Rais asiachiwe zigo la rushwa

MAADILI YA NYONGEZA KWA MAWAZIRI NA WAKUU WA MIKOA

50. Sehemu ya Nne ya Sheria inaweka masharti maalumu kwa mawaziri na wakuu wa mikoa. Wakuu wa wilaya hawakuhusishwa ingawaje wameorodheshwa kama viongozi wa umma. Maadili yaliyotajwa katika sehemu hii ni yale ambayo yanafahamika na kuzingatiwa na nchi zote zinazofuata mfumo wa Baraza la Mawaziri.

Maadili haya yanajulikana kama uwajibikaji wa pamoja (Collective responsibility) na yamekuwa yakitekelezwa hapa nchini kwa misingi ya tabia za kikatiba (“Constitutional Convention”). Tume haioni sababu ya kuliweka suala hili katika Sheria ya Maadili.

Kwanza, hakuna ushahidi wa ugumu katika utekelezaji wa dhana ya uwajibikaji wa pamoja kiasi cha kuhitaji itungwe sheria kulinda uwajibikaji huo. Tume imeridhika kuwa hali haionyeshi hivyo.

Pili udhibiti wa uwajibikaji huo unasimamiwa na Rais ambaye anao uwezo wa kikatiba wa kuwadhibiti na kuwachukulia hatua za kinidhamu mawaziri wake na wakuu wa mikoa au wilaya. Aidha, sharti la kutoa siri za Baraza la Mawaziri tayari linasimamiwa na Sheria ya Usalama wa Taifa na Sheria ya Kiapo.

Kuliwekea jambo moja masharti yale yale katika sheria mbalimbali kunaweza kuleta utata katika utekelezaji. Utata huu utatokana na kuweka vigezo vya ni lini kutoa siri za barazani ni uvunjaji wa maadili na lini inakuwa ni utendaji kosa la jinai chini ya Sheria ya Usalama wa Taifa au Sheria ya Kiapo. Tume inapendekeza sehemu hii ifutwe.

 

USIMAMIZI WA MAADILI YA VIONGOZI

51. Sehemu ya tano ya sheria inahusu taratibu za usimamizi wa maadili ya viongozi na vyombo vya kusimamia utekelezaji wa maadili hayo. Vyombo vya kusimamia utekelezaji wa maadili ni:

 

(a) Sekretariati ya Maadili chini ya uongozi wa Kamishna, ambaye kazi yake ni:

(i) Kupokea taarifa za mali;

(ii) Kupokea malalamiko au taarifa kuhusu ukiukwaji wa maadili; na

(iii) Kuchunguza ukiukwaji wa maadili.

(b) Baraza (Tribunal) lenye wajumbe watatu ambalo kazi yake ni kuendeleza uchunguzi ulioanzishwa na Sekretariati kuhusu ukiukwaji wa maadili;

(c) Rais, Spika na mamlaka za nidhamu ambao wamepewa mamlaka ya kupokea nakala za taarifa za uchunguzi uliofanywa na Baraza na kuwasilishwa kwa Kamishna wa Maadili;

(a) Bunge ambalo litapokea nakala ya taarifa ya uchunguzi itakayowasilishwa mezani na Spika;

(b) Kamati inayoundwa chini ya kifungu cha 25(1) kwa madhumuni ya kuitisha na kuchukua ushahidi kwa kiapo;

(c) Vyombo vya upelelezi kama vile Polisi, Taasisi ya Kuzuia Rushwa, Tume ya Kudumu ya Uchunguzi ambavyo vinaweza kuombwa kufanya uchunguzi na Baraza chini ya kifungu cha 25(7).

52. Ni dhahiri kuwa vyombo vyenye uwezo wa kusimamia utekelezaji wa maadili ni vingi. Hivyo uchunguzi wa ukiukaji wa maadili utachukua muda mrefu kabla ya kuuthibitisha. Aidha, kwa kuwa baada ya uchunguzi kukamilika mamlaka za nidhamu nazo zimepewa nafasi yake, itachukua muda mrefu zaidi kabla adhabu haijatolewa dhidi ya aliyekiuka maadili. Hali hii haiwezi kujenga imani ya wananchi katika uadilifu wa uongozi.

