Nidhamu mahakimu imeshuka

 

Mapendekezo

Tume inapendekeza kama ifuatavyo:-

 (i)Ajira ya makarani wa mahakama katika ngazi zote ifanywe baada ya tathmini ya tabia ya waombaji kufanywa na idara. Kila inapowezekana idara itumie vyombo vingine vya taifa kupata taarifa za waombaji wa kazi hiyo;

 (ii)Idara ibuni mpango wa kudumu wa elimu ya kujiendeleza kwa makarani wa mahakama kwa kanuni na taratibu mbalimbali zinazotumika mahakamani. Mpango huu uwe na utaratibu wa kupima viwango vya ujuzi. Makarani wasipande madaraja kabla hawajafaulu mitihani itakayokuwa inatungwa;

 (iii)Idara iwe na utaratibu wa kudumu wa kufahamu mienendo ya makarani wa mahakama na kuwachukulia hatua haraka makarani ambao wanajihusisha katika vitendo vya rushwa au ambao wanawasaidia wadaawa kuchelewesha haki kwa kuficha majalada;

(iv)Mamlaka ya mahakama iwachukulie hatua za nidhamu wasimamizi ambao kwa makusudi au uzembe wanashindwa kujaza taarifa za siri za makarani au kutoa taarifa ambazo si sahihi.

  

AJIRA NA MAMLAKA YA NIDHAMU YA MAHAKIMU

 321. Ajira ya mahakimu inafanywa kwa mujibu wa Ibara ya 112 ya Katiba. Madaraka hayo ni ya Tume ya Utumishi wa Mahakama (Judicial Service Commission). Sheria iliyotungwa mahususi kwa ajili ya ajira na nidhamu ya mahakimu ni Judicial Service Act, (Cap 508) ambayo inaunda Tume ya Utumishi wa Mahakama.

 Kueleza utaratibu wa nidhamu ya watumishi hao na kuunda mabaraza ya mahakama za wilaya na mikoa. Wajumbe wa Tume hiyo ni Jaji Mkuu ambaye ni Mwenyekiti, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji mmoja wa Mahakama Kuu, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu na wajumbe wawili ambao watateuliwa na Rais.

 322. Kwa upande mwingine, mahakimu wa mahakama za mwanzo wanaajiriwa na Tume Maalumu ya Utumishi wa Mahakama. Tume hii inaongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu. Utaratibu wa kuajiri unaanzia katika maombi ya kwenda kusoma masomo ya cheti cha sheria. Maombi hayo hupelekwa kwenye bodi za wilaya.

 Baada ya usaili majina ya wale wanaoteuliwa na bodi hutumwa kwa Msajili wa Mahakama ya Rufaa. Wote waliochaguliwa wanaitwa kwenye usaili wa Tume Maalumu. Wanaofaulu usaili huo hutakiwa kujiunga na masomo ya cheti cha sheria kwa muda wa mwaka mmoja. Wale wanaofaulu mtihani na kuonekana kuwa na tabia nzuri huteuliwa kuwa mahakimu.

 323. Ajira ya mahakimu wa wilaya inatokana na kupandishwa vyeo kwa mahakimu wa mahakama za mwanzo ambao wamefikia daraja la mwisho na kuonyesha umahiri katika utendaji wao wa kazi. Aidha idara imeanza kuwaajiri baadhi ya mahakimu wakazi, sifa ya kwanza ya kuajiriwa ni kuwa na shahada ya sheria na wahusika wawe wamepitia mafunzo ya uanasheria (internship) katika Idara ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

 Utaratibu huu wa mafunzo ulikuwa wa mwaka mmoja. Hivi sasa yanachukua miezi sita tu. Shabaha ya mafunzo haya ni kuwawezesha wahitimu kupata elimu ya sheria kwa vitendo na kujifunza mambo ambayo hayafundishwi katika nadharia, kama vile elimu ya maadili; kutunza vitabu vya fedha, mawasiliano na wateja n.k.  Katika nchi nyingine za Madola, mafunzo haya hufanyika rasmi katika chuo baada ya kuhitimu. Haya ni mafunzo muhimu kwa taaluma ya uanasheria kwa sababu mhitimu hawezi kuajiriwa kufanya kazi ya sheria kitaalamu kama hajahitimu chuo cha mafunzo haya.

