Uhamiaji, mahakimu rushwa tu

Mianya ya rushwa

282.  Mianya ya rushwa katika Idara ya Uhamiaji inatokana na baadhi ya vifungu vilivyomo katika Sheria ya Uhamiaji. Lakini sehemu kubwa ya mianya ya rushwa ni matokeo ya usimamizi wa kazi usioridhisha wa watumishi wa idara hiyo na kupuuzwa kwa umuhimu wake katika utaratibu mzima wa uendeshaji wa serikali.

Kupuuzwa huko kumesababisha uongozi kukata tamaa kwa kukosa nyenzo za kusimamia ufanisi na baadhi ya maofisa uhamiaji kujichukulia fursa iliyojitokeza kujinufaisha binafsi katika utekelezaji wa majukumu ya Idara ya Uhamiaji.

 283. Mianya inayotokana moja kwa moja na sheria huhusisha vifungu vyenye kutoa “discretionary powers” kwa maofisa uhamiaji, hususan katika kutolea maamuzi masuala yanayowakutanisha ana kwa ana ofisa uhamiaji na mteja. Kwa mfano, hati ya kibali cha kuishi cha Daraja A huambatana na dhamana ya malipo ya fedha taslimu ambazo kiwango chake kimeelezewa kuwa kitakachoafikiwa na ofisa uhamiaji kwamba kitatosheleza gharama za kumwondoa nchini mwombaji pamoja na watu wanaomtegemea atakaoishi nao hapa nchini itakapobidi.

 

284. Mianya mingine ya rushwa inatokana na yafuatayo:

 i) Kuwepo vyombo vingi vinavyoshughulikia maombi ya hati za ukazi nchini ambavyo ni pamoja na Idara ya Uhamiaji, Idara ya Kazi na Kituo cha Uwekezaji Rasilimali (IPC) na Usalama wa Taifa;

ii) Kutokuwa wazi kwa utaratibu wa kutoa hati za uhamiaji na hivyo kuwapa fursa baadhi ya watumishi wa idara kuwasumbua wateja;

iii) Kuruhusu watu wa kati (agents) kuwasilisha maombi kwa niaba ya waombaji;

iv) Wananchi kutozielewa sawa sawa sheria za uhamiaji.

v) Kuwapa madaraka makubwa ya kutolea maamuzi ya mwisho masuala nyeti kama vile idhini ya vibali vya ukazi Daraja B maofisa uhamiaji bila udhibiti wa lazima wa Mkurugenzi wa Uhamiaji.

 285. Taratibu za uhamiaji (“The Immigration Regulations, 1995”) zimependekeza mgawanyo wa ada za malipo ya hati za vibali vya Daraja A katika mafungu mawili ya wawekezaji katika kampuni, viwanda, uvuvi, madini na usafirishaji na wawekezaji katika biashara za maduka ya bidhaa za matumizi ya kila siku, za nyama, vifaa vya ujenzi na kadhalika. Kuweka viwango vinavyotofautiana vya ada za malipo ya hati za vibali vya kundi moja, ni dhahiri kunasababisha udhaifu na kustawisha rushwa.

 286. Vitendo vya rushwa ndani ya Idara ya Uhamiaji vinahusisha maeneo na vitendo vifuatavyo:

 (a)  Maofisa Uhamiaji hupokea rushwa kutoka kwa watu wasiokuwa raia wa Tanzania na ambao sheria inawazuia kuingia nchini (“Probihited immigrants”) ili wawawezeshe kuingia au kuendelea kuishi nchini;

(b) Maofisa Uhamiaji hupokea rushwa kutoka kwa waombaji wa vibali vya kuishi nchini ili wasizingatie kikamilifu masharti ya vibali hivyo;

(c)  Maofisa Uhamiaji hupokea rushwa kutoka kwa waajiri wa raia wa kigeni hapa nchini ili wawezeshe kutochukuliwa hatua za kisheria kwa kukiuka taratibu za uajiri wa raia wa nchi za kigeni katika kampuni au viwanda vyao;

(d) Maofisa Uhamiaji hupokea rushwa kutoka kwa raia wa nchi za kigeni ili wawape hati za kusafiria za Tanzania kinyume na sheria;

(e)  Maofisa Uhamiaji hupokea rushwa ili wawaruhusu wageni wenye vibali vya kuishi nchini vya Daraja A na Daraja B kuendelea kuishi nchini wakifanya shughuli tofauti na walizopokelea vibali;

(f)   Maofisa Uhamiaji kupokea rushwa ili wasiwachukulie hatua wageni wenye hadhi ya ukimbizi kuishi nje ya makambi rasmi, hususan katika mikoa ya mipakani mwa nchi.