 

UTARATIBU WA KUSIMAMIA UTEKELEZAJI WA MAADILI

53. Sheria imetoa utaratibu ufuatao:

(a) Maofisa kutoa tamko la mali kwa Kamishna wa Maadili;

(b) Kamishna kuweka kumbukumbu katika daftari;

(c) Kamishna kupokea taarifa za ukiukwaji wa maadili;

(d) Kamishna kuagiza uchunguzi ufanywe ama na Sekretatiati au kwa niaba ya Sekretariati;

(e) Kamishna kujiridhisha kama kesi ya kujibu imethibitika kabla kiongozi hajajieleza;

(f) Kama kesi ya kujibu ipo;

(i) Ikiwa mtuhumiwa ni Rais, Kamshina kuwasilisha malalamiko kwa Rais na kwa Spika.

(ii) Kama ni kiongozi mwingine Kamishna kuwasilisha malalamiko kwa Rais na Spika.

54. Hali hii inaweza kusababisha viongozi wa umma waliokiuka maadili ya aina moja washughulikiwe ama na vyombo tofauti au kwa taratibu tofauti. Tume inapendekeza kifungu cha 23(2) cha sheria kirekebishwe ili;

(a) Kama tuhuma zinamhusu Rais, Rais ahitajiwe kutoa maelezo; na

(b) Kama tuhuma zinamhusu kiongozi yeyote wa umma, kiongozi huyo ahitajiwe kujieleza bila kumtaarifu Rais au Spika.

55. Pamoja na kupewa jukumu la kupokea na kuchunguza ukiukwaji wa maadili, si Kamishna wa Maadili wala Baraza (Tribunal) waliopewa mamlaka ya kutamka kama mtuhumiwa ana hatia ya kukiuka maadili au la. Tume imebaini hili kama upungufu mkubwa. Tume inapendekeza Kamishna wa Maadili apewe uwezo wa kutamka kama tuhuma imethibitishwa au la.

56. Baada ya kutafakari kwa undani kuhusu utaratibu uliowekwa na sheria kuchunguza tuhuma, Tume inapendekeza kuwa utaratibu wa uchunguzi uwe ni wa kupokea ushahidi wa moja kwa moja bila kupitia hatua kama za upelelezi wa makosa ya jinai.

Pale ambapo kiongozi aliyeteuliwa atathibitika amekiuka maadili aondolewe madarakani. Kama mtuhumiwa atakuwa ni mbunge, basi Kamishna awasilishe taarifa kwenye Bunge na nakala kwa chama chake. Bunge litatoa uamuzi wa kumvua kiti.

 

ADHABU

57. Ibara ya 125(4) na (5) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inaeleza kuwa Bunge litatunga sheria itakayoainisha misingi ya maadili ya viongozi wa umma na kufafanua adhabu zinazoweza kutolewa kwa kuvunja misingi hiyo.

Hata hivyo Sheria ya Maadili ya Viongozi ya 1995 haifafanui adhabu itakayotolewa kwa ukiukwaji wa maadili. Ili kujenga imani ya wananchi katika sheria yenyewe ya maadili na pia ili sheria iweze kufuatwa na viongozi na kusimamiwa kikamilifu na vyombo vinavyohusika, sharti adhabu ya ukiukwaji wa maadili ijulikane wazi kuwa ni kuondolewa madarakani na kushtakiwa kwa mujibu wa sheria za nchi kama kosa hilo la maadili linavunja sheria za jinai.

