Majaji, mahakimu ni shida

url-1V:  WAJIBU WA UMMA NA VYOMBO VYA HABARI

1. Umma wa Tanzania umekuwa unakerwa sana na kuenea kwa rushwa nchini, hasa ile inayodaiwa na watumishi wa umma katika ngazi za chini kutokana na hali ngumu ya maisha. Rushwa ya aina hii imeufikisha umma pahala pagumu kiasi kwamba umeshawishika kukata tamaa ya kupata haki yoyote ile bila ya kutoa rushwa.

Kwa mfano wazazi huko vijijini wamekwishajenga imani kwamba hawawezi kufanikiwa kuwaandikisha watoto wao shuleni bila ya kuwa na fedha mfukoni, hawawezi kupata haki katika vyombo vya dola na mahakama bila ya kuwa na fedha za kuhonga n.k.

Umma umefikia uamuzi huu potofu kutokana na mambo mawili muhimu. Jambo la kwanza ni kwamba wananchi wengi hasa wa vijijini bado hawajafahamu haki zao kikatiba. Rushwa inahusu watoaji (wananchi wanaohitaji huduma), na wapokeaji (watu wenye dhamana katika Serikali na mashirikaya umma).

Kama wananchi kwa ujumla wataelewa vizuri haki zao na hivyo kukataa kuzinunua kwa kutoa rushwa ni dhahiri kwamba itatoweka yenyewe. Wananchi wanatakiwa kuelimishwa kuhusu haki zao ili waweze kuzidai pale ambapo wataona kuwa wanadhulumiwa au kucheleweshwa.

Hapa ndipo umuhimu wa vyombo vya habari unachukua nafasi na wajibu wa kipekee kwa umma. Vyombo hivi vina uwezo wa kuwaelimisha wananchi kuhusu haki zao katika jamii. Aidha, kwa kuwa vinaelewa vizuri maadili ya taifa na vina utaalamu wa kufanya uchunguzi, vitaweza kusaidia kuwafichua wale wote wanaokiuka maadili kwa kudai na kupokea rushwa. Taarifa zao zikiwa za kweli itakuwa rahisi kwa uongozi wa taifa kumuwajibisha kiongozi atakayehusika.

2. Jambo la pili ambalo ni baya zaidi, ni kwamba hata kama umma utapata mwamko kuhusu haki zao na hivyo kukataa kuzinunua na badala yake kuwafichua wale wote wanaoomba rushwa, umeelekea kukata tamaa baada ya kuona kwamba uongozi ambao ulikuwa unaamini kwamba ungelikuwa kimbilio lao umetumbukia katika baa la rushwa.

Umma wa Tanzania unashindwa kuwafichua wale wote wenye kudai na kupokea rushwa kutokana na ukosefu wa uongozi safi na wenye kuwajibika ndani ya vyombo vya dola kama polisi, mahakama, Taasisi ya Kuzuia Rushwa na Usalama wa Taifa.

Kwa hiyo kazi kubwa iliyoko mbele yetu ni kusafisha safu ya uongozi uliopo katika Serikali yenyewe, mashirika ya umma pamoja na vyama vya siasa. Baada ya hapo itabidi kuchukua hatua za kujenga uongozi wenye nia ya dhati ya kupambana na adui rushwa katika ngazi zote kwa kuwachukulia hatua wale wote watakaofichuliwa. Kwa kufanya hivyo tutakuwa tumerudisha imani ya wananchi kwa vyombo vya dola na hivyo kuchochea kasi ya kufuta rushwa nchini.

 

VI: WAJIBU WA UONGOZI WA JUU

3. Tumekwisha kuonyesha umuhimu wa kusafisha safu za juu za uongozi. Ili kazi hii ya kupiga vita rushwa iendelee kwa kasi, Rais hana budi kuonyesha njia.

4. Watanzania ni waelewa sana na wamechoshwa na ubadhirifu wa wale wanaowaongoza. Wanangojea kuona hatua madhubuti ili wamsaidie Rais na Serikali yake kuondokana na rushwa. 

