Polisi waliiharibu TAKUKURU

 

YALIYOJITOKEZA

 

154. Tume imetafakari kwa undani muundo wa taasisi na shughuli za kurugenzi zote. Katika kufanya hivyo, umuhimu wa Kurugenzi ya Mafunzo, Utafiti na Elimu kwa Umma umetiliwa maanani hasa kwa kuzingatia jukumu lake zito la kuzuia rushwa. Aidha, umuhimu wa kugundua na kufuatilia asilimia kubwa ya tuhuma za rushwa pia unazingatiwa.

Ufanisi wa taasisi katika kupambana na rushwa utategemea uwezo wa Kurugenzi ya Uchunguzi kugundua asilimia kubwa ya tuhuma za rushwa na kuzipeleleza kikamilifu. Umuhimu wa uendeshaji mashtaka mahakamani umepewa uzito unaostahili.

155. Baada ya kutafakari nafasi ya Kurugenzi ya Uchunguzi na ile ya Sheria na Mashtaka, Tume ina maoni yafuatayo:

(a) Kwa vile Sheria ya Kuzuia Rushwa inatoa fursa kwa wapelelezi wote kuwa waendesha mashtaka, si sahihi iwepo kurugenzi yenye wanasheria pekee.

(b) Pamoja na kwamba misingi ya uendeshaji kesi mahakamani inahitaji mpelelezaji asiwe ndiye anayeendesha kesi mahakamani, misingi hii haizuii ofisa yeyote wa Kurugenzi ya Uchunguzi ambaye hakuhusika na upelelezi kuendesha kesi mahakamani.

(c) Matarajio ya mpelelezaji ni kuhakikisha kesi iliyopelelezwa vizuri na ina ushahidi wa kutosha kwa mafanikio mahakamani.

(d) Utenganishaji wa upelelezi na uendeshaji mashtaka haujaleta ufanisi katika shughuli za taasisi bali umeongeza urasimu.

156. Hivyo basi, Tume inapendekeza kuwa kurugenzi za uchunguzi na ya sheria na mashtaka ziunganishwe ili kuimarisha upelelezi na uendeshaji mashtaka. Katika kurugenzi hiyo kiwepo Kitengo cha Sheria na Mashtaka pamoja na cha Uchunguzi. Kurugenzi hii iongozwe na ofisa mwandamizi atakayesaidiwa na maofisa wawili wenye ujuzi na uwezo unaolingana na wadhifa wao.

Aidha, Kitengo cha Ufundi na Mawasiliano (Technical Communication) kiwe pia chini ya Kurugenzi ya Uchunguzi kuiwezesha kurugenzi kusimamia vizuri upelelezi bila urasimu.

157. Tume pia imetafakari nafasi na shughuli za Kurugenzi ya Mafunzo, Utafiti na Elimu kwa Umma kwa kina. Shughuli za mafunzo ni muhimu sana na zinapaswa kupewa kipaumbele. Shughuli za uchambuzi wa miundo, taratibu, sheria na mienendo kwa madhumuni ya kugundua mianya ya rushwa nayo ni muhimu pia. 

Aidha, elimu kwa umma ni jukumu mojawapo la taasisi katika kuhamasisha umma dhidi ya vitendo vya rushwa na kuwashirikisha wananchi katika mapambano dhidi ya rushwa. Shughuli za kurugenzi hii ni nzito na ni nyingi mno. Tume inapendekeza Kitengo cha Mafunzo kihamishiwe Kurugenzi ya Utawala na Utumishi na kurugenzi hii ijulikane kama Kurugenzi ya Uzuiaji Rushwa, Utafiti na Elimu kwa Umma (Corruption Prevention, Research and Community Education). Kurugenzi ipewe nyenzo za kuiwezesha kufanya kazi ipasavyo.