58. Kifungu cha 32 cha Sheria ya Maadili kinampa waziri mamlaka ya kutunga kanuni na taratibu za kutekeleza sheria bila ya kutoa tafsiri ya neno ‘Waziri’ kuwa ni Rais. Tume inafikiria Bunge lilitarajia Rais ndiye atakayetunga kanuni na taratibu hizo. Hata hivyo, Tume inapendekeza tafsiri hiyo iwekwe kwenye sheria pamoja na kukiandika upya kifungu hicho ili kutilia maanani mapendekezo yaliyotolewa kuhusu mali zitakazotangazwa.

59. Ni maoni ya Tume kuwa marekebisho haya yafanyike mapema ili azma ya Serikali ya kuondoa rushwa na kuendesha shughuli za umma kwa uwazi na kuzingatia sheria, ionekane mapema.

60. Mwisho, wakati wa kampeni za uchaguzi, Rais Benjamin William Mkapa aliahidi atatangaza mali zake na za mke wake akichaguliwa kuwa Rais. Kwa hakika alifanya hivyo mara baada ya kuapishwa. Alifuatiwa na Makamu wa Rais, Dk. Omar Ali Juma. Baada ya hapo Mwanasheria Mkuu wa Serikali akatangaza kuwa sheria haikuhitaji viongozi watangaze mali zao. 

61. Tume imeshindwa kuelewa mantiki ya ushauri huo wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Pamoja na kwamba sheria haitamki kuwa viongozi watangaze mali zao hadharani, sheria pia haikatazi kitendo hicho. Kwa hiyo Tume haikuelewa maana ya matamshi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali baada ya Rais ambaye ndiye mwenye madaraka ya kuandaa kanuni za utekelezaji wa sheria hii kutangaza mali zake hadharani.

62. Kitendo cha Rais na Makamu wake kutangaza mali walizonazo kilipokewa na hisia za matumaini kwa wananchi. Kiliwatia moyo na kuwaongezea imani kwa viongozi wao. Nje ya mipaka yetu, kilipokewa kama kitendo cha uwazi kinachostahili kuigwa na viongozi wote Afrika. Tanzania ilionekana mwanzilishi wa mwenendo utakaowaongezea heshima viongozi wa Afrika.

63. Tume imelitafakari kwa undani suala la kutangaza mali hadharani. Imeridhika ni haki ya wananchi kujua mali walizonazo viongozi wao. Ni haki pia ya wananchi kuwadhibiti viongozi wanaokiuka misingi ya viapo vyao. Kwa hivyo basi, Tume inapendekeza kuwa utaratibu wa viongozi kutangaza mali zao hadharani uandaliwe na kila kiongozi afanye hivyo.

Hatua za haraka za utekelezaji kuhusu uongozi

64. Nchi yetu imekuwa ikiteua Tume nyingi sana ili kuchunguza mambo mbalimbali. Isipokuwa kwa Tume chache tu – ya Nsekela, Nyalali na Mtei ambazo sehemu ya mapendekezo yake yalitekelezwa – nyingi ya Tume hizi mapendekezo yake yameishia kuota vumbi katika makabati ya ofisi mbalimbali.

65. Hatari hiyo inaikabili hata Tume hii pia; na hasa tukikumbuka kwamba hii si Tume ya kwanza kuhusu rushwa. Aidha, kwa vile madhambi ya rushwa yanaanza na viongozi wenyewe ambao wanatakiwa kusimamia utekelezaji wake, inakuwa vigumu zaidi.

66. Hivyo mapendekezo yoyote ambayo yatatolewa ili kutekeleza taarifa hii sharti yalenge katika kupiga vita udhaifu wa huko nyuma.

67.  Kama ilivyoelezwa huko nyuma, wananchi hawana imani na uongozi na baadaye katika taarifa hi kuna maelezo kuonyesha kwamba wananchi hawana imani na vyombo vya dola, hasa mahakama na polisi. Vita vya kweli dhidi ya rushwa lazima visimamiwe na viongozi wa nchi na vyombo vya dola.

Lakini mwelekeo wa viongozi na vyombo vya dola ni tofauti kabisa. Viongozi na watendaji wengi ambao Tume imezungumza nao hawaonyeshi kuelewa kwamba tatizo ni kubwa na wengi wanaamini mengi yanayosemwa kuhusu rushwa ni majungu.