(g)  Maofisa Uhamiaji kupokea rushwa ili waweze kushawishi taarifa nzuri za maombi ya uraia kwa ngazi za juu.

 

Upungufu wa uongozi

 287. Pamoja na upungufu wa baadhi ya vifungu vya sheria, imeshaelezwa kuwa tatizo la upungufu katika usimamizi limechangia kwa kiasi kikubwa kuzorotesha ufanisi wa utendaji kazi wa Idara ya Uhamiaji na kuchochea rushwa. Mamlaka kuu ya uongozi wa Idara ya Uhamiaji ni Waziri wa Mambo ya Ndani ambaye Mkurugenzi wa Uhamiaji anawajibika kwake kwa mujibu wa sheria.

 Taratibu za uwajibikaji wa idadi kubwa ya maofisa uhamiaji ni ndefu na zinazohitaji uamuzi wa juu zaidi ya Mkurugenzi wa Uhamiaji, yaani uamuzi wa waziri. Uamuzi huo umekuwa ukicheleweshwa sana kufikiwa na hivyo kusababisha kuendelea kwa vitendo vinavyolalamikiwa ikiwemo rushwa.

 288. Matatizo mengi ya Idara ya Uhamiaji ni matokeo ya udhaifu wa uongozi uliotokana na upeo duni na uliosababisha nyenzo za kazi zilizo chache na dhaifu kama vile ukosefu wa “stationaries,” magari machache na mabovu, majengo duni ya ofisi, uhaba wa nyumba za kuishi wafanyakazi, vyombo duni vya mawasiliano, ukosefu wa kuoanisha maendeleo ya sayansi na teknolojia katika utendaji, na kadhalika.

 Aidha, tatizo la uongozi limesababisha kutokuwepo utaratibu wa mafunzo ya maofisa uhamiaji kwa kipindi cha miaka kadhaa hivi sasa kutokana na kukosekana kwa chuo cha kufundishia. Idara ya Uhamiaji ilikuwa ikikitumia Chuo cha Polisi kwa mafunzo ya maofisa wake, lakini walinyimwa fursa ya kukitumia miaka mingi iliyopita. Kadhalika uamuzi wa kupitisha hati ya “The Immigration Regulations, 1995” kufuatia “The Immigration Act, 1995” haujafanywa hadi sasa hivi ingawa hati hiyo ni ya mwezi Desemba, 1995.

 

Mapendekezo

 289. Kutokana na matatizo yaliyoelezwa, Tume inatoa mapendekezo yafuatayo katika jitihada za kupambana na wimbi la rushwa inayoikabili Idara ya Uhamiaji:

 (a)  Taratibu za utolewaji wa pasi na vibali vya kuishi nchini uwe wa wazi na urahisishwe;

 (b)  Baada ya waziri kuwa ndiye mamlaka kuu ya kutoa maamuzi kuhusiana na Idara ya Uhamiaji, inapendekezwa kuwa mamlaka hayo apewe Katibu Mkuu. Yaani Mkurugenzi wa Uhamiaji awajibike kwa Katibu Mkuu wa Wizara badala ya waziri. Utekelezaji wa pendekezo hili utasaidia pamoja na mambo mengine kuharakisha maamuzi;

 (c)   Serikai itambue upya wajibu na umuhimu wa Idara ya Uhamiaji kuwa sehemu muhimu ya udhibiti wa ulinzi, usalama na uchumi wa taifa na hivyo kusaidia kikamilifu katika utatuzi wa matatizo yanayoathiri ufanisi wake. Masuala muhimu yanayohitaji ufumbuzi wa haraka ni pamoja na suala la mafunzo, zana na maeneo ya ofisi;