324. Kwa upande wa mafunzo ya mahakimu wa mahakama za mwanzo na wilaya, elimu ya maadili haikuwekwa kwenye mitaala ya stashahada. Hivyo mahakimu hao wameachwa wajifunze wenyewe maadili hayo au wawaige mahakimu wakazi na majaji. Kwa bahati mbaya mahakimu wakazi na majaji  nao hawana wanapoiga.

Baadhi ya vitendo vinavyofanywa na mahakimu vinaonyesha upungufu wa maadili ya taaluma ya sheria. Aidha, kada ya mahakimu wakazi ambayo nayo inalalamikiwa kwa vitendo vya rushwa ndiyo kisima wanachotoka majaji kwa utaratibu wa sasa wa kuwateua majaji kama “promotion”.

 325. Sheria ya Tume ya Utumishi wa Mahakama inatamka bayana kwamba hakimu hawezi kuondolewa au kufukuzwa kwenye kazi ya uhakimu hadi utaratibu ulioainishwa katika sheria umezingatiwa.

Mashtaka au tuhuma zinazomkabili hakimu ni sharti apewe nafasi ya kuzijibu tuhuma hizo na pili uchunguzi (inquiry) wa tuhuma hizo uwe umefanywa. Malalamiko dhidi ya mahakimu yanaweza kuwasilishwa kwa viongozi wasimamizi wa idara au kwenye bodi za mahakama.

Walalamikaji wanaweza kufanya hivyo wao wenyewe, lakini uzoefu umeonyesha kwamba malalamiko hayo yanapitia kwa viongozi wa Serikali, kama vile DC au RC, mawaziri, wabunge n.k. Hii inatokana na Tume na bodi kutofahamika kwa wananchi. Wananchi wengi wenye malalamiko wamekuwa wakilalamika bila kujua waende wapi.

Matokeo ya wananchi kutojua chombo kinachohusika, kumewafanya mahakimu wasiostahili kufanya kazi ya uhakimu na ambao wangechukuliwa hatua kama malalamiko dhidi yao yangefikishwa kwenye bodi hizo, kuendelea kueneza kansa ya rushwa katika Idara ya Mahakama.

 326. Muundo wa bodi hizi unamjumuisha Mkuu wa Mkoa kama Mwenyekiti wa Bodi ya Mkoa na Hakimu Mkazi Mfawidhi. Kuna wajumbe wengine wawili. Kwa upande wa wilaya, Mwenyekiti wa Bodi ni DC na Katibu wake ni Ofisa Tawala wa Wilaya. Bodi ina wajumbe wengine wawili wanaoteuliwa kutokana na ofisi zao.

 327. Sheria inatamka waziwazi kwamba bodi za wilaya na mikoa zitawatangazia wananchi katika mikoa yao kuhusu nafasi za mahakimu wa mwanzo. Matangazo hayo ni nadra kutolewa katika mikoa hapa nchini. Vile vile bodi zinapaswa kujitangaza ili kuwajulisha watu ambao wana malalamiko dhidi ya mahakimu. Hili pia halifanyiki.

 Nguvu ya mabaraza ya wilaya imepungua sana kutokana na ujuzi mdogo wa sheria wa makatibu wa bodi hizi. Makatibu hawa wanalazimika kuomba ushauri wa mahakimu ambao ndio wanaolalamikiwa badala ya makatibu kuwa ndio wachambuzi wa mwisho wa maswala yanayopelekwa kwenye bodi hizo. Aidha, utaratibu huu unaweza kutumiwa na mahakimu ambao ni makatibu wa bodi za mikoa au wilaya kuwapendelea mahakimu wenzao.

 328. Bodi hizi zinaporidhika kwamba kuna sababu za kumsimamisha hakimu anayetuhumiwa, zitamjulisha Jaji Mkuu ili amsimamishe hakimu huyo. Jaji Mkuu naye akiridhika atachukua hatua hizo wakati wa kusubiri uchunguzi kufanyika na baada ya Waziri wa Sheria kutoa kibali.

 Utaratibu huu ni mrefu sana na ikiwa mamlaka zinazohusika zitachelewa kuchukua hatua ama kwa uzembe au kwa mawasiliano mabovu, unachelewesha kutatua matatizo kwa haraka na kuendelea kuwavunja wananchi moyo. Hali hii imechangia kufanya wananchi wapoteze imani na uongozi wa mahakama.

