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa michango yenu ya hali na mali na kwa kututia moyo katika kushughulikia tukio hili kubwa lililoathiri maisha na shughuli za wananchi pale mkoani Kagera.

Mheshimiwa Spika, vilevile, kwa niaba ya Serikali, na kipekee, nitumie fursa hii kuishukuru Jumuiya ya Wafanyabiashara Nchini, Waheshimiwa Mabalozi, Wawakilishi wa Mashirika ya Umma na ya Kimataifa waliopo nchini, viongozi wa vyama vya siasa na wananchi kwa ujumla, ambao waliitikia wito wa Serikali wa kushiriki na kusaidia juhudi za Serikali za kuwasaidia waaathirika wa tetemeke la ardhi. Tunawashukuru sana wote waliotuunga mkono kwa fedha na vifaa mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada hizo zinazofanywa, Serikali imeshatoa na inaendelea kukusanya michango kutoka kwa wananchi na wadau mbalimbali. Hivyo, kwa wananchi na wadau walio tayari kuchangia wanaweza kutumia Akaunti ya Maafa iliyofunguliwa katika Benki ya CRDB yenye Namba.015 222 561 7300 kwa jina la KAMATI MAAFA KAGERA – Swiftcode: CORUtztzkwa kutuma fedha kwa njia ya kawaida au Mobile Banking. Vilevile, michango hiyo inaweza kutumwa kwenye Namba za simu za mkononi, 0768-196-669 (M-Pesa), au Namba 0682-950-009 (Airtel Money) au Namba 0718-069-616 (Tigo Pesa).

Nawaomba wananchi wote, Sekta Binafsi na Jumuiya ya Kimataifa tuonyeshe mshikamano kuungana na Serikali katika kusaidia wenzetu walioathirika na tetemeko hilo kwa kutoa michango ya hali na mali.

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwahakikishia Watanzania wote kuwa Serikali itaendelea kuratibu michango yote itakayotolewa na kuifikisha kwa walengwa. Aidha, Serikali itaendelea kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa kuimarisha uwezo wetu wa ndani wa kukabiliana na majanga ya aina hii na mengineyo.

 

SHUGHULI ZA BUNGE

Mheshimiwa Spika, tunahitimisha mkutano huu tukiwa tumepata fursa ya kujadili Miswada, Maazimio na Kauli mbalimbali za Mawaziri. Miswada iliyowasilishwa na Serikali na kusomwa kwa mara ya pili na pia kusomwa mara ya tatu ni kama ifuatavyo:-

Kwanza: Muswada wa Sheria ya upatikanaji wa Habari wa mwaka 2016; (The Access to Information Bill, 2016);

Pili: Muswada wa Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini wa Mwaka 2016; (The Valuation and Valuers Registration Bill, 2016);

Tatu: Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wa mwaka 2016; (The Government Chemist Laboratory Authority Bill, 2016);

Nne: Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Wanataaluma wa Kemia wa Mwaka 2016; (The Chemist Professionals Bill, 2016);

Tano: Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo wa Mwaka 2016; (The Tanzania Agricultural Research Institute Bill, 2016);

Sita: Muswada wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi wa Mwaka 2016; (The Tanzania Fisheries Research Institute Bill, 2016).

Miswada ya Sheria ya Serikali iliyosomwa kwa mara ya kwanza ni:-

(a) Muswada wa Sheria ya huduma za Hbari za Mwaka 2016 (The Media services Bill, 2016).

(b) Muswada wa Sheria ya marekebisho ya Sheria mbalimbali (Na. 3) wa Mwaka 2016 (The Written Laws Micellianeous Amendments) (No.3) Bill, 2016).

Mheshimiwa Spika, katika Bunge hili, Serikali ilitoa kauli zifuatazo:-

Kwanza: Kauli ya Serikali kuhusu hali ya chakula nchini na uzalishaji kwa msimu wa mazao kwa mwaka 2015/2016; na upatikanaji wa chakula kwa mwaka 2016/2017;

Pili: Kauli ya Serikali kuhusu tukio la tetemeko la ardhi lililotokea tarehe 10 Septemba, 2016 Mkoani Kagera na Mikoa mingine ya Kanda ya Ziwa.

