Zikiwa zimebakia wiki tatu kabla ya Shirikisho la Kandanda Duniani (FIFA) kutoa tuzo ya Mwanasoka Bora kwa mwaka 2012/2013, mashabiki na wadau mbalimbali wa mchezo huo wanaendelea kubishana kuhusu nani anastahili kutwaa tuzo hiyo kati ya wachezaji mahiri watatu waliofika fainali.

Wanasoka hao ni mshambuliaji wa timu ya taifa ya Argentina pamoja na klabu ya Barcleona ya Hispania, Lionel Messi, anayetajwa kuwa bora kuliko wote duniani. Wengine katika ngwe hiyo ni nahodha na mshambuliaji tegemeo wa timu ya taifa ya Ureno na klabu ya Real Madrid ya Hispania, Cristiano Ronaldo na kiungo mahiri wa timu ya taifa ya Hispania na klabu ya Barcleona, Andres Iniesta.

Makocha na wachezaji wamekuwa wakilumbana kuhusu nani kati ya miamba hiyo mitatu anastahili kushinda tuzo hiyo ya juu zaidi katika medani ya kandanda.

 

Hata hivyo, wengi wanaamini kwamba Messi ndiye bora zaidi siyo kwa Ronaldo au Iniesta peke yao isipokuwa kwa wachezaji wote duniani wakiwemo Xavi, Mario Balotelli, Sergio Aguero, Gianluigi Buffon, Andrea Pirlo na mshambuliaji mahiri kuliko wote nchini Brazil hivi sasa, Neymar.

 

Tayari Messi amevunja rekodi iliyowekwa miaka 40 iliyopita na aliyekuwa mshambuliaji wa timu ya taifa ya Ujerumani Magharibi (wakati huo) na klabu ya Bayern Munich, Gerd Mueller, aliyefunga jumla ya mabao 85 mwaka 1972.

 

Jumatano iliyopita, Messi alifikisha mabao 88 mwaka huu alipofunga mara mbili, katika mechi ya Kombe la Mfalme (Copa del Rey) kwenye Uwanja wa Nuevo Arcangel, dhidi ya Cordoba wakati Barcelona iliposhinda kwa mabao 2 – 0.

 

Siku tatu kabla ya hapo, mshambuliaji huyo tishio zaidi duniani katika kizazi hiki, aliisaidia timu yake kuinyuka Real Betis mabao 3 – 1 katika mechi ya Ligi Kuu ya Hispania (La Liga), ambayo ilifanyika kwenye Uwanja wa Manuel Ruis de Lopera.

 

Kabla ya kuvunja rekodi hiyo ya Mueller iliyodumu kwa miaka 40, Messi (25) alianza kwa kuivunja kwanza iliyowekwa na Mfalme wa Kabumbu Duniani, raia wa Brazil, Edson Arantes du Nascimento, maarufu zaidi kwa jina la Pele, aliyefunga mabao 75 mwaka 1973 na kumfanya awe wa pili, hivyo kwa hivi sasa ni mfungaji bora wa tatu wa muda wote.

 

Messi alifanya hivyo usiku wa kuamkia Novemba 12, mwaka huu, alipofumania nyavu mara mbili katika ushindi wa mabao 4 – 2 wa La Liga kwa Mallorca na kufikisha jumla ya mabao 76.

Tayari ana rekodi nyingine ya kuwa mchezaji wa kwanza kupachika mabao matano katika mechi moja ya Ligi ya Mabingwa ya Ulaya, na pia anakaribia kuwa mwanasoka wa kwanza kushinda tuzo ya Ballon d’Or mara nne mfululizo.

 

Tofauti na Gerd Muller aliyezitikisa nyavu mara 85 mwaka 1972 au Pele aliyefunga mabao 75 mwaka 1973, kazi hiyo sasa ni ngumu kutokana na kuwepo ushindani mkubwa uwanjani, hivyo kwa kufunga idadi hiyo ya mabao 88 mwaka huu pekee, Messi amethibitisha kwamba siyo mwanasoka wa kawaida uwanjani.

 

Ndani ya La Liga, Messi pia anaongoza kwa kupachika mabao akiwa tayari na 23 mpaka ilipofika mwishoni mwa wiki. Anafuatiwa mbali na Radamel Falcao wa Atletico Madrid (mabao 16), Ronaldo (mabao 13).

 

Uwezo huo pia unazungumzwa kwa namna yake na mshambuliaji mahiri wa klabu ya Anzhi Makchachkala ya Urusi, Samwel Eto’o aliyediriki kumwita Messi kuwa “Mungu” wakati akimpongeza kwa kuweka rekodi mpya ya kufunga mabao duniani.

 

Mbali na Eto’o aliyekuwa na Messi katika klabu ya Barcelona kabla ya kuhamia Inter Milan ya Italia mwaka 2009, makocha na wachezaji wengine duniani pia wamekuwa wakimtabiria neema, lakini hata hivyo mwenyewe anasema vinginevyo.

 

Anaamini kwamba Andres Iniesta ni muhimu zaidi anapokuwa na timu yoyote dimbani, hivyo iwapo atakuwa Mwanasoka Bora Duniani kwake itakuwa ni furaha, jambo ambalo hata hivyo hakuna mdau mwingine wa kandanda aliyewahi kulizungumza hadharani.

 

Baadhi ya makocha hususan wa Klabu ya Real Madrid ambayo ndiyo hasimu mkubwa wa Barcelona katika La Liga, Jose Mourinho amekuwa akihangaika kumpigia debe Ronaldo ili ashinde tuzo hiyo, juhudi ambazo bado haziungwi mkono na wengi.

 

Wanaotaka aumalize utawala wa Messi aliyeshinda tuzo hiyo kwa miaka mitatu mfululizo, wanadai kuwa Ronaldo ana rekodi bora zaidi ikiwemo ya kuiwezesha klabu yake ya Real Madrid kutwaa taji la La Liga kwa msimu wa mwaka 2011/2012 uliomalizika Mei, mwaka huu.

 

Wanasema kuwa pamoja na Messi kuwa kinara wa mabao duniani kote hivi sasa, alishindwa kuiwezesha Barcelona kutwaa bingwa msimu uliopita.

 

Pia wanaliponda Kombe la Mfalme au Copa del Rey kwa madai kwamba halimo katika mataji yanayotambuliwa rasmi na FIFA.

 

Hata hivyo, yeye pia ameshindwa kuisaidia Ureno kutwaa Kombe la Dunia na hata la Ulaya, hivyo kwa kutumia kigezo hicho na hata cha ubingwa wa vilabu, wote wanafanana kwani kila mmoja ameisaidia klabu yake kuwa bingwa wa taji la kitaifa huku Messi akiwa juu zaidi yake.

 

Katika hali hiyo, swali linalopasua vichwa vya wengi linazidi kubakia lilelile la je, Ronaldo atafanikiwa kumng’oa Messi na kutwaa tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia, ile ambayo ilipangwa kutolewa Januari 7, 2013?

 

 

 

1793 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!