 (d)  Idara ya Uhamiaji iimarishwe pamoja na vinginevyo, kwa kupewa uwezo wa utunzaji wa kisasa wa kumbukumbu mbalimbali. Upo umuhimu mkubwa wa kuwekeza katika eneo la kompyuta na zana nyingine za mawasiliano;

 (e)   Bajeti ya Idara ya Uhamiaji ijitegemee badala ya kuwa sehemu ya wizara jambo ambalo limesababisha wakati mwingine bajeti yake kutumika katika kutekeleza “commitments” nyingine za wizara zisizo na uhusiano wa moja kwa moja na Idara ya Uhamiaji;

(f)   Lifanywe zoezi mahususi la kuhamisha maofisa uhamiaji, hususan walioko kwenye vituo vya mipakani kama hatua ya awali ya ndani ya idara ya  kuondoa rushwa iliyosababishwa na mahusiano ya karibu baina yao na wateja kwa kuzoeana;

 (g)  Vifungu vya sheria vyenye kutoa “discretionary powers” kwa maofisa, hususan kwa maamuzi ambayo yanawakutanisha ofisa na mteja virekebishwe ili maeneo ya fedha yawekewe viwango visivyoweza kubadilishwa kwa ridhaa;

 (h) Pasiwepo tofauti za ada za malipo ya hati za vibali vya kuishi nchini vya Daraja A. Kwa hiyo kifungu kinachohusika katika rasimu ya taratibu za uhamiaji za 1995 kirekebishwe kwa madhumuni hayo;

 (i) Masilahi ya maofisa uhamiaji yaoanishwe na masilahi ya watumishi wa vyombo vingine vya dola na kodi ili ipunguze kasi ya rushwa inayosababishwa na ushindani unaotokana na tofauti kubwa ya masilahi, hasa kwa kuwa watumishi huwa wote hufanya kazi bega kwa bega katika vituo vingi vya kazi za maofisa uhamiaji;

 (j) Majukumu ya msingi ya “The Alien Immigrant Board” yawe kusimamia ufanisi wa Idara ya Uhamiaji kwa kuhakikisha kuwa idara inapata nyenzo zinapohitajika kwa mwelekeo wa kiutendaji wa kisasa. Majukumu yaliyoorodheshwa katika Sheria ya Uhamiaji, 1995 pekee hayana uwiano na hali halisi ya utendaji na kimsingi hayatekelezeki;

 (k)  Idara ya Uhamiaji itayarishiwe utaratibu utakaowezesha uthibitisho wa tabia na mienendo ya kimaadili ya maofisa uhamiaji wa mara kwa mara ili kuhakikisha kwamba hawajipatii mali na fedha kwa njia ya rushwa. Utaratibu huo uanze na zoezi la ki-idara la kuwatambua maofisa ambao wamekuwa wakijihusisha na rushwa na bado wapo kazini; hatua za kisheria na kinidhamu zichukuliwe dhidi ya watakaopatikana na tuhuma kwa kadiri itakavyofaa;

 (l) Idara ya Uhamiaji itangaze ufunguzi wa ukurasa mpya wa utendaji pasipo rushwa kwa kutayarisha vijitabu na kuvisambaza kwenye ofisi ya balozi ndani na nje ya nchi, katika viwanda na kampuni maarufu kwa kuajiri wataalamu raia wa kigeni na penginepo. Aidha, iweke matamshi katika mabango sehemu zote za huduma yatakayotangaza vita dhidi ya rushwa;

(m) Ili kukabiliana na wimbi la uingiaji wa raia wa nje nchini kwa madhumuni ya ajira, Tume inapendekeza Idara Kuu ya Utumishi iandae orodha maalumu ya fani na taaluma ambazo pekee ndizo zitakazoruhusiwa kuwa na waajiriwa wageni. Orodha hii itasaidia kupunguza matumizi mabaya ya “discretionary powers” miongoni mwa maafisa wa Idara ya Kazi na wale wa Uhamiaji.

