Wiki iliyopita gazeti hili lilichapisha sehemu ya kwanza ya mahojiano kati ya Ridhiwani Kikwete (pichani) na JAMHURI. Leo tunakulete sehemu ya pili na ya mwisho ya mahojiano hayo.

JAMHURI: Mitandao ya kijamii unaisoma? Unajisikiaje wewe na Mheshimiwa Kikwete mnavyoshambuliwa?


RIDHIWANI: Hivi vitu kwanza tumshukuru Mungu kwa sababu Mungu amewapa watu nafasi ya kusema. Mitandao hii inatoa nafasi ya kuwafanya watu watoe yaliyomo moyoni mwao. Taarifa iliyosomwa na Waziri Mkuu mwaka 2007 ilionesha CCM ilikuwa imefanikiwa kutekeleza asilimia 98 ya Ilani ya Uchaguzi. Kufikia mwaka 2009 ikawa imetekelezwa kwa asilimia 100.

Malalamiko ya watu juu ya shida zao hayawezi kwisha kwa utekelezaji wa Ilani. Yanaendelea kuwapo siku hadi siku. Ni sawa na mtu ukiwa na shida ya hela ukalipwa mshahara mwisho wa mwezi, shida itakuwa palepale mwisho wa mwezi ujao. Hivyo, media ina nafasi kubwa ya kumkumbusha kiongozi kuwa kuna kitu au jambo hujalitekeleza vizuri mzee. Mitandao ya kijamii haitumiki vizuri. Watu wametengeneza makundi ambayo kazi kubwa wanayofanya ni ku-damage image (kuharibu heshima) za watu. Unaona kuwa huyu mtu anasema kwa sababu anataka Mzee (Rais Kikwete) aharibikiwe.


Masuala ya ufisadi: Mtu anamnyooshea kidole kwamba huyu Mzee amehusika. Bahati mbaya zaidi, wapo viogozi wengine wanachukua mambo ya mitandao wanayahamishia kwenye majukwaa ya siasa kupata umaarufu. Wanataka kuonesha kuwa kila mtu ni mwizi nchi hii. Kama kuna mtu ana ushahidi apeleke.


Miaka miwili au mitatu ya mwanzo (2005-2007), ilikuwa inasumbua. Unasoma unasema kama nchi yenyewe ni hivi basi Mzee (Rais Kikwete) awaachie nchi yao. Lakini mwisho tukaona bora kushikilia Ilani. Mzee wangu amefanikiwa sana – anastahili apongezwe. Watanzania hawahitaji kusikiliza manung’uniko. Migogoro ya dini


JAMHURI: Hivi karibuni nchi yetu imekumbwa na migogoro ya kidini, wewe unaizungumziaje?

 

RIDHIWANI: Nchi hii thamani yake ni kubwa sana. Yapo mambo ambayo viongozi hasa wa dini wanalea migogoro ambayo mwisho wa siku waathirika wake ni jamii nzima na wao wakiwamo. Sisi tokea tumezaliwa tunajua kwamba Wakristo hawachinji.


Tetesi za mtaani, ambazo siwezi kuzithibitisha, zinasema kwenye miaka ya 1960 either (labda) yalikuwa ni makubaliano, kwamba watakaochinja ni Waislamu. Leo unaanzisha mgogoro kwamba tunataka haki ya kuchinja?


Hivi wewe pale nyumbani kwako ukichinja kuku wako au mbuzi ukala nani atakuuliza? Kwa nini uende nje ya geti lako uanzishe mgogoro kwamba Wakristo wanataka kuanzisha bucha zao? Katika mazingira kama hayo inakuwaje tena? Kwamba Wakristo wanalilia haki hizo?


Ukiuliza haki ya binadamu kuishi, pamoja na kwamba Mungu anataka watu waishi, zamani wakati wa mapambano ya watu kutafuta utawala ilikuwa ni mauaji yasiyo na huruma kwa watu. Wazungu wanatoka Milton Keynes wanamchinja mfalme wa London kwa nia ya kutawala lile eneo, hata walipokuja Afrika kutaka kutawala maeneo waliwaua viongozi wa Kiafrika ili waweze kupata hadhi ya kutawala katika maeneo yale.