329. Ili kukabiliana na matatizo yaliyoainishwa hapa juu, Tume inapendekeza kama ifuatavyo:-

(i)Mamlaka inayohusika (Tume ya Utumishi wa Mahakama) iweke utaratibu wa kuchambua na kuchuja watu wanaoomba kazi ya uhakimu katika ngazi zote kwa kushirikiana na vyombo vingine vya taifa badala ya kutegemea usaili na vyeti vya waombaji tu;

 (ii)Tume ya Utumishi wa Mahakama ifanye uchambuzi yakinifu ili kuhakiki madaraja ya mahakimu wote. Wale watakaogundulika kuwa wamecheleweshwa kupandishwa vyeo na wanastahili, wapandishwe. Mahakimu wasiostahili kuwa kwenye madaraja ya juu na ambao tabia na mienendo yao ni ya shaka shaka waachishwe kazi;

(iii) Mamlaka ya mahakama ielekeze vyuo vinavyotoa stashahada kwa mahakimu wa Mahakama za Mwanzo na Wilaya kuweka elimu ya maadili ya taaluma ya wanasheria katika mitaala ya vyuo hivyo;

 (iv)Serikali ianzishe chuo rasmi cha mafunzo ya wanasheria (Law School) wanaomaliza shahada ya sheria (LL.B)

 (v)Jaji Mkuu asikae kwenye Tume ya Utumishi wa Mahakama wakati tume inaposikiliza shauri la nidhamu kwa mahakimu.

 (vi)Bodi za mahakama za wilaya ziundwe upya. RC na DC wabaki kuwa wenyeviti wa bodi hizo mkoani na wilayani. Makatibu wa bodi wawe ni mawakili wa Serikali watakaopelekwa mikoani na wilayani. Wajumbe wa bodi hizo wawe ni watu huru, lakini Idara ya Mahakama iwakilishwe na Hakimu Mkazi (Mkoa) na Hakimu wa Wilaya. Muundo ulivyo sasa unawahusisha wanasiasa na vyama vya siasa. Jambo hili liangaliwe upya ili kuondoa uwakilishi wa vyama vya siasa.

(vii)Taarifa ya shughuli za Tume ya Kuajiri ya Mahakama zikiwemo bodi za mahakama za wilaya na mikoa ziwasilishwe kwenye Bunge na Waziri wa Sheria ili Bunge lipate nafasi ya kujua kinachoendelea kwenye shughuli za tume na bodi.

  

AJIRA NA MAMLAKA YA NIDHAMU YA MAJAJI

330. Mamlaka inayoteua majaji ni Rais baada ya kushauriana na Tume ya Kuajiri ya Mahakama Kuu. Sifa za mtu anayeteuliwa kuwa jaji ni sifa maalumu zilizotajwa katika sheria ya mawakili ambazo ni lazima mtu awe nazo ili aweze kuandikishwa kuwa wakili. Sifa maalum ni:-

 (a)Awe ni mtu mwenye shahada ya sheria inayotambulika na Baraza la Elimu ya Sheria (Council of Legal Education). Wajumbe wa baraza hili ni Jaji Mkuu; Mwanasheria Mkuu; Dean wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; Mawakili wawili waliochaguliwa na Chama cha Mawakili (Tanganyika Law Society) au;

 (b)Awe anafanya kazi zinazohusiana na taaluma ya sheria (Legal practitioner) na ana sifa za kuwakilisha kesi katika nchi yoyote ya Madola au nchi yoyote ambayo imetajwa na Waziri wa Sheria; au.

 (c ) Awe amesajiliwa kama wakili (solicitor) katika mahakama za Uiingereza (England, Ireland au Scotland); au.

 (d)Awe ameliridhisha Baraza kwamba amepitia mafunzo ya sheria kwa vitendo (internship) kwa muda usiopungua miezi sita au amekuwa katika utumishi serikalini kwa kazi ya sheria kwa muda usiopungua miezi sita; na kuridhisha kwamba anazijua sheria, kanuni na taratibu za kuendesha mashauri Tanzania Bara.

 331. Mtu anayetarajiwa kuteuliwa kuwa jaji ni lazima awe na sifa hizi kwa muda usiopungua miaka mitano. Hata hivyo, Rais baada ya kushauriana na Tume ya Kuajiri ya Mahakama anaweza kutengua sharti la muda na kumteau mtu ambaye hajafikisha miaka mitano endapo mtu huyo ana uwezo; ujuzi; na kwa kila hali anafaa kukabidhiwa madaraka ya Jaji wa Mahakama Kuu na kuna sababu za kumfanya mtu huyo astahili kukabidhiwa madaraka hayo.