 

Kurugenzi ya Utawala na Utumishi

158. Kurugenzi hii inayo majukumu muhimu kama Kurugenzi ya Huduma kwa kurugenzi zote za taasisi. Ufanisi wa taasisi unategemea kwa kiwango kikubwa mazingira ya kufanyia kazi ambayo huchangia moyo wa utendaji kazi. Tume imebaini umuhimu wa kuwepo kurugenzi hii. Hata hivyo imebainika bado kuna upungufu katika kutimiza majukumu yaliyoainishwa na muundo. Upungufu huu umechangia katika kuvunja moyo watumishi.

Hali hii si ya kuridhisha katika chombo nyeti kama taasisi. Hivyo basi Tume inapendekeza utendaji kazi wa kurugenzi uimarishwe kuiwezesha kutoa huduma zifaazo kwa kurugenzi nyingine na hivyo kuboresha masilahi ya watumishi na ufanisi wa taasisi.

159. Taasisi ya Kuzuia Rushwa ni taasisi inayofanya kazi ngumu sana. Wananchi wengi wakiwemo viongozi hawaipendi. Watumishi wake wanajikuta wanatengwa au kubaguliwa. Hali hii inafanya maisha yao yawe magumu. Matokeo yake taasisi na maofisa wake hufanya kazi katika mazingira magumu. Kuna haja ya serikali kuangalia suala hili kwa undani.

 

Kamati za Taasisi

160. Taasisi inazo kamati mbili zinazosaidia katika uimarishaji wa utendaji wa shughuli zake.

 

Kamati ya Udhibiti na Tathmini

161. Kamati hii inaongozwa na mwenyekiti wake ambaye ni Katibu Mkuu wa Rais. Wajumbe wake ni Mkurugenzi wa Taasisi, Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa na Katibu wa Rais. Katibu wake ni Mkurugenzi wa Utawala wa Taasisi ya Kuzuia Rushwa. Kamati hii hukutana mara moja kwa mwezi.

162. Shughuli za kamati hii pamoja na kushauri juu ya utendaji wa taasisi, ni kupokea taarifa za viongozi wanaotuhumiwa kuhusika na vitendo vya rushwa na kuzifanyia uchambuzi.

Hatua zinazoweza kuchukuliwa ni pamoja na kumshauri rais, kupeleka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali au Mkurugenzi wa Mashtaka au Polisi, kumshauri Katibu Mkuu wa Rais akiwa mkuu wa utumishi hatua za kuchukua kulingana na kanuni za utumishi au kuzirudisha taasisi ili kufanyiwa uchunguzi zaidi. Kamati hii pia inashughulikia upandishwaji vyeo watumishi wa taasisi na kupitisha bajeti ya taasisi.

163. Tume imetafakari nafasi ya kamati hii na kuridhika na umuhimu wake. Taasisi ya Kuzuia Rushwa ni chombo chenye jukumu zito na mamlaka makubwa. Utendaji wake wakazi unaingilia haki za Rais. Aidha, mamlaka yake yanaweza kutumiwa vibaya. Hivi sasa hakuna chombo rasmi cha kutathmini utendaji kazi wa taasisi wala kupokea malalamiko dhidi ya maofisa wake.

164. Tume inapendekeza kamati hii iongezewe majukumu ishughulikie pia tathmini ya utendaji kazi wa taasisi, malalamiko dhidi ya maofisa wa taasisi na kutoa ushauri kwa Rais.

 

Kamati ya Wakurugenzi

165. Kamati hii inajumuisha wakurugenzi wote, katibu wao akiwa Mkurugenzi wa Utawala. Pamoja na kusimamia utendaji wa kila siku, nidhamu, mapendekezo ya wanaopandishwa vyeo, kupitia bajeti pia hujadili taarifa za tuhuma za rushwa dhidi ya watumishi wa serikali kabla ya kupelekwa kwenye Kamati ya Udhibiti na Tathmini.