5. Tume inapendekeza kwamba pamoja na umuhimu wa kusafisha ngazi za juu za uongozi, Rais awaagize viongozi wapya wanaoteuliwa kuongoza vyombo vya dola kusafisha safu za wasaidizi wao. Atakayeshindwa kufanya hivyo na kashfa zikajitokeza mahali pake pa kazi, awajibike bila msamaha na asihamishiwe sehemu nyingine. Pia vyombo hivyo, hususan Jeshi la Polisi, Idara ya Usalama wa Taifa na Taasisi ya Kuzuia Rushwa vijenge mshikamano katika kupambana na rushwa.

 

SHERIA YA MAADILI YA VIONGOZI YA 1995

6. Ibara ya 132(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaunda Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma. Ibara hii pia inaipa sekretarieti hiyo uwezo wa kupeleleza mienendo na tabia za viongozi wa umma kwa madhumuni ya kuona kama inazingatia na  masharti ya uongozi yaliyowekwa na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya 1995, Sheria Na. 13 ya 1995.

 

VIONGOZI WA UMMA

7. Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma imeorodhesha viongozi wanaohusika na masharti ya sheria katika kifungu cha 4 cha sheria hiyo na imewagawa katika makundi sita kama ifuatavyo:

 

(a) Wanasiasa.

(b) Watendaji wakuu wa wizara na idara za Serikali na wa Serikali za Mitaa.

(c) Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.

(d) Watendaji wakuu wa mashirika ya umma.

(e) Majaji na mahakimu.

(f) Wajumbe wa kudumu wa tume mbalimbali.

 

Viongozi wa umma wanatofautiana kuhusu:

(a)  Aina ya majukumu au wajibu walionao.

(b) Masharti ya kazi.

(c)  Mamlaka na taratibu za kuwapa nyadhifa na kuwaondoa madarakani.

28. Viongozi wa kisiasa wamegawanyika katika makundi mawili. Wale wa kuteuliwa na Rais na wale wanaochaguliwa kwa uchaguzi na kuondoka madarakani pindi kipindi chao kinapomalizika. Hawa hawana masharti au mamlaka yanayosimamia mienendo yao. Wale wa kuteuliwa wanaweza kuondolewa madarakani wakati wowote. Aidha, viongozi wa kisiasa hawana mamlaka au taratibu nyingine zinazosimamia mwenendo wao na nidhamu kazini isipokuwa masharti ya uteuzi na maelekezo ya Rais.

29. Watendaji wakuu wa wizara au idara za Serikali ni watumishi wa Serikali wanaoteuliwa na Rais. Hawa hutawaliwa na kanuni za kudumu za Serikali (Standing Orders) pamoja na sheria ya utumishi serikalini. Sheria na kanuni hizo ndizo zinazoweka masharti ya uteuzi, mwenendo na nidhamu ya watumishi hao.

30. Viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama huteuliwa na Rais na kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria na kanuni zinazoongoza shughuli za vyombo hivyo. Jeshi la Ulinzi linatawaliwa na sheria ya Jeshi la Wananchi ya 1966 (Na.32/66).

Sheria hiyo inaweka masharti ya nidhamu ya askari, maofisini na utekelezaji wake. Askari na maofisa wote wa Jeshi la Ulinzi wanapaswa kuheshimu sheria hiyo, vile vile wakuu wa Jeshi la Polisi na Jeshi la Magereza husimamiwa na sheria zinazotawala vyombo vyao. Sheria hizi zimeweka kanuni zinazotawala mienendo na taratibu za viongozi na maofisa wa vyombo hivyo.

31. Viongozi wa mashirika ya umma huteuliwa na Rais. Watendaji wakuu wengine huteuliwa na bodi. Watendaji hao hufanya kazi chini ya usimamizi wa bodi za mashirika yao. Bodi hizo zinayo mamlaka ya kusimamia masuala ya utendaji kazi na nidhamu. Aidha, bodi za mashirika zina uwezo wa kudhibiti ukiukaji wa masharti na miiko ya kazi na kuwaondoa au kupendekeza kuwaondoa katika madaraka yao watendaji hao wanaokiuka masharti na maadili ya kazi.