Jambo la kutisha zaidi ni kwamba wengi wa viongozi watendaji wanaonyesha kuamini kwamba rushwa imeenea zaidi ngazi za chini na kati katika utumishi wa umma. Maelezo yao kuhusu hatua zilizochukuliwa huko nyuma kupambana na rushwa zinahusu watumishi wa ngazi za chini na kati.

Kwa mfano Idara ya Polisi imekuwa ikichukua hatua kuhusu askari wanaohusika na rushwa na waliwasilisha kwenye Tume orodha ya askari mia ishirini na tatu (123) waliofukuzwa kutokana na vitendo vya rushwa katika miaka sita iliyopita (1991 – 6).

Kati ya hao zaidi ya mia moja (100) ni konstebo na mmoja tu ni Assistant Superitendent. Hakuna hata ofisa mmoja wa ngazi ya juu aliyeachishwa kwa kosa la rushwa. Lakini maoni ya wengi, pamoja na askari wa ngazi ya chini, wanasema askari wenye vyeo vya juu na maofisa ndio walarushwa wakubwa. Hali ni hiyo hiyo kwa mahakama, idara za serikali na mashirika ya umma.

68. Sababu kubwa inayotolewa na viongozi watendaji kuhusu kuenea kwa rushwa ni makali ya maisha na ukosefu wa vitendea kazi. Ili kumaliza au kupunguza rushwa viongozi watendaji katika utumishi wa umma wanapendekeza mishahara iongezwe na fedha za vitendea kazi ziongezwe.

69. Suala la ugumu wa maisha kama kimojawapo cha vishawishi kutoa na kupokea rushwa ni kweli na limetajwa katika taarifa hii. Hata Rais anatambua hali hii. Katika tamko lake wakati wa kutangaza Tume hii alisema;

“Jitihada za Serikali kuinua uchumi wetu zinadhihirika na zitaongezwa nguvu. Uchumi ukiboreka na waajiriwa kuweza kupata mishahara inayokimu matumizi ya msingi ya maisha, vishawishi vya kutoa na kupokea rushwa vitapungua. Lakini sambamba na harakati za kufufua uchumi, mapambano dhidi ya rushwa hayana budi yaendelee kwa kutumia mbinu mbalimbali.”

70. Tume imetambua uzito wa jambo hili na katika taarifa hii kuna mapendekezo mengi kuhusu kuongeza mishahara na marupurupu mengine na kuboresha mazingira ya ajira na kazi kwa ujumla. Pamoja na kutoa mapendekezo hayo, Tume imebaini viongozi watendaji wengi wanatumia ugumu wa maisha kama kisingizio ili waendelee kujihusisha na vitendo vya rushwa.

71. Walarushwa wakubwa siyo wale wanaopokea kima cha chini cha mshahara. Ni watu wanaopokea mishahara mizuri, wana nyumba za kuishi na kupangisha, wana magari ya kutembelea na ya biashara, wanakula na kuvaa vizuri, wanasomesha watoto wao katika shule za malipo makubwa nje na ndani ya nchi na kadhalika. Kwa watu kama hawa kuongeza mishahara peke yake hakutaweza kuwafanya waache kula rushwa. Kutawafanya waongeze thamani ya rushwa!

72. Kwa upande wa viongozi wa ngazi za juu hali ni mbaya zaidi. Kila kiongozi anajiona yeye ni safi. Kila kundi la viongozi linajiona wao ni safi. Kilichobaki ni kulaumiana. Viongozi wa serikali wanalaumu mahakama na polisi kuwa ndio walarushwa. Mahakama inalaumu serikali. Wabunge wanalaumu serikali na mahakama. 

Viongozi wa chama tawala wanalaumu serikali na vyombo vyake na viongozi wa vyama vya upinzani wanalaumu chama tawala, serikali na vyombo vyake. Kila kundi la viongozi wanalo kundi la kulaumu na kujionyesha wao hawana dosari na wakipewa madaraka watalimaliza tatizo la rushwa.