Mheshimiwa Spika, kipekee, naomba kutumia fursa hii kumshukuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali, pamoja na Wataalam wake, kwa mchango wao mkubwa katika kuandaa miswada hiyo kwa umakini mkubwa na hivyo kuwawezesha Waheshimiwa Mawaziri kuiwasilisha Bungeni kwa weledi mkubwa. Aidha, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao mizuri. Serikali itazingatia ushauri na maoni yenu wakati wa utekelezaji.

Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu jumla ya maswali 110 ya msingi na mengine 222 ya nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Serikali. Vilevile, jumla ya maswali matano ya msingi na ya nyongeza ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu ya kila Alhamisi yaliulizwa na kupata majibu.

 

MWENENDO NA MWELEKEO WA HALI YA UCHUMI

Mheshimiwa Spika, katika siku za hivi karibuni, kumekuwepo na wasiwasi kuhusu mwenendo wa hali ya uchumi, hususan mtiririko wa fedha kwenye uchumi wa Taifa. Napenda kutumia fursa hii kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge na Watanzania kwa ujumla kuwa mwenendo wa uchumi ni wa kuridhisha na unaendelea kuimarika. Aidha, tathmini iliyofanyika kuhusu viashiria vya uimara wa sekta ya fedha, inaonesha kuwa Mabenki yetu bado yapo salama, na yana mitaji ya kutosha na mwenendo wa sekta ya fedha ni wa kuridhisha. Aidha, Wizara ya Fedha na Mipango, Benki Kuu ya Tanzania na Taasisi ya Taifa ya Takwimu zinafuatilia kwa karibu kuhusu mwenendo wa Hali ya Uchumi Nchini. Mathalan, tarehe 14 Septemba, 2016 Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Profesa Benno Ndulu, alitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu mwenendo wa hali ya uchumi nchini ambapo alilihakikishia Taifa na Jumuiya ya Kimataifa kwamba hali ya uchumi wetu ni shwari kabisa na si mbaya kama inavyodhaniwa na baadhi ya watu.

Mheshimiwa Spika, katika taarifa hiyo ya Benki Kuu pamoja na mambo mengine, imebainishwa kwamba katika robo ya kwanza ya mwaka 2016, ukuaji wa uchumi wa Tanzania umeendelea kuwa wa kuridhisha. Pato la Taifa lilikua kwa asilimia 5.5 ikilinganishwa na asilimia 5.7 kipindi kama hicho mwaka 2015.Ukuaji huo ulitokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme, huduma za mawasiliano, utangazaji na huduma ya intaneti; kuongezeka kwa uchimbaji na madini. Shughuli za kiuchumi zilizokua kwa kasi ya juu katika kipindi hicho ni sekta ya fedha kwa asilimia 13.5, mawasiliano asilimia 13.4 na utawala wa umma asilimia 10.2.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia mwenendo huo mzuri wa viashiria vya shughuli za uchumi, ni dhahiri kwamba mwelekeo wa uchumi katika kipindi kijacho unatoa matumaini ya uchumi kuendelea kuimarika kama ilivyokadiriwa hapo awali na kufikiwa kwa lengo la ukuaji wa Pato la Taifa la asilimia 7.2 kwa mwaka 2016. Hii inachangiwa pia na ukweli kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga vizuri katika kuimarisha uchumi endelevu; usimamizi thabiti wa rasilimali za umma; na ujenzi wa miundombinu bora yenye kuimarisha lengo la kujenga uchumi wa viwanda chini ya Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano.