 

Utendaji wa Taasisi

166. Pamoja na kuwepo kwa taasisi hapa nchini, vitendo vya rushwa vimekuwa vinaongezeka kwa kasi na vimekuwa vinafanywa bila woga. Hali hi imeashiria mawazo kwa wananchi kuwa taasisi imeshindwa kutimiza majukumu yake. Aidha, taasisi yenyewe imeshutumiwa kukuza vitendo vya rushwa. Kwa hali hiyo Tume imelazimika kutafuta kwa undani matatizo ya taasisi na sababu nyingine ambazo zimechangia katika hali hii.

 

Kiini cha matatizo

167. Matatizo ya utendaji na ufanisi wa taasisi ulianza tangu ilipoanza shughuli zake kutokana na uteuzi wa watendaji.

168. Watendaji walioanzisha taasisi walikuwa ni maofisa wa polisi. Matatizo yaliyotokana na uamuzi huo ni haya yafuatayo:

i) Maofisa wa polisi waliopewa majukumu ya Taasisi ya Kuzuia Rushwa waliichukulia taasisi kama Kitengo cha Polisi, hivyo kuendesha shughuli za taasisi kama za kipolisi (kusaka na kukamata wahalifu).

ii) Kwa kufanya shughuli za taasisi ziwe kama za polisi, jukumu kuu la taasisi ambalo lilikuwa la kuzuia na kushauri jinsi ya kuzuia rushwa liliachwa, hivyo usakaji ukapewa umuhimu wa juu kuliko kuzuia tatizo lisitokee.

iii) Wengi wa polisi waliojiunga na taasisi walikuwa hawana elimu ya kutosha. Wengi wa watendaji walikuwa “non gazetted officers” na wale waliokuwa na vyeo vya ngazi ya kati hawakuwa na ujuzi wa kutosha. Hivyo ukosefu huu wa elimu na taaluma uliinyima taasisi watendaji wenye utaalamu katika taaluma zao.

iv) Kwa kuwa watendaji wengi walikuwa na elimu ya chini, uwezo wao na upeo wa kutathmini masuala mbalimbali ulikuwa finyu. Matokeo yake ni kwamba taasisi ilishughulikia kesi za hongo zilizokuwa rahisi kushughulikia.

v) Upungufu uliokuwepo kwenye utendaji wa taasisi kutokana na usimamizi hafifu na ukosefu wa utaalamu viliifanya taasisi ifanye kazi kwa namna iliyoifanya iogopwe na wananchi badala ya kuwa chombo cha kuwasaidia kuondokana na kero ya rushwa.

vi) Jitihada za serikali za kurekebisha dosari hizi zilizofanywa miaka ya mwisho ya 1970 kwa kuiweka taasisi chini ya Ofisi ya Rais na kupeleka wataalamu wa fani mbalimbali kama wanasheria, hazikutatua tatizo bali matatizo yalibadilika na kuwa ya mgongano kati ya wataalamu na maofisa waliokuwepo.

Mgawanyiko huo uliizuia taasisi kufanya kazi kama sheria ilivyotamka, hivyo kufanya uwepo udhaifu uliotoa mwanya wa rushwa na kuenea kwa vitendo vya rushwa. Aidha, mabadiliko ya muundo yaliyofanywa mwaka 1992 na kuipa umuhimu Kurugenzi ya Mafunzo, Utafiti na Elimu kwa Umma hayajaleta ufanisi kwa kuwa mfumo wa utendaji bado haujabadilishwa na taasisi haijapewa nyenzo za kuiwezesha kufanya shughuli hizo.

169. Ufanisi wa taasisi, kwa sehemu kubwa ulitegemea uwezo wake wa kugundua na kufikisha mahakamani asilimia kubwa ya tuhuma za rushwa. Taasisi ilitegemewa ifanye upelelezi wake kitaalamu. Uwezo wake wa kugundua vitendo vya rushwa ungetoa tishio kwa wahalifu. Hata hivyo taasisi imeshindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo na hivyo kutoa mawazo kwamba haina haja ya kuwapo.