 

MAHAKAMA

 290.  Mahakama ni idara inayohusika na utoaji wa haki kwa mujibu wa mgawanyo wa madaraka [ya] dola kama yalivyoainishwa katika Katiba ya nchi. Kwa wananchi wa kawaida, Mahakama inaonekana kama ndiyo Serikali kwa kuwa ndiyo inayotatua migogoro baina ya wananchi inapofikishwa huko.

Mahakama ndiyo inayoonyesha nguvu za dola kwa kuwaadhibu wahalifu na kutatua migogoro inayohusiana na kesi za madai. Hivyo mahakama huonekana kwa wananchi kuwa chombo chenye mamlaka mazito yanayotishia adhabu kwa wahalifu, kuwafidia na kuwalinda walioathirika na uhalifu au dhuluma.

 Kwa nantiki hii, mahakama inachukua nafasi muhimu katika jamii na kama itatimiza wajibu wake ipasavyo itawatia wananchi moyo na kuheshimika. Vinginevyo itaua matumaini ya raia na kupoteza imani na hivyo kuonekana siyo kimbilio la wenye kiu ya haki, bali msaliti wa matarajio ya wananchi.

 291. Mahakama kama chemchemi ya haki inatarajiwa kusimamia haki bila woga, upendeleo au hila. Mbele ya sheria wananchi wote si tu ni sawa bali wanaonekana ni sawa bila kubaguliwa kwa misingi ya nyadhifa zao au uwezo wao wa kifedha. Haki haipaswi kuwa na macho kuweza kupambanua tajiri na maskini.

Kwa hiyo mahakama ni chombo kinachoweza kufanikisha ulinzi wa haki na kupiga vita rushwa ambayo huhujumu haki. Mahakama inaweza kufanya hivyo kwa kutoa adhabu zinazostahili kwa watoaji na wapokeaji rushwa. Inaweza pia kutafsiri sheria inayohusika na udhibiti wa rushwa kwa namna ambayo itafanikisha makusudio ya sheria hiyo badala ya kuitafsiri kama sheria na kanuni ya adhabu (Penal Code).

Uamuzi wa mahakama unaweza kuwa chimbuko zuri la uboreshaji wa Sheria ya Kuzuia Rushwa kwa kubainisha upungufu wake na kupendekeza marekebisho gani yafanywe na Bunge. Aidha, kwa kutumia mamlaka yake ya kusimamia vyombo vingine vya dola, mahakama inaweza kudhibiti vyombo hivyo visiwe kero kwa wananchi kwa kuvuruga haki zao.

292. Mahakama ina nafasi kubwa katika kuleta na kudumisha amani nchini iwapo wananchi watajenga imani yao kwenye chombo hiki. Wananchi wakianza kuwa na mashaka na maamuzi ya mahakama au kuhisi kwamba mahakimu au majaji wanapotoshwa katika utendaji wao kwa sababu ya rushwa au utovu wa uadilifu katika kazi hiyo ya utoaji haki, amani iko hatarini kupotea na kuwafanya wananchi wajichukulie sheria mikononi mwao ili kusimamia haki kama watakavyoitafsiri wao.

Aidha, pale ambapo Mahakama itasaliti misingi ya utendaji kazi, kuna hatari ya kukaribisha migongano baina ya utawala (Executive) na mahakama. Kwenye migongano hiyo, utawala wa sheria utaathirika vibaya.

293.  Katika ziara zake nchini kote na katika vikao mbalimbali ambapo Tume ilikutana na wananchi, Mahakama imejitokeza kama moja ya Idara ya Serikali zilizolalamikiwa kwa kutumbukia katika vitendo vya rushwa kwa kiwango kikubwa sana. Wananchi wengi waliofika kuiona Tume hawaamini hivi sasa kuwa wanaweza kupata haki mahakamani bila kuhonga. Wanaamini kama “mahakamani kuna sheria tu, lakini hakuna haki.”

 294. Asilimia kubwa ya tuhuma za rushwa zinaelekezwa kwa mahakimu wa mahakama za mwanzo. Mahakama hizi ziko karibu sana na wananchi na ndizo zinazogusa maisha ya raia wengi vijijini. Mahakimu hawa wamekuwa wakifanya kazi jinsi wapendavyo bila kuzingatia misingi na miiko ya kazi zao. Baadhi yao wanadaiwa kutoa hukumu bila kusikiliza kesi.