32. Majaji huteuliwa na Rais kuzingatia masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Majaji na mahakimu hutawaliwa na Sheria ya Utumishi wa Mahakama. Majaji hawawezi kuondolewa kazini isipokuwa kwa mapendekezo ya Tume ya Uchunguzi iliyoteuliwa na kufanya uchaguzi kwa mujibu wa Ibara ya 110 ya Katiba. Aidha, majaji na mahakimu wamejiwekea wenyewe kanuni za maadili ya maofisa wa mahakama ya 1984.

33. Wajumbe wa tume mbalimbali huteuliwa na Rais na kutenda kazi zao kwa mujibu wa masharti ya uteuzi na sheria zinazoainisha tume hizo au kuweka majukumu yake.

34. Kutokana na mchanganuo wa aina ya viongozi uliofanywa hapa juu kwa kuzingatia aina ya kazi na wajibu, masharti na taratibu za utekelezaji wa kazi zao, watu waliotajwa na sheria kuwa ni “viongozi wa umma” wanatofautiana kwa kila hali isipokuwa tu kwamba kazi wanazozifanya ni za umma (public duties).

35. Tume imetambua umuhimu wa kuwepo maadili kutawala mienendo, tabia na utendaji kazi wa watumishi wa umma. Tume imetambua umuhimu wa kuwepo maadili kutawala mienendo, tabia na utendaji kazi wa watumishi wa umma.

Aidha, Tume inatambua kuwa maadili ni kanuni muhimu zilizowekwa au kukubaliwa na kikundi cha watu, ambazo zinaainisha mambo yanayokubalika au yasiyokubalika katika kikundi hicho au katika mahusiano au shughuli miongoni mwa wanachama au wahusika wa kikundi hicho.

Kanuni hizo huwa ndicho kioo cha watu walio nje ya kikundi cha kukitazama au kukipima kikundi kinachohusika na maadili hayo.

36. Watumishi katika utumishi wa serikali, viongozi wa majeshi ya ulinzi, majaji na mahakimu na watendaji wakuu wa mashirika ya umma wanatawaliwa na kanuni ambazo zipo kudhibiti mienendo, tabia na utendaji wao wa kazi.

Sheria ya maadili inawagusa pia viongozi wote ambao ajira yao inatawaliwa na sheria hizo. Tume inaliona jambo hili la viongozi kutawaliwa na sheria mbili zenye utaratibu tofauti kama linaweza kuleta utata katika utekelezaji na kutosimamia vizuri madhumuni ya sheria ya maadili au hizo sheria na kanuni nyingine.

Tume inapendekeza kwamba viongozi wa umma ambao ajira na mienendo yao inatawaliwa na sheria tofauti na sheria ya maadili, waondolewe kwenye orodha iliyotajwa kwenye sheria ya maadili na waendelee kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria na taratibu zinazotawala ajira yao.

37. Kama viongozi wa umma ambao ajira zao zinatawaliwa na sheria nyingine wataondolewa kwenye sheria ya maadili, viongozi wa umma watakaobaki ni viongozi wa kisiasa. Tume inaridhika kwamba utaratibu huu utarahisisha utekelezaji wa sheria ya maadili kwa viongozi hao.

Tume imebaini kwamba sheria na kanuni zinazotawala ajira za viongozi wa umma wasio wanasiasa, zinatakiwa kufanyiwa marekebisho ili misingi iliyomo kwenye sheria ya maadili iwekwe kwenye sheria na kanuni zinazotawala ajira na nidhamu ya viongozi hao.

38. Orodha ya viongozi wa umma watakaoainishwa kwenye sheria ya maadili iwajumuishe wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Spika wa baraza hilo ambao hawamo kwenye orodha hiyo.