Baada ya kugundua hili jambo kwamba ni baya ikaanzishwa adhabu ya kifo kwa anayeua. Anapelekwa mahakamani, anashtakiwa na ikithibitika kweli ameua kwa kukusudia, anauawa.


Mkristo anaposema anadai haki ya kuchinja, lazima ana sababu nyuma yake; sababu ambayo hakuna anayejitokeza kuieleza wazi. Baadhi ya watu wanaanza kupata wasiwasi kuwa labda siasa zimeingizwa. Sisi Watanzania, viongozi wetu wa kiroho, masheikh na mapadri watumie Baraza la Amani wakutane, wajadiliane.


Hii haki, hata kama Mkristo ataambiwa achinje haitakuwa suluhu ya matatizo yanayoanza kupandikizwa. Tatizo lipo, uhuru wa kuabudu umekubaliwa kote duniani. Umekubalika dunia nzima. Kwa Tanzania Mwislamu anaruhusiwa kuoa wake wanne, lakini si kwa Mwislamu wa China au Marekani – hawezi kuwa na wake wanne. Leo hii wewe bwana Balile unaweza kuamua ukaenda kwenye mti ukawa unaendesha ibada yako, tunao uhuru wa kutosha.


Vyombo vya dola vinapaswa kuangalia hili. Kama kuna misikiti ya wanaharakati, wahusika wasakwe. Misikiti yote ni ya Mungu, sasa iweje leo tuwe na misikiti ya wanaharakati. Kuna makanisa yana watu 20, wengine wanatamani Papa angeruhusu hata wanawake wawe mapadri, lakini kuna wanaosimamia misingi ya Kanisa, wanasema hapana. Vyombo vya Ulinzi na Usalama viangalie. Haiwezekani kuwa watu wanakaa misikitini wanapanga mbinu mbaya, vyombo vyetu vijipenyeze misikitini na makanisani wakitoka tu mnawakamata. Nchi yetu imekuwa nchi ya matukio – kila siku kuna tukio. Haiwezekani majambazi wapange mbinu za wizi au kuteka watu na wafanikishe bila kukamatwa. Vyombo vya dola wakajipenyeze huko.

Historia ya Ridhiwani

JAMHURI: Historia yako kwa ufupi ikoje?


RIDHIWANI: Wengi wamemjua Ridhiwani kuanzia mwaka 2005. Wanasema hata huo u-NEC amepewa kwa sababu ni mtoto wa Rais. Jamani, mimi nasema nimeanza kukisotea chama nikiwa na umri wa miaka mitano. Nilikuwa nakwenda vidudu (shule za awali), natoka vidudu; pale nyumbani amebaki babu, akanichukua na kunipeleka Chama Cha Mapinduzi nikacheze chipukizi pale Bagamoyo. Wakati huo baba alikuwa jeshini na ni Kamisaa wa Siasa.


Baba alipoteuliwa kuwa Katibu wa CCM wa Wilaya ya Nachingwea [mwaka 1987], niliendelea kuwa chipukizi. Kipindi kile ni chama kimoja. Nikawa nacheza gwaride kwa watoto wa darasa la kwanza na la pili, nikachaguliwa nikawa kiongozi wa gwaride, wakati huo ni mtoto mdogo wa darasa la kwanza.


Nimeendelea kufanya hivyo hata nilipokuja Dar es Salaam nikiwa darasa la tatu. Walinifundisha kina Rama Kisauti, mfanyakazi ofisi za CCM Ilala; Rajiv Fundikira (Vijana) na Josephat Ndurango, yuko Vijana Dodoma. Martha Thomas, yuko pale Bagamoyo, naye alinifundisha.


Baadaye nikachaguliwa Kiongozi wa Chipukizi, Forodhani na baadaye Chipukizi Wilaya ya Ilala. Nakumbuka nilimvisha skafu Dk. Salim Ahmed Salim na Mzee Pius Msekwa kwenye graduation (mahafali) pale Forodhani.


Nikiwa darasa la sita mwaka 1992 niligombea Ujumbe wa Mkutano Mkuu wa Chipukizi Taifa. Raymond Mangwale, tulimchagua kuwa Mwenyekiti wa Chipukizi Taifa, sasa ni Katibu wa CCM.