 332. Sifa maalumu zinawahusu pia watu wanaoteuliwa kuwa Kaimu Jaji. Kaimu Jaji huteuliwa kama nafasi ya ujaji ipo wazi au kama kuna ongezeko kubwa la kesi ambazo zinahitaji ateuliwe Kaimu Jaji. Kazi hii ya ukaimu inaweza kuwa ni kwa kipindi kitakachokuwa kimetajwa katika hati ya uteuzi; kazi alizoteuliwa kufanya kumalizika; au hadi hapo uteuzi utakapofutwa na Rais.

 333.  Katiba inatamka bayana kuhusu utaratibu wa kumwondoa Jaji katika kazi hiyo. Rais hawezi kumwondoa Jaji katika kazi hiyo isipokuwa kwa  kufuata utaratibu ulioainishwa katika Katiba. Hata hivyo mambo yafuatayo yatamwondoa Jaji katika kazi hiyo:-

(a)Kama Jaji atafika umri wa miaka sitini au kama atastaafu kwa hiari atakapofikia umri wa miaka hamsini na tano; na Rais akakubali.

 (b)Kama Tume iliyoteuliwa na Rais kuchunguza tabia ya Jaji kushindwa kutekeleza kazi yake kwa sababu ya maradhi au tabia mbaya inayoathiri maadili ya kazi ya Jaji au Sheria ya Maadilli ya Viongozi wa Umma. Tume hii itakuwa na wajumbe ambao ni majaji wa Mahakama Kuu au Mahakama ya Rufani katika nchi yoyote ya Jumuiya ya Madola. Wakati umefika wa kuangalia upya utaratibu huu na kuufanya uwe wa ndani ili hatua za haraka ziwe zinachukuliwa kama kuna tuhuma kuhusu Jaji.

 334. Tume inapendekeza kama ifuatavyo:-

 (i)Muda wa miaka mitano ambao umewekwa kwenye Katiba kama muda wa chini wa kuwa na sifa maalumu ni mfupi mno; muda huo uongezwe kuwa miaka kumi na mitano ili ulingane na uzito wa kazi  ya ujaji;

 (ii)Utaratibu wa kuteua majaji ufanywe kwa makini na usifanywe kama ni kuwapandisha ngazi mahakimu wakuu, kada ambayo imekubuhu kwa kansa ya rushwa.

 (iii)Watu watakaoteuliwa wawe ni watu ambao michango yao katika taaluma ya sheria inajulikana na msimamo wao katika masuala maalumu ya jamii unajulikana.

(iv)Majaji wapewe pensheni ya kutosha ili wasishawishike kufanya biashara au kazi ya uwakili baada ya kustaafu; au

 (v)Majaji wapewe pensheni ya kuanzia maisha baada ya kustaafu (Golden handshake);

(vi)Mishahara na marupurupu ya majaji bado ni ya chini. Mishahara hiyo iongezwe ili kukidhi mahitaji ya majaji na kulingana na umuhimu wa kazi hizo;

 (vii)Utaratibu wa kuwateua majaji wanaokaimu kazi ya ujaji utumike mara kwa mara ili kusaidia kuondoa mlundikano wa kesi katika Mahakama Kuu; Kaimu Jaji anapoteuliwa asifanye kazi katika kituo chake cha kazi isipokuwa kama Kaimu Jaji huyo alikuwa ni hakimu sehemu hiyo;

 (viii)Utaratibu wa kumwondoa Jaji katika kazi yake ubadilishwe ili kusiwe na ulazima wa kuwatumia majaji kutoka katika himaya nyingine kuchunguza tuhuma za Jaji. Utaratibu huo uwe ni wa ndani ya nchi.