 

AINA YA MAADILI

39. Kifungu cha 4 cha Sheria kinafafanua neno “Code” kuwa ni kanuni za maadili ya viongozi wa umma yaliyowekwa na au kwa mujibu wa Sheria ya Maadili. Kwa mantiki hiyo kuna maadili ya aina mbili; kwanza ni maadili yaliyowekwa na sheria yenyewe na pili ni maadili yatakayowekwa baadaye kwa mujibu wa sheria hiyo.

Kwa kuwa maadili ni lazima yazingatiwe na wanaohusika na adhabu itolewe kwa ukiukwaji wake, sharti maadili hayo yawe dhahiri na bayana ili wahusika wayafahamu.

40. Ibara ya 132(4) inalipa Bunge mamlaka ya kutunga sheria itakayoainisha misingi ya maadili ya viongozi wa umma itakayozingatiwa na watu wote wanaoshika nafasi za madaraka zitakazotajwa na Bunge. Misingi ya maadili imefafanuliwa katika Ibara ndogo ya (5).

Vile vile Katiba imelipa Bunge mamlaka ya kutunga sheria kuweka masharti ya watu kufukuzwa au kuondolewa kazini kwa makosa ya kuvunja maadili ya viongozi. Sheria iliyotungwa na Bunge kwa ajili hii ni Sheria ya Maadili tunayoifafanua.

Sheria hii inampa Rais, katika sehemu ya pili, mamlaka ya kuweka maadili kwa shabaha ya kujenga imani ya wananchi kwa uadilifu wa viongozi wao. Tume imeyatafakari mamlaka aliyopewa Rais na inaona kwamba  haikuwa, lazima kwa Rais kupewa mamlaka hayo.

Mamlaka hayo ni ya Bunge kama yalivyoelezwa kwenye Katiba. Rais atabaki na mamlaka ya kuhakikisha kwamba Serikali inaongozwa na viongozi wa umma anaowateua yeye na wale ambao ajira yao kwenye utumishi wa Serikali wanakuwa na maadili. Maadili hayo si lazima yatungiwe sheria tofauti na zile zinazotawala ajira hizo.

41. Pamoja na maoni yaliyo hapo juu, sheria kama ilivyotungwa ina kasoro na upungufu unaoifanya isikidhi madhumuni ya kuitunga. Kasoro na upungufu huo ni kama ifuatavyo:

(a) Kifungu cha 5 cha sheria kinampa Rais wajibu wa “to work towards the evolution of ethical standards designed to provide a basis for enhancing public confidence in the integrity of public leaders and in the decision-making process in the government.” Aidha, kifungu hiki kinaorodhesha mambo manne yatakayomuongoza Rais katika kuweka kuweka kanuni za maadili ambayo ni:

(i) Mgongano kati ya masilahi ya umma na ya binafsi katika utekelezaji wa shughuli za kiongozi wa umma;

(ii) Kuvutia na kutoa nafasi kwa watu wote wenye uwezo toka nyanja zote kukubali nafasi za utumishi wa umma;

(iii) Kuweka kanuni za kusimamia mgongano wa masilahi ya umma na ya binafsi, hata baada ya kiongozi wa umma kutoka madarakani;

(iv) Kupunguza fursa za kutokea mgongano wa masilahi ya binafsi na ya umma na kutatua migongano hiyo kwa njia ambayo itazingatia zaidi kuhifadhi masilahi ya umma.

 (b) Kifungu cha 6 kinaorodhesha misingi itakayotumika kama vigezo vya utungaji wa kanuni za maadili ya viongozi yatakayowekwa. Kifungu cha 7 kinampa Rais madaraka ya kuweka kanuni za maadili.

Tume inaona kwamba vifungu vya 5, 6 na 7 vya Sheria ya Maadili havieleweki na havina ufasaha unaotakiwa katika sheria. Kifungu cha 5 kinampa Rais jukumu la “to work towards the evolution of ethical standards.”

