IDARA YA UHAMIAJI

257. Uhamiaji ni idara ndani ya Wizara ya Mambo ya Ndani yenye majukumu na wajibu kama ilivyoainishwa katika Sheria ya Uhamiaji (The Immigration Act, 1995). Majukumu ya Idara ya Uhamiaji yanajumuisha kuzuia uingiaji nchini Tanzania wa watu ambao si raia wa Tanzania ambao kwa mujibu sheria hawatakiwi nchini (prohibited immigrants), pamoja na kudhibiti utokaji na uingiaji nchini wa raia na wasio raia. Aidha, idara pia ina jukumu la kudhibiti wageni wanaoishi nchini visivyo halali au wanaokiuka masharti yanayoambatana na ruhusa ya kuishi nchini.

258. Idara ya Uhamiaji ina majukumu muhimu na nyeti kitaifa. Ukiukaji wa maadili unaweza kuleta maafa makubwa kwa Taifa na raia wake, kwa mfano kwa kuruhusu kuingia au kukaa nchini mgeni ambaye lengo lake ni kujuhumu usalama, utulivu na amani ya Taifa.

259. Idara ya Uhamiaji ni macho ya Taifa. Nafasi iliyonayo inaifanya na inaihitaji iwe mstari wa mbele kugundua mgeni ambaye kuwapo kwake nchini kunaashiria hujuma kwa nchi, ziwe za kisiasa au kiuchumi. Aidha, inapaswa kuwazuia kuingia nchini wageni wasiotakikana. Kujihusisha kwenye vitendo vya rushwa si tu kunahujumu  jitihada za nchi katika ulinzi wa maslahi ya raia, bali pia ni usaliti wa dhamana idara iliyokabidhiwa na Taifa. Ni kwa mantiki hii rushwa lazima ichukuliwe kama kitu cha hatari inaponyemelea idara hii. 

260. Idara hii pia inalo jukumu kubwa la kudhibiti pasi za kusafiria za Tanzania na kuhakikisha haziangukii kwenye mikono ya watu wasiostahili. Kwa nchi za nje idara imekuwa inasaidiwa na ofisi za ubalozi kutoa na kudhibiti pasi hizi. Hata hivyo, umekuwa na upungufu mkubwa kwenye udhibiti huo. Miaka miwili iliyopita pasi 390 za usafiri za Tanzania ziliibwa zikiwa kwenye ofisi zetu za ubalozi au zikisafirishwa kwenda huko au kurejeshwa nchini. Pasi 300 zilipotea zikiwa njiani kwenda Moscow, Urusi, New Delhi, India na Rome, Italia; 6 zilipotea kwenye ubalozi wetu Lagos, Nigeria; 4 zilipotea Luanda, Angola; 32 zilipotea Rome, Italia; 26 zilipotea njiani zikirudishwa nchini kutoka Addis Ababa, Ethiopia na 22 kutoka Maputo, Msumbiji.

Pasi hizi zinaweza kuwa ziko mikononi mwa wahalifu wa kimataifa na wasafirishaji wa dawa za kulevya, jambo ambalo linalichafulia Taifa letu jina na heshima. Aidha, Tume imepata taarifa kuwa pasi za Tanzania zinamilikiwa na watu wa mataifa ya kigeni kama Walebanoni, Wapakistani na Wahindi. Hili limewezekana kutokana na wizi wa pasi pamoja na upungufu wa uaminifu kwa baadhi ya watumishi wa Idara ya Uhamiaji. 

261. Huduma za Uhamiaji ni kati ya huduma za Serikali zinazolalamikiwa sana si tu na wananchi, bali pia na wageni. Rushwa inasemekana hutawala katika maombi ya pasi za kusafiria yanayofanywa na waombaji raia. Utaratibu wa kupata pasi ni mrefu na huchukua muda mrefu. Hali hii huzaa mianya ya watumishi wa idara wasio waaminifu kudai hongo.

Tume imepata malalamiko kutoka kwa wageni wasio raia, wanaotafuta vibali vya kuishi humu nchini. Mbali na utaratibu wa kutoa vibali hivyo kuwa mrefu, baadhi ya waombaji inabidi watoke nje ya nchi vibali vyao vya muda vinapokwisha halafu ndipo warudi nchini waombe vibali vingine vya muda wakati wakingojea majibu ya vibali vyao.

