Ujangili nje nje (2)

Wiki iliyopita JAMHURI ilieleza habari za uchunguzi kuhusu ujangili unaofanywa na baadhi ya wananchi katika Kijiji cha Mkata na vijiji jirani na Hifadhi ya Taifa ya Mikumi

mkoani Morogoro.

Katika uchunguzi huo, tulibaini biashara ya wanyamapori-mbichi na inayochomwa katika Kijiji hicho, huku viongozi wenye dhamana ya kudhibiti uhalibifu huo wakiwa hawajishughulishi.

 

Katika sehemu hii ya pili ya makala hii, kuna maelezo ya viongozi mbalimbali waliohojiwa kuhusu ujangili na juhudi za kuukabili.

 

Je, ujangili na biashara ya wanyamapori havina baraka za maofisa na askari wa Idara ya Wanyamapori? Je, uhalifu huu hauna uhusiano na Jeshi la Polisi?

 

Maswali haya yanaulizwa na wananchi wengi. Matukio ya karibuni ya polisi kukamatwa na nyara za Serikali yanaondoa shaka ya kuwahusisha polisi kwenye uhalifu huu.

Kauli ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Mvomero

Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Mvomero, Sarah Limuna, ameiambia JAMHURI kwamba anashangazwa kusikia kuwa wanyamapori wanawindwa licha ya muda uliowekwa kisheria kumalizika.


“Uwindaji ni Julai hadi Desemba, sasa wanapoendelea kuua wanyama hata baada ya muda kwisha kwa kweli sielewi,” anasema.

 

Anapoulizwa kama uwindaji haramu upo, anajibu, “Siwezi kusema upo au haupo. Ujangili unafanywa kwa kificho. Mara kwa mara nimekuwa nawasiliana na Tanapa kuwakamata majangili. Pale Doma tuna bwana nyamapori. Nimempa usafiri, sasa nitafuatilia kujua ni kwanini ana usafiri na nyamapori inauzwa haradhani.”

 

Anaongeza: “Kama nilivyosema, ujangili unafanywa kwa siri, ukiwauliza wananchi watasema hakuna kitu kama hicho (ujangili); lakini kuna wakati nilipata Mkata nikaambiwa nyamapori ipo pale. Lakini nilipofika wakasema ni nyama ya mbuzi.”

Bwana nyamapori Doma azungumza

Peter Mayapila ndiye bwana nyamapori anayewajibika kudhibiti rasilimali hiyo katika eneo lote la Doma linalohusisha vijiji kadhaa kikiwamo Mkata. Kwa maelezo yake, ameifanya kazi hii kwa miaka 39 sasa.

 

Anasema kwamba wanashirikiana na Tanapa katika ulinzi wa wanyamapori, lakini anakiri kwamba kazi hiyo inamuwia vigumu kutokana na mtandao wa ujangili kuwa mpana.

 

“Peke yangu kudhibiti ni ngumu, nawajibika katika vijiji vingi-Mkata, Doma, Msongozi, Misengele na vingine vingi,” anasema.

 

Pater, kama walivyo “watetezi” wengine, anasema mara nyingi nyama inayouzwa ni ya ng’ombe. “Wamekuwa wakiuza nyama ya ng’ombe na kusema ni nyamapori.

 

Lakini sikatai kuwa nyamapori haiuzwi, unajua kuna siasa nyingi sana kwenye ujangili, hata ukihoji viongozi wa vijiji wakati mwingi hawasemi, hawatoi ushirikiano kutokomeza maovu kwa sababu wahusika wengi ni ndugu zao,” anasema.


Ninapomwuliza kama na yeye ni mmoja wa washiriki wa biashara ya nyamapori, Peter anang’aka na kusema, “Uliza kijijini, mimi siuzi.”

Wizara ya Maliasili yanena

Mkurugenzi Msaidizi Anayehusika na Mapambano dhidi ya Ujangili, Paul Sarakikya, anakiri kuwa vita dhidi ya ujangili ni kazi ngumu, lakini ushindi lazima upatikane.


“Ujangili upo kila mahali kwa sababu mbalimbali. Ujangili unaanzia ngazi ya kijiji hadi ‘level’ ya juu kabisa. Mtandao ni mkubwa mno.


Watu wanaona ujangili ni mapambano yanayowahusu watu wanyamapori tu.

“Kuna uongozi kuanzia ngazi ya kitongoji, kuna Serikali za vijiji kwanini ujangili ushamiri ilhali viongozi wapo katika ngazi hizo? Kwenye Idara tuna uhaba wa maofisa-lakini kwenye vijiji, wilaya, mikoa kote kuna viongozi.