 

MWENENDO WA UKUSANYAJI WA MAPATO YA SERIKALI KWA MWEZI JULAI NA AGOSTI, 2016

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuongeza na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kuchukua hatua mbalimbali. Katika mwaka 2016/17, mapato ya Serikali yanatarajiwa kuongezeka na hivyo kupunguza utegemezi wa kibajeti kutoka kwa Washirika wa Maendeleo. Aidha, Serikali imeendelea kudhibiti utoaji wa misamaha ya kodi ili kuleta tija kwa Taifa katika ukusanyaji mapato.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017, Serikali imelenga kukusanyamapato ya ndani, ikijumuisha mapato ya Halmashauri, ya jumla ya shilingitrilioni 18.46, sawa na asilimia 62.5 ya bajeti yote ya shilingi trilioni 29.5.Takwimu za mwenendo wa ukusanyaji mapato zinaonesha kuwa katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Agosti, 2016, mapato yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), yalikuwa shilingi trilioni 2.168 ikilinganishwa na makadirio ya kukusanya shilingi trilioni 2.113, sawa na asilimia 103 ya lengo. Aina za kodi zilizochangia sana katika ongezeko hilo ni pamoja na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya mashine za kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato. Mapato yasiyo ya kodi kwa kipindi hicho yalikuwa shilingi bilioni 271.1; sawa na asilimia 60 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 448.4. Aidha, mapato kutoka vyanzo vya Halmashauri yalikuwa Shilingi bilioni 45.4; ikiwa ni asilimia 41 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 110.9. Napenda kutumia fursa hii kuzihimiza Wizara na Halmashauri kuongeza jitihada za ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuchukua hatua zifuatazo:-

Kwanza: Kuendelea kuimarisha usimamizi wa ukusanyaji wa mapato ikiwa ni pamoja na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maeneo ya biashara, viwandani, migodi, bandarini, kwenye viwanja vya ndege na maeneo ya mipakani ili kuhakikisha kodi stahiki zinakusanywa;

Pili: Kusimamia kikamilifu matumizi ya vifaa na mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato ili kuongeza ufanisi na kudhibiti upotevu wa mapato;

Tatu: Kuendelea kupanua wigo wa walipa kodi, ikiwa ni pamoja na kurasimisha sekta isiyo rasmi ili iweze kuingia katika mfumo wa kodi;

Nne: Kuimarisha ufuatiliaji wa mapato yanayokusanywa na taasisi na mamlaka mbalimbali za Serikali na Halmashauri zote nchini; na

Tano: Kuendelea kuchukua hatua za kudhibiti na kupunguza misamaha ya kodi isiyo na tija.

 

MPANGO WA SERIKALI WA KUHAMIA DODOMA

Mheshimiwa Spika, tarehe 23 Julai, 2016 Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati akihutubia Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi hapa Dodoma alieleza kuhusu dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kukamilisha mchakato na ahadi ya Serikali ya kuhamia katika Mji wa Makao Makuu – Dodoma. Aidha, Mheshimiwa Rais alirejea kauli hiyo tarehe 25 Julai, 2016 wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa Nchini ambayo yalifanyika Kitaifa kwa mara ya kwanza katika Viwanja vya Mashujaa, mjini Dodoma. Mheshimiwa Rais alisisitiza kuwa anatarajia kwamba Serikali yake yote itakuwa imehamia Dodoma katika kipindi cha miaka minne na miezi minne, hadi kufikia mwisho wa mwaka 2020.

Mheshimiwa Spika, napenda kuwafahamisha Waheshimiwa Wabunge na Wananchi kwamba Mpango wa sasa wa Serikali wa kuhamia Dodoma ni mwendelezo wa utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 iliyozingatia agizo lililotolewa tarehe 1 Oktoba, 1973 kwenye Mkutano Mkuu wa 16 wa Chama cha TANU. Hivyo, hatua zinazochukuliwa sasa na Serikali ya Awamu ya Tano ni mwendelezo tu wa utekelezaji wa mipango ya awali iliyokuwa inatekelezwa mwaka hadi mwaka na Serikali za Awamu zilizopita, kuanzia Awamu ya Kwanza lilipotolewa tamko hilo mwaka 1973; chini yaUongozi wa Rais wa Awamu ya Kwanza na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza azma hiyo ya Serikali ya Awamu ya Tano, baada ya tamko la Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli la tarehe 23 Julai 2016, yafuatayo yamefanyika:

Kwanza: Tarehe 26 Julai, 2016 nilikutana na Viongozi wa Mkoa wa Dodoma (Viongozi wa Chama na Serikali wa Mkoa na Wilaya, Wazee maarufu, Viongozi wa Madhehebu ya Dini na Wadau mbalimbali) ili kuwajulisha kuhusu mkakati wa sasa wa Serikali wa kuhamia Dodoma. Aidha, niliutaka Uongozi wa Mkoa wa Dodoma kuwasilisha mapendekezo ya mpango kazi wa kutekeleza uamuzi wa Serikali wa kuhamia Dodoma;

Pili: Katika kipindi cha siku 14, Uongozi wa Mkoa wa Dodoma uliwasilisha kwangu Taarifa ya Serikali kuhamia Dodoma kama ilivyokusudiwa. Aidha, tarehe 15 Agosti, 2016 Mkoa uliwasilisha Mpango huo katika Kikao cha Baraza la Kazi la Mawaziri pamoja na Makatibu Wakuu na kupata ushauri na maoni yao ya kuuboresha;

Tatu: Serikali imeunda Kamati Ndogo chini ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu Dodoma (CDA) kwa lengo la kufanya mapitio ya upatikanaji wa Ofisi na Makazi na miundombinu muhimu. Kamati hiyo inashirikisha Taasisi mbalimbali za Serikali zilizopo Dodoma na Kitaifa, zikiwemo TBA, DUWASA, TANROADS, TEMESA, TANESCO, SUMATRA, TTCL, Jeshi la Polisi na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji;

Nne: Aidha, Serikali imeunda Kamati ya Kitaifa ya Makatibu Wakuu ambao wanaratibu zoezi zima na utaratibu wa Serikali kuhamia Dodoma;

Tano: Tarehe 1 Septemba, 2016, Serikali ilikutana na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Fedha, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Sekta Binafsi zinazohusika na ujenzi wa miundombinu nchini. Lengo la kikao hicho lilikuwa ni kupata mawazo ya Sekta Binafsi, Taasisi za Fedha na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ili kuisaidia Serikali kuboresha mikakati ya kuhamia Dodoma kwa kuzingatia kuwa Serikali peke yake haiwezi kukamilisha jambo hili. Katika kikao hiki tumekubaliana kwamba kuanzia sasa kuwepo na vikao baina ya Makatibu Wakuu na Wadau wa Sekta Binafsi, angalau mara moja kwa mwezi chini ya Uenyekiti wa Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Kamati hiyo akiwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu. Kikao hicho kitakuwa cha mashauriano na kupeana mrejesho wa utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuhamia Dodoma kwa kuzingatia mchango wa sekta ya umma na sekta binafsi katika ujenzi wa miundombinu ya kiuchumi na kijamii, uwekezaji na uzalishaji biashara na huduma mbalimbali;

Sita: Serikali pia imeunda Kamati Maalum ya Wataalam Washauri itakayoshirikiana na CDA kufanya Mapitio ya Mpango Kamambe (Master Plan) wa Mji wa Dodoma ili kubaini mahitaji halisi ya sasa na siku zijazo katika upeo wa miaka 50 na zaidi. Zoezi hili litahitaji ushirikishwaji mkubwa wa jamii na sekta binafsi. Lengo la Serikali ni kuwa na mji uliopangwa vizuri na unaozingatia vigezo mbalimbali vya Kimataifa.

Mheshimiwa Spika, napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba Serikali ya Awamu ya Tano inatambua jitihada kubwa zilizofanywa na Serikali za awamu zilizopita zilizoongozwa na Chama cha Mapinduzi za kuweka miundombinu mbalimbali muhimu ya kufanikisha mpango wa Serikali kuhamia Dodoma. Tathmini iliyofanywa na OWM, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, pamoja na wadau mbalimbali, inaonyesha kuwa kwa ujumla miundombinu iliyopo Dodoma kwa sasa ina uwezo wa kutosheleza mahitaji ya Serikali kuhamia Dodoma kwa awamu kuanzia mwezi huu wa Septemba, 2016 hadi mwaka 2020. 

 

>>ITAENDELEA