170. Tume imeridhika na umuhimu wa taasisi katika jamii yetu. Imebaini kuwa imeshindwa kufanya kazi yake kutokana na udhaifu uliopo pamoja na ukosekanaji wa msaada wa makusudi kutoka serikalini. Kwa mfano, kwa muda wa miaka mitano taasisi haijatengewa fedha za mafunzo.

Hivi sasa taasisi haina magari yanayoaminika. Kwa kanda za Kaskazini, Magharibi na Nyanda za Juu magari yaliyopo ni ya 1986. Hata Makao Makuu hivi sasa hakuna gari hata moja la kufanyia upelelezi. Isitoshe kwa kipindi cha miaka mitatu taasisi haitengewi fedha za kutosha kwa ajili ya upelelezi. Matokeo yake tuhuma hazifuatiliwi. Hali hii haiwezi ikatoa mazingira mazuri ya kuiwezesha taasisi itimize majukumu yake.

171. Kutokana na muundo uliopo (establishment) ingepaswa kuwa na maofisa na wapelelezi 130 kwa kanda na Makao Makuu. Pamoja na jitihada za kuwapata wataalamu wenye uwezo zaidi katika taasisi, bado kuna upungufu wa watumishi. Taasisi ina jumla ya maofisa na wapelelezi 44 nchi nzima.

172. Sheria ya Kuzuia Rushwa inatamka kuwa taasisi itakuwa idara ya umma (public department) chini ya uangalizi na usimamizi wa Rais. Sheria hiyo inampa fursa Rais kuandaa muundo, taratibu na kanuni za nidhamu za taasisi.

173. Mantiki ya tafsiri ya nafasi ya taasisi inaonyesha sheria haikukusudia taasisi iwe kama idara nyingine za wizara za serikali. Ilipaswa iwe idara yenye muundo, taratibu na kanuni zake za nidhamu. Hali halisi haikuwa hivyo. Ingawaje utendaji kazi wa taasisi unaifanya iwe kama chombo cha dola, viwango vya mishahara na masuala ya kiutumishi hutoa sura kama taasisi ni idara kama zilivyo idara nyingine za serikali. Hali hii imebainishwa na mambo yafuatayo:

i) Taasisi ya Kuzuia Rushwa haichukuliwi kama chombo cha dola na hivyo kutoshirikishwa kwenye vikao vya mikoa na taifa vya ulinzi na usalama. Matokeo yake taasisi imejikuta inatengwa. Viongozi wengi hawapendi kuishirikisha katika maswala ya kitaifa.

ii) Mishahara na mapato mengine ya watumishi wa taasisi ni vya chini sana kulinganisha na mishahara ya watumishi wa idara nyingine za usalama kama kiambatanisho “B”  kinavyoonyesha.

Wakati taasisi ilipoanza kazi ikiitwa Kikosi cha Kuzuia Rushwa mishahara ya kuanzia kwa maofisa wa ngazi za chini ilikuwa ikilingana na wa askari polisi mwenye cheo cha mrakibu msaidizi (Assistant Superintendent of Police) hivi sasa hata konstabo wa polisi wanapata mshahara mkubwa kuliko ofisa wa taasisi.

174. Muundo uliopo wa taasisi umegawanyika katika makao makuu na ofisi za kanda. Hivi sasa kuna ofisi sita za kanda. Kwa hali hii uwakilishi wa taasisi mikoani na wilayani haukidhi mahitaji ya taifa. Kuna haja ya kusambaza shughuli za taasisi ili ziwe karibu na wananchi na kuboresha utendaji kazi katika kupunguza kero za wananchi. Kipaumbele kipewe kwenye ufunguaji wa ofisi za taasisi kila mkoa na kila wilaya.