Sheria haitamki namna Rais atakavyotekeleza hilo na hali hii inasababisha uwepo ugumu wa kupima kama jukumu hilo limetekelezwa au Rais analitekeleza kwa ufanisi na kiwango gani.

Aidha, kipengele cha (2) cha kifungu cha 5 cha sheria kinamtaka Rais aongozwe na “the need to evolve, and foster, sound rules and ethical standards in the public service” wakati anapoyatekeleza majukumu manne yaliyoorodheshwa katika kifungu kidogo hiki.

Kwanza haieleweki kuna tofauti gani au inakusudiwa nini wakati kifungu kidogo (1) cha kifungu cha 5 kinamtaka Rais “to work towards the evolution of ethical standards” na kifungu kidogo cha (2) kinamtaka Rais aongozwe na “the need to evolve and to foster sound rules and ethical standards.”

Pili haieleweki kama mambo yaliyoorodheshwa katika kifungu kidogo cha (2) ndiyo maadili yenyewe au ni mwongozo tu ambao Rais ataufuata katika kuweka maadili, au kama ni vigezo vya maadili yatakayowekwa.

(c )  Mkanganyiko wa aina hii unaonekana pia katika kifungu cha 6 ambacho kinaorodhesha misingi itakayotumika katika maadili (“Principles to be invoked by the code”), wakati ibara ya 135(5) ya Katiba nayo inaweka “Misingi ya Maadili ya Viongozi.”

Aidha, haileweki kama mamlaka ya Rais chini ya kifungu cha 7 ya “declare requirements and rules regarding ethical standards,” ni jambo lile lile au tofauti na “to establish a code of ethics under the Act” ilivyokusudiwa katika ainisho la neno “code.”

42.  Kutokana na mkanganyiko unaojitokeza Tume imeridhika kuwa sehemu  ya pili ya sheria hii haiweki bayana suala la maadili ya viongozi yanayokusudiwa yawekwe na Rais.

43. Tume inaona kuwa hitilafu hii ni upungufu mkubwa katika Sheria ya Maadili ya Viongozi, upungufu ambao utaathiri utekelezaji wa sheria ya udhibiti wa tabia na mienendo ya viongozi.

44.  Kutokana na kasoro zilizojitokeza Tume inapendekeza sheria ifanyiwe marekebisho kuzingatia yafuatayo:

(a) Maadili yote yanayostahili yaorosheshwe kwenye sheria na hali ikihitaji Bunge liweze kuongeza orodha ya maadili hayo kwa kupitisha maazimio;

(b) Adhabu ya ukiukwaji wa maadili iwekwe bayana na mojawapo ya adhabu iwe ni kiongozi kuondolewa madarakani au kupoteza sifa ya kushika uongozi;

(c) Sheria itamke kuwa kiongozi atakayekabiliwa na tuhuma nzito na za wazi atajiuzulu au ataomba kujiuzulu.

MAADILI YA VIONGOZI WOTE

45. Sehemu ya tatu ya sheria inazungumzia maadili ya viongozi wote (Code of Ethics applicable to all public leaders). Aina ya maadili zilizowekwa kwenye sheria ni kama ifuatavyo:

(a) Hatua za kiongozi kuwasilisha kwa Kamishna wa Maadili tamko la mali na madeni yake binafsi, ya mke wake na ya mtoto wake ambaye hajaoa au kuolewa na mwenye umri wa chini ya miaka 18;

(b) Ni kosa kwa kiongozi wa umma, hali akijua, kujipatia masilahi makubwa ya kifedha kwa njia zisizo halali au kumsaidia mtu mwingine kujipatia masilahi kama hayo;

(c) Kiongozi wa umma haruhusiwi kuzungumza kwenye kikao bila kutoa taarifa kwenye kikao hicho, kuhusu masilahi aliyonayo ya kifedha katika jambo linalojadiliwa na kikao hicho;

(d) Kiongozi wa umma anahitajiwa kutoa tamko la masilahi yoyote aliyonayo katika kondrasi ya serikali.