Licha ya kuwa gharama kwa hawa wageni, utaratibu huu unatoa mianya mikubwa ya rushwa kwa waombaji kushawishi watumishi wa idara ama watumishi wa idara kukawiza kushugulikia maombi ili walipwe hongo kwanza. Pia tume imebaini ukosefu wa uwazi katika tarabibu za utoaji vibali vya kuishi nchini.  

262. Huko Kigoma, tume ilipata malalamiko kuhusu maofisa wa Uhamiaji kufumbia macho wageni kutoka nchi za jirani kuishi nchini bila vibali. Baadhi ya maofisa hawa wamekaa hapo mpakani zaidi ya miaka 10 na hivyo kujenga uhusiano wa karibu na wageni kutoka nchi za jirani.

Wananchi walidai kuwa wakati kazi ya kukabiliana na tatizo la rushwa katika idara lililofanyika mwaka 1995, alistaafishwa ofisa safi na kuwaacha wale wanaotuhumiwa kuhusika katika vitendo vya rushwa na hivyo kuruhusu wageni waishi nchini bila vibali.

263. Idara inaongozwa na Mkurugenzi wa Uhamiaji ambaye ndiye mtendaji mkuu. Watendaji chini yake huitwa maofisa Uhamiaji. Mkurugenzi anawajibika kwa Waziri wa Mambo ya Ndani. 

264. Katika kutekeleza wajibu wake, Idara ya Uhamiaji inafanya mambo yafuatayo: 

(a)  Kutoa vibali vya ukazi nchini kwa watu wasio raia wa Tanzania na wenye sifa zilizotajwa katika sheria;

(i)  Kutoa pasi za kusafiria nje ya nchi kwa raia wa Tanzania.

(ii) Kutoa ruhusa za kuingia nchini (viza) kwa wageni wasio raia wa Tanzania;

(iii) Kutoa ruhusa maalumu za kuingia nchini (referred visa) kwa raia wa mataifa yanayohitaji udhibiti maalumu wa kiuhamiaji;

(iv)  Kutoa uraia kwa raia wa mataifa ya kigeni wanaoomba kuwa raia wa Tanzania na wenye sifa na wanaotimiza masharti;

(v)  Kufanya doria za ukaguzi katika viwanda, mahoteli, nyumba za kulala wageni n.k. ili kuwagundua raia wa nchi za nje waliomo nchini kinyume na sheria au waliokiuka masharti ya kuwapo kwao nchini.

265.  ‘The Immigrationn Act, 1995’ imeunda bodi inayoitwa “The Alien Immigrant Board” yenye majukumu yafuatayo: 

Kumshauri Mkurugenzi wa Uhamiaji na mamlaka nyinginezo zinazohusika kuhusu vigezo vya kutoa vibali vya kufanya kazi nchini kwa wasio raia;

Kumshauri Mkurugenzi wa Uhamiaji na mamlaka nyingine zinazohusika kuhusu vigezo vya kuwapa leseni za biashara au vibali vya ukazi nchini vya Daraja B wasio raia wa Tanzania; 

Kumshauri Mkurugenzi wa Uhamiaji na mamlaka nyingine zinazohusika kuhusu namna bora ya kuendesha udhibiti wa kutekelezwa kwa masharti ya ukazi na mienendo ya wageni wenye vibali vya Daraja A na Daraja B;

Kumshauri Mkurugenzi wa Uhamiaji na mamlaka nyingine zinazohusika iwapo au sivyo aina ya biashara au ajira inayoombwa na raia wa kigeni haiwezi kutekelezwa na raia wa Tanzania; 

266. Wajumbe wa ‘The Alien Immigrant Board’ ni:

(a)   Mwenyekiti ambaye anateuliwa na Rais; anatakiwa awe na sifa ya kuwa Ofisa Mwandamizi kutoka wizara yenye kuhusika na Uhamiaji;

(b)  Katibu wa Bodi ambaye ni Kamishna wa Kazi katika Serikali ya Muungano (au mwakilishi);

(c)   Kamishna wa Kazi katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (au mwakilishi);

(d)  Maofisa waandamizi mmoja mmoja kutoka Serikali ya Muungano na ya Mapinduzi Zanzibar na wawakilishi wa taasisi zifuatazo:

i)  Wizara zinazoshughulikia biashara na viwanda.

ii)  Taasisi zinazohusika na masuala ya mipango.

iii) Taasisi zenye majukumu ya utumishi serikalini.