175. Pamoja na matatizo ya ndani ya taasisi yaliyofanya rushwa ikaendelea kushamiri bila kupata mdhibiti, yapo matatizo ya nje yaliyosaidia kushamiri kwa hali hiyo. Baadhi ya matatizo hayo ni:

i) Ingawaje mwaka wa 1983 Serikali ilionyesha nia ya kupambana na rushwa pamoja na maovu mengine, ilibainika kwamba viongozi walioyaunga mkono mapambano hayo walikuwa wachache. Jitihada za kampeni dhidi ya wahujumu uchumi hazikuzaa matunda yaliyotegemewa.

Hata baada ya Chama Cha Mapinduzi kulifanyia uchambuzi wa kina tatizo la rushwa nchini mwaka 1989 na kupeleka mapendekezo yake serikalini kwa utekejezaji, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa kutekeleza mapendekezo hayo wala hakukuwepo na ufuatiliaji.

Rushwa iliendelea kushamiri kutokana na ukosefu wa dhamira ya kisiasa. Ukosefu wa dhamira hiyo ulizidi kudidimiza utendaji na ufanisi wa taasisi. Tume imeridhika kuwa Serikali nayo haikutoa uzito kwenye juhudi za kupambana na rushwa na haikutoa kipaumbele katika uimarishaji wa taasisi.

Hali hii ilifanya Serikali isiweze kugundua upungufu na udhaifu wa taasisi na kuchukua hatua za dhati kuifanyia marekebisho na kuiimarisha.

ii) Upungufu uliopo katika Sheria ya Kuzuia Rushwa (Na. 16 ya 1971) ni kikwazo kingine kinachozuia taasisi kutekeleza wajibu wake. Upungufu huo utazungumziwa kwenye sehemu ya Sheria ya Kuzuia Rushwa.

 

Mapendekezo 

176. Ili kurekebisha hali hii na kuiwezesha taasisi kufanya kazi yake, Tume inapendekeza mambo yafuatayo:

(1) Mwelekeo wa utendaji wa taasisi ubadilishwe na jukumu la kwanza la taasisi liwe uzuiaji rushwa na kuelimisha umma.

(2) Taasisi iimarishwe kuifanya chombo cha kisasa chenye uwezo wa kugundua na kufuatilia asilimia kubwa ya vitendo vya rushwa. Muundo wake pia uangaliwe upya kuweza kukidhi mahitaji ya sasa. Serikali ichukue hatua za makusudi kuipa nyenzo na uwezo wa kifedha.

(3) Ili pendekezo hili liweze kufanikiwa hapana budi Taasisi ya Rushwa ifanye kazi kwa kushirikiana na wananchi na ijitangaze ili wananchi waweze kusaidiana nayo katika kupambana na rushwa. Aidha, taasisi iwe na ofisi katika kila mkoa na baadaye kila wilaya.

(4) Viwango vya mishahara vya watumishi wa taasisi viboreshwe kulingana na uzito na unyeti wa majukumu.

(5) Taasisi iimarishwe kwa kupewa vifaa vya kufanyia kazi na kwa kuzingatia umuhimu wa kazi zake ipewe kibali cha kuajiri wataalamu ili kuwa na watumishi wa kutosha.

(6) Aidha, ili kuiwezesha taasisi kufanya kazi kwa ufanisi, ipewe madaraka kusimamia matumizi yake kwa kuipa fungu (vote).

(7) Watumishi wa taasisi waelimishwe juu ya maadili ya kazi zao mara kwa mara na wanapokosa wachukuliwe hatua za kinidhamu mara moja bila kulindana.

(8) Ushauri wa taasisi katika masuala ya rushwa upewe uzito unaotakikana.

(9) Watumishi wa taasisi wanaotuhumiwa kuhusika na ukiukwaji maadili wachukuliwe hatua badala ya kuhamishwa. Uhamisho usiwe njia ya kurekebisha makosa.