Matamshi ya viongozi imekuwa ni mbinu ya kuwania madaraka. Watu hawa wakipata madaraka wanabadilika na kuanza lugha ya utetezi. Tume inaona hili ndilo tatizo kubwa kuliko yote katika mapambano dhidi ya rushwa.

73. Tume inaamini ili kupambana na rushwa hatua za mwanzo ni lazima zihusu uongozi. Rais aliposhika madaraka alitangaza mali zake, alikataa kuitwa mtukufu, alikataa habari kumhusu yeye zisiwe ndiyo zinaandikwa kurasa za mbele za magazeti na alisema siyo lazima picha yake ionekane kwenye noti.

Ukiacha Makamu wa Rais, hakuna viongozi wengine waliofuata mfano wake. Badala yake viongozi wengine wanafanya kinyume. Wabunge wanataka ulinzi, wanataka wapigiwe saluti, wanataka haki nyingi ambazo kwa mwananchi wa kawaida ni ndoto, lakini hawatangazi mali zao na kadhalika.

74.  Tumeeleza hatua mbazo zimewahi kuchukuliwa huko nyuma kwa jitihada za kupambana na rushwa. Hatua hizo ni pamoja na kutunga sheria, kuunda vyombo vya kushughulikia rushwa, kufanya kampeni dhidi ya rushwa, msako na kutaja majina.

Pamoja na hatua zote hizo, mafanikio yalikuwa duni na viongozi hawakuguswa. Tume inaamini sasa umefika wakati wa taifa kuelekeza nguvu zake kwenye uongozi. Hatua zitakazochukuliwa zilenge kuwafanya viongozi wafuate maadili, wafanye kazi kwa pamoja badala ya mtindo wa kulaumiana, kuwaondoa viongozi ambao hawafai, kuwalinda viongozi wazuri na kuweka utamaduni wa uwazi na kuwajibika.

Mapambano dhidi ya rushwa ni ya wote na hasa viongozi. Kila kiongozi ni lazima aonekane safi machoni mwa wananchi, aonekane anawaandama walarushwa katika eneo lake la uongozi na kama hawezi aondoke hata kama yeye mwenyewe hatuhumiwi kwa kula rushwa. Kazi ya kupambana na rushwa asiachiwe Rais peke yake.

75. Kwa kuwa rushwa imeenea kila mahali, viongozi wote ni lazima wachukue hatua za waziwazi kupambana na rushwa. Kwa msingi huo Tume inapendekeza:

(a) Rais aitishe taarifa za viongozi wote wanaotuhumiwa kuhusika na vitendo vya rushwa kutoka kwenye vyombo vya dola vyote vya ulinzi na usalama kwa madhumuni ya kuzifanyia kazi. Wakati juhudi za serikali zinachukuliwa kuimarisha Taasisi ya Kuzuia Rushwa, Rais aunde chombo maalumu cha muda ambacho kazi yake itakuwa kupeleleza na kuwafikisha mahakamani watakaoonekana na tuhuma za rushwa.

Chombo hicho kipewe muda maalumu wakati vyombo vya dola vinavyohusika na kazi hiyo vinasafishwa na kuimarishwa.

 

(b) Taarifa za viongozi zifanyiwe tathmini ya kina ili kumuwezesha Rais kutambua aina ya viongozi alionao.

(c) Rais atoe agizo la wazi kwa viongozi wote kuchukua hatua za wazi za kupambana na rushwa na walarushwa katika maeneo yao katika kipindi cha muda wa miezi sita. Hatua zitakazochukuliwa zitangazwe na umma uzifahamu. Watu watakaochukuliwa hatua watangazwe. Baada ya kipindi hicho kama kiongozi hakuchukua hatua kuwaridhisha wananchi basi aondolewe madarakani.