Sekondari nilipofika form III nikaacha mambo ya siasa. Baadaye hawa kina Rajabu Luwavi, Mary Chatanda (Katibu CCM Mkoa wa Arusha), nikaja kufahamiana nao nikiwa Mkwawa Secondary School, Iringa. Rais [Benjamin] Mkapa alikuja kuhudhuria sisi makada tulialikwa, wakati huo Boniface Makene (mtumishi Ofisi ya Makamu wa Rais) akiwa Rais wa Serikali ya wanafunzi (1998).


Tulivyorudi shuleni ndiyo nikaanza kushiriki siasa. Uchaguzi wa Vijana wa Wilaya ya Bagamoyo, Said Mtanda tulimsaidia sana (Mbunge wa Mchinga), akawa Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Bagamoyo, akanichagua mimi kuwa mhamasishaji wake, pale ndipo nilipopikika rasmi (2001).


Chuoni tulikuwa tunafanya harakati za wanafunzi. Nikiwa second year (mwaka wa pili) nikachaguliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Halima Mdee (Mbunge wa Kawe) ndiye alikuwa Waziri wangu na Zitto Kabwe alikuwa Waziri Mkuu. Tukapamba moto siasa za wanafunzi kuhakikisha zinakwenda.


Lakini kumbe hatukujua kuwa kuna siasa nyuma ya pazia. Tulikuwa tunashindana baadaye tukagundua kuwa kumbe nyuma kuna harakati, na hasa mwaka 2002 mkutano wa Chadema uliofanyika Kilimanjaro ulipomchagua Zitto kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu.


Zitto nilikuwa nakaa naye chumba kimoja. Baada ya kuona mwelekeo huo, alimleta Mary Mugulusi, nilimkataa. Siku hizi anafanya kazi BP (Puma), ile movement ikaendelea. Makene tulimsaidia akapita kwenye uwaziri mkuu.


Mwaka 2002 kipindi cha likizo ndiyo tulifanya kambi kubwa sana ya vijana kule Bagamoyo, tukamwalika Benno Malisa.


JAMHURI: Ilikuwaje ukachaguliwa Ujumbe wa NEC Bagamoyo?


RIDHIWANI: Bagamoyo kuna sura mbalimbali. Kuna historia ambayo familia yetu sisi inafungamanishwa na ile jumuiya nzima. Mzee Mrisho Kikwete alikuwa mtawala katika eneo la Ukwere na utawala wake ulikuja hadi huku Pwani ya Bagamoyo, Abdallah Mizega alikuwa mfanyabiashara, Tamla Mizega ndiyo majina ya mwisho na, Kikwete ni jina la katikati na tumeamua tulitumie kama la ukoo. Babu aliji-establish (alijijenga) Bagamoyo akajulikana maeneo yote. Baba yangu amefanya kazi Bagamoyo na Chalinze akiwa mbunge, maeneo yote haya sisi jina letu liko vizuri. Ipo ile hali ya heshima ambayo familia yetu imewekewa, inawezekana wakasema huyu kijana tusimpinge tumpe heshima ya wazee wake.


Mimi nimekulia Bagamoyo, babu yangu mimi alikuwa ananielekeza jinsi ya kuishi na wazee. Kila likizo lazima tupelekwe Bagamoyo. Siku ya kwanza ukifika Bagamoyo, babu yetu sisi alikuwa akituchukua na kutuzungusha kila nyumba. Nakumbuka alinipeleka kwa Mzee Sharrif Ahmed, babu anatumia nafasi hiyo ananitambulisha, ‘amekuja likizo nimeona ni muhimu akaja akakusalimia.’ Kaka Khalfani, walikuwa wana marafiki wengi. Jioni walikuwa wananichukua wananipeleka kwenye michezo, nazungumzia mazingira ambayo sisi kama familia tulikuwa tunaishi.


Jamii inatutambua kama sehemu yao, Bagamoyo ya Pwani, lakini baba akaenda hadi Chalinze, nimekwenda katika kila kijiji, kila mji wa Bagamoyo, baba na babu walikuwa wananipeleka wanasema twende hapa, twende pale.


Pili, watu hawakujitokeza si kwamba Ridhiwani tunamwogopa, au tunampenda sana, ila ni kutokana na heshima, kama kipindi cha pili wakiamua kunipa fursa hiyo itakuwa imetokana na mazuri niliyowafanyia. Tatu, ni mshikamamo wangu. Kati ya mwaka 2007-2012 nilichaguliwa kuwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Wilaya na Mkoa.