(10) Kanuni za utumishi na nidhamu zitungwe mara moja kusimamia na kudhibiti mienendo ya maofisa wa taasisi.

 

SHERIA YA KUZUIA RUSHWA

177. Sheria ya Kuzuia Rushwa ya 1971 inaainisha makosa ya rushwa na kuunda Taasisi ya Kuzuia Rushwa. Aidha, sheria hii inatamka majukumu na mamlaka ya Taasisi ya Kuzuia Rushwa. Sheria hii ilifuta Sura ya 400 ya Sheria za Tanzania iliyokuwa inatumika nchini tangu mwaka 1958.

178.  Dhana ya mabadiliko yaliyotokea katika sheria ya 1971 ambayo ndiyo bado inatumika, ilikuwa ni kubana zaidi mianya ya rushwa na kurahisisha upelelezi. Mwishoni mwa miaka ya 1960 ueneaji wa rushwa ulianza kuonekana waziwazi. Aidha, mbinu mpya za rushwa zilianza kujitokeza. Serikali katika kukabiliana na  hali hii ililazimika kuimarisha matumizi ya sheria kama njia mojawapo ya kupambana na rushwa.

 

Makosa ya rushwa

179. Makosa ya rushwa yanayoainishwa katika Sheria ya Kuzuia Rushwa ya mwaka 1971 yamegawanyika katika makundi sita ambayo yanafafanuliwa hapa chini.

 

(i) Hongo (Corrupt Transactions)

Makosa ya hongo yaliyoainishwa katika kifungu cha 3 cha sheria yamegawanyika katika makundi mawili. Kwanza kudai, kuomba au kupokea au kupata kwa njia ya rushwa, au kukubali kupokea au kujaribu kupokea kitu chochote kama kishawishi au zawadi ili kutimiza au kutotimiza kitu chochote kinachohusiana na shughuli za mwajiri wake.

180. Kundi la pili linahusu utoaji au kuahidi kutoa fadhila ya aina yoyote kama kishawishi au zawadi kwa mtumishi kufanya au baada ya kufanya au kutofanya kitu chochote kinachohusiana na shughuli za mwajiri wake.

181. Inabainika kuwa sheria inawaona wapokeaji na watoaji kuwa na hatia kama dhamira yao itakuwa kufanikisha matakwa yao kwa njia ya rushwa. Hata hivyo, kama mmojawapo atajihusisha katika vitendo vya rushwa kwa madhumuni ya kuumbua vitendo vya rushwa sheria inamsetiri. Sheria inatambua matumizi ya mitego katika hongo kuwanasa walarushwa.

Tume imeridhika kuwa kifungu kinachohusiana na hongo (corrupt transactions) kinatosheleza na kibaki jinsi kilivyo. Hata hivyo, ili kulinda ushahidi wa yule anayetumika kama chambo, Sheria ya Kuzuia Rushwa ifanyiwe marekebisho ili iseme wazi kuwa taratibu zinazotumika kushughulikia ushahidi wa washiriki (accomplices) zisitumike kuathiri ushahidi wa chombo (decoys).

182.  Makosa ya hongo hutokea katika mazingira ya siri. Pale ambapo pande zote zinaridhika, hongo hupokelewa na huduma hupatikana. Hali hii inatokea kwenye mazingira ambayo rushwa imechukuliwa kama kitu cha kawaida na imekwisha shamiri.

Ili sheria iwe na makali, ni vyema jitihada zikachukuliwa kuhakikisha wananchi wanaodaiwa hongo ili wapate huduma wanakataa kutoa hongo na kwa upande mwingine watumishi wanaoshawishiwa wapokee hongo ili watoe upendeleo nao wasikubali kufanya hivyo.

 

Je, unajua Jaji Warioba katika ripoti hii aliyoiandaa mwaka 1996 alizigusaje taasisi nyingine? Usikose JAMHURI wiki ijayo. Mhariri.

By Jamhuri