(x)Umri wa kustaafu majaji uongezwe kufikia miaka sabini na miaka sitini na tano kwa kustaafu kwa hiari. Majaji wanaostaafu watumike kama washauri katika mambo ya kuboresha utoaji wa haki kwa njia ya usuluhishi (ADA) au mahakamani;

(xi)Majaji wapewe nafasi ya kuhudhuria mafunzo mafupi au mikutano ndani na nje ya nchi ili kupanua upeo wao katika mambo mengi ya jamii na kujifunza mambo mapya. Aidha, baada ya majaji kuteuliwa wapewe mafunzo maalumu kabla hawajaanza kazi hiyo;

  

AJIRA YA MAJAJI WA MAHAKAMA YA RUFANI

 335. Majaji wa Mahakama ya Rufani wanateuliwa na Rais baada ya kushauriana na Jaji Mkuu. Sifa za mtu kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani ni zile zile sifa maalumu ambazo zinatumika kuwapata majaji wa Mahakama Kuu.

336. Mahakama ya Rufani inatumika jengo lilelile linalotumiwa na Mahakama Kuu. Upo msongamano mkubwa katika jengo hili jambo ambalo linaathiri kazi na heshima ya mahakama hii.

 Pia kufanyia kazi kwenye jengo moja kumefanya Mahakama ya Rufaa na Mahakama Kuu zionekane kama ni kitu kimoja. Aidha kuwepo kwa mahakama hizo katika jengo moja kumemeza mipaka ya madaraka ya Jaji Kiongozi kuhusiana na uendeshaji wa Mahakama Kuu na hivyo kuifanya isiweze kusimamia udhibiti wa mahakimu kama ipasavyo.

  

Mapendekezo

337. Tume inapendekeza kwamba:-

(i)Sifa maalumu kwa majaji wa Mahakama ya Rufani zitofautishhwe na sifa maalum za mawakili. Kipindi cha miaka mitano kinachotamkwa ni kifupi mno kwa mtu yeyote kuonyesha umahiri wake wa taaluma ya sheria hadi kuchaguliwa kuwa Jaji wa Rufaa. Kipindi hiki kiongezwe hadi kufikia miaka ishirini au zaidi;

 (ii)Kwa kuwa Mahakama ya Rufani ndiyo chombo cha mwisho katika kutafsiri sheria na kuamua juu ya masuala mazito ya sheria, majaji wa rufani wawe ni watu ambao wametoa michango mikubwa  katika taaluma ya sheria kama walimu, majaji n.k na msimamo wao katika masuala ya jamii ujulikane kuliko ilivyo sasa ambapo si rahisi wafuatiliaji wa mambo ya sheria kujua msimamo wa majaji katika masuala hayo – kwa mfano; mazingira; haki na wajibu wa raia; n.k.

 (iii)Idadi ya majaji iongezwe.

 

UTENDAJI WA KAZI WA MAHAKIMU NA MAJAJI

338. Mahakimu na Majaji wana wajibu mkubwa wa kuamua mashauri yanayopelekwa mbele yao. Katika kufanya kazi hiyo huweza kutafsiri sheria zilizotungwa na Bunge. Shughuli zote hizi zinahitaji waongozwe na sheria na haki. Kama Mahakaimu na Majaji watapotoka, au watavuruga utendaji haki siyo tu watalaumiwa bali watateremsha hadhi ya Mahakama.

 Kama malalamiko hayatashughulikiwa haraka ipasavyo lawama zitaelekezwa kwenye dola. Kwa upande mwingine, kama Mahakama zitatoa tafsiri inayohujuma matarajio ya jamii, basi utulivu na amani utakuwa mashakaani, dhuluma itashamiri na rushwa itaendelea kuwa kero ya jamii. Hali niyo inayojitokeza hivi sasa.

 339. Tume imebaini kuna upungufu mkubwa wa usimamizi baina ya Mahakama Kuu kwa Mahakama za Hakimu Mkazi. Udhibiti wa Mahakimu ni duni sana. Upungufu huu umechangia, kwa kiasi kikubwa, ongezekeo la vitendo vya rushwa katika Mahakama hizi.

 Upungufu huu uko katika sura mbili. Kwanza mamlaka ya usimamizi ya Majaji wa Mahakama Kuu juu ya mienendo ya mashauri katika Mahakama za chini yamekuwa hayatumiwi kikamilifu. Vinginevyo Majaji wangebaini mapema dosari ya kupokea chochote na kurekebisha dosari hizo.

 Sura ya pili inahusu uwezo wa kuweza kuwachukulia hatua za kinidhamu. Anaweza kumsimamisha wakili wa kujitegemea hana uwezo wa kumdhibiti hakimu anayeonekena dhahiri anaenda kinyume cha miiko ya kazi. Aidha Tume imepata ushahidi unaoonyesha jinsi hakimu anavyoweza kupuuza maagizo ya Jaji Mfawidhi.