Wanafanya nini? Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya, Polisi, watendaji wa idara za wanyamapori wote hawa wanafanya nini katika nchi nzima? Sisi hatuwezi kwenda kila mahali-sana sana tukifika ni kuzima moto tu, hasa wakati huu wa sikukuu; lakini kwenye maeneo hayo kuna viongozi. Uongozi ni kazi.


“Mwulizeni Mkuu wa Hifadhi ya Mikumi, waulizeni viongozi wa vijiji – kuna ujirani mwema, msaada wanapata, tatizo nini? Wana mafungu ya uhifadhi, madaraka yao wanayatumiaje? Kuwaangalia wakurugenzi, katibu mkuu au waziri pekee ni kuwaonea. Uhifadhi na kulinda rasilimali za nchi ni kazi ya kila Mtanzania. Kuna madaraka wilayani, kuna madaraka mikoani-lazima tuulizane kuwa tunafanya nini kwenye uhifadhi? Tusioneane aibu.


“Tutalaaniwa wanyamapori wakiisha…tutalaaniwa. Mbona waliotutangulia waliwatunza?” Anahoji Sarakikya kwa hisia kali.


Ushiriki wa askari/maofisa wa Tanapa

JAMHURI imejiridhisha pasi na shaka kuwa ujangili unashamiri kwa sababu ya msada mkubwa wa baadhi ya askari na maofisa wanyamapori hasa katika Hifadhi ya Taifa ya Mikumi.


Katika matukio kadhaa yaliyoripotiwa hivi karibuni, askari wa Tanapa aliyetambuliwa kwa jina la Dotto, alikamatwa akiwa na mhutumiwa mwingine wa ujangili, Mrosso Anthony (Christian Joseph).


Uchunguzi unaonyesha kuwa Dotto alikuwa askari katika Kituo cha Mgoda. Alikamatwa na kupelekwa mahabusu polisi.


Hata hivyo, kesi ya watuhumiwa hao haikuendelea kwa kile kinachoelezwa kwamba maofisa wengine wa Tanapa waliamua kuingilia kati “kumwokoa mwenzao”.


“Huu ujangili hauwezi kukoma kwa sababu wanaoshirikiana na majangili ni baadhi ya askari wa Tanapa na askari polisi,” anasema mtoa habari wetu.


Kamanda wa Kikosi cha Ujangili

Kamanda wa Kikosi Dhidi ya Ujangili (KDU) Kanda ya Mashariki, Masalu, anakiri kuwa Mrosso ni miongoni mwa watuhumiwa wa ujangili waliokuwa wakisakwa kwa muda mrefu.


Anasema mapambano dhidi ya ujangili yatafanikiwa endapo wananchi watashirikiana na viongozi katika ngazi zote.


“Huwezi kumaliza ujangili kwa kuwatumia maofisa wa wanyamapori pekee. Hii vita ni yetu sote kama kweli tumedhamiria kulinda rasilimali hii muhimu,” anasema Masalu.


Ofisa Maliasili Mkoa wa Morogoro

Ofisa Maliasili Mkoa wa Morogoro, Joseph Chuwa, anakiri kuwa ujangili upo katika vijiji kadhaa mkoani humo, na kwamba tatizo hilo si la mkoa huo pekee, bali kwa sasa ni nchi nzima.

 

“Ujangili hasa wa tembo umeshamkiri. Hapo karibu na Mkata unaposema hivi karibuni kuna tembo aliuawa. Tunachofanya ni kupata taarifa za kiintelejensia-kubaini mtandao mzima wa ujangili wa nyara za Serikali. Kuna ujangili wa wanyamapori, kuna nyama zinauzwa.


“Lakini wakati mwingine kwenye maeneo kama Mkata kuna nyama za ng’ombe zinauzwa huku wanunuzi wakidanganywa kuwa ni za pori . Watu wanakula vibudu, nawashauri wawe macho. Hata hivyo, hii haina maana kwamba ujangili wa wanyamapori haupo. Tunahitaji nguvu za pamoja za wananchi wote kupambana na vitendo hivi,” anasema Chuwa.


Kuhusu matumizi ya simu za mkononi ndani ya hifadhi na mapori, Chuwa anasema ni vigumu kuyazuia kwa kuwa pamoja na ukweli kwamba majangili huyatumia kufanikisha ujangili, pia husaidia askari wanyamapori kuwanasa watuhumiwa.


Je, nini kimetokea baada ya JAMHURI kuuweka wazi mtandao wa ujangili katika eneo la Mkata? Usikose toleo lijalo.

 

1104 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!