Tume imepata mifano inayoonyesha baadhi ya mahakimu hawa kwa kushirikiana na polisi, hukamata watu wasio na hatia na kuwadai hongo ndipo waachiliwe. Aidha, hakimu mmoja alitoa hukumu na kumnyima haki ya kukata rufaa aliyekuwa ameshindwa.

 Hakimu mwingine katika Mahakama ya Mwanzo Somanda amewaondoa wananchi katika maeneo waliyopewa wakati wa operesheni vijijini. Alipoambiwa kwamba uamuzi wake unapingana na maelekezo ya Jaji Mkuu juu ya suala hili, alisema Jaji Mkuu hakuandika waraka.

 Huko Ushirombo, Hakimu aliandika hukumu njiani na kumtia mwananchi mmoja hatiani bila kufuata utaratibu wa kesi na sheria. Aidha, kuna matukio mengi ambayo wananchi wamefungwa magerezani kwa kutumia amri za mahakama, lakini shauri linapofuatiliwa mahakamani, majalada wala usajili wa kesi hizo katika masjala ya mahakama havitaonekana.

 Vitendo hivi vya rushwa na unyanyasaji katika mahakama hizi vimekuwa kero kubwa kwa wananchi na vimefanya wananchi wengi kupoteza imani na mahakama hizi.

 295. Mahakama za wilaya na mahakama za Hakimu Mkazi nazo zinalalamikiwa na wananchi. Mmomonyoko wa maadili katika safu hizi unaanza kuonekana dhahiri. Kutoka Mkoa wa Kilimanjaro, Tume ilipokea taarifa ya Hakimu Mkazi kukaa peke yake bila kuwepo mlalamikaji wala mlalamikiwa na kushughulikia maombi ya kukaza hukumu na kutoa amri ya kukamata fedha kwenye akaunti ya benki ya mlalamikiwa bila kumpa mlalamikiwa fursa ya kujitetea.

Vitendo vya aina hii huzaa hisia za rushwa na kuteremsha heshima ya mahakama. Aidha, katika ziara yake mkoani Kigoma kwenye kikao chake na wananchi Kigoma mjini, Tume ilielezwa jinsi Hakimu Mkazi wa hapo alivyokuwa amepoteza heshima yake kutokana na vitendo vyake vilivyo kinyume na miiko ya kazi zake.

Wananchi hao walieleza kuwa kama hakimu huyo hatahamishwa basi serikali itabeba lawama kwa lolote litakalomsibu. Mahakimu wa aina hii ndio baadaye wanapanda hadi kwenye ngazi ya ujaji. Tume ilichukulia maneno haya kwa uzito unaostahili na kufikisha ujumbe huu kwa mamlaka inayohusika.

296. Katika Mahakama Kuu, kuna tuhuma dhidi ya majaji kuhusiana na vitendo vya rushwa ili kupotosha haki. Hawa wanatuhumiwa kupokea rushwa ama wao wenyewe au kupitia kwa makarani au mawakili. Hata hivyo Tume imeridhika kuwa rushwa inahusishwa na majaji wachache wa Mahakama Kuu na ni rahisi kuidhibiti.

297. Tuhuma za rushwa mahakamani zinawalenga pia makarani na washauri wa mahakama (Court Assessors). Kuhusu washauri wa mahakama, pamoja na kuwa viwango vyao vya posho ni vidogo na mara nyingi huchelewa kulipwa, bado washauri hao wanahudhuria vikao vya mahakama.  Hali hii huzaa hisia kuwa kuhudhuria kwao mahakamani kunawawezesha kupata chochote.

298. Kutokana na kupungua kwa imani katika Idara ya Mahakama, wananchi wameanza kuwa na hofu kwamba vita dhidi ya rushwa kwa njia za kutumia sheria haitaleta mafanikio yoyote kwa vile baadhi ya mahakimu na majaji ambao wanatakiwa kuwaadhibu walarushwa kwa kufuata sheria, nao wanajihusisha na rushwa.