(d) Sheria ya Kuzuia Rushwa iweke utaratibu wa kupeleka taarifa katika Bunge kuhusu hatua zilizochukuliwa kupambana na rushwa katika kipindi cha miezi kumi na miwili na taarifa hiyo ijadiliwe bungeni.

(e) Viongozi wote wa ngazi za juu watangaze mali zao na utaratibu uwekwe wa kuhakiki mali hizo.

(f) Serikali iandae utaratibu wa kusafisha safu ya watendaji.

(g) Vyombo vyote vya uongozi ikiwa ni pamoja na vyama vyote vya siasa vichukue hatua za kusafisha safu za uongozi.

76. Tanzania ni nchi moja. Pamoja na kwamba ndani ya Jamhuri ya Muungano kuna serikali mbili kila moja ikiwa na vyombo vyake, lakini ni ukweli usiokwepeka kwamba suala la rushwa halina mipaka. Kwa hiyo Tume inapendekeza kwamba wakati umefika wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuwa na sheria moja ya kuzuia rushwa.

 

SURA YA NNE

UTUMISHI SERIKALINI

77. Shughuli zote za utendaji wa Serikali zimekabidhiwa kwa watumishi wa Serikali kwa niaba ya Rais. Utendaji serikalini unasimamiwa na sheria (Sheria ya Utumishi Serikalini na Sheria ya Usalama kazini), kanuni (Kanuni za Utumishi Serikalini, Kanuni za Fedha, Kanuni za Kudumu) na nyaraka mbalimbali (Nyaraka za Utumishi na Nyaraka za Hazina n.k.).

Lengo la kuwepo kwa sheria, kanuni na nyaraka hizo ni kuhakikisha kwamba utendaji wa Serikali unakuwa na ufanisi mzuri ulio wa uwazi na usio na upendeleo.

78. Kutokana na nchi yetu kujitawala kwa muda sasa, ilitegemewa kwamba utendaji wa serikali ungekuwa unaongezeka ubora wake kila mara. Kwa hali hiyo maendeleo ya nchi nayo yangekuwa mazuri.

Kinyume na hali hiyo utendaji wa Serikali umekuwa unashuka siku hadi siku na hali ni mbaya kiasi cha kuhitaji msaada wa mpango maalumu wa kuufufua (Civil Service Reform Program). Hali hii imefikiwa baada ya kuua utamaduni wa utawala.

Wakati wa kujitawala tulirithi kada ya watawala iliyokuwa imebobea katika fani ya utawala baada ya kupitia mafunzo mbalimbali. Ofisa alipanda ngazi kufuatia uwezo wake na baada ya kupitia mafunzo mbalimbali na kufaulu mitihani iliyohusika. 

Taratibu hizo tumezitelekeza. Ufanisi katika wizara na idara za Serikali umezorota sana. Utoaji wa huduma za jamii umeshuka kiasi kwamba sasa ni kero kubwa kwa wananchi. 

79. Kufifia kwa utendaji wa Serikali kumewafanya wananchi kukosa imani na Serikali. Hali hiyo imetokana na kwamba licha ya utendaji wake kuwa mbovu, watumishi wa Serikali wamekuwa wa kwanza kujihusisha na vitendo vya rushwa. Kushamiri kwa rushwa katika utumishi wa Serikali na wa umma kwa jumla kunatokana na matatizo mbalimbali yakiwemo:

i) Ukiukwaji makusudi wa taratibu kwa manufaa binafsi;

ii) Udhaifu katika usimamizi wa taratibu na kanuni;

iii) Uhaba wa fedha unaosababisha uhaba wa vitendea kazi na mafunzo kwa watumishi;

iv) Kiwango kidogo cha mishahara ya watumishi.

 

Mpendwa msomaji, usikose sehemu ya saba ya ripoti ya Rushwa ya Jaji Warioba aliyoitoa mwaka 1996, ambayo hadi leo ikisomwa maudhui yake utafiriki imechapishwa wiki hii. Mhariri

1924 Total Views 1 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!