 Mfano huo umeambatanishwa kama kielelezo “A”, “B”, “C” na “D”, Hali hii imesababishwa na mfumo wa nidhamu wa Idara nzima ya Mahakama kuwa chini ya Jaji Mkuu. Utiifu wa Mahakimu unaoegemea zaidi kwa Jaji Mkuu kuliko Majaji Wafawidhi walio karibu nao umetawala na kuharibu uwajibikaji wa Mahakama kwa majaji wa Kanda.

 340. Upungufu mwingine uliobainika na unaothiri utendaji kazi wa idara ni ukosefu wa nyenzo pamoja na ufinyu wa bajeti. Upungufu huu umeathiri kwa kiwango kikubwa safari za ukaguzi ambazo ndizo zingeimarisha usimamizi na udhibiti katika Idara ya Mahakama.

Ili utendaji wa Mahakimu na Majaji uwezo kuwa thabiti wanahitaji kupewa nyenzo za kazi. Juzuu za sheria ndiyo nyenzo ya kwanza. [Mahakama] hazina Juzuu za sheria. Kasoro hii hufanya utendaji wao uwe wa kubabaisha tu. Aidha, ripoti za kesi mbali mbali zilizoamuliwa huko vyuma (Law reports) hazitolewi na kusambazwa mikoani. Vitabu hivi vina umuhimu mkubwa katika kuwaongoza Mahakimu na Majaji katika kesi zilizokwisha amuliwa siku za nyuma na kusaidia kutoa maamuzi yanayoshabihiana.

341. Mahakama zinazohusika na ukaguzi wa mahakama za chini zinahitaji vyombo vya usafiri ili kufanya kazi hiyo. Katika maeneo mengi ambayo Tume iliyatembelea ukaguzi huo haufanyiki. Matokeo ya upungufu huu ni kwamba mahakimu wamejisahau na wanapokosea wanakosa ushauri au kusahihishwa makosa yao.

342. Baadhi ya majaji na mahakimu wana tabia ya kusikiliza kesi za madai kwenye ofisi zao badala ya kutumia kumbi za mahakama zilizotengwa kwa ajili hiyo. Tabia hii ina athari nyingi. Kwanza ofisi za majaji haziwezi kuchukua watu wengi wanaotaka kusikiliza mashauri au mawakilli wanaotaka kujifunza namna mawakili waandamizi wanavyoendesha na kusimamia kesi zao ili kuongeza ustadi wao wenyewe.

Wadaawa wengi wanashindwa kuhudhuria kesi zao na makarani wa mahakama wanautumia mwanya huu kupokea rushwa kutoka kwa wadaawa wanaotaka kesi zao kusikilizwa mapema. Kama shauri limekuwa katika Mahakama ya wazi, Jaji angetangaza mashauri hayo yatasikilizwa lini na wadaawa wangeomba tarehe za karibu.

Aidha, utaratibu huu unajenga tabia ya wadaawa kuingia kwenye ofisi za majaji bila kufuata utaratibu unaohitaji mtu kuandamana na karani anapotaka kumwona jaji. Hitilafu hii inajenga hisia kwamba baadhi ya majaji wanapokea rushwa ili watoe hukumu zinazowapendelea wadaawa wengine na kupotosha haki.

343. Utaratibu wa  kusikiliza kesi unaruhusu Jaji kuwa na karani. Hivi sasa imekuwa ni desturi kila Jaji kuwa na karani yule yule kwa muda mrefu. Baadhi ya makarani hao wanatumia nafasi hizo kujipatia fedha kutoka kwa wenye mashauri mahakamani kwa visingizio mbalimbali. Wengine hudanganya wadaawa kuhusu uwezo wao wa kupanga kesi isikilizwe mapema au kumfanya Jaji aandike hukumu “nzuri” au hata kupoteza majalada na vielelezo. Malalamiko haya si ya kupuuza.

 

Je, unafahamu Jaji Warioba katika ripoti hii aliyoiandaa mwaka 1996 anashauri ni hatua zipi zichukuliwe kudhibiti makarani na Mahakimu wasio na nidhamu? Usikose JAMHURI wiki ijayo. Mhariri.

2348 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!