46. Sharti la kiongozi kutangaza mali zake limewekewa vikwazo kiasi kwamba, shabaha ya sharti hilo haieleweki. Vikwazo hivyo vinatokana na mambo yafuatayo:

(a) Kutenganisha mali inayotakiwa kutangazwa (declarable assets) na mali isiyotakiwa kutangazwa (non-declarable assets),

(b) Kujumuisha katika mali isiyotakiwa kutangazwa mali kama nyumba ya kuishi, vyombo vya burudani na  mashamba ya familia, vitu vya sanaa na magari na vyombo vingine vya usafiri binafsi, pamoja na fedha itokanayo na mashamba au shughuli binafsi za kiongozi, akiba na  mikopo kutoka kwa mwajiri na jamaa zake,

(c) Kuweka sharti katika kifungu cha 10 kuwa mali na masilahi ya viongozi wa umma na familia zao na mali ambayo si ya kibiashara haihitajiki kutangazwa.

47. Tume ina maoni kuwa kigezo cha “mali isiyohitajika kutangazwa” kilichowekwa na sheria kinapingana na misingi ya madhumuni ya maadili. Kitendo cha kutenganisha mali katika mafungu ya mali inayotakiwa na isiyotakiwa kutangazwa inapingana na kudhoofisha madhumuni ya Sheria ya Maadili.

Kifungu cha 6(6) kinamhitaji kiongozi wa umma kutekeleza na kuendesha shughuli iliyowekwa na kifungu hicho kwamba kiongozi wa umma anatakiwa atekeleze kazi zake na kuendesha shughuli zake za binafsi kwa hali ambayo itaruhusu au kuwezesha shughuli hizo kuwa wazi mbele ya macho ya wananchi.

Kama kiongozi ana nyumba ya kuishi au kupangisha, magari na mashamba ni vema wananchi wakajua anavyo na jinsi alivyovipata. Aidha, kama mali ni ya mwenzi wa ndoa au mtoto wa kiongozi ni vema ifahamike wazi ili kiongozi, mwenzi wake wa ndoa au watoto wasituhumiwe kwa kujipatia mali kwa kutumia nafasi za kiongozi.

48. Baada ya kuridhika kwamba vifungu vyote vinavyoweka vikwazo vya kutangaza mali zote na mienendo ya viongozi vinadhoofisha madhumuni ya sheria hii. Tume inapendekeza kwamba vifungu vya 9, 10 na 11 vifutwe ili kuweka sharti la lazima kwa viongozi wa umma kutangaza mali zao bila vipingamizi vilivyomo kwenye sheria ya sasa. Hatua hii itaifanya sheria kuyaweka maadili katika watumishi wa umma wazi.

49. Tume inaliona sharti la kiongozi kutojipatia masilahi makubwa ya kifedha kwa njia zisizofaa katika kifungu cha 12 nalo lina vipingamizi visivyo vya lazima:

Kwanza, maneno “significant percuniary advantage” yaliyomo kwenye sheria hayatoi maana bayana ni kitu gani hasa kinachokusudiwa, jambo ambalo litafanya utekelezaji wa sharti hili kuwa mgumu; Tume inapendekeza neno “significant” liondolewe kwenye sheria; 

Pili, kiongozi anaweza kujipatia masilahi mengine ambayo siyo ya kifedha (pecuniary), kwa kufanya mambo yaleyale yaliyotajwa katika kifungu hiki. Kwa mfano anaweza kujipatia nyumba ya kuishi, magari shamba, kazi kwa jamaa zake na kadhalika mambo ambayo kwa mujibu wa kifungu cha 9 ni “non-declarable assets.”

 

Je, unafahamu Jaji Warioba katika Ripoti hii ya rushwa aliyoiandaa mwaka 1996 ameeleza nini juu ya maadili ya viongozi wakiwamo mawazi, wakuu wa mikoa na wilaya? Usikose sehemu ya sita ya ripoti hii itakayochapishwa neno kwa neno hadi mwisho.

1672 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!