Utaratibu wa kutoa hati mbalimbali

 

Pasi (Passport)

267. Pasi ni hati maalumu ya kiserikali na inayokubalika kimataifa kama kielelezo cha uraia wa taifa fulani. Mwombaji wa pasi lazima awe amethibitika kuwa raia wa Tanzania. Kwa hiyo moja ya masharti ya kupata pasi ni kuwa raia. Mwombaji anajaza fomu maalumu ya maombi ya pasi inayoambatishwa na uthibitisho wa uraia wa Tanzania.

268. Mara nyingi pasi huombwa na watu ambao wanasafiri nje ya nchi. Kwa hiyo pamoja na sharti la msingi lililoainishwa hapo juu, masharti mengine hutegemea madhumuni ya safari ya mwombaji nje ya nchi:

(a)   Mwombaji anayeomba pasi kwa madhumuni ya kusafiri nje ya nchi kwa ajili ya masomo anahitajika kuambatanisha fomu yake ya maombi na hati zenye kuthibitisha nafasi ya masomo, barua ya mdhamini wa masomo pamoja na vyeti vyenye sifa za kujiunga na masomo hayo.

(b) Uombaji wa pasi kwa madhumuni ya safari za kibiashara nje ya nchi sharti uambatane na uthibitisho wa mawasiliano ya kibiashara na wenyeji wa mwombaji katika nchi anayokwenda, leseni halali ya biashara ya mwombaji wa pasi, hati za kuandikishwa biashara (Memorandumu and Articles of Association and Certificate of Incorporation) pamoja na tiketi ya safari ya kwenda na kurudi.

(c)   Fomu za maombi ya pasi kwa ajili ya safari ya matembezi ya burudani nje ya nchi sharti ziambatishwe na kiapo cha mdhamini kutoka kwa atakayekuwa mwenyeji wa mwombaji katika nchi anakokwenda. Kiapo hicho kiwe kimethibitishwa na ubalozi wa Tanzania au mwakilishi katika nchi hiyo. Aidha, viambatisho vingine ni pamoja na tiketi ya safari ya kwenda na kurudi na idhini ya maandishi ya mzazi wa kijana wa umri chini ya miaka 18 au barua ya mwajiri kwa mtu mzima.

(d)  Maombi kwa ajili ya safari ya ubaharia yanahitajika yaambatane na mkataba wa kazi na nchi inayohusika pamoja na vitambulisho vya ubaharia, vyeti vya ujuzi wa mwombaji na barua kutoka Chama cha Mabaharia.

(e) Maombi kwa ajili ya safari za kuajiriwa nje ya nchi lazima yaambatane na mkataba wa ajira, vyeti vya ujuzi na uthibitisho wa kutimia kwa masharti kama inavyoelekezwa na Idara ya Kazi.

269. Hatua mbalimbali zinazofuatwa wakati wa uombaji wa pasi ni hizi zifuatazo:

(a)   Fomu ya maombi ya pasi iliyojazwa kikamilifu na mwombaji hukabidhiwa kwa Ofisa Uhamiaji katika kituo cha utoaji pasi ikiwa na viambatisho vyote kama ilivyoainishwa katika aya ya (11).

(b)  Baada ya kuzikagua nyaraka hizo na kuridhika na usahihi wake, Ofisa Uhamiaji huziwekea alama ya usahihi na kumtaarifu mwombaji aende kulipia katika dirisha la malipo. Iwapo nyaraka hazijakamilika au sio sahihi, mwombaji hurejeshewa na kuelezwa upungufu huo ili aurekebishe.

(c)   Baada ya kufanya malipo na kukabidhiwa stakabadhi yaSerikali ya kukiri malipo hayo na nakala ya stakabadhi hiyo kuambatishwa na fomu ya mwombaji, ndipo mwombaji anapoelezwa na ofisa uhamiaji siku ya kurudi kwa ajili ya kufuatilia pasi yake.

(d)  Pasi hukabidhiwa kwa mwombaji na Ofisa Uhamiaji baada ya kujitambulisha. Utaratibu unaruhusu mwombaji kuonana na kiongozi wa Ofisa Uhamiaji ambaye hataridhika na hoja za  nyaraka zake kutokidhi masharti.

270. Sehemu ya kaunta mahali nyaraka za maombi ya pasi zinapotolewa na kupokewa ndiyo inayolalamikiwa mno kuhusika na vitendo vya kupokea rushwa kutoka kwa waombaji pasi. Baadhi ya maofisa Uhamiaji wanachukua fursa ya masharti na taratibu kutokuwa wazi kuwazungusha waombaji ili hatimaye watoe rushwa. Lakini baadhi ya waombaji ndiyo huwa chanzo cha rushwa kwa kutaka njia za mkato baada ya kutotimiza kikamilifu masharti ya uombaji.