Katika baadhi ya vikao na wananchi Tume ilipewa mawazo kwamba iundwe Mahakama Maalumu ya Kupambana na Makosa ya Rushwa (Mahakama hii imeundwa na Rais John Magufuli mwaka 2016) kwa kuwatumia majaji wenye uadilifu na tabia zisizokuwa na mashaka kama ilivyofanyika wakati wa operesheni ya wahujumu uchumi ambapo mahakama iliyotegemewa kutoa haki ilionekana imeingiliwa na rushwa. Tumefika hatua ambapo wananchi wanaamini kwamba haki sasa inaweza kuuzwa na kununuliwa na watu wenye fedha kama bidhaa yoyote.

299. Mwananchi mmoja aliyekutana na Tume alieleza wasiwasi wake kuhusu utendaji haki wa Mahakama Kuu baada ya majaji waliopo sasa kustaafu. Alisema ingawaje kuna rushwa katika Mahakama Kuu ni majaji wachache tu wanaohusika na wengi wao bado waadilifu ni waaminifu.

Hofu yake ilikuwa kuwa endapo majaji wa sasa wakistaafu na nafasi zao zikachukuliwa na majaji walioteuliwa kutokana na mahakimu wakazi waliopo basi rushwa itashamiri sana Mahakama Kuu. Hofu hii inatokana na tabia ya mahakimu hawa na utaratibu wa kuwateua majaji, kana kwamba ni kuwapandisha vyeo mahakimu wakazi bila hata kuwachuja, kujua tabia na uadilifu wao katika utoaji wa haki.

300. Malalamiko mengi dhidi ya mahakama hivi sasa yanalenga pia utoaji wa amri za “temporary injunctions” ambazo hutolewa na mahakama. Malalamiko hayo yako kwenye sura mbili. Moja ni kuhusu namna zinavyotolewa bila kuzingatia matakwa yote ya sheria. Pili, amri hizo zimekuwa zikipatikana haraka haraka wakati wadaiwa wengine hawapo na pasipo kuwapelekea wito wa kuitwa shaurini.

Wakati mwingine zimetolewa kama njia ya kumkomoa mtu. Baadhi ya taasisi zilizoathirika sana na “injunction” ni Benki ya Taifa ya Biashara. Benki inapotaka kuchukua mali za wateja waliokopa na kushindwa kulipa, wateja hawa hukimbilia mahakamani na kuomba “injunctions” ambazo hutolewa haraka bila wawakilishi wa benki kuwepo. Hivi sasa kuna “injunctions” 387 dhidi ya benki. Benki haiwezi kukusanya mikopo hiyo na wakati huo huo haiwezi kuuza dhamana zilizotolewa kwa ajili ya mikopo hiyo.

301. Sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji wa mashauri zinataka mahakama iwasomee wadaiwa hukumu iliyoandikwa na mahakama hiyo. Ni haki ya kila mdaiwa anayehusika na kesi kupewa hukumu hiyo iliyoandikwa ili aweze kuona kama kuna sababu na viini vya kutosha vya kukata rufaa kama atakavyoona inafaa.

Tume imebaini kwamba nakala za hukumu hazitolewi kwa wadaiwa katika mikoa mingi. Sababu zinazotolewa kwa kasoro hii ni upungufu wa karatasi; upungufu wa wapiga chapa na uhaba wa mashine za chapa. Hata hivyo kuna malalamiko kwamba nakala za hukumu ni mradi wa watumishi wa mahakama.

Baadhi ya mahakama hutumia njia hii ili makosa yao ya utendaji ya makusudi yasifahamike kwa mamlaka ya juu. Aidha ni kosa la nidhamu kama hakimu au jaji hataandika hukumu kwa wakati unaostahili. Kosa hili peke yake linaweza kumwondoa hakimu au jaji katika kazi yake kama ambavyo imekwishatokea siku za nyuma.

 

Je, unafahamu Jaji Warioba katika ripoti hii aliyoiandaa mwaka 1996 anazungumziaje kiwango cha rushwa ndani ya Idara ya Mahakama na mbinu zinazotumiwa na makarani kupokea rushwa? Usikose JAMHURI wiki ijayo. Mhariri.

By Jamhuri