Mimi najua mtu mmoja baada ya mwingine na wapi anakaa. Ukiziunganisha na nyingine, mapenzi yao wenyewe labda wameamua kusema tumpe heshima.


JAMHURI: Hivi huu ujumbe wa NEC umeupata hivi hivi bila kupenyeza rupia?


RIDHIWANI: Hakika sikupenyeza rupia. Unampa nani wakati wote ni ndugu zangu wale? Ukienda pale utakuta koo za ndugu zangu ambao ni Kiongo, Mizega, Onelo, Jumbe, Shaibu Mtawa (Wanatoka upande wa mama – mama yake Mtawa ni dada mkubwa wa mamake Baba yangu).


Bagamoyo tumeoleana wenyewe kwa wenyewe. Ni familia chache kukuta ameoa mtu wa Mwanza. Kimsingi, hatujaiteka Bagamoyo; ni kwamba sisi ndiyo tupo pale Bagamoyo. Bagamoyo ni ya watu waliopo. Said Bwanamdogo, anatokea upande wa Mlaonelo, maana yake dada wa kina Onelo (Mzigua), Ridhiwani (Mkwere), hata akina Kawambwa hawa ni jamii moja.

Tetesi za kugombea ubunge

JAMHURI: Umemtaja Dk. Shukuru Kawambwa. Taarifa zilizopo ni kwamba utagombea ubunge hapo Bagamoyo. Unazizungumziaje?


RIDHIWANI: Kawambwa ana wasiwasi, Said Bwanamdogo ana wasiwasi. Hata mbunge wa Kibaha aliwahi kuniuliza kwamba kama unagombea hapa. Mimi nasema bado sijafikia sehemu ya kuamua kuwa nautaka ubunge au la, bali kwa sasa nafanya kazi ya kuimarisha chama ndani ya Wilaya ya Bagamoyo.


Najenga chama tusipate upinzani ambao haukustahili kuwapo. Kazi kubwa ni kumsaidia mbunge wangu; hadi mwaka 2015 chama kikiwa vizuri ndiyo hali yako itakuwa vizuri. Sijaamua.


JAMHURI: Unasema upinzani usiostahili kuwapo. Unamaanisha nini hapa?


RIDHIWANI: Bagamoyo hakujawahi kuwa na chama cha upinzani. Nchi yetu kwa asilimia kubwa zaidi ni Chama Cha Mapinduzi. Ilionekana wazi watu wengi hawakupendelea vyama vingi. CCM ni chama pekee kinachoweza kuilea nchi hii.


Maeneo mengi CCM wanaanguka kutokana na migogoro ya ndani. Watu wanasema hatumtaki huyu kwa sababu ni mtu wa fulani. Tumeyashuhudia haya Mbeya Mjini na Nyamagana – inanisikitisha. Watu waliamua tu kwamba Masha hatumtaki, wakamwangusha. Bado mimi naamini kwamba Chama Cha Mapinduzi tuna mengi zaidi ya wenzetu wanaopamba magazeti kwa malalamiko na maandamano.


Chadema hawajajenga shule, daraja, hata nyumba mbili za walimu. Kama tusipofanya haya, watu watatafuta mbadala, watatafuta mtu mwingine, si wanayemwamini katika sera za chama chake, bali huyu aliyepo ameshindwa kututimizia haya.


Mimi kama m-NEC nawaambia wananchi nini chama chetu kimefanya, nini kinatarajiwa kufanywa na malengo ya muda mrefu. Pia nikutane na wananchi wa maeneo husika, waniambie nini wanataka chama kiwafanyie. Wakipoteza imani lazima watafute mtu wa kuifanya hii kazi.


Najikita Bagamoyo kufunga milango ili mpinzani asijekuta hata hema la kupumzikia pale. Chadema walimleta Makamu Mwenyekiti, [Said] Arfi kwenye uchaguzi wa vijijini, tulipambana naye tukamshinda kwa kutumia sekretariati ya wilaya. Hawakupata hata kura moja, hata kijiji kimoja. Mimi nasema katika uchaguzi labda aje Mungu ndiye anayeweza kuwaambia Bagamoyo kuwa CCM haifai, wakamwelewa.


1932 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!