271. Aidha, matumizi ya wakala katika kufuatilia upatikanaji wa pasi kwa ajili ya baadhi ya waombaji kunasababisha ongezeko la tabia ya rushwa katika utaratibu wa utoaji pasi. Watu hao (wakala) hutoa rushwa kwa maofisa Uhamiaji ili kuharakishiwa pasi na wakati mwingine kupata pasi bila kukamilisha masharti.

 

Viza (Visa)

272. Viza ni kibali chenye kuonyesha aina ya ruhusa iliyotolewa kwa raia wa nchi ya kigeni anayeingia nchini. Kuna aina tatu za viza: viza ya kawaida, viza ya safari zaidi ya moja (multiple visa) na viza rejea. Utaratibu na masharti ya kupata aina mbalimbali ya viza ni kama ifuatavyo:

 

(a)  Viza ya kawaida

Mwombaji hujaza fomu maalumu ya maombi ya viza ambayo huiambatanisha na hati ya dhamana yenye stempu ya ushuru, pasi ya mwombaji, nakala mbili za picha ya mwombaji, barua yenye ufafanuzi wa madhumuni ya safari ya mwombaji pamoja na fedha za ada ambazo kiwango chake hutegemea utaifa wa mwombaji.

 

(b) ‘Multiple visa’

Pamoja na masharti ya kupata viza ya kawaida, masharti ya ziada yanayoambatana na viza ya safari za mara kwa mara kuja na kutoka Tanzania ni pamoja na uthibitisho wa umuhimu wa safari hizo. Kwa mfano, uwekezaji au kuwa na ubia na kampuni iliyopo nchini au kwa mwanafunzi zinaweza kuwa sababu za msingi za kupata ‘multiple visa.’

 

(c) Viza rejea (Referred Visa)

Visa rejea inawahusu raia wa mataifa yenye matatizo maalumu kama yanavyoainishwa na serikali mara kwa mara. Masharti ya upatikanaji viza rejea hayatofautiani sana na yale ya utoaji ‘multiple visa’ isipokuwa tu utaratibu wa uidhinishaji.

273. Mwanya wa rushwa katika taratibu za kutolewa viza unatokana na hatua ya mwanzo ya kukabidhi nyaraka ambapo mwombaji au wakala anakutana ana kwa ana na Ofisa Uhamiaji. Baadhi ya maofisa Uhamiaji huchukua fursa hiyo kushawishi kupewa rushwa.

 

Vibali vya ukazi nchini

274. Sheria inaainisha aina tatu za vibali vya kuishi nchini: vibali vya Daraja A, Daraja B na Daraja C. 

275. Hati za vibali vya Daraja la A hutolewa kwa wageni ambao wanaingia nchini kwa madhumuni ya kufanya biashara, shughuli miradi ya kilimo, ufugaji wa kisasa, utafutaji wa uchimbaji na madini na viwanda. Masharti yanayoambatana na vibali vya ukazi vya Daraja A ni pamoja na mahali atakaporuhusiwa mwombaji kuishi akiwa Tanzania. Aina ya biashara au taaluma wanayoruhusiwa kuifanya na kipindi cha ukazi.

276. Hati za vibali vya Daraja B hutolewa kwa raia wa kigeni wenye sifa za waajiriwa nchini katika nafasi ya ajira ambayo kwa maoni ya Mkurugenzi wa Uhamiaji ni yenye manufaa kwa taifa, lakini hayupo mtaalamu raia wa Tanzania anayeweza kuijaza. Utaratibu wa kuwasilisha maombi na kushughulikiwa hati za Daraja B ni wa kujaza fomu maalumu ya maombi na kuwasilisha Idara ya Uhamiaji pamoja na vielelezo vifuatavyo:

(a) Mapendekezo yenye kuafiki ajira hiyo kutoka kwa Kamishna wa Kazi

(b) Ushahidi wa uhalali wa kampuni inayotaka kumwajiri mtaalamu mwombaji vikiwemo ‘Memorandum and Articles of Association’, ‘Certificate of Incorporation’ na ‘Organization Chart.’

(c)  Mkataba wa ajira.

(d) Ushahidi wa utaalamu wa mwombaji unaohusiana na ajira inayoombewa ukazi.

(e)  Historia ya maisha ya mwombaji (Curriculum Vitae).

277. Hati ya ukazi ya Daraja C hutolewa kwa raia wa kigeni wanaoomba kuingia nchini kwa madhumuni tofauti na yanayotolewa vibali vya Daraja A na Daraja B kama vile uanafunzi, utafiti na umisionari.

278. Yapo malalamiko mengi yenye tuhuma za utoaji vibali vya ukazi hususan vile vya Daraja B kwa misingi ya rushwa nje ya taratibu zilizoelezewa na sheria. Rushwa imesababisha kuwapo hapa nchini kwa raia wengi wa nchi za kigeni wakifanya kazi ambazo raia wetu wanayo elimu na ujuzi kamili wa kuzifanya.

279. Maofisa wa kampuni zinazohitaji kuwaajiri raia wa kigeni ambao wanatumika kuwaombea raia hao vibali vya ukazi vya Daraja B nao wamekuwa chanzo cha kushamiri kwa rushwa miongoni mwa maofisa Uhamiaji. Maofisa hutoa rushwa kwa maofisa Uhamiaji wanaohusika ili wawaharakishie au wapinde taratibu za kupata vibali hivyo.

 

Uraia

280. Moja ya majukumu ya Idara ya Uhamiaji ni kushughulikia maombi ya uraia wa Tanzania chini ya vifungu vya sheria ya uraia. Masharti ya uandikishaji uraia yamo katika sura ya 452 kifungu cha 2(1) kwa uraia wa ‘registration’ na 7 kwa uraia wa ‘naturatlization.’ Masharti hayo ni kama ifuatavyo:

(a)  Mwombaji awe ameishi kihalali nchini Tanzania kwa miaka mitano kwa wanaoomba uraia wa ‘registration,’ na miaka saba kwa wanaoomba uraia wa ‘naturalization.’

(b)  Mwombaji awe anajua kwa ufasaha lugha za Kiswahili au Kiingereza

(c)  Mwombaji awe mwenye tabia nzuri.

(d) Kwamba awe mtu anayefaa kwa maslahi ya Taifa 

281. Utaratibu unaofuata ni kama ifuatavyo:

(a)  Mwombaji achukue fomu za maombi ya uraia katika ofisi ya Uhamiaji iliyo karibu naye na kuzijaza. Baada ya hapo anazipeleka fomu hizo katika ofisi ya kata ambayo anaishi mwombaji.

(b) Mwombaji anatakiwa atangaze kwenye magazeti nia yake ya kutaka uraia wa Tanzania. Pia huchukuliwa alama za vidole polisi ili ijulikane kama hajawahi kupatikana na makosa ya jinai.

(c) Ofisi ya kata ikishakamilisha kumjadili mwombaji, maombi hupelekwa kwa Mkuu wa Wilaya na Ofisa Uhamiaji ambaye ndiye katibu wa vikao vyote vya  uraia. Ofisa Uhamiaji anaiarifu Kamati ya Wilaya inayohusika kufikiria maombi ya uraia ambayo ni pamoja na kuwasilisha taarifa zozote nyingine muhimu.

(d) Baada ya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kumaliza kuyajadili maombi hayo, nayo huyapeleka kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na mapendekezo yake.

(e) Baada ya maombi kujadiliwa katika kikao cha mkoa, Ofisa Uhamiaji wa Mkoa anayatuma kwa Mkurugenzi wa Uhamiaji yakiwa pamoja na mapendekezo ya wilaya na mkoa, matokeo ya uchunguzi wa alama za vidole na vipande vya kujitangaza  gazetini. Pia anaambatanisha nakala ya hati ya mwombaji ya kuishi nchini.

(f) Mkurugenzi wa Uhamiaji baada ya kupokea maombi hayo atahakikisha kuwa tangu tangazo litoke gazetini limemaliza angalau miezi mitatu na kuyapitia maoni yaliyotolewa na wananchi kama yapo. Baada ya kuridhika kuwa maombi yamekamilika, Mkurugenzi atamshauri Waziri wa Mambo ya Ndani kuyakubali au kuyakataa maombi hayo.

(g)   Naye Waziri wa Mambo ya Ndani kwa kutumia uwezo alionao kisheria chini ya Sheria ya Uraia ataamua kukubali au kuyakataa maombi hayo na uamuzi wa waziri ni wa mwisho, hauwezi kutenguliwa na mahakama yoyote.

 

Je, unafahamu Jaji Warioba katika ripoti hii aliyoiandaa mwaka 1996 anazungumziaje kiwango cha rushwa ndani ya Idara ya Uhamiaji? Usikose JAMHURI wiki ijayo. Mhariri